|
Chimbuko na msingi wa somo/mada hii ni kauli tukufu ya mwenyezi Mungu Mtukufu
ndani ya kitabu chake kitukufu allipomwambia Mtume wake; "... NA UFUNGAPO NIA
MTEGEMEE ALLAH (tu ufanye uliloazimia) HAKIKA ANAWAPENDA WAMTEGEMEAO." (3:159)
Tutafahamu kutokana na kauli hii ya Mwenyezi Mungu kwamba "azma" ni
nguvu fulani ya utendaji ambayo huwa ndani ya nafsi ya kila mtu, ni nguvu hii ambayo
humsukuma mtu kulitenda lile alitakalo, liwe ni jema au baya. Bila ya kuwa na nguvu hii ya
utendaji "azma" binadamu hawezi kutenda/kufanya jambo lolote lile liwalo, la
shari au la kheri. Kwa mantiki hii tunaruhusika kabisa kuigawa azma katika makundi mawili:
- Azma njema (ya kheri)
- Azma mbaya (ya shari)
Azma njema, ambayo ndio somo letu na ambayo ndio iliyotajwa ndani ya aya hapo juu
ni ile inayompelekea mtu kuwa na subira, kuridhia kukabiliana na vikwazo na magumu yote
atakayokutana nayo katika safari ya utekelezaji wa maazimio yake mema. Azma hii njema
itamfanya mtu kuwa thabiti asiyeyumbishwa na yeyote/lolte katika kutekeleza amali zake
njema mpaka ayahakikishe matakwa yake. Katika kuyafanya yote hayo, mtu mwenye azma hii
njema humtegemea sana mola muumba wake katika kufikia ufanisi na matokeo bora ya azma
yake. Huamini kuwa hakuna yeyote au nguvu yoyote kutoka kwa yeyote inayoweza kumsaidia
katika hayo aliyoyaazimia ila kwa nguvu, matakwa na mapenzi ya Mwenyezi Mungu, Bwana Mlezi
wa viumbe wote.
Azma yaani nguvu/msukumo wa utendaji una athari kubwa sana katika maisha ya kila
siku ya binadamu katika ulimwengu huu aishimo hivhi sasa na ule ujao. Azma huathiri kwa
kiwango kikubwa maeneo yafuatayo:-
- Akili
- Tabia
- Itikadi
- Akili:- Hebu tujaribu kuangalia ni kwa kiasi gani azma inavyoweza kuliathiri eneo
hili mama katika mwili wa binadamu. Azma ndio kichocheo kikubwa katika kuamsha ari na
kumuhamasisha mtu kujikomboa kutoka hali duni aliyomo kwenda katika hali bora zaidi. Azma
inapoungana na neema ya akili aliyozawadiwa mwanadamu na mola wake, hapo ndipo utamuona
mwanadamu anaweza kugundua vitu na zana mbalimbali ambazo zinamsaidia kuyaboresha na
kuyarahisisha maisha yake na kuyaongezea utamu na ladha maisha haya. Hapo ndipo binadamu
huutumia ukhalifu wake kwa kuyatawala mazingira yake na kuzitumia rasilimali zilizomo
duniani kwa ajili ya manufaaa ya vizazi vya wanadamu. "YEYE NDIYE ALIYEKUUMBIENI
VYOTE VILIVYOMO KATIKA ARDHI (kabla hajakuumbeni ili mkute kila kitu tayari)
"
(2:29)
Azma kwa kushirikiana na akili humsukuma binadamu kuwa mdadisi, udadisi huu
humsukuma kuwa mtafiti. Utafiti ambao humfikisha katika pwani ya ugunduzi. Ugunduzi huu
ndio humfanya binadamu kupiga hatua mbele katika maendeleo. Kutumia akili, kutafiti na
hatimae kugundua ni jambo jema ambalo uislamu unalihimiza sana, tusome kwa mazingatio:
"AMBAO HUMKUMBUKA ALLAH WAKIWA WIMA NA WAKIKAA NA WAKILALA NA HUFIKIRI UMBO LA MBINGU
NA ARDHI (pia namna gani Allah alivyoumba wakasema:)" MOLA WETU!HUKUVIUMBA HIVI BURE.
UTUKUFU NI WAKO BASI TUEPUSHE NA ADHABU YA MOTO" (3:191) Tuzidi kusoma:
"
NAMNA HIVI ALLAH ANAKUBAINISHIENI AYA(zake) MPATE KUFIKIRI
(mfikiri) KATIKA (mambo ya ) DUNIA NA (mambo ya ) AKHERA." (2:219 220)
Ni azma pia kwa msaada wa akili ambayo humsukuma binadamu kukaa chini, kutafakari
na hatimaye kuibuka na jawabu na ufumbuzi wa matatizo yanyomkabili kutokana na ujinga,
maradhi, umasikini na itikadi potofu. Hapo ndipo binadamu huweza kugundua dawa anuwai za
kumtibu maradhi mbalimbali yanayomsumbua na kuvuruga utendaji wake. Akagundua zana stadi
zitakazomsaidia kuutokomeza umasikini.
- Tabia: Tabia ya mtu pia kwa kiasi kikubwa huathiriwa na kutawaliwa na azma. Hii ni
kwa sababu tabia ya mtu haiwezi kabisa kujulikana na watu wengine ila kwa kupitia nguvu
hii ya utendaji iliyomo ndani yake. Mtu anapoimiliki nguvu hii na ikamuelekeza kutenda
matendo yayokubalika kiutu, kimaadili na kiitikadi matendo haya yanapokuwa dhahiri mbele
ya wanajamii wamzungukao, hapo ndipo jamii husika humtia mtu huyo katika daftari la watu
wenye tabia njema, watu wakubalikao katika jamii. Ama yule ambaye hushindwa kuimiliki azma
yake, azma hii ikampelekea kutenda matashi ya nafsi yake bila ya kuangalia madhara au
manufaa yua matendo hayo kwake na kwa jamii ni dhahiri kuwa utendaji wake utakuwa ni mbaya
mbele ya hadhira (jamii). Hapo ndipo jamii humhukumu kupitia utendaji wake huo kuwa ni mtu
mbaya mwenye tabia na athari mbaya kwa jamii. Kwa ujumla tunasema kwamba azma ndio
huidhirihirisha nje tabia ya mtu, iwe ni nzuri inayokubalika au ile mbaya isiyokubalika.
- Itikadi: Itikadi au Imani hili pia ni eneo ambalo huathiriwa sana na azma. Nguvu
hii ya utendaji azma ndio humsukuma mwanaitikadi au muumini wa imani fulani kutenda na
kuishi kwa mujibu wa imani yake. Humfinyanga kuitetea imani yake kwa gharama yoyote ile
hata ikibidi rorho yake. Humuandaa kusubiri na kuvumilia misukosuko na matatizo mbalimbali
ya kimaisha. Tusome pamoja na tutafakari:- "MTAPATA MISUKOSUKO KATIKA MALI ZENU NA
NAFSI ZENU, NA MTASIKIA UDHIA MWINGI KWA WALE WALIOPEWA KITABU KABLA YENU NA KWA
MUSHRIKINA. NA KAMA MKISUBURI NA KUJILINDA NA ALIYOYAKATAZA ALLAH (mtakuwa mmefanya jambo
zuri) KWANI MAMBO HAYA NI KATIKA MAMBO MAKUBWA YA KUAZIMIA MTU KUYAFANYA."(3:186) Hii
ndio azma na namna iinavyotawala na kuathiri akili, tabia na itikadi ya binadamu. Kutokana
na umuhimu huu, tunaweza kusema kuwa uislamu wa mtu haukamiliki ila pale atakapojipamba na
tabia/hali hii ya "azma". Muislamu ni lazima awe mtu mwenye azma, na sio azma tu
bali azma njema. Hii ni kwa sababu mtu anapoikosa nguvu hii ya utendaji "azma"
jepesi huliona gumu, dogo huliona kubwa na liwezekanalo huwa kwake ni muhali na hivyo
kumfanya abakie nyuma kimaendeleo. Akili yake itadumaa, haitoweza kudadisi kutafiti wala
kugundua, vipi utamtazamia mtu kama huyo kuwa na maendeleo?!
|