Chimbuko la somo letu la leo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani
ya Qur-ani Tukufu "
.WALA USITAWANYE (mali yako ) KWA UBADHIRIFU
HAKIKA WATUMIAO KWA UBADHIRIFU NI NDUGU WA MASHETANI (wanamfuata shetani) NA SHETANI NI
MWENYE KUMKUFURU MOLA WAKE (17: 26-27).
Huu ndio ukatikati wa matumizi, kutumia mali kwa kiasi cha haja kama
ilivyo ndani ya Qur-ani na hii ndio desturi ya Uislamu. Bwana Mtume Rehema na Amani
zimshukie alikuwa akimuomba Mola wake akisema: "Ewe Mola wa haki! Ninakuomba
(uniwezeshe) kukuogopa katika siri na dhahiri, na ninakuomba neno la ikhlasi katika
ghadhabu na ridhaa na ninakuomba ukatikati wa matumizi katika ufakiri na
ukwasiNasaai na Al-Haakim kutoka kwa Ammaar Ibn Yaasir
Ukatikati wa matumizi ni kutokufanya ubadhirifu na ufujaji katika
matumizi ya mali sambamba na kutokujidhili na kujidhiki katika matumizi. Ukatikati wa
matumizi ni pamoja na kuwa na mipango mizuri (bajeti) ya matumizi ya kila siku (ya muda
mfupi) na yale ya muda mrefu (ya mwaka au miaka) . Hii ni sifa/tabia ya msingi na muhimu
anayotakiwa kila muislamu bali kila mtu kujipamba nayo. Inatakikana mtu awe anajiwekea
akiba japo kidogo kutokana na pato lake ili iweze kumsaidia wakati wa dharura /haja na
wakati wa utu uzima ambapo hataweza kuchuma tena. Ni dhahiri kuwa hili la kujiwekea akiba
halitawezekana ila kwa kuwa na mipango thabiti na matumizi mazuri ya mali. Ukatikati wa
matumizi ni kutokutumia zaidi ya haja kwani huo utakuwa ni ubadhirifu na ufujaji ambao
tumekatazwa na kukemewa na Mola wetu na pia ni kutokutumia chini ya haya na il-hali unacho
cha kukutosha, huko kutakuwa ni kujidhiki kusiko na nafasi katika Uislamu. Utakuta mtu
amehodhi na kumiliki mali kiasi alichojaaliwa na Mola wake lakini anajidhiki yeye
mwenyewe, mkewe, wanawe, ndugu na jamaa zake . Mola wake amemkunjulia yeye anajidhiki ni
akili gani hii, ni ya nini basi neema hii? Wakati wa Bwana Mtume mtu mmoja alikuja kwa
Mtume Rehema na Amani zimshukie hali (namna alivyo) yake haikumpendeza
Mtume, akamuuliza Unayo mali? Akamjibu : Naam, (Mtume) akamuuliza tena,
Ni aina gani ya mali uliyonayo? Akajibu: Nina kila aina ya mali aliyonipa
Mwenyezi Mungu (Yaani anao ngamia, ngombe, mbuzi, Kondoo, mazao na matunda) Mtume
akamwambia , Basi hakika Mwenyezi Mungu anapenda kuiona athari ya neema zake
alizokuneemesha Tirmidhiy na Al-Haakim. Mwenyezi Mungu Mtukufu pia anatuambia juu ya
hili: "NA NEEMA YA MOLA WAKO ISIMULIE". (93:11) yaani izungumze kwa njia ya
kushukuru si kwa ajili ya kujisifia na kujigamba . Ni vema ikakumbukwa kuwa kuizungumza
neema ya Mwenyezi Mungu aliyokueneemesha hakukomelei tu kuitaja kwa ulimi bali kwa hali
pia. Huna sababu hata kidogo ya kujidhili kwa njaa, kuacha kujenga nyumba nzuri, kula
chakula kizuri, kuvaa vizuri na kuwadhiki mkeo , wanao na wazazi wako na Il-hali neema ya
Mola wako i mikononi mwako. Hujakatazwa kutumia kwa nafasi na kiasi ulichokatazwa ni
ubadhilifu na ufujaji, tusome na tutafakari
.. NA KULENI (vizuri)
NA KUNYWENI (vizuri) LAKINI MSIPITE KIASI HAKIKA YEYE (Mwenyezi Mungu) HAWAPENDI WAPITAO
KIASI (wapindukiao mipaka)" (7:31). Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie
anatuasa "Bora ya dinari (pesa) anayoitumia mtu ni ile dInari anayoitumia kwa
ajili ya familia yake, na dinari anayoitumia kwa ajili ya (chakula cha) farasi wake katika
njia ya Mwenyezi Mungu na dinari anayoitumia kwa ajili ya wenziwe katika jihadi
Muslim na Turmidhiy.
Na akasema tena Mtume kumwambia Saad Ibn Abiy waqasi
Hakika hukutoa cho chote (chakula /matumizi) ukitafuta kwa utoaji huo radhi za
Mwenyezi Mungu ila utapewa ujira kwa, hata kile unachokitia ktika kinywa cha mkeo
Bukhaariy na Muslim.
Ukatikati wa matumizi, kutumia kwa kiasi ni sifa/tabia muhimu sana na
yenye faida kubwa sana. Tabia hii humuingiza Muislamu katika fungu la waja wa Mwenyezi
Mungu awapendao. Mwenyezi Mungu anatuambia NA WAJA WA RAHMANI (Mwenyezi Mungu mwingi
wa Rehema)
"(25:63) akaisifia hali yao wenyewe namna walivyo, hali yao pamoja na
wanadamu wenzao yaani namna wanayoishi nao, hali yao naye yaani mahusiano na mafungamano
yao na Mola wao, kisha ndipo akaitaja hali yao na mali zao. Akasema, NA WALE AMBAO
WANAPOTUMIA HAWATUMII KWA FUJO WALA HAWAFANYI UBAHILI BALI WANAKUWA KATIKATI BAINA YA
HAYO (25: 67).
Hawa ndio waja wa Rahmani hawaitumii neema ya Mola wao kwa fujo na
wala hawafanyi ubahili kwao wenyewe, familia zao, jamaa na ndugu zao pamoja na jirani zao.
Wala hawafanyi ubahili kutoa kuwasaidia waislamu wenzao katika majanga mbalimbali
yanayowasibu kama vile kufuta ujinga, maradhi, umasikini uliokithiri, mafuriko, ukame na
kadhalika. Na zaidi ya yote hayo hawafanyi ubahili kutoa haki ya Mwenyezi Mungu liyowapasa
yaani Zakah. Hawa hawafanyi kabisa ubadhilifu na ufujaji katika matumizi yao
ubadhirifu/ufujaji ni pale mtu anapotumia neema ya mali aliyopewa katika njia za maasi
kama vile ulezi, madawa ya kulevya, zinaa, kuchezea kamari, kuingilia disko na mambo
mengine ya haramu au kutumia katika mambo ya Mubah kwa kupita kiasi, akawa anakula anasa
na kutupa, anabadili nguo kutwa, mara nne, ana magari ya kutembelea yeye na familia yake
zaidi ya matatu, hii pia ni aina ya ubadhirifu. Muislamu hatakiwi kujitanua sana katika
matumizi zaidi ya haja au uwezo wake, mtu ajikune pale unapofikia mkono wake. Muislamu
anatakiwa apime na kuwa na uwiano baina ya mapato na matumizi yake, matumizi yasizidi
mapato yake, bali matumizi yawe chini kuliko mapato na ikiwezekana awe na akiba anayoiweka
kutokana na mapato yake, hayo huu ndio ukatikati wa matumizi unaozungumzwa na Uislamu.
Muislamu hatakiwi kujitnua mno kusikokuwa na sababu ila ufakhari na sifa tu, kiasi cha
kumweka katika mzigo wa madeni yasiyolipika. Muislamu lazima atambue kuwa kuchukua deni
bila ya kuwa na uhakika wa kulipa ni kosa/dhambi , ajue kuwa deni ni udhalili, ni utumwa,
ni hangaiko la moyo na ni mzigo akhera. Kwanini basi ajitie kaitka janga hili bila ya
sababu ya msingi?! Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie anatuonya
"Atakayechukua mali za watu kwa lengo la kulipa, Allah atamlipia (yaani atampa uwezo
wa kulipa ) na atakayechukua mali za watu (deni) kwa lengo la kuzitilifu, Allah atamtilifu
(yaani atamuagamiza yeye na mali yake hiyo ya dhulma)Bukhaariy na Ibn Maajah.
Hivi ndiyo anavyokuwa au anavyotakiwa kuwa Muislamu, anapotumia
hatumii kwa fujo wala hafuji mali ovyo ovyo kwani anaitakidi kuwa Mtume -Rehema na Amani
zimshukie- amekataza na kukemea ufujaji wa mali, ufujaji wa neema, Hakika Mwenyezi
Mungu Mtukufu amekuharanishieni kuwaasi mama (zenu) kuwazika watoto wa kike wakiwa hai,
kufanya ubahili na kuomba, na anachukia kwenu, usengenyi, kuuliza sana, na ufujaji wa
mali" Suyuty al-Jaamii As-Swaghyr.
Itakidi kuwa mali yoyote uliyonayo mkononi unayomiliki si yako hiyo
ni ya jamii nzima utakapoitumia usivyostahili utakuwa umejidhulumu wewe mwenyewe bali na
jamii nzima. Kwa mantiki hii, tunasema yeyote anayeitumia pesa yake katika kubugia tumbaku
au kuvuta sigara kwa mfano, huyu anajifujia mali yeye na anaifujia jamii pia . Anajidhuru
yeye mwenywe kwa pesa yake mwenyewe kwa sumu ya tumbaku isio na chembe ya faida mwilini
mwake. Kumbuka mali ni neema inakupasa kuihifadhi na kuwa na matumizi sahihi/halali. Kuna
miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiislamu inayohitaji msaada wa mitaji, waislamu
wanahitaji mashule, wanahitaji mahospitali, wanahitaji misikiti, mayatima wanahitaji
kulelewa, wasiojiweza wanahitaji matunzo, waislamu wamegubikwa na umasikini na njaa
wanahitaji kukwamuliwa. Kwa nini basi, pesa hii tunayoifuja katika uvutaji wa sigara,
ulevi, kamari, disko, na zina isielekezwe kule katika maeneo hayo?! Ubadhirifu na ufujaji
umekuwa ndio nembo yetu, tunafanya ubahili kutoa katika mambo ya kheri na tunaona fakhari
na sifa kutoa katika mambo ya shari na haramu. Tunatumia mamilioni ya pesa katika
kudhamini mashindano ya urembo, matamasha ya muziki na kadhalika huku mayatima wanakosa
haki yao ya kupatiwa elimu. Waislamu tubadilike sasa, tuzidhibiti nafsi zetu, tuwe na
kipimo na kiasi katika matumizi/utoaji wetu. Tuwe wakatikati na matumizi yetu ya kila
kitu, hii ndio sifa na tabia ya Muislamu.