Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Akhlaaq-Tabia  

"Hakika si vingine nimetumwa kuja kutimiza TABIA NJEMA" Hadith Tukufu

KUJUA KWAMBA MAISHA YA MAFANIKIO NI MAFUPI SANA

 Faida

 

 m)          Kujua kwamba maisha ya mafanikio ni mafupi sana:

         Mtu mweledi anajua kwamba maisha yake ya sawa sawa, maisha ya mafanikio na utulivu, ni maisha mafupi sana. Kwa hivyo basi, kwa kuukiri na kuujua ukweli huu, anajua ya kwamba haitakikani kwake kuzidi kuyafupisha kwa kuwa na wahaka/huzuni na jakamoyo. Kwani yote hayo ni kinyume na maisha ya sawa sawa, kwa ajili hiyo huionea unyimi sehemu kubwa ya maisha yake kuporwa na wahaka/huzuni/jakamoyo. Na katika hili hapana tofauti baina ya mja mwema na yule aliye muovu. Lakini muumini yeye katika wasifu huu, ana fungu toshefu la Duniani na Akhera.

Na pia inatakikana mja atakapo patwa na la kuchukiza au akachelea kupatwa nalo, yeye kulinganisha baina ya baki ya neema zipatikanazo kwake, zile za kidini na zile za kidunia. Na baina ya yale machukivu yaliyo mpata, katika huo mlinganisho utamdhihirikia wingi wa neema alizo nazo na hivyo kumezwa kwa machukivu yaliyo msibu. Nae akawa mwepesi mno wa fuadi na bali na hivyo kuyaepa kabisa madhara ambayo yangeweza kumpata kutokana na wahaka/jakamoyo.

Na hali kadhalika alinganishe baina ya madhara anayo yachelea kumtokea na baina ya imkani nyingi za kusalimika na mabaya hayo. Kwa mantiki hii basi, asiiache imkani dhaifu kuzishinda imkani nyingi zenye nguvu. Kwa kufanya hivi, utaondoka wahaka/huzuni/wasiwasi na jakamoyo lake. Na akadirie imkani kubwa kabisa ambazo kuna uwezekano wa kumsibu, basi aifanye makini na kuituliza nafsi yake kwa ajili ya kutokea kwake ikiwa yamekadiriwa kutokea. Na ajishughulishe kuondosha yale ambayo hayajatokea na kuyaondosha au kuyapunguza yale yaliyo kwisha tokea.

Na katika jumla ya mambo nufaishi, ni wewe kujua kwamba maudhi ya watu wanayo kufanyia khususan kauli zao chafu, hayakudhuru wewe bali huwadhuru wao wenyewe. Yatakudhuru tu iwapo utaishughulisha nafsi yako kuyajali na kuyapa nafasi ya kuzimiliki hisia zako. Basi ni wakati huo ndipo yatakapo kudhuru kama yanavyo wadhuru wao. Lakini ikiwa wewe hutayajali, basi hayatakuwa na upenyo wa kukudhuru kwa lolote.

Na utambue ya kwamba maisha yako yanafuata fikra zako, basi zikiwa fikra hizo ni katika  yale ambayo manufaa yake huirejea dini au Dunia, basi maisha yako yatakuwa ni mazuri yenye kunadi saada (mafanikio ya kweli). Na kama  fikra zako hazitakuwa hivyo, basi hapana shaka kwamba hali itakuwa kinyume na hivyo.

Na miongoni mwa sababu za kuondosha wahaka/huzuni, ni wewe kuimakinisha nafsi yako kutokutaka shukurani ila kwa Allah. Kwa hivyo usijali wala kulazimisha kushukuriwa na yule uliye mtendea wema. Kama alivyo sema Allah Atukukiaye kwa upande wa waja wake makhsusi: “HAKIKA SISI TUNAKULISHENI KWA WAJIHI WA ALLAH. HATUTAKI KWENU MALIPO WALA SHUKRANI”. [76:09] Na hili linakokotezeka zaidi katika muamala wa wake na watoto na wale ambao una mafungamano nao ya karibu. Basi wakati wowote utakapo imakinisha nafsi yako juu ya kuwaondoshea shari/madhara, hapo utakuwa umejiondoshea shari wewe mwenyewe na utakuwa umejipumzisha.

Na katika jumla ya vileta raha na amani ya moyo, ni wewe kuyaweka mbele ya macho yako mambo yenye manufaa na tenda amali katika kuyatekeleza. Na wala usiyageukie mambo yenye kudhuru, ili kwa kufanya hivyo upumbazike na sababu zenye kuleta wahaka/huzuni na wasiwasi na jakamoyo.

Na miongoni mwa mambo yenye manufaa, ni wewe kuzimaliza kazi/amali zako katika wakati huo na kuwa na faragha katika wakati ujao. Kwa sababu kazi kama zitakuwa hazikumalizwa, zitakurundikia kazi zilizo tangulia na hizi za sasa na hivyo kuwa mzigo mzito usio bebeka juu yako. Lakini utakapo kimaliza kila kitu kwa wakati wake, utayaingia mambo yajayo kwa nguvu ya fikra na nguvu ya kazi.

Na inatakikana uchague na kuteua katika matendo/kazi nufaishi, ile yenye umuhimu mkubwa kuliko zote, kisha inayo ifuatia hiyo na kama hivi kwa mpango huu. Na upambanue baina ya ile inayo pondokewa na kupendwa zaidi na nafsi yako. Kwani kinyume chake husababisha uchovu, ukimwa na maharibiko. Na jisaidie juu ya hilo kwa kuleta fikra sahihi na kuomba ushauri, kwani katu hakujuta aliye omba ushauri. Na ukistadi kwa makini unacho taka kukifanya, utakapo thibitisha kuwa kina manufaa na ukaazimia kukitenda, basi hapo mtegemee Allah, kwani hakika Allah anawapenda wamtegemeao.

Mpendwa msomaji wetu-Allah akurehemu-kwa auni na taufiq yake Allah, mfululizo wa makala: NJIA FAIDISHI KWA MAISHA YENYE MAFANIKIO, umetamatia. Tunamshukuru Allah kwa ukamilifu na tunamuomba maghufira kwa mapungufu. Tumuombe Allah atuwafikishe kukutana juma lijalo katika mfululizo wa makala mpya.

 

  



 | Tuandikie |