Muislamu
halioni suala la kumtegema Allah katika mambo yake kulli {yote} kama ni
wajibu wa kimaumbile tu, bali anaona na kuamini kuwa ni fardhi ya dini na
itikadi isiyopambanuka ya Uislamu. Itikadi hii inatokana na agizo la Mola
wake Mtukufu: “… NA MTEGEMEENI ALLAH IKIWA NYINYI NI WAUMINI.”
[5:23]
“…
NA WAUMINI WAMTEGEMEE ALLAH TU.” [64:13] Amri na maagizo haya
yaliyosheheni ndani ya Qurani Tukufu ndiyo yanayokufanya kumtegemea
Mwenyezi Mungu mtukufu kuwe ni sehemu ya itikadi ya muislamu. Kwa maneno
mengine tunaweza kusema kuwa muislamu anapoyategemeza kusema kuwa muislamu
anapoyategemeza mambo yake yote kwa Allah, huwa yumo katika kuifuta dini
ya Mola wake na huwa na fungu la ajira mbele ya Allah. Wala kumtegemea
Allah si kama wanavyofahamu majahili wa uislamu kuwa ni kusema tu kwa
ulimi bila ya kujishughulisha na sababu {vyanzo} vya matakwa ya mja. Sivyo
kabisa, kumtegema Allah si, kuacha kufanya kazi na ukaomba, kuridhia
umasikini na kuishi maisha duni chini ya hisia za kumtegemea Allah. Bali
muislamu anafahamu kwa yakini kuwa kumtegemea Allah ambako ni sehemu ya
Imani na itikadi yake, ni kumtii Allah kwa kufanya sababu zote husika ili
kufikia matakwa/mahitaji yake fulani kama ni suala la riziki, basi hufanya
kazi kwa juihudi na maarifa huku akiamini kuwa kazi aifanyayo ni sababu tu
na mruzukaji wa kweli ni Allah pekee “KWA YAKINI ALLAH NDIYE MTOAJI WA
RIZIKI, MWENYE NGUVU, MADHUBUTI.” [51:58]
Ikiwa
ni suala la elimu, basi huitafuta kwa bidii huku akiitakidi kuwa ni elimu
ni wajibu wa kidini, elimu ni mali ya Allah ampayo mwanadamu:
“AMEMFUNDISHA MWANADAMU (Chungu ya) MAMBO ALIYOKUWA HAYAJUI.” [96:5]
Kama ni
ugonjwa, basi hutumia dawa kwa itikadi kuywa dawa ni sababu tu ya kupona,
bali mponyaji wa kweli hata bila ya kupona, bali mponyaji wa kweli hata
bila dawa ni Allah pekee: “NA NINAPOUGUA, YEYE NDIYE ANAYENIPONESHA.”
[26:80]
Hii
ndio dhana ya kumtegemea Allah katika uislamu, muislamu wa kweli hategemei
kuvuna bila ya kupanda wala haamini kuwa kupanda ndio kuvuna, bali kupanda
ni sababu tu ya mavuno apendapo Allah kwani yeye pekee ndiye muweza wa
kila kitu kwa sababu unaweza kupanda na usivune: … NA ALLAH NI MWENYE
UWEZA JUU YA KILA KITU.” [2:284]
Kauli
jumla, kumtegemea Allah kwa muislamu hakumaanishi zaidi ya kufanya kazi,
kutumai, kutuliza moyo na kuitakidi kwa kukata kuwa alitakalo Allah ndilo
huwa na asilolitaka kamwe hilo haliwi hata kama watu wote wangelitaka, na
kwamba Allah hamrejeshi patupu mwenye kumtegema kupitia sababu za kimaisha
kwani kila kitu kina sababu: “YEYE NDIYE ALIYEFANYA ARDHI IWE INAWEZA
KUTUMIKA (Kwa kila myatakayo) KWA AJILI YENU. BASI NENDENI KATIKA PANDE
ZAKE ZOTE NA KULENI KATIKA RIZIKI ZAKE, NA KWAKE YEYE NDIO MAREJEO (yenu
nyote).” [67:15]
Muislamu
anaamini utaratibu {suna} ya Allah katika ulimwengu ambayo ni kazi
{juhudi} + kumtegemea Allah = matunda. Kutokana na imani yake hii,
muislamu hufanya kazi na kila linalohitajika kwa juhudi na ukamilifu ili
kuyafikia malengo yake ya kimaisha. Haitakidi hata kidogo kwamba kazi hizo
anazozifanya pekee ndizo zinamdhaminia kukamilisha malengo yake na
kumpatia mafanikio. Bali huona kule kufanya sababu [kazi] ni amri na
utaratibu wa Mola wake ambao hana budi kuutii kama anavyomtii katika mambo
mengine anayomuamrisha kutenda au kumkataza kutenda. Ama suala la kupata
matokeo/natija ya kazi aifanyayo na kufuzu katika matakwa yake, hili
analitegemeza kwa Allah, kwani yeye tu ndiye muweza wa hilo. Wangapi
wamefanya kazi ngumu za suluba na hawakupata! Hatuwaoni wakulima,
waliolima, wakapanda na bado hawakuvuna! Kutokana na hili, mtazamo wa
muislamu katika sababu za kimaisha [kazi] ni kwamba kuzitegemea sababu
pekee na kuziona kuwa ndio kila kitu katika kupata mahitaji ya mwanadamu
ni ukafiri. Na kwa upande mwingine mtu kuacha kufanya kazi na ilhali anao
uwezo wa kufanya kazi, haya ni maasi.
Hii
ndio dhana sahihi ya kumtegemea Allah kuivaa sifa hii. Mtume wa Allah
Rehema na Amani zimshukie anatuambia: “Lau nyinyi mtamtegemea Allah kama
ipasa kumtegemea, basi ningeruzikiwa kama anavyoruzukiwa ndege, hudamka
asubuhi akiwa na njaa na hurejea jioni akiwa ameshiba.” Tirmidhiy