KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

DONDOO ZA WIKI

ALAMA ZA KIYAMA: -KUKITHIRI KWA BIASHARA

Kukithiri kwa biashara na Mwanamke kumsaidia mume wake katika biashara.

 Ndugu msomaji wetu mwema-Allah akurehemu-sote; sisi, wewe, yule na wao kwa pamoja tumpe sikio la usikivu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-atutajie alama hiyo, kwa kinywa chake anasema kama ilivyo pokewa kutoka kwa Abdullah bin Masoud-Allah awawiye radhi-ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:

 “Mbele punde ya Kiyama (Kabla ya Kiyama kwa kitambo kifupi, kutakuwa na) kusalimiana kwa kujuana na kuenea (kukithiri) kwa biashara mpaka mwanamke amsaidie mume wake (katika biashara)”. Al-Haakim & Ahmad-Allah awarehemu.

Endelea

SWALA ZA KUPATWA JUA NA MWEZI

Fiq-hi kama fani maalumu ya sheria yenye matawi mawili makuu; tawi la mambo ya ibada na lile la mambo yanayoitwa “Muamalaati”, ina Istilahi zake. Istilahi ya neno “Kusuufu”, hutumiwa na Mafaqihi kumaanisha kuzuilika kwa mwanga wa jua  kuifikia dunia bila ya kujali kuwa ni mzuiliko wa sehemu tu ya jua au ni jua zima. Kwa maana hi Mafaqihi wanaposema “Swalaatul-Kusuufi”, huwa wanamaanisha swala ya kupatwa kwa jua. Na hali kadhalika wameitumia Istilahi ya neno “Khusuufu” kumaanisha kuzuilika kwa mwangaza wa mwezi kuifikia dunia, iwe ni  mwezi wote au nusu yake. Kwa maana hii wanapoitumia ibara “Swalaatul-Khusuufi” huwa wanaikusudia swala ya kupatwa kwa mwezi, elewa. Na hali kadhalika kunajuzu kuitumia mojawapo ya Istilahi mbili hizi mahala pa Istilahi ya pili; yaani tunaweza kusema “Swalaatul-Kusuufi”, tukiikusudia swala ya kupatwa kwa mwezi na kinyume chake.

Endelea

UJIRA/MALIPO YA KUNYONYESHA

Ujira/malipo ya mama amnyonyeshaye mtoto, yanapaswa kulipwa na baba mzazi wa mtoto husika. Iwapo mume amemtaliki mkewe au kinyume chake, hapo ni bora mtoto akanyonyeshwa na mama yake. Na mama analazimika kutokumnyima mtoto wake maziwa yake ambayo ni haki yake. Ni wajibu wa baba katika hali na mazingira kama haya, kubeba gharama za mama wa mtoto bila kukosa. Ikiwa kutokana na mazingira yasiyo epukika mama hawezi kumnyonyesha mwanawe au baba kwa sababu zake mwenyewe anataka mtoto anyonyeshwe na wanawake wengine. Ni wajibu wa kidini wa baba kubeba gharama zote za mwanamke atakaye fanya kazi hiyo ya unyonyeshaji.

Endelea

MTUME AJARIBU KUISHI KWA AMANI NA MAYAHUDI

Mtume wa Allah ajaribu upeo wa juhudi yake kuishi kwa amani na Mayahudi , lakini maumbile yao ya usaliti yaliwashinda.

Hivi ndivyo yalivyokuwa maisha baina ya Mayahudi na majirani zao waislamu, yalikuwa ni mrorongo wa chuki na mifundo isiyopoa wala kukatika. Pamoja na yote haya, bado Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-hakupenda kujibu uhasama huu wa Mayahudi. Wala hakutaka kulipa uadui atendawao kwa uadui mfano wake, bali alikuwa akitafuta sana fursa itakayo muwezesha kuleta suluhu baina yake na wao ili waweze kuishi kwa amani na usalama. Na kamwe Mtume hakuanza kuwafanyia uadui, bali alifanya kila juhudi iliyokuwa ndani ya uweza wake kuwaita katika meza ya amani, mapenzi na ushirikiano.

Endelea

KUNDI LA KWANZA: MAULAMAA...Inaendelea

Halafu jua kwamba ghururi (madanganyo) na fitina zimewazidi wadau wa elimu (maulamaa) na kupa mgongo na mghafala umetawala. Wakaacha kuitendea elimu waliyo nayo, kwa ajili hiyo elimu ikawa imebakia ndimini mwao na haimo mioyoni mwao. Na imebakia kaulini mwao, haimo matendoni mwao, kwa sababu hiyo basi elimu ikawa ni hoja dhidi yao, kama alivyo sema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Elimu ni (aina) mbili; elimu iliyomo moyoni, basi hiyo ndiyo elimu iliyo na manufaa. Na elimu iliyo ulimini, hiyo ni hoja ya Allah dhidi ya mwanadamu”. Na katika jumla ya dua zake Bwana Mtume, alikuwa akiomba: “Ewe Mola wa haki! Hakika mimi ninakuomba elimu yenye manufaa”. Na akijilinda na kutaka hifadhi dhidi ya elimu isiyo nufaisha na moyo usio na unyenyekevu.

Endelea

Additional information