|
Muislamu si mtu
wa ajizi wala hawi mvivu bali ni mtu thabiti, mtendaji kazi na huwa na
pupa ya maendeleo. Ajizi na uvivu, hizi ni tabia mbaya ambazo Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akimuomba Allah amkinge na
kumuepusha nazo. Ni mara nyingi sana Bwana Mtume alikuwa akiomba: “Ewe
Mola wa haki! Hakika mimi ninajilinda kwako kutokana na ajizi, uvivu,
uoga, udhaifu wa ukongwe na ubakhili”.Bukhaariy & Muslim.
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-hakuwa mvivu, bali mwenyewe alikuwa mchapa
kazi hodari na akauusia umati wake kufanya kazi,akasema: “Yapupie yenye
manufaa kwako, na jilinde kwa Allah na wala usifanye ajizi. Likikupata
jambo usiseme lau ningefanya kadha ingekuwa kadha, lakini wewe sema
amelikadiria Allah (linipate) na yeye hulitenda alitakalo. Kwa sababu
(neno) lau hufungua amali ya shetani”. Muslim.
Kwa kuwa
muislamu ameamrishwa kumfuata Mtume wake na kumfanya kuwa ndio kigezo
chake ndio maana huwezi kumuona muislamu akiwa mvivu au mwenye ajizi. Kama
ambavyo huwezi kumshuhudia muislamu kwa maana ya neno lenyewe akiwa
muoga wala bakhili. Itamkinika vipi muislamu kubweteka na kuacha
kufanya kazi na kupupia manufaa na maendeleo yake. Na ilhali yeye ni
muumini wa “mfumo sababu” na kanuni ya ulimwengu ya “tafuta
utapata”, “panda utavuna”. Muislamu hupupia kufanya amali njema
zitakazomnufaisha leo hapa katika uso wa ardhi na kesho kule akhera kwenye
maisha ya milele. Kwa sababu anauamini wito wa Allah unaomtaka kuwa
mshindani katika mambo ya kheri: “YAENDEENI UPESI (mambo ya kukupatieni)
SAMAHANI YA MOLA WENU NA PEPO AMBAYO UPANA WAKE NI KAMA UPANA WA MBINGU NA
ARDHI…”. [57:21]
Tukiizingatia
aya hii itatudhihirikia kwamba mambo yote mazuri kama pepo ya Allah,
maisha mazuri duniani na akhera hayapatikani bure bure tu. Mtu abweteke,
afanye uvivu, aache kuhangaika na kujishughulisha, kisha atarajie kupata
maisha bora na pepo ya Allah! La, hasha hili ni muhali ni lazima ayaendee
mbio kama inavyosema aya. Aingie mashindanoni khasa katika kuhakikisha
kuwa anayapata mambo mazuri mazuri: “…NA KATIKA (kupata) HAYA
WASHINDANE WENYE KUSHINDANA”. [83:26]
SURA ZA AJIZI
NA UVIVU.
Ukitaka kujua
kama tayari umeshatambaliwa na tabia mbaya za ajizi na uvivu, zifuatazo ni
baadhi ya sura zake. Hebu jikague mwenyewe kama umeshakumbwa na umuombe
Mola wako akunasue.
- Mtu
kusikia adhana na akaacha kuuitikia wito huo wa swala, akaendelea na
utamu wa usingizi au akaendelea na baraza ya porojo. Au kazi isiyo ya
dharura mpaka wakati wa swala ukawa finyu (karibu kutoka). Kisha tena
ndio anainuka wangu wangu kwenda kuswali peke yake mwishoni mwa
wakati. Hii ni ajizi na uvivu , jiepushe.
- Mtu
kutumia muda mwingi mno katika baraza za kahawa, karata, bao,
kutumbulia macho runinga (televisheni) kutwa au kuzungukazunguka hovyo
mitaani bila ya malengo wala muelekeo. Anapoteza muda wote huo na
ilhali anakabiliwa na mlolongo wa mambo mengi muhimu yanayomlazimu
kuyatekeleza. Hii kama sio ajizi au uvivu ambo utakaokugharimu
maishani ni nini basi?!
- Mtu
kuacha kujishughulisha na mambo yenye manufaa kwake kama vile kusoma
na kujiendeleza kielimu au kufanya kazi halali na kujipatia riziki
yake ya halali. Kazi ambazo zitamdhaminia mafanikio duniani na akhera,
akaziacha na kuendekeza uvivu na huku akitoa hoja za uzee. Au kazi hii
mimi siiwezi ni ngumu au mimi si mtu wa kufanya kazi kama hizi au kazi
hii inaninyima hata fursa ya kupumzika. Siku, majuma, miezi na
hatimaye miaka inapita na yeye kabweteka tu hataki kufanya kazi kwa
manufaa yake mwenyewe ya ulimwengu huu na ule ujao. Huu nao ni uvivu
na ajizi aliyokua akijilinda nayo Mtume wa Allah kwa Mola wake.
- Mtu
kufungukiwa na milango ya kheri kama vile kupata fursa ya kwenda
kuhiji. Allah amemneemesha kwa kumpa neema ya mali na afya njema na
bado asiitumie fursa na neema hii kuitekeleza nguzo hii ya Uislamu. Au
kupata fursa ya kukutana na mtu mwenye shida anayehitaji huruma na
msaada, akaacha kumsaidia na ilhali Allah amempa uwezo wa kumsaidia.
Au mtu akapata bahati ya kuudiriki mwezi mtukufu wa Ramadhani, akiwa
mzima mwenye afya njema na amani. Kisha akaacha kuzivuna fadhila
adhimu za mwezi huo mtukufu kwa kushindwa kusimama usiku kufanya
ibada. Au mtu kapata bahati ya kuwadiriki wazazi wake wawili, au mmoja
wao katika hali ya utu uzima. Kisha akashindwa kuivuna pepo na
samahani (maghfira) ya Mola wake eti kwa sababu tu ya kuacha
kuwatendea wema kama alivyoagizwa na Mola wake. Hii pia haiachi
kuwa ni aina ya uvivu na ajizi itakayokutia khasarani leo na kesho.
Muombe na umbembeleze Mola wako akuepushe navyo.
- Mtu
kuishi maisha duni na ya dhiki huku akimsingizia Mola wake kuwa ndiye
aliyemkadiria maisha hayo. Hachukui hatua zo zote za makusudi ili
kujikwamua kutokana na hali hiyo kwa kuzidisha bidii katika kazi. Hii
nayo ni sura nyingine ya uvivu na ajizi ambao si sifa ya muislamu.
Uvivu na ajizi
hujishakilisha katika sura nyingi, hizi ni baadhi yake tu na ni kipimo cha
hizo nyingine ambazo hatukuwafikiwa kuzitaja.
|