|
ii.
Fadhila/ubora wa
subira chini ya kivuli cha Sunnah (hadithi):
Na miongoni mwa yaliyo pokewa katika Sunnah katika kutaja
fadhila/ubora wa subira, ni hadithi zifuatazo:
1.
Imepokewa kutoka kwa Anas-Allah
amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Hakika Allah Ataadhamiaye amesema: Nitakapo muonja mja wangu kwa
vipenzi vyake viwili [macho], kisha akasubiri, nitampa badali ya pepo
kutokana na viwili hivyo”. Bukhaariy [10/100]-Allah amrehemu.
2.
Imepokewa kutoka kwa Abu
Hurayrah-Allah–amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-amesema: “Allah amesema: Hana mja wangu muumini kwangu mimi
malipo yoyote pindi nitakapo ichukua roho ya mpenzi wake miongoni mwa
watu wa dunia, ila pepo”. Bukhaariy [11/207]-Allah amrehemu.
3.
Imepokewa kutoka kwa Atwaa Ibn
Abi Ribaah amesema: Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi-aliniambia: Je,
nisikuonyeshe mwanamke katika watu wa peponi? Nikamjibu: Kwani
[nionyeshe]. Akasema: Huyu mwanamke mweusi [umuonaye], alimjia
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasema: Hakika mimi ninaangushwa na
kifafa na ninafunukwa na nguo, basi niombee kwa Mungu (aniponye). Mtume
akasema: “Ukitaka subiri na utapata pepo na ukitaka nitakuombea Mungu
akuafu”. Akasema: Nitasubiri, kisha akasema: Hakika mimi ninafunukwa na
nguo [nikiangushwa), basi niombee kwa Mungu nisifunukwe. Mtume
akamuombea”. Bukhaariy [10/99] & Muslim [2576]-Allah awarehemu.
4.
Imepokewa kutoka kwa Abu Saidi
Al-Khudriy-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah–Rehema na Amani
zimshukie- amesema: “...na atakaye isubirisha nafsi yake, Allah
atampa nguvu za kusubiri. Na hakupata kupewa mtu kipawa bora na
kikunjufu kuliko subira”. Bukhaariy [11/303] & Muslim [1053]-Allah
awarehemu
5.
Imepokewa kutoka kwa Swuhaibu
Ar-ruumiy-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah–Rehema na Amani
zimshukie-amesema: “Ajabu iliyoje kwa jambo la muumini, hakika jambo
lake lote ni kheri na hilo haliko kwa yeyote ila kwa muumini. Ikimfika
raha hushukuru, basi ikawa ni kheri kwake na ikimfika dhara [taabu],
husubiri na ikawa ni kheri kwake”. Muslim [2999]-Allah amrehemu.
6.
Imepokewa kutoka kwa
Jaabir-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alisema: “Watatamani watu wenye afya [duniani] siku ya
Kiyama, pale watu walio onjwa [kwa maradhi hapa duniani] watakapo pewa
thawabu. Lau kwamba ngozi zao zingekatwa kwa mikasi”. Tirmidhiy
[2402]-Allah amrehemu.
7.
Imepokewa kutoka kwa Abu
Hurayrah-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah–Rehema na Amani
zimshukie-amesema: “Mabalaa hayaachi kumuandama muumini mwanaume na
muumini mwanamke, katika nafsi yake, watoto wake na mali yake, mpaka
akutane na Allah ilhali hapana dhambi yoyote juu yake”. Tirmidhiy
[2399] & Al-Haakim [4/314]-Allah awarehemu.
8.
Imepokewa kutoka kwa Ummu
Salamah-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilimsikia Mtume wa Allah–Rehema na
Amani zimshukie-akisema: “Hapana muislamu yeyote anaye patwa na msiba
akasema aliyo amrishwa na Allah [kuyasema wakati huo]: “INNAA LILLAAHI
WA INNAA ILAYHI RAAJIUUN-HAKIKA SISI NI WA ALLAH, NA KWAKE YEYE HAKIKA
TUTAREJEA”...Ewe Mola wa haki! Nakuomba unipe ujira katika msiba huu
na unipe badali bora kuliko huo [msiba] akisema hivyo, Ila Allah atampa
badali bora kuliko huo. (Anaendelea) kusema: Zama alipo kufa Abu Salamah
[mume wangu], nikasema: Nani [mume] bora kuliko Abu Salamah; swahaba wa
Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie? Halafu Allah akanitia azma,
basi nikasema [maneno] hayo [aliyo yafundisha Allah]. Anasema: Basi
nikaolewa na Mtume wa Allah”. Muslim [918]-Allah amrehemu.
9.
Imepokewa kutoka kwa Abu Maalik
Al-Ashiariy-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-amesema: “Twahara ni sehemu ya imani na AL-HAMDULILLAH
inajaza mizani [ya mja siku ya hisabu]. NA SUB-HAANALLAH na
AL-HAMDULILLAH zinajaza (thawabu zake eneo) lililo baina ya mbingu na
ardhi. Na swala ni nuru, sadaka ni hoja, subira ni mwangaza na Qur-ani
ni hoja ya kukuokoa [ukiifuata] au kukuangamiza [ukiacha kuifuata]. Watu
wote hudamka, basi mwenye kuiuza nafsi yake, yuko mwenye kuikomboa [na
moto] au mwenye kuiangamiza”. Muslim [234]-Allah amrehemu.
Ndugu mwema-Allah akurehemu-huu ni mpetwapetwa tu ulio
chujwa kutoka katika mlango wa kutaja fadhila/ubora wa subira. Na lau si
kuchelea urefusho wenye kuchosha, basi tungeendelea kukuletea utungo wa
fadhila hizo chini ya kivuli cha maneno ya Mtume wako-Rehema na Amani
zimshukie. Na tunataraji katika hadithi chache hizi tulizo zinukuu, kuna
mazingatio na ukumbusho: “...KWA MWENYE MOYO AU AKATEGA SIKIO...”
[50:37] Kama ambavyo kuna ndani yake kani impelekeayo mja mwema kusubiri
katika yote yanayo msibu huku akiamini kuwa: “HAUTOKEI MSIBA KATIKA
ARDHI WALA KATIKA NAFSI ZENU ILA UMEKWISHA ANDIKWA KATIKA KITABU KABLA
HATUJAUUMBA...” [57:22]
|