|
i.
Kuhangaikia
kupunguza magumu ya Dunia kwa kukadiria mabaya zaidi yanayo weza
kutokea:
Na katika jumla ya sababu za kuondosha wahaka,
huzuni, shaka, wasiwasi na jakamoyo pale mja anapo sibiwa na majanga ya
Dunia. Ni mja huyo kuhangaika kuyapunguza na kuyaona hafifu, kwa
kukadiria mabaya zaidi yanayo weza kumtokea kuliko hayo yaliyo msibu na
aifunge nafsi yake juu ya hilo. Atakapo fanya hivyo, basi na
ajishughulishe kuyapunguza yale yanayo mkinika kuyapunguza kwa kadiri ya
imkani. Basi kwa ufungaji huo wa nafsi na muhangaiko huo wenye manufaa,
huondoka wahaka na jakamoyo lake. Na kunakuwa kutoa juhudi hiyo katika
kuvuta/kuleta manufaa na katika kuondosha madhara, ni jambo jepesi kwa
mja.
Zitakapo mshukia mja sababu za khofu, maradhi, ufakiri
na kukosa avipendavyo miongoni mwa vipendwa mbali mbali. Basi na
ajikinge na hilo kwa kuwa na utulivu na aifunge nafsi juu ya utulivu
huo. Kwani hakika kuifunga nafsi juu ya uwezekano wa kutokea kwa magumu,
kunayafanya magumu hayo kuwa mepesi na hivyo kuondosha dhiki iletwayo
nayo. Na khususan pale atakapo ishughulisha nafsi yake kuyaondosha kwa
kadiri ya uweza wake. Basi kwa ajili hiyo hukusanyika kwa upande wake
ufungaji wa nafsi pamoja na juhudi nufaishi ambayo humfanya kuacha
kuyashughulikia masaibu na majanga. Na ailazimishe nafsi yake kuzifanya
mpya kila mara nguvu zake za kupambana na magumu ya maisha. Pamoja na
kumtegemea Allah katika hili na kuwa na imani njema kwake kuwa anaweza
kila kitu.
Na wala hapana shaka yoyote kwamba mambo haya yana faida
yake kubwa katika kupatikana kwa furaha na ukunjufu wa moyo. Pamoja na
yale anayo yatarajia mja miongoni mwa thawabu za Dunia na Akhera. Na
hili ni jambo lionekanalo dhaahiri katika maisha yetu ya kila siku na
limethibiti kiamalia kwa baadhi yetu.
j.
Nguvu ya moyo na
kutokuuzonga kwa wahaka:
Na miongoni mwa dawa kubwa kabisa za maradhi ya
moyo bali pia na maradhi ya mwili, ni kuwa na nguvu ya moyo na
kutokuuzonga na kuushakizia mawazo na taswira mbaya ambazo huletwa na
fikra mbaya. Kwa sababu mwanaadamu atakapo jisalimsha kwa taswira na
moyo wake ukashakizika kwa viathiri miongoni mwa khofu, maradhi,
ghadhabu na tashwishi za visababishi machungu. Na kutazamia kutokea kwa
magumu na kuondoka kwa vipendwa nafsi, hilo litamtumbukiza katika
wahaka, jakamoyo na wasiwasi na maradhi ya moyo na mwili.
Na pindipo moyo utakapo tawakali na kumtegemea Allah na
wala usijisalimishe kwa fikra mbaya, wala usimilikiwe na taswira mbovu,
ukamuamini kidhati Allah na ukazitumai fadhila zake. Huondokwa na
wahaka, wasiwasi na jakamoyo na huondokwa na mengi miongoni mwa maradhi
ya moyo na mwili. Na hupata nguvu, ukunjufu na furaha ambayo hakumkiniki
kuielezea.
Ni hospitali nyingi zimesheni wagonjwa waathirika wa
mawazo mabaya au yaliyo pindukia mpaka na fikira potoshi. Na ni mara
nyingi sana mambo haya yameathiri nyonyo za watu wenye nguvu za kimaada
na kimaana, seuze watu wanyonge. Na ni mara nyingi tu mawazo yamepelekea
wadau wake kuangukia katika lindi la upite na uwenda wazimu! Na
msalimika ni yule aliye opolewa na Allah na akamuwafikisha kupigana
jihadi na nafsi yake ili kupata sababu nufaishi zenye kuutia moyo nguvu,
zenye kuondosha wahaka wake. Allah Atukukiaye amesema: “...NA ANAYE
MTEGEMEA ALLAH YEYE HUMTOSHA...” [65:03] Kwa mantiki hiyo basi, mwenye
kumtegemea Allah ni mtu mwenye moyo thabiti usio athiriwa na
fikra/mawazo mabaya na wala hatikiswi na vituka/vizuka. Hili ni kwa
sababu ya kujua kwake kwamba huo ni udhaifu wa nafsi na khofu ambayo
haina hakika. Na pamoja na hivyo, anajua kwamba Allah amekwisha chukua
dhamana kwa yule atakaye mtegemea Yeye, kumtosheleza na kumtoshea kuliko
timia. Basi yeye na amuamini kidhati Allah na aiyakinishe ahadi yake
hiyo. Hapo utaondoka wahaka wake na jakamoyo lake na uzito wake utageuka
kuwa wepesi na khofu yake kuwa amani.
Katika kauli yake Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie: “Muumini mwanaume asimchukie muumini mwanamke, akiichukia
kwake tabia moja, atairidhia kwake tabia nyingine”. Kuna faida mbili
kubwa:
FAIDA YA KWANZA: Kuna muongozo/maelekezo ya namna ya
kuamiliana na mke, ndugu, rafiki, mwenzi katika shughuli na kila ambaye
mna mahusiano ya namna fulani baina yenu. Kwamba inakupasa uwe makini na
yakini ya kuwa yeye kama binaadamu ni lazima atakuwa na
aibu/kasoro/mapungufu au jambo unalo lichukia. Utakapo lichomozea na
kulikuta hilo, basi hapo linganisha baina ya kasoro hiyo na ile nguvu ya
mahusiano na ubakiaji wa mapenzi unao kuwajibikia. Ulinganishe kwa
kukumbuka mazuri aliyo nayo na makusudio khususi na yale enevu. Kwa njia
hii ya kuyafumbia macho makosa/mapungufu na kuyaangalia mema/mazuri,
hudumu ule usuhuba/muambatano na yale mafungamano na raha hutimia na
kupatikana kwako.
FAIDA YA PILI: Kunapatikana kuondoka kwa jakamoyo na
wasiwasi na kunabakia utakaso wa moyo na kupatikana kwa raha na amani ya
moyo baina pande zote mbili.
Mtu ambaye hakuongozeka na muongozo huu wa Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-bali akaligeuza suala hili. Akayaangalia
makosa/mapungufu na kuyapa upofu mema/mazuri, huyo ni lazima utampata
wasiwasi. Na hapana shaka mahusiano yake na wale anao fungamana nao na
hivyo kusababisha kukatika kwa haki nyingi ambazo zinamlazimu kila mmoja
wao kuzichunga.
Na wengi miongoni mwa watu wenye hima za juu
wanazidhibiti nafsi zao wakati wa kutokea kwa majanga na mazonge, kwa
subira na utulivu. Lakini wakati wa mambo mepesi ya hovyo wanapatwa na
jakamoyo na kukosa amani ya moyo. Sababu ya hili ni kwamba wao
wamezidhibiti nafsi zao katika mambo makubwa na kujisahau katika mambo
madogo. Basi kwa ajili hiyo, hayo madogo waliyo yadharau yakawadhuru na
kuathiri amani ya mioyo yao na hivyo kuziharibu raha zao. Kwa hivyo basi
mtu makini mwenye akili kunjufu, ni yule anaye idhibiti nafsi yake na
kuifanya imara juu ya mambo madogo na yale makubwa. Na si hivyo tu, bali
anamuomba Allah Mola Mlezi wake msaada juu ya hayo makubwa na madogo
yanayo msibu katika mchakato mzima wa maisha yake katika ardhi hii ya
Manani. Na amuombe asimtupe mkono japo kwa kitambo cha upepesi wa jicho,
basi wakati huo ndipo yatakapo kuwa mepesi kwake madogo kama yalivyo
kuwa mepesi kwake makubwa. Naye atabakia kuwa mtulivu wa nafsi, mwenye
amani ya moyo na mwenye raha ya maisha.
|