|
Msingi wa somo hili lililobeba anuani hii ni kauli ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu isemayo : NA MNAPOAMKIWA KWA MAAMKIO YEYOTE YALE, BASI ITIKIENI KWA YALIYO
BORA KULIKO HAYO, AU REJESHENI YAYO HAYO. HAKIKA ALLAH ANAFANYA HISABU YA KILA KITU
[4:86]
Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia mtakapotolewa salamu kwa kuambiwa
ASSALAAM ALEYKUM, basi nyie jibuni/itikieni kwa kusema WA-ALAYKUMUS SALAAMU WARAHMATULLAH
na mkitolewa salamu kwa kuambiwa ASSALAAMU ALEYKUM WARAHMATULLAH, basi nyinyi itikieni kwa
kusema WA-ALAYKUMUS SALAAM WARAHMATULLAH WABARAKATUH. Au itikieni salamu kama
mlivyosalimiwa bila ya kuongeza ziada yeyote. Kwa mfano mtu akikusalimia ASSALAAMU
ALEYKUM, nawe uitikie WA-ALAYKUMUS SALAAM na kama hivi.
Haya ndio maamkizi rasmi ya kiislamu kama alivyotufundisha Bwana
Mtume Rehema na Amani zimshukie -. Kwa hiyo waislamu wanatakiwa wasalimiane kwa
salamu hii, kwa sababu chimbuko la salamu hii ni jina tukufu la Mwenyezi Mungu ASSALAAMU
è MWENYE SALAMA/MTOAJI WA SALAMA. Bwana Mtume Rehema na
Amani zimshukie anatuthibitishia ukweli huu, aliposema : Hakika ASSALAAMU ni
jina miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu Mtukufu lililowekwa ardhini, basi enezeni
salamu baina yenu Bukhariy kutoka kwa Anas.
Maamkizi na salamu hii ya kiislamu yanabeba nembo ya AMANI na UTULIVU
kutokana na asili ya neno lenyewe. Kama vile muislamu anamwambia mwenziwe : Usikhofu Amani
ya Allah i pamoja nawe.
Salamu hupelekea watu kuzoeana na kupendana na pia ni dalili na
ishara ya adabu njema. Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie anatuambia :
Je, nikufundisheni/nikufahamisheni jambo mtakapolitenda mtapendana ?, Enezeni
salamu baina yenu Muslim, Abu Daawoud, Tirmidhiy na Ibn Majah kutoka kwa Abu
Hurayrah. Enezeni salamu maana yake mtoleeni salamu mumjuaye na msiyemjua.
Maamkizi/Salamu hii ndiyo salamu ya watu peponi, Tunasoma :
NA MAAMKIANO YAO HUMO NI (kusema) SALAAMUN (ALEYKUM)
[10:10]
TANBIHI : Isieleweke kuwa ni HARAMU waislamu kuamkiana kwa maamkizi
mengine yasiokuwa haya, bali maamkizi haya ndiyo yapewe umuhimu na nafasi ya kwanza. Kisha
ndipo wanaweza kuendelea na salamu kama vile : Shikamoo !, Habari Gani ? Subalkheri ! Good
morning na kadhalika.
Muislamu anatakiwa kufuata adabu/taratibu zifuatazo katika
salamu/maamkizi
- Mdogo aanze kumtolea salamu mkubwa, wachache waanze kuwatolea salamu walio wengi,
aliyesimama amtolee salamu aliyekaa, aliyepanda kipando amtolee salamu aendaye kwa miguu.
Muongozo huu tunaupata kupitia hadithi zifuatazo :
- Amesema Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie Mdogo amsalimie
mkubwa, na mpita njia (amsalimie) aliyekaa, na wachache (wawasalimie) walio wengi
Bukhariy kutoka kwa Abu Hurayrah.
- Aliyepanda amsalimie aendaye kwa miguu, na aendaye (amsalimie) aliyekaa, na
wachache (wawasalimie) walio wengi Bukhariy.
- Ni karaha kumtolea salamu mtu aliyeshughulishwa na jambo, mpaka amalize, kama vile
msomaji, muadhini, mlaji, anayeswali, na aliyeko msalani.
- Ukikutana na kundi la watu, usimkhusishe mtu mmoja na salamu yako kwa kumwambia
ASSALAAMU ALYEKUM Said (Mathalan). Bali wote watolee salamu hata kama huwajui. Imepokelewa
na Abdallah ibn Umar Allah awawie Radhi kwamba mtu mmoja alimwuliza Bwana
Mtume Rehema na Amani zimshukie Uislamu upi ndio bora ? (Mtume) akajibu
Lisha chakula, na umtolee salamu umjuaye na usiyemjua Bukhariy na Muslim.
- Toa salamu kwa sauti yenye kusikika kwa upole na bashasha. Sio unatoa salamu kwa
sauti ya ukali huku ukiwa umenuna au umekunja uso.
- Unapoingia nyumbani mwako, mtolee salamu mkeo na watu wote wa nyumbani. Bwana Mtume
Rehema na Amani zimshukie alimwambia Anas ibn Maalik : Unapoingia
nyumbani kwako, watolee salamu, itakithiri kheri ya nyumba yako Tirmidhiy.
Tunauthibitisha muongozo huu kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu : NA MNAPOINGIA
KATIKA MAJUMBA TOLEANENI SALAMU; (maamkio haya) NI ZAWADI ITOKAYO KWA ALLAH, YENYE BARAKA
NA MEMA
[24:61]
- Jitahidi siku zote kuwa wewe ndio wa kwanza kuwatolea watu salamu. Bwana Mtume
Rehema na Amani zimshukie amesema : Hakika bora zaidi ya watu mbele ya
Mwenyezi Mungu ni yule awaanzaye watu kwa salamu Abuu Dawoud na Tirmidhiy.
Hizi ni baadhi tu ya taratibu za salamu.
KUTAKA IDHINI YA KUINGIA (KUBISHA HODI)
Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia : ENYI MLIOAMINI ! MSIINGIE
NYUMBA AMBAZO SI NYUMBA ZENU MPAKA MUOMBE RUHUSA (mpige hodi) NA MUWATOLEE SALAMU WALIOMO
HUMO
. [24:27]
Na akasema tena : NA WATOTO MIONGONI MWENU, WATAKAPOBALEGHE
BASI NA WAPIGE HODI KAMA WALIVYOPIGA HODI WALE WA KABLA YENU
[24:59]
Katika aya hizi Mwenyezi Mungu Mtukufu anatufundisha adabu na
taratibu za kuingia katika nyumba za watu, anatutaka :
- Tubishe hodi kabla ya kuingia. Na hodi hubishwa mara tatu, kama hapana majibu
katika mara tatu hizo, basi shika njia uondoke. Huu ndio muongozo tuupatao katika kauli ya
Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie : Kubisha hodi ni mara tatu,
ukipewa idhini (ingia) na kama hukujibiwa rudi/nenda zako Bukhariy na Muslim.
- Tuwatolee salamu watu wa nyumba tuikusudiayo. Imepokelewa kutoka kwa Kildah ibn
Al-Hanbal Allah amuwie radhi amesema : Nilikwenda kwa Mtume Rehema na
Amani zimshukie nikaingia na sikumtolea salamu, akasema Rudi (toka nje,
uingie tena) useme : Assalaam Aleykum, je niingie? Abu Dawoud na Tirmidhiy.
- Ukisha bisha hodi, kaa pembeni ya mlango, kuliani ama kushotoni. Usikae mkabala na
mlango, kiasi cha kufunguliwa mlango tu, ukaweza kuona ndani moja kwa moja. Bwana Mtume
Rehema na Amani zimshukie anatuambia Hakika si vinginevyo
kubisha hodi kumewekwa kwa ajili ya jicho Bukhaariy na Muslim.
- Unapobisha hodi ukaulizwa wewe ni nani, sema mimi ni fulani, taja jina lako na wala
usiseme mimi. Haya ndio maelekezo tunayopata katika hadithi zifuatazo :
Imepokelewa kutoka kwa Ummu Haniy Allah amuwie Radhi
amesema : Nilimwendea Mtume Rehema na Amani zimshukie naye akiwa anakoga na
Fatmah akiwa anamsitiri, (Mtume) akauliza Nani huyo?(baada ya Ummu Haniy
kumtolea salamu). Nikajibu : Ni mimi Ummu Haniy. Bukhaariy na Muslim.
Imepokelewa na Jaabir Allah amuwie Radhi amesema :
Nilimuendea Mtume Rehema na Amani zimshukie nikagonga mlango, (Mtume)
akauliza : Nani huyo ? nikajibu : mimi (Mtume) akasema Mimi, mimi
Kana kwamba Mtume aliichukia jawabu hiyo (isiyotaja jina) Bukhaariy na Muslim.
Hizi ni baadhi tu ya adabu na taratibu za kubisha hodi kama
zilivyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie.
|
| |
TUJIFUNZE
NA TUKUBALI : kuwa salamu ya kiislamu ni miongoni mwa nembo na alama zinazomtambulisha
muislamu katika jamii na uma wa kiislamu, bali hata nje ya jamii ya kiislamu. Haya
jifakharishe kwa kuitumia salamu yako ya kiislamu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia :
NAMNA HIVI; ANAYEZIHESHIMU ALAMA ZA (dini ya) ALLAH, BASI HILO NI JAMBO KATIKA UTAWA
(Ucha Mungu) WA NYOYO [22:32]
Ewe Muislamu sikia raha, jawa na
furaha na ona fakhari kuamkiana kwa mtindo wa kiislamu, acha kuiga desturi za watu
wengine. Haikutoshi kuwa salamu yako inatambulika mbinguni na ndio maamkizi ya watu wa
peponi ?! Tunataraji na wewe kuwa miongoni mwao.
Watoto wetu walio wakubwa
wasiingie vyumbani mwa wazazi wao ila baada ya kubisha hodi na kupewa idhini ya kuingia.
Hii ni kwa sababu wasiingie ghafla na kuyakuta wasiyotakiwa kuyaona.
|