Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Akhlaaq-Tabia  

"Hakika si vingine nimetumwa kuja kutimiza TABIA NJEMA" Hadith Tukufu

HAYA (SONI)                              Inaendelea...

 

         Hakika haya ni muhimili wa kheri na ni elementi katika kila tendo linalo ichafua, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Uchafu haukuingia katika kitu ila hukitia towa na haikuwa haya katika kitu ila hukipamba kitu hicho”. Tirmidhiy-Allah amrehemu.

Lau haya ingeli jivika kiwiliwili ikawa mtu, basi angeli kuwa (mtu huyo) ni nembo ya wema na utengenevu. Imepokewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimwambia: “Lau haya ingeli kuwa ni mtu, basi angeli kuwa ni mtu mwema. Na lau kuwa uchafu ungekuwa ni mtu, basi angeli kuwa ni mtu muovu/mbaya”. Twabaraaniy-Allah amrehemu.

Na katika jumla ya mtu kuwaonea haya watu, ni kuzijua daraja za wenye haki na kumpa kila mwenye kustahiki heshima, heshima yake. Kwani anao kijana kwa wale walio mzidi umri na anao mwanafunzi kwa waalimu zake, mwenendo unao simama juu ya msingi wa kuwa na adabu na utangulizi. Basi si vema na wala haipendezi yeye (kijana) kuinua sauti yake mbele yao na wala asipige hatua mbele yao (asiwatangulie katika kutembea). Imepokewa katika hadithi: “Nyenyekeeni kwa yule mnaye jifunza kwake”. Twabaraaniy-Allah amrehemu.

Kadhaalika katika hadithi nyingine: “Ewe Mola wa haki! Ninakuomba zisinidiriki zama ambazo humo hafuatwi anaye jua na wala hastahiwi humo mtu mpole”. Ahmad-Allah amrehemu.

Na haya si uwoga, kwani mtu mwenye haya mara nyingine huweza kuona bora kumwaga damu yake kuliko kumwaga maji ya uso wake (machozi). Na huo ndio ushujaa katika taswira yake ya juu kabisa. Na pengine ikiwepo katika haya sehemu/kitu katika khofu, pamoja na kwamba hiyo inaweza ikawa ni khofu ya mtu bora kuchelea tabia zake njema na sifa zake bora, kuondoshwa/kupotezwa na mazingira hatarishi. Na khofu/uchelea wa aina hiyo ni mkabala wa ujasiri katika sehemu zake unamotakiwa na kusifiwa.

Pale zamani Mayahudi walipo rudi nyuma wasiende kupigana na wale walio takabari katika ardhi takatifu: “WATU WAWILI MIONGONI MWA WACHAMNGU AMBAO ALLAH AMEWANEEMESHA, WALISEMA: WAINGILIENI KWA MLANGONI. MTAKAPO WAINGILIA BASI KWA YAKINI NYINYI MTASHINDA...”. [05:23] Basi hawa ambao wanao mcha Mungu na wanaogopa aibu/fedheha na wanaona haya kutimua mbio, hao ndio ambao lau vita vitatokea, wangeli ongoza hujuma dhidi ya adui na kuukurubisha ushindi.

Na wala hapana shaka kwamba haya iliyo kamilika, hutanguliwa na maandalizi maumbile yaliyo tayari. Kwani ziko tabia nyingi ambazo ufedhuli/usafihi unakurubia kuwa ni sehemu yake iliyo lazimiana nazo. Katika wakati ambapo unamuona mtu fulani ni mwingi wa soni, dhaifu wa hisia kwa kiwango kikubwa. Lakini hizo soni, pamoja na ukweli kwamba ni elementi inayo jitokeza kupitia haya, inapatikana katika kheri (wema) na shari (uovu). Na pengine inaweza kumtumbukiza mdau wake kwenye mashaka/shida na hali ngumu. Ama haya, basi haiwi ila ndani ya wigo wa mipaka ya sheria, kwa mantiki hiyo basi yule anaye ogopa kuwakosoa na kuwakemea wafanyao ya batili, huyo hazingatiwi kuwa ni mtu mwenye haya. Kwani hakika haya ya kweli, haiwi kwenye upande wa batili na wala haina nafasi kwa watu pindi wanapo potea. Na wala haina nafasi katika nyenendo pale anapo kuwa mtu mahala akiinusuru haki hapo. Washirikina walipata kuukosoa Uislamu eti ya kwamba umeyadharau masanamu na ukayafedhehesha kwa kushindwa kwake hata kuumba nzi, tena si tu huko kuumba nzi bali hata kushindwa kujihami pale yanapo shambuliwa na nzi. Wakasema: Hakika hali ilivyo si sehemu ya haya kushambuliwa miungu yao kwa mtindo huo. Hapo ndipo ikashuka kauli yake Allah Ataadhamiaye: “HAKIKA ALLAH HAONI HAYA KUTOA MFANO WA MBU NA ULIO WA ZAIDI YAKE. AMA WALE WALIO AMINI HUJUA YA KWAMBA HIYO NI HAKI ILIYO TOKA KWA MOLA WAO  MLEZI, LAKINI WALE WALIO KUFURU HUSEMA: NI NINI ANALO KUSUDIA ALLAH KWA MFANO HUU?...” [02:26]

Kwa hivyo basi, kudhihiri kwa masanamu katika sura hii ya ajizi (ushindwa) na uduni ni haki: “...LAKINI ALLAH HASTAHI KWA JAMBO LA HAKI...”. [33:53]

Na katika njia ya kuthibitisha haki, muislamu hamuogopi yeyote na wala hachelei ubaya. Na haya katika daraja zake za juu na tukufu kabisa, inakuwa kwa Allah Ataadhamiaye, kwa hivyo sisi basi, tunakula katika kheri zake na tunapumua katika anga lake na tunatembea kwenye ardhi yake na tunafunikwa na mbingu yake. Na mtu kwa mkabala wa neema (wema) ndogo anaona haya kumtendea ubaya aliye mneemesha neema hiyo. Basi iweje watu wasione haya kumtenda ubaya Mola Muumba wao ambaye zinawafunika neema zake tangu utotoni mpaka mwanandanini na kwenye maisha baada ya hapo ya milele?!

Hakika haki za Allah kwa waja wake ni kubwa mno, lau waja wangeli zipa haki yake stahiki, basi wangeli ziendea haraka kheri kuzitenda kwa utashi wao. Na wangeli kaa mbali na maasi kwa kuona haya kwa kuzikabili kheri tupu kwa upingaji na uduni. Imepokewa kutoka kwa Ibn Masoud-Allah amuwiye radhi: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Muoneeni haya Allah haki ya haya, tukasema: Ewe Mtume wa Allah! Hakika sisi tunamuonea haya Allah – tunamshukuru Allah (kwa hilo) – (Mtume) akasema: Huko siko kumuonea haya Allah, haki ya haya ni kuhifadhi kichwa na kilivyo navyo, tumbo na lililo vibeba na ukumbuke kufa na kuchakafuka. Na aitakaye Akhera, huacha pambo (starehe) la maisha ya Dunia na akaifadhilisha Akhera kuliko Dunia. Atakaye yafanya hayo, hakika huyo ndiye amemuonea Allah haya haki ya haya”. Tirmidhiy-Allah amrehemu.

Mawaidha haya – ambayo inasemekana ni ya Ibn Masoud – yamekusanya nyingi miongoni mwa adabu za Uislamu na njia za maadili. Kwani ni wajibu wa muislamu kuuepusha ulimi wake kuingia kwenye batili, na ayazuie macho yake kuona tupu au kutazama matamanio. Na sikio lake aliepushe kuiba siri au kufichua ubaya. Na ni juu yake kuliachisha haramu tumbo lake na alikinaishe na kilicho kizuri (cha halali) kipatikanacho. Kisha tena ajilazimishe kuutumia wakati wake katika yanayo mridhi Allah na kuzifadhilisha thawabu zilizoko kwake. Basi zisimdunishe starehe zihadaizo za Dunia, akiyafanya hayo kwa hisia kwamba Allah anamuona na kwa kukimbia kuchupa mipaka upande wa Allah, bila ya shaka huyo atakuwa amemuonea haya haki ya haya.

Hakika kutetemeka kwa mtu na kubadilika kwa rangi ya uso wake katika baadhi ya hali, ni dalili ya utukufu ulio jificha na tabia njema, na “haya ndio kheri yote”. Ama pale itakapo ondoka rangi na pako la haya usoni mwa mtu, kama linavyo dondoka gamba/gome bichi la mti mbichi. Hapo huwa haya imetoa rukhsa ya kuondoka kwa maadili mema na mtu huyo ndiye aambiwaye: “Usipo stahi (usipo kuwa na haya), basi tenda utakalo”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Na haya kwa mjumuisho huu, ndio dini yote, inapo wekwa kwenye kundi la amali njema, basi hiyo ni sehemu ya imani na ni athari yake. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Imani ina mafungu sabini na kadhaa, bora lake (mafungu hayo) ni kauli ya ‘Laa Ilaaha Illal-laah’ na la chini yake ni kuondosha udhia njiani. Na haya ni sehemu ya imani”. Muslim-Allah amrehemu.

Hakika mwanaadamu mbele ya watu anao waheshimu, huwania kuwaridhi na hudhibiti mwenendo wake kikamilifu. Kwa sababu hiyo basi, huzungumza kwa heshima na huwa na hadhari katika matendo yake. Na kwa muktadha huo basi, muislamu anaye jua kupitia mafundisho ya dini yake ya kwamba katu yeye haghibu (hatoweki) kwenye uoni wa Allah, kwani Yeye yu pamoja naye katika hali zake zote, mchana na usiku. Kunampasa khofu yake kwa Allah iwe ni kubwa mno, na kuwa na adabu na sheria zake kwa ukamilifu mkubwa.



 | Tuandikie |