Hii
pia ni miongoni mwa tabia njema ambazo muislamu anapaswa kujijpamba nazo
kuhusiana na hili tunasoma: NA UMPE JAMAA (YAKO) HAKI YAKE NA MASIKINI NA
MSAFIRI ALIYEHARIBIKIWA, WALA USITAWANYE (mali yako) KWA UBADHIRIFU.”
[17 : 26]
Tuzidi
kusoma kwa kutafakari: “WALA USIFANYE MKONO WAKO (kama) ULIOFUNGWA
SHINGONI MWAKO, WALA USIUKUNJUE OVYO OVYO, UTAKUWA NI MWENYE KULAUMIWA (ukifanya
hivyo) NA KUFILISIKA (ukiukunjua ovyo ovyo). “[17:29]
Kwa
mujibu wa aya muislamu si mtu mbadhirifu na pia si bakhili. Aya hizi ndizo
zinazoibeba sera nzima ya mali na namna ya kuitumia katika uislamu.
Muislamu anaamini kuwa Allah ndiye muumba wake na ndiye aliyemuumbia
ulimwengu na vyote vilivyomo ndani yake ikiwa ni pamoja na mali: “YEYE
NDIYE ALIYEKUUMBIENI VYOTE VILIVYOMO KATIKA ARDHI (kabla hajakuumbeni ili
mkute kila kitu tayari) - - -.” [2 : 29]
Na
akamfanyia mali kuwa ni pambo la maisha yake hapa duniani: “MALI NA
WATOTO NI PAMBO LA MAISHA YA DUNIA ---.” [18 : 46] Hii ndio sababu
tunaona kuwa ni tabia bali ni maumbile ya mwanadamu kuipenda mali: “NA
MNAPENDA MALI PENDO LA KUPITA KIASI.” [89 : 20]
“WATU
WAMETIWA HUBA YA KUPENDA WANAWAKE NA WATOTO NA
MIRUNDI YA DHAHABU NA FEDHA NA FARASI WANAOTUNZWA VIZURI NA WANYAMA
NA MASHAMBA NA HAYO NI MATUMIZI YA MAISHA YA DUNIA NA KWA ALLAH NDIKO KWENYE
MAREJEO MAZURI (3:14) kwa kuwa tayari Qur-ani tukufu imeshatuthibishia
kwamba ni sehemu ya maumbile ya mwanadamu kupenda mali, ndipo tunamuona
huyu mwanadamu akiitafuta na kujilimbikizia mali kwa hila, mbinu na juhudi
za upeo wake. Anachokijua yeye ni kupata mali na kuitumia bila ya kujali
anaipataje na anaitumiaje. Muislamu hawi hivi kwa sababu anatambua
“KISHA KWA HAKIKA MTAULIZWA SIKU HIYO JUU YA NEEMA (mlizopewa
mlizitumiaje)” (102:8) Muislamu anaitakidi kwamba mali kwa dhati yake
yenyewe kama mali haina thamani wala ubora bali thamani na ubora wake
unajidhihirisha katika matumizi yake. Ni matumizi haya ndio huzaa manufaa,
faida na kumletea ustawi na maslahi mwanadamu. Manufaa na faida hizi ndizo
humpelekea mtu kuipenda mali na kuhangaika kuitafuta kwa udi na uvumba.
Uislamu
haumkatazi muislamu kuitafuta na kuimiliki mali bali
unachokiangalia na kukisisitiza ni namna ya kuchuma na jinsi ya
kuitumia: “NA UTAFUTE KWA YAKE (mali) ALIYOKUPA ALLAH MAKAZI MAZURI YA
AKHERA, WALA USISAHAU SEHEMU (fungu) YAKO YA DUNIA NA UFANYE WEMA KAMA
ALLAH ALIVYOKUFANYIA, WALA USITAFUTE KUFANYA UFISADI KATIKA NCHI, BILA
SHAKA ALLAH HAWAPENDI MAFISADI” (28:77).
Kupitia
aya hii hatutashindwa kuona kuwa mali imekusudiwa imnufaishe mwanadamu
katika maisha haya ya ulimwengu huu, ale, anywe, avae na alale, mahala
pazuri bila ya kufanya ubadhilifu”……NA KULENI (Vizuri) NA KUNYWENI (vizuri)
LAKINI MSIPITE KIASI TU. HAKIKA YEYE (Allahl) HAWAPENDI WAPITAO KIASI
(7:31).
Kadhalika
aitumie mali kwa kuyanunua maisha ya milele ya akhera kwa kuitumia katika
njia za kheri zitakazomuhakikishia manufaa kwanza yeye mwenyewe binafsi na
jamii nzima ya wanadamu. Aitumie namna hii ya mali aliyoneemeshwa na
kuchaguliwa kupewa na Mola na sio kwa uhodari wake, juhudi wala elimu yake
kwa kukidhi haja zake binafsi za kimaisha, familia yake khasa na jamii kwa
ujumla. Aitumie kuwasaidia ndugu, jamaa, marafiki, majirani, wagonjwa na
wasiojiweza bila ya kuwasahau mayatima. Awape
huku akiamini kuwa ni haki yao kutoka kwa Mola wao na sio ihsani na
msaada kutoka kwake ambao atautoa akitaka na kumpa amtakaye yeye:
“……NA WAPENI KATIKA MALI YA ALLAH ALIYOKUPENI………” (24:33).
Hii ndio nadharia (dhana) ya mali katika Uislamu, ni sehemu ya imani ya muislamu
kuamini kwamba kila kilichomo mikononi mwake ikiwa ni pamja na yeye
mwenyewe ni miliki yha Allah: (vyote) VILIVYOMO MBINGUNI NA VILIVYOMO
ARDHINI NI VYA ALLAH……(2:284) Mwanadamu atakapoitumia mali yake katika
mambo ya kheri na akaisaidia jamii, basi bila ya shaka atakuwa ni kipenzi
cha jamii hiyo kwani ni maumbile ya mwanadamu kumpenda muhisani wake na
kumchukia bakhili. Ziada ya hayo atapendwa na Mola wake, Mwenye mali yake:
“…….NA ALLAH ANAWAPENDA WAFANYAO WEMA / IHSANI (3: 134).
Uislamu
haukumkataza muislamu kutafuta na
kumiliki mali lakini pia haukumruhusu kuwa mbadhirifu:”……..WALA
USITAWANYE (mali yako) KWA UBADHILIFU. HAKIKA WATUMIAO KWA UBADHILIFU NI
NDUGU WA MASHETANI (wanamfuata shetani)…….” (17:26-27) wala
haukumuhalalisha ubakhili:”……BILA SHAKA ALLAH HAWAPENDI WENYE KIBURI
WAJIVUNAO AMBAO HUFANYA UBAKHILI (wao) NA HUWAAMURU WATU (wengine) NA
WANAYAFICHA ALIYOWAPA ALLAH KWA FADHILA ZAKE………” (4:36-37).
Zidi
kuona ubakhili usivyokuwa na nafasi katika
mfumo sahihi wa maisha unaowafaa wanadamu wa rangi, lugha na zama zote:
“NA AFANYAJE UBAKHILI, ASIWE NA HAJA NA VIUMBE WENZAKE. NA AKAKABIDHISHA
MAMBO MEMA (asifanye) TUTAMSAHILISHIA
NJIA YA KUENDEA MOTONI. NA MALI YAKE HAYATAMFAA ATAKAPOKUWA
ANADIDIMIA (motoni humo).” (92:8-11) Mtu anapojifanyia ubakhili yeye
mwenyewe, akajidai na kujidhiki na il-hali ameneemeshwa na Mola wake kwa
neema ya mali. Tena akaizuia na akaacha kuitumia katika njia za kheri kwa
manufaa yake na ya jamii yake. Kazi yake ikawa ni kuchuma na kulimbikiza
tu, huyu ni mtu mbaya achukiwaye machoni mwa jamii, asiyependeza mbele yao
bali mbele ya mwenye mali yake (Allah) Huyu hana njia ya kuikwepa adhabu
ya Allah iliyotajwa ndani ya aya hii: (…..NA WALE WAKUSANYAO DHAHABU NA
FEDHA WALA HAWAZITOI KATIKA NJIA YA ALLAH, WAPE HABARI ZA ADHABU
INAYOUMIZA. (inayowangoja). SIKU (mali yao) YATAKAPOTIWA MOTO KATIKA MOTO
WA JAHANAMU, NA KWA HAYO
VINACHOMWA VIPAJI VYA NYUSO ZAO NA MBAVU ZAO NA MIGONGO YAO, (na huku
wanaambiwa) HAYA NDIYO (yale mali) MLIOJILIMBIKIZIA (mliojikusanyia)
NAFSI ZENU, BASI ONJENI (adhabu ya) YALE MLIYOKUWA MIKIKUSANYA (9:34-35).
Kadhalika mtu akiikanusha na kuifukuza neema ya mali aliyopewa na Mola
Muumba wake, tena bila ya kujaza fomu ya maombi kwa kufanya
ubadhilifu, ufisadi katika ardhi na kuwadhuru wenziwe. Huyu pia
adhabu kali inamngojea kwa mbele ya Allah: (NA
(kumbukeni) ALIPOTANGAZA MOLA WENU (kuwa): “KAMA MKISHUKURU,
NITAKUZIDISHIENI, NA KAMA MKIKUFURU (jueni) KUWA ADHABU YANGU NI KALI SANA
( 14:7). Ni vema tukatambua na kuelewa kwamba Allah alipomuumba mwanadamu
na akamuumbia mali za ardhini na baharini na kamjaza huba ya mali.
Hakumuacha hivi hivi tu, achume mali kwa namna aitakayo, aibe,
anyang’anye, adhulumu, ale rushwa ili mradi tu apate mali na kuipiga
teke dhiki. Akishaipata
aitumie atakavyo, alewe, azini, awakandamize wanyonge na……….na…….
Ikiwa yuko anayeitakidi hivyo basi ajue anajidanganya mwenyewe. Iwapo
Mjapani mwanadamu mwenzetu, anatugengeneza gari na kutuwekea
muongozo wa kulitumia na tukienda kinyume na muongozo huo, bila
shaka litaharibika na halitofanya kazi kama lilivyokusudiwa na
mtengenezaji. Sasa ni vipi basi, Allah amuumbe mwanadamu, ampe na mali,
kisha akamuacha hivi hivi bila ya kumpa muongozo wa namna uya kuichuma na
kuitumia. Hili ni muhali kwa Allah kwa sababu linampa sifa ya upungufu.
Rejea muongozo wa namna ya kuitumia mali katika aya zilizofungua somo letu
hili.