Uislamu
unamtaka muislamu ajithamini mwenywe kabla ya kudai kuthaminiwa na jamii.
Yeye mwenyewe aseme kauli au atende matendo yatakayompa thamani na daraja
mbele ya Mola Muumba wake, Mtume wa Allah, waumini wenziwe na jamii ya
wanadamu kwa ujumla. Tusome: “…….NA UTUKUFU HASA NI WA ALLAH NA
MTUME WAKE NA WA WAUMINI LAKINI WANAFIKI HAWAJUI”. (63:8)
Utukufu
wa nafsi/kujithamini sambamba na kujithaminisha ni mali na pambo la
muumini. Kwa sababu hii ndiyo sifa inayomfanya mtu azikwae ngazi kuufikia
utukufu, daraja na heshima. Chanzo kikuu cha sifa hii ni mtu kujijua
kwanza yeye mwenywe ni nini atende au asitende nini na kwa nini, sambamba
na kuijua nafsi yake mbele ya Mola wake na mbele ya viumbe wenzake. Mtu
akiyatambua yote hayo, itampelekea na kumuongoza kujiheshimu yeye mwenyewe
ili jamii imuheshimu pia. Atajichunga katika kauli, matendo, uvaaji,
utembeaji na namna zake nyingine za kuchanganyika na jamii. Ikumbuke kuwa
utakavyojitokeza kwa jamii ndivyo jamii itakavyokupokea. Turejee na
tupekue kurasa za historia, tutamkuta Mtume wa Mwenyezi Mungu-Rehema na
Amani zimshuke- anajitokeza kwa jamii yake katika sura ya ukweli na
uaminifu na jamii nayo inampokea na kumkubali kuwa ni Mkweli Muaminifu.
Mtu
akijipamba na sifa hii ni lazima tu atajulikana kupitia kauli/matendo yake
ya kila siku na hayo ndiyo tunayoyaita matunda ya utukufu wa
nafsi/kujithamini. Miongozi mwa matunda mapevu na matamu ya mti huu ni:-
1.
Kujipamba na tabia njema.
Mtu
akijithamini ni lazima atakuwa na tabia njema. Tabia njema ndiyo sifa kuu
aliyokuwa nayo Bwana Mtume-Rehema
na Amani zimshukie, Mola wake anamsifia: “NA BILA SHAKA WEWE UNA
TABIA NJEMA KABISA” (68:4).
Kadhalika
tabia njema ndiyo ilikuwa sababu ya mafanikio aliyoyapata Mtume wa
Mwenyezi Mungu na kufanikiwa kufanya mapinduzi yaliyobadilisha hali na
itikadi za watu kwa muda mfupi tu. Mola wake anamkumbusha juu ya hili,
anamwambia “BASI KWA SABABU YA
REHEMA ITOKAYO KWA ALLAH UMEKUWA LAINI KWAO (Ewe Muhammad) NA KAMA
UNGEKUWA MKALI NA MWENYE MOYO MGUMU BILA SHAKA WANGALIKUKIMBIA…….”
(3:159).
2.
Kusubiri juu ya matatizo na majanga mbalimbali .
Mtu
mwenye kujithamini utu wake anapofikwa na matatizo mbalimbali ya kimaisha
kama maradhi, dhiki ya maisha, misiba hapapatiki wala kubabaika. Hii ni
kwa sababu anaelewa fika na kuamini kuwa yote yamfikayo ni mtihani kutoka
kwa mola wake. Kwa hiyo husubiri na kutafuta ufumbuzi kutoka kwa Mola
Mwenyezi. Kuhusiana na tabia hii ya mwanadamu kupapatika anapofikwa na
matatizo, Qur-ani inasema “ KWA HAKIKA BINADAMU AMEUMBWA HALI YA KUWA
MWENYE PAPATIKO, INAPOMGUSA SHARI HUWA MWENYE FAZAA” (70: 19-20).
Muumini
hauvunji utu wake anaposibiwa na matatizo na shida kadha wa kadha kwa
kuwaendea waganga na watabiri. Kujithamini humzuilia kabisa na hilo na
husema: “……NAMI NINAMKABIDHI (namwachia) ALLAH MAMBO YANGU: HAKIKA
ALLAH ANAWAONA WAJA (wake wote) “ (40: 44.)
3.
Huwa haonyeshi uhitaji wake.
Muumini
huitukuza nafsi yake kwa kutokuudhihirisha uhitaji wake kwa watu. Si tabia
ya muislamu kupita huku na kule akimueleza kila mtu shida na matatizo
yake. Bali shida zake hubakia kuwa ni siri
isiyofichuliwa ila kwa watu maalum wanaomuhusu tu, halalami kwa
kila mtu. Qur-ani inawataja watu hawa: “….ASIYEWAJUA HALI ZAO
ANAWADHANI KUWA NI MATAJIRI KWA SABABU YA KUJIZUIA KWAO (na kuomba)
UTAWAFAHAMU (kuwa wahitaji) KWA ALAMA ZAO (zinazoonyesha ufakiri, lakini)
HAWAOMBI WATU WAKAFANYA UNG’ANG’ANIZI………” (2:273).
4.
Watu humuheshimu.
Mtu
akijithamini yeye mwenyewe bila shaka atawathamini na wenziwe na hivyo
kuziba kabisa mianya ya kuvunjiwa heshima na kufanyiwa utovu wa adabu.
Hili linatokana na ukweli kwamba ni maumbile ya mwanadamu kutenda kama
anavyotendewa. Ukimtukana nae atajibu, ukimdharau nae atakudharau,
ukimpenda nae atakupenda, ukimuheshimu nae
atakuheshimu. Hayo ni sehemu ya umbile aliloumbiwa mwanadamu.
Inatakikana
kwa muumini mwenye akili
na kujithamini asijiingize katika kusema na kutenda kila ambalo
litakuwa ni sababu ya kudharauliwa na kuvunjiwa heshima. Bwana Mtume –
Rehema na Amani zimshukie – anatuambia: “ Haitakikani kwa muumini
kujidhalilisha. (Maswahaba) wakamuuliza: vipi atajidhalilisha? Akawajibu:
“kwa kujiingiza kwenye mabalaa asiyoyaweza”.