|
i/. SUBIRA NA KUSTAHAMILI MAUDHI.
Miongoni mwa tabia nzuri na njema ambazo muislamu
hujipamba nazo ni kuwa na subira na kustahamili maudhi. Tusite hapa na
tujiulize kabla hatujaendelea, subira ni nini? Kwa ibara nyepesi yenye
kufahamika haraka tunaweza kuiarifisha subira kuwa ni hali ya mtu kuizuia
nfsi yake dhidi ya ayachukiayo. Tuliweke wazi ainisho na arifisho hili,
muislamu mathalan huizuia nafsi yake dhidi ya iyachukiayo. Inaeleweka wazi
kwamba nafsi inachukia na haipendi ibada na mambo ya twaa na badala yake
humvutia mtu kwenye maasi, uonvu na uchafu kwani ndio maumbile yake: “--- KWA
HAKIKA (kila) NAFSI NI YENYE KUAMRISHA SANA MAOVU ISIPOKUWA ILE AMBAYO MOLA
WANGU AMEIREHEMU ---“ [12:53]
Muislamu huilazimisha na kuondosha nafsi katika maumbile
yake haya ya kupenda maovu na kuipeleka katika twaa, haipi kabisa nafasi ya
kuyakurubia maasi ambayo hujidhihirisha katika sura nzuri yenye kuvutia na
ladha tamu yenye kutamanisha na kutia uchu. Kadhalika huizuia kupapatika
inapofikwa na balaa na majanga mbalimbali. Silaha pekee anayoitumia muislamu
katika vita vyake hivi vigumu ni SUBIRA inayomuwezesha kusubiria ladha ya
maasi na kumeza shubiri ya njema aitoayo Mola wake ikiwa ni mkabala wa twaa
wazitendazo waja wake. Kamio la Allah la ahabu kali itakayowafika watendao
maasi pia hutoa mchango mkubwa kwa muislamu katika vita yake hii dhidi ya
nafsi yake. Muislamu anakumbuka kwamba daima qadari ya Allah ni yenye kupita;
haipingwi na wala hina kuzizi, hukumu yake ni ya uadilifu; isiyo na dhulma
wala upendeleo kwa ye yote. Mwanadamu akisubiri au akipapatika itapita tu,
kwa hivyo ni vema asubiri ili apate ujira mkubwa kwani kupapatika kwake
hakutamaanisha kingine zaidi ya kupata dhambi na hukumu ya Allhah kubakia
pale pale.
Subira na kutokupapatika wakati wa majanga
mbalimbali ni miongoni mwa tabia ambazo ni zao la mazoezi na mapambano ya
muda mrefu yaendeleayo muda wa maisha ya mtu. Muislamu humuomba Mola wake
amruzuku subira akiamini kuwa anaitekeleza amri ya Mola wake isemayo: “ENYI
MLIOAMINI! SUBIRINI NA MUWASHINDE MAKAFIRI (katika kusubiri) NA KUWENI. IMARA
(nyoyo zenu) NA MCHENI ALLAH ILI MPATE KUFAULU.” [3 : 200]
Aya inabainisha kwamba subira ni sifa ya waumini
hawi na subira ni alama ya kufaulu. Pia anaitekeleza amri isemayo: “ENYI
MLIDAMINI! JISAIDIENI (katika mambo yenu) KWA SUBIRA NA SWALA; BILA YA SHAKA
ALLAH YU PAMOJA NA WANAOSUBIRI.” [2 : 153]
Hapa pia inatubainikia kwamba subira na swala vina
mchango na msaada mkubwa katika kuyafanikisha mambo yetu mbalimbali katika
harakati za maisha yetu ya kila siku.
Wenye subira wako pamoja na Mola wao aliyewataka kuwa na subira nao wakamtii
wakasubiri, kwa ajili hiyo akawaahidi msaada wake katika shughuli na mambo
yao yote. Katika kusubiri kwake, muislamu huitia matendoni amri ya Mola wake:
“NA SUBIRI, NA KUSUBIRI KWAKO KUSIWE ILA KWA AJILI YA ALLAH TU ---.” [16 :
127]
Tunafahamikiwa kutokana na aya hii kwamba ili
subira itoe matunda mema ni lazima muislamu ahakikishe kwamba subira yake ni
kwa ajili tu ya kutarajia kupata radhi na ujira wa Allah tu na si vinginevyo:
“--- NA KWA YAKINI SISI TUTAWAPA WALIOSUBRI UJIRA WAO (Mkubwa kabisa) KWA
YALE MAZURI WALIYOKUWA WAKIYATENDA.” [16 : 97]
Hebu ione thamani na kima cha subira kupitia kauli
hii tukufu ya mtukufu Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie isemayo: “Na
atakyejizuia na machafu, Allah atamuwezesha kujizuia nayo, na
atakayejikwasia na kuomba (watu),
Allah atampa ukwasi, na atakayesubiri, Allah atamsubirisha. Na hajapewapo ye
yote kipawa kilicho bora na kikunjufu kuliko subira.” Bukhaariy
Hii ndio subira tunayoikusudia au ikusudiwayo na
uislamu. Ama kustahamili maudhi pia ni sehemu ya subira iliyo ngumu zaidi kwa
wanadamu wengi. Kustahamili maudhi ndio bidhaa ya masadiki na ndio nembo ya
watu wema. Ukitaka kuwajua na kuwafahamu watu wema, basi zitizame hali zao
wanapoudhiwa, utaona ni namna gani wanavyoziangusha mweleka nafsi zao katika
kukabiliana na maudhi watendewayo. Kustahamili maudhi hudhihiri pale muislamu
anapoudhiwa na kubughudhiwa kwa ajili ya Allah, hapo akaonysha subria na
uvumilivu wake. Mfano mzuri wa kupigwa na kuigwa katika hili ni mtume wa
Allah Rehema na Amani zimshukie. Namna makurayshi walivyomfanyia maudhi
yasiyohimilika kwa ajili ya kuwafikishia ujumbe wa Allah. Malaika wanatumwa
na Allah kuja kutoa msaada, wanamtaka idhini Bwana mtume ya kuwaangamizia
mbali watu wabaya wale. Ndugu yangu muislamu unafikiri mtume wako alifanya
nini. Anamuelekea Mola wake na kumuomba awasamehe waja wake badala ya
kuwaombea na kuwaidhinishia adhabu na maangamivu. Hapo ndipo malaika Mkuu
jibril Amani ya allah imshukie anampa Mtume wa Allah shahada na tuzo ya juu
ya uvumilivu anamwambia: “Amesema kweli aliyekuita MPOLE MWENYE HURUMA.”
Katika kustahamili maudhi, muislamu haulipi ubaya
aliotendewa kwa ubaya bali hulipa uovu kwa wema ikiwa ni kulitekeleza agizo
la Mola wake: “ONDOSHA MABAYA (unayofanyiwa) KWA (kulipa) MEMA ---.” [23 :
96]
Na lile lisemalo: “MAMBO MAZURI NA MABAYA HAYAWI
SAWA ONDOSHA (Ubaya unaofanyiwa kwa mema); TAHAMAKI YULE AMBAYE BAINA YAKO NA
YAKE KUNA UADUI ATAKUJA KAMA NI JAMAA (yako) MWENYE KUKUFIA UCHUNGU.”[41 :
34]
Jifunze kustahamili maudhi kupitia tukio hili
lililomtokea Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie siku moja Mtume wa Allah
aliwagawia maswahaba mali iliyopatikana vitani. Mmoja wa mabedui (waliokuwepo
hakuridhika na mgao ule alioupata) akasema: Mgao huu haukukusudiwa dhati ya
Allah {Mtume kafanya upendeleo}. Habari zile zikamfikia Mtume wa Allah,
akageuka na kuwa mwekundu {kutokana na mtambao wa ghadhabu na hasira}. Kisha
akasema: Allah amrehemu ndugu yangu Mussa alifanyiwa maudhi makubwa kuliko
haya na akasubiri {nami nasubiri},” Bukhaariy na Muslim. Huyu hapa Mola wetu
akitusimulia ustahamilivu wa Mitume wake Rehema na Amani ziwashukie kutokana
na maudhi waliyoyapata kutoka kwa watu wao katika kuwafikisha ujumbe wa Mola
wao: “NA TUNA NINI TUSIMTEGEMEE ALLAH, NA HALI AMETUONYESHA NJIA ZETU NA
TUTAYAVUMILIA MNAYOTUUDHI BASI KWA ALLAH TU WATEGEMEE WATEGEMEAO.” [14 : 12]
Nabii Issa mwana wa Mariam Amani na Rehema
iwashukie alikuwa akiwaambia wana wa israil: “Mliambiwa hapo kabala (yangu
katika Taurati) kwamba jino (hung’okwa) kwa jino na pua (hukatwa) kwa pua.
Nami sasa ninakuambieni msikabiliane na shari (ubaya) kwa shari, bali
atakayekupiga shavu lako la kulia wewe mgeuzie shavu la kushoto. Na
atakayekutwalia mtandio wako, wewe mpe na shuka yako.” Imam Ghazaali katika
IHYAAD ULUUMID DIYN.
Kustahamili
maudhi ni mizani inayopima uzito wa imani ya mja. Baadhi ya maswahaba wa
Mtume Allah awawiye radhi walikuwa wakisema: “Tulikuwa hatuihisabu imani ya
mtu kuwa ni imani kama hakuyasubiria maudhi.” Kupita mifano hai hii yenye
kujieleza na kujitafsiri yenyewe ya subira na ustahamilivu wa maudhi,
muislamu anatazamiwa aishi maisha ya subira na ustahamilivu huku akitaraji
radhi na maghufira adhimu kutoka kwa Mola wake. “NA ANAYESUBIRI NA KUSAMEHE
(atalipwa wema wake.) BILA SHAKA HILO NI KATIKA MAMBO MAKUBWA YA KUAZIMIWA
KUFANYWA (na kila muislamu)”. [42:43]
|