Murua ni sifa njema ambayo muislamu wa kweli anapaswa kujipamba nayo
ili kuweza kuitoa sura ya Uislamu wake nje watu/ulimwengu uweze kuuona Uislamu wake. Kwa
hivyo Murua ni mwonzi/kioo kinachotoa nje taswira ya Uislamu wa mtu. Hii ni sifa ambayo
humpelekea na kumsukuma mtu kushikamana na tabia zote njema na kujipamba na sifa na ada
nzuri. Tabia hii huchangiwa kwa kiasi kikubwa na hima kubwa anayokuwa nayo mtu katika
kuyapupia mambo mema ya kheri na kuchunga heshima na hadhi yake. Vigezo viwili hivi:
- Kupupia kufanya kheri
- Kuchunga hadhi.
Ndivyo vyanzo vikuu vya tabia hii njema ya murua. Mtu akiwa na ari
kubwa katika kutenda mambo mema na akawa na hadhari kuu katika kuchunga heshima yake
isivunjwe, basi ni dhahiri kuwa ari na hadhari hiyo vitamfanya ahodhi tabia njema na
kujipamba na sifa nzuri na kujiepusha na kila ambalo kwa namna moja au nyingine
litapelekea kuvunjika heshima yake machoni mwa watu. Natija ya hali hii ni mtu kuwa
mkarimu, na ukarimu ni miongoni mwa sifa tukufu za Mwenyezi Mungu Mtukufu ambazo muislamu
anatakiwa ajipambe nazo. Amesema Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie
Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mkarimu apendaye ukarimu, na hupenda tabia tukufu
na huchukia tabia duni (mbaya) Abu Nuim, Twabaraaniy, Al-Haakim na Al-baihaqiy.
Kadhalika hali hii itamzalishia mwenye kuwa nayo tabia ya kutokuwaudhi na kuwakera wenzake
au kuwasababishia madhara jambo ambalo uislamu unalikemea vikali kabisa. Bwana mtume
Rehema na Amani zimshukie anatuasa katika hili - Atakayedhuru au kusababisha
madhara, Allah atamshushia madhara (na yeye) na atakayefanya uzito naye atafanyiwa uzito
na Allah. Ahmad, Abuu Daawoud, Tirmidhy, Nasani na Ibn Maajah.
Tunaweza kuigawa tabia hii ya murua katika mapote/makundi mawili makuu,
kama ifuatavyo:
1: Murua ambao uzaao tabia tukufu na sifa njema katika nafsi ya
mwanadamu. Aina hii ya murua humsukuma mja kushikamana na dini kwa maana yake halisi,
kujipamba na tabia/sifa njema kama vile kusema ukweli, kutekeleza ahadi, kusaidia masikini
na mayatima, ukarimu na kadhalika. Pia humlazimisha kujiepusha na mambo ya haramu kama
vile kusema uwongo, kutoa ushahidi wa uwongo, kula mali ya yatima, kula riba na mengi
mengineyo.
2: Murua hutoao/huletao athari kwa watu wengine. Aina hii ya murua humpelekea mtu kutoa
ushauri, nasaha kwa wenziwe kwa nia njema ya kujenga na kutengeneza kwa sababu anaiamini
kauli ya Mtume wake; Atakayemshauri nduguye (mwanadamu mwenziwe) jambo ili-hali
anatambua kuwa uongofu uko katika jambo jinigine, hakika amemkhini Abuu Daawoud na
Al-haakim, atakuwa na huruma kwa viumbe wenzake, atatekeleza amana kwa kuifanyia kazi
kauli ya mola wake; HAKIKA ALLAH ANAKUAMRISHENI KUZIRUDISHA AMANA KWA WENYEWE
(wanaozistahiki) ... (4:58) Atauzuilia mkono, ulimi na viungo vyake vyote na kila la
haramu na ataweza kutunza siri. Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie
anatuambia kuhusiana na suala zima la murua; Atakayeamiliana (Atakayechanganyika na
wenziwe kimaisha) na watu, akawa hawadhulumu, akazungumza nao akawa hawaongopei na
akawaahidi akawa havunji ahadi basi huyo ndiye mtu ambaye umekamilika murua wake na
kudhihiri uadilifu wake na imewajibika kumfanya ndugu. Katika hadithi hii tukufu,
Bwana Mtume anatubainishia sifa za mtu mwenye murua, sifa hizo ndizo zitkazotusaidia
kumjua ni nani ana murua na nani si mtu wa murua. Sifa hizo kwa mujibu wa hadithi ni
pamoja na:-
- Kutokuwa dhalimu. Mtu aliye mkamilifu wa murua hayuko tayari kudhulumu wala kudhulumiwa,
hili linatokana na kuikiri, kuikubali na kuimini kwake kauli ya mola wake isemayo;
................... MSIDHULUMU WALA MSIDULUMIWE. (2:279) Muislamu hakubali
kudhulimiwa kwa sababu anaamini kufanya hivyo ni katika jumla ya kuutekeleza uislamu wake
kuvitendo. Tusome kwa tafakari, mazingatio na mwisho tutende kwa mujibu wa tafakari na
mazingatio yetu; NA WALE WANAOLIPIZA KISASI BAADA YA KUDHULUMIWA, HAO HAKUNA NJIA YA
KULAUMIWA. BASI LAWAMA IKO JUU YA WALE WANAODHULUMU WATU NA WAKAWAFANYIA JEURI KATIKA
ARDHI PASIPO HAKI; HAO NDIO WATAKAOPATA ADHABU IUMIZAYO. (42: 41 42)
Amesema Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie katika
hadithil qudsiy: Amesema Mwenyezu Mungu Mtukufu; enyi waja wangu, hakika mimi
nimeiaharamisha dhulma juu ya nafsi yangu, na nimeifanya baina yenu kuwa ni haramu, basi
msidhulumiane
. Muslim. Hii ni mojawapo mongoni mwa sifa za
mtu aliye na mrurua kamili kwa mujibu wa hadithi.
- Sifa ya pili ya tu mkamilifu wa murua ni kutokusema uwongo. Muislamu uliyekamilika murua
wake hathubutu na wala hajasisri kabisa kusema uwongo, kwa sababu anaamini kuwa
kusema/kuzua uwongo ni sifa ya makafiri wasioziamini aya za Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Kuhusiana na hili tunasoma MWANAOZUA UWONGO NI WALE WASIOZIAMINI AYA ZA ALLAH NA HAO
NDIO WAONGO (16:105) kadhalika muislamu mkamilifu wa murua hasemi uwongo kwa kuwa
anayekubali, anayaamini na kuyafuata mafundisho ya Mtukufu Mtume wake Rehema na
Amani zimshukie aliposema;
.. jiepusheni na uwongo, kwani
uongo huongozea/hupelekea katika uovu na uovu hupelekea motoni, na mtu haendelei kusema na
kuupupia uwongo mpaka ataandikwa mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa ni muongo. Ahmad,
Bukhaariy, Muslim, Abuu Daawoud na Tirmidhiy.
- Kutokuvunja ahadi. Hii ndio sifa ya tatu ya mtu mkamilifu wa murua. Muislamu aliyeiva na
kukomaa kimurua havunji ahadi aliyoitoa yeye mwenyewe kwa khiyari yake, kwa sababu
anatambua kutekeleza ahadi ni amri ya mola muumba wake, Tusome:
..NA TIMIZENI AHADI KWA HAKIKA AHADI ITAULIZWA (SIKU YA
KIYAMA) (17:34) NA TIMIZENI AHADI MNAZOZITOA KWA JINA LA ALLAH MNAPOAHIDI; WALA
MSIVUNJE HIZO AHADI BAADA YA KUZITHUBUTISHA
(16:91)
Muislamu anaizingatia na kuitia matendoni kauli ya Mtume wake Rehema na Amani
zimshukie: Hana Imani asiyekuwa na amana na wala hana dini asiyekuwa na ahadi
Ahmad, Abu Yaalaa, Ibn Hibbaan na Al-baihaqiy.