|
Tangu zama na
zama kumekuwepo na kelele za wanadamu juu ya kiu yao ya kuitaka kuiona
jamii ya wanadamu ulimwenguni kote ikiishi katika amani na utulivu.
Chimbuko na msingi wa amani na utulivu huu uwe ni uadilifu, uadilifu ambao
utamuaminisha mtu na dhuluma na kumuhakikishia haki zake zote. Ustaarabu
na mifumo mbalimbali ya maisha iliyobuniwa na kufumwa na wanadamu wenyewe
katika nchi zao. Walioibuni mifumo hiyo wamejaribu kuzitekeleza ndoto za
jamii zao katika kuzihakikishia maisha mazuri na hduma bora za kijamii
hiyo imeweza kutimiza ndoto hizo lakini imeshindwa vibaya kabisa
kusimamisha uadilifu utakaoleta amani na utulivu. Kwani ni chini ya
mwavuli wa amani na utulivu ndio mwanadamu anaweza kuiona ladha na tamu ya
maisha mazuri na huduma bora za kijamii. Itoshe kuwa ni ushahidi dhahiri
kwamba mifumo hiyo imeshindwa kuleta uadilifu namna mataifa mbalimbali
yalivyotumbukia katika maafa na majanga kutokana
na uadui, dhuluma na kiburi. Yote haya ni ushahidi usipoingika
kwamba “mifumo binadamu” haiwezi kusimamisha uadilifu duniani.
Uadilifu ambao utakuwa ndio chemchem itakayotoa maji safi na salama {amani
na utulivu}
Historia
imetuthibitishia kwamba hakuna “mfumo” binadamu” wo wote ule, si wa
magharibi wala wa mashariki unaoweza kusimamisha udilifu zaidi ya “Mfumo
sahihi wa maisha ulioweka nguzo madhubuti za uadilifu zinazomuhakikishia
kila mtu haki zake za:-
§
Kuishi, kuabudu, kusema, kushauri, kukosoa
§
Kijamii {kupata elimu, kufanya kazi, kupata mahitaji ya msingi,
kusikilizwa}
§
Usalama wa maisha, mali na hadhi/heshima yake
§
Kuchagua mfumo wa maisha kwa mujibu wa itikadi yake, na kudalika
Ni
kutokana na umuhimu na nafasi hii ya uadilifu katika maisha ya mwanadamu,
ndipo muislamu anauona uadilifu kwa maana yake pana kama ni wajibu ulio
juu ya wajibati zote. Mtazamo na uoni huu wa muislamu unatokana na
amri/agizo la Allah: “KWA HAKIKA ALLAH ANAAMRISHA UADILIFU NA KUFANYA
HISANI, NA KUWAPA JAMAA (na wengineo) NA ANAKATAZA UCHAFU NA UOVU NA
DHULMA ---.” [16:90] Na Allah akatangaza wazi ya kwamba anawapenda watu
waadhilifu, kinyume cha tangazo hili pia chafanya kazi ya kwamba madhalimu
hawana nafasi ya kupendwa.” --- HAKIKA ALLAH ANAWAPENDA WAFANYAO
UADILIFU.” [60:8]
Allah
ameamrisha uadilifu katika kusema na kutenda (hukumu).” --- NA MSEMAPO
(katika shahada na penginepo) SEMENI KWA UADILIFU (insafu) HATA KAMA NI
JAMAA (usimpendelee kwa ajili ya ujamaa ulio baina yenu au kwa ajili ya
mrungura na mambo kama haya) ---.” [6:152]
Huo
ni uadilifu wa maneno (katika kusema) na huu ni uadilifu katika kutenda
(hukumu): HAKIKA ALLAH ANAKUAMRISHENI KUZIRUDISHA AMANA KWA WENYEWE
(wanaozistahiki). NA MNAPOHUKUMU BAINA YA WATU MUHUKUMU KWA UADILIFU
(haki) ---“ [4:58]
Ni
kutokana na agizo na muongozo huu kutoka kwa Mola wake, muongozo ambao
akiufuata utamuhakikishia amani na utulivu. Ndio muislamu anafanya
uadilifu katika kauli na matendo (hukumu) yake. Anautanguliza uadilifu
mbele katika mambo yake sehemu ya tabia yake isiyotengeka nae. Uadilifu
unakuwa ni pambo linalomfanya apendeze na kukubalika na wapenda haki po
pote pale. Kwa uadilifu kutoka katika chuo kikuu cha uadilifu {Uislamu}.
Shahada hii inamfanya kuwa muadilifu asiyeyumbishwa na mapenzi, ujamaa au
rushwa katika kutenda haki. Shahada hii inamlazimisha kumtendea uadilifu
na haki hata yule ambaye ni adui yake mkubwa, inamfanya avitofautishe vitu
viwili hivi, uadui na uadilifu/haki kwa kutarajia kuvuna mapenzi na radhi
ya Mola wake. “ENYI MLIOAMINI! KUWENI WASIMAMIZI (Wa kupitisha haki)
KWA AJILI YA ALLAH, MUWE MKITOA SHAHADA (ushahidi) KWA UADILIFU.
WALA KUCHUKIANA NA WATU KUSIKUPELEKEENI KUTOWAFANYIA UADILIFU (insafu).
FANYENI UADILIFU, HUKO NDIKO KUNAKOMKURUBISHA MTU NA UCHA MUNGU NA MCHENI
ALLAH, HAKIKA ALLAH ANAZO HABARI ZA (yote) MNAYOYATENDA.”[5:8] Tunaweza
kuigawa tabia hii ya uadilifu katika mafungu yafuatayo:-
i/.
Uadilifu kwa Allah:
Huu haumaanishi
kingine zaidi ya kutomshirikisha Allah katika ibada na sifa zake. Kumtii
bila ya kumuasi, atajwe na akumbukwe bila ya kusahauliwa. Ashukuriwe kwa
neema zake zisizodhibitika bilA ya kukufuriwa. Mja akiyatenda haya
atahesabika kuwa ameonyesha uadilifu wake mbele ya Mola Muumba wake.
Uadilifu huu utamvisha vazi la ucha Mungu na kumfanya kipenzi cha Mola
wake.
ii/.
Uadilifu kwa wanadamu:
Huu unamtaka
mwanadamu awe muadilifu kwa wanadamu wenziwe kwa kumpa haki kila
anayeistahiki kwa mujibu wa sheria. Katika kulitekeleza hili asiuweke
mbele ya macho yake ujamaa, urafiki, rushwa, uadui na kadhalika. Huu
unahusisha pia kuwafanyia uadilifu na kuwapa haki wanazozistahiki wake kwa
kila aliye na zaidi ya mke mmoja. Katika hili watoto pia hawaachwi nyuma,
asiwapendelee hawa zaidi kuliko wale.
iii/.
Uadilifu katika itikadi:
Huu unamtaka mtu
asiitakidi ila kweli na haki na ayaone mambo kwa uhakika wake kama
yalivyo. Aithibitishe itikadi yake hiyo kupitia nafsi yake mwenyewe na
ulimwengu unaomzunguka huku akiamini kuwa anaifanyia kazi kauli ya Mola
wake: “TUTAWAONYESHA (ukweli wa) MANENO YETU HAYA KATIKA NCHI ZA MBALI
NA KATIKA NAFSI ZAO WENYEWE MPAKA IWABAINIKIE KWAMBA HAYA NI KWELI ---.”
[41 : 58]
Sura/Picha
ya uadilifu katika uislamu:
Hebu uone
uadilifu unavyofanya kazi katika uislamu. Huyu hapa Mtume wa Allah Rehema
na Amani zimshukie anatupigia mfano usio na mfano katika kutekeleza
kimatendo misingi ya uadilifu na usawa katia uislamu. Anatekeleza uadilifu
katika haki bila ya ubaguzi wala upendeleo baina ya mwenye nguvu na
mnyonge, baina ya mkubwa na mdogo wala baina ya mtukufu na aliye duni.
Anawaangalia wote hawa kwa jicho la usawa mbele ya sheria. Hampendelii
tajiri kwa sababu ya utajiri wake kama asivyompendelea mtukufu/mwenye
hadhi kwa sababu tu ya utukufu/hadhi na daraja yake machoni mwa jamii
sawasawa kama yalivyo meno ya chanuo. Huyu hapa mwanamke mtukufu
anapatikana na hatia ya wizi katika zama zake Mtume. Jamaa zake
wanahangaika kutoka kulificha suala hili ili lisimfikie Bwana Mtume kwani
wwanatambua fika kwama hukumu ya mwizi ni ile aiyoitoa Allah: “NA MWIZI
MWANAMUME NA MWIZI MWANAMKE, IKATENI MIKONO YAO (ikiwa ni) MALIPO YA YALE
WALIYOYACHUMA (Hii) NDIYO ADHABU ITOKAYO KWA ALLAH NA ALLAH NI MWENYE
NGUVU NA MWENYE HAKIMA.” [5 : 38].
Habari
hizi za kuiba kwa mwanamke mtukufu huyu zikimfikia Mtume ni lazima
atapandishwa kizimbani na hatimaye hukumu hii ya Allah kupitishwa dhidi
yake. Kwa kuiona hatari hii wakamtafuta mtu atakayemuombea mwanamke huyu
kwa Mtume asikatwe mkono. Ni nani basi atakayeifanya kazi hii, hakuna
mwingine ila mtu aliye karibu zaidi na Mtume aliamua nini na hatima ya
mwanamke yule ilikuwaje, huyu hapa mama wa waumini, Bi Aysha (mkewe Mtume)
Allah amuwiye radhi anasimulia kwamba liliwahangaisha Makurayshi suala la
mwanamke wa kabila la Makhzuum aliyeiba. Wakasema. Ni nani atayezungumza
na Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie kuhusiana na suala lake?!
wakasema: Hakuna atakayethubutu ila usaamah Ibn Zayd, kipenzi cha Mtume wa
Allah usaamah (akaenda) akamzungumza Mtume, Mtume akamuuliza huku akiwa
amebadilika kwa ghadhabu kama asiyemjua: Unaomba msamaha katika hukumu
miongoni mwa hukumu za Allah (isitekelezwe)? Kisha Mtume akainuka na kutoa
khutba kisha akasema: “Hakika waliangamia waliokuwa kabla ya yenu kwa
sababu alipokuwa akiiba mtukufu miongoni mwao walimauchia (bila ya
kumuhukumu). Na anapoiba mnyonge miongoni mwao humsimamishia hukumu.
Ninaapa kwa jina la Allah,
lau kama Fatmah Binti Muhammad (mwanangu) angeiba, basi ningemkata mkono
wake. Bukhaariy na Muslim.
Maneno
haya ya Mtume wa Allah yanabainisha sababu ya kuangamizwa kwa nyumati
zilizopita kuwa ni kukosekana uadilifu na usawa miongoni mwao na
kutawaliwa na adui wa haki ubaguzi na upendeleo katika jamii hizo. Pia
yanathibitisha kwamba Uislamu ni dini inayolingania kulinda na kuheshimu
haki, usawa na uadilifu na inawatizama watu wote kwa jicho la usawa mbele
ya sheria.
Matunda
ya uadilifu katika utawala.
Miongoni mwa
matunda mazuri ya uadilifu katika utawala ni kuenea kwa amani ya nafsi.
Mtawala kama ni muadilifu hana sababu ya kuwakhofu na kuwaogopa raia wake.
Ukweli wa hili linathibitishwa na kisa kichopokewa kwamba kaisari (mfalme
wa urumi wa wakati huo) alimpeleka mjumbe wake kwa Umar Ibn Khatwab
(kiongozi wa dola ya Kiislamu) akamchunguze na kumpeleleza kiongozi huyu
shujaa anayeheshimwa na kuogopewa na madola mengine na anayependwa na raia
wake, Ajue ni nini siri ya mafanikio yake, kisha amletee ripoti. mpelelezi
huyu alipofika Madinah (makao Makuu ya dola ya kiislamu wakati huo)
aliwauliza wenyeji: Mfalme wenu yuko wapi? Wakamjibu: Sisi hatuna mfalme
bali tunaye Amiri (kiongozi) naye ametoka amekwenda nje ya mji. Akatoka
kwenda kumfuata huko aliko, akamkuta amelala mchangani na kuifanya mto
fimboyake ndogo aliyokuwa akitembea nayo. Alipomuona katika hali hii
(akiwa hana ulinzi wowote) moyo wkae ukaingiwa na
unyenyekevu akaseema: Mtu ambaye wafalme wote hawapati usingizi kwa
kumuogopa hii ndio hali yake: Ewe umar umefanya uadilifu, ukalala kwa
amani bila ya walinzi na mfalme wetu anafanya dhuluma, anakesha kwa khofu
hapato usingizi.!
Huu
ndio uadilifu na matunda yake, waliotumwa Mitume kuja kuutangaza na
kuusimamisha ulimwenguni kote ili dunia iwe ni kisiwa cha amani, “KWA
HAKIKA TULIWAPELEKA MITUME WETU KWA DALILI WAZIWAZI NA TUKAVITEREMSHA
VITABU NA UADILIFU PAMOJA NAO, ILI WATU WASIMAMIE
UADILIFU……………….(57: 25)
|