|
Kimaumbile mwanadamu
ni kiumbe mwenye tabia ya ubinafsi, tabia ya kujifikiria yeye mwenyewe.
Tabia ya kujipendelea na kutanguliza mbele maslahi yake. Haya ndiyo
maumbile ya mwanadamu: “…NA NAFSI ZIMEWEKEWA UBAKHILI MBELE (ya macho
yake) …” [4:128]
Mwanadamu ni mchoyo
apendaye kupokea bila kutoa, kufaidi bila kufidisha na husema mimi mimi na
wala hasemi uma uma. Ni maafa na janga kubwa uma/jamii kuwa na wananchi
wenye mioyo/roho za ubinafsi, hawa hawana nafasi ya kuangalia maslahi ya
uma. Hawawezi kujitolea muhanga kwa ajili ya maendeleo ya uma, uma wenye
watu wenye roho hii ya ubinafsi hauwezi kupiga hatua ya maendeleo. Muumini
wa kweli hawi mbinafsi bali huyatanguliza mbele maslahi ya uma kabla ya
maslahi yake binafsi. Hii inatokana na kule kuamini kwake kwamba kila
alicho nacho ni neema aliyopewa na Mola wake na ni mtihani kwake. Imani
hii ndiyo humfikisha kusema: “…HAYA NI KWA FADHILA ZA MOLA WANGU, ILI
ANIJARIBU NITASHUKURU AU NITAKUWA MWIZI WA FADHILA…” [27:40]
Muumini analikubali
agizo na wito wa Mola wake katika kutoa kile alichomneemesha katika njia
za kheri na kuyatanguliza mbele maslahi ya uma. Anafanya yote haya huku
akiwa na imani isiyo na shaka kwamba atakuta jazaa ya kutoa huku mbele ya
Mola wake na ziada na kwamba Allah atampa badali ya anachokitoa: “…NA
CHO CHOTE MTAKACHOTOA, BASI YEYE ATAKILIPA, NAYE NI MBORA WA
WANAORUZUKU…” [34:39]
Muumini wa kweli
hana chembe ya shaka moyoni mwake kwamba baya lo lote litakalomsibu katika
njia ya kujitoa muhanga kwa ajili ya maslahi ya uma, Allah atamjaza jazaa
iliyo bora kabisa: “NA KAMA MKIUAWA KATIKA NJIA YA ALLAH AU MKIFA (si
khasara kwenu) KWANI MSAMAHA NA REHEMA ZINAZOTOKA KWA ALLAH (kukujieni) NI
BORA KULIKO VILE WANAVYOKUSANYA (hapa ulimwenguni)”. [3:157]
Imani ya kweli
humtoa mja katika ubinafsi na kumjaza moyo wa kuupenda na kuutanguliza
uma. Answaar; wenyeji wa Madinah wamepiga mfano ambao historia ya wanadamu
haijapatapo kuusajili katika kuwapendelea na kuwatanguliza mbele ndugu zao
wa imani kuliko nafsi zao. Mapokezi mema yaliyosheheni mapenzi (upendo),
moyo wa kutoa na ukarimu ulioonyeshwa na Answaar kwa ndugu zao Muhaajirina
ni mfano hai unaotoa taswira ya maisha ya jamii ya kiislamu yanavyopaswa
kuwa. Answaar walifikia hatua ya kuwagombea wageni wao,kila mmoja akitaka
mgeni afikie kwake mpaka kiasi cha kuamua kupiga kura na aliyeshinda ndiye
aliyemchukua mgeni. Hili lilitokana na idadi ya wenyeji kuwa kubwa kuliko
idadi ya wageni wao na upeo wao katika kufahamu fadhila za udugu huu wa
imani na kutoa kwa ajili ya Allah. Huu ni upeo na daraja ya juu ya imani,
huu ni ushindi wa Answaar dhidi ya ubinafsi na ubakhili ambao ni sehemu ya
maumbile ya mwanadamu. Hivi ndivyo Allah anavyolisajili tukio hili la utu
ndani ya Qur-ani Tukufu, tusome na tuzingatie: “NA WALE WALIOFANYA
MASKANI YAO HAPA (yaani Madinah) NA WAKAUTAKASA UISLAMU (wao bara bara)
KABLA YA (kuja) HAO (Muhajiri huko Madinah) NA WAKAWAPENDA HAO WALIOHAMIA
KWAO, WALA HAWAPATI, HAWAONI DHIKI NYOYONI MWAO KWA HAYO WALIYOPEWA (hao
Muhajiri) NA WANAWAPENDELEA KULIKO NAFSI ZAO INGAWA WENYEWE WANA HALI
NDOGO. NA WAEPUSHWAO NA UBAKHILI WA NAFSI ZAO HAO NDIO WENYE KUFAULU KWELI
KWELI”. [59:9]
Na aangalie mtu hali
na imani ya jamii hii ya mwanzo ya kiislamu ailinganishe na jamii yetu ya
leo, bila ya shaka ataona kuna tofauti kubwa kabisa. Kwa nini basi iwepo
tofauti na sio tofauti tu bali tofauti kubwa, kubwa sana. Ikiwa wale
walikuwa ni waislamu na sisi leo ni waislamu, kwa nini tunashindwa kuwa
kama wao?! Ni dhahiri kuwa wenzetu wale imani iliwakolea na kujaa katika
nyoyo zao na hivyo kusababisha watawaliwe na moyo wa kutoa, kuweka mbele
maslahi ya uma na kujitoa muhanga. Ama sisi leo, ninajasiri kusema kuwa
bado nyoyo zetu hazijatawaliwa na imani ya kweli na hivyo kutoa mwanya wa
ubinafsi, upendeleo na ubakhili kuzikalia kiurahisi kabisa nyoyo zetu.
Ndio ikawa leo hakuna muislamu anayemjali muislamu mwenziwe bali mwanadamu
mwenziwe. Kila mmoja wetu ameyaweka mbele ya macho yake maslahi binafsi.
Hakika uislamu kama mfumo sahihi wa maisha umemsawirishia muislamu taswira
maalumu ya maisha, iwe ni maisha binafsi au maisha jamii. Uislamu unamlea
muislamu kuwa na upendo, huruma na kuitendea wema jamii yake bali jamii
nzima ya wanadamu. Unawataka watu wa tabaka la juu kimaisha (matajiri)
kuwasaida ndugu zao wa tabaka la chini (maskini), kuwaangalia kimalezi
mayatima na kuwakomboa mateka wa kivita. Huu ni moyo wa huruma ambao
uislamu unaujenga ndani ya moyo wa muumini kiasi cha kumfanya ayatende
yote hayo bila ya kutarajia jazaa, sifa wala shukrani kutoka kwa hao
anaowasaidia. Bali anachotaraji kwa kufanya hivyo ni radhi ya Mola wake
tu: “NA HUWALISHA CHAKULA MAYATIMA NA MASKINI NA WAFUNGWA, NA HALI YA
KUWA WENYEWE WANAKIPENDA (chakula hicho). (Husema wenyewe katika nyoyo zao
wanapowapa chakula hicho): TUNAKULISHENI KWA AJILI YA KUTAKA RADHI YA
ALLAH (tu) HATUTAKI KWENU MALIPO WALA SHUKRANI”. [76:8-9]
Hii ni huruma
inayotokana na imani ya kweli ambayo ni miongoni mwa matunda ya malezi ya
Uislamu. Malezi ambayo yanamfanya mtu atoe kwa radhi yake mwenyewe katika
kuisadia jamii yake bila ya kulazimishwa, kama zinavyofanya serikali mbali
mbali kuwatenza nguvu wananchi kulipa kodi.
Kila ambaye
amejisalimisha chini ya bendera ya Uislamu ana dhima shingoni mwake ya
kujitoa muhanga kwa nafsi (roho) na mali yake kama anavyomtaka Mola wake.
Afanye tijara (biashara) isiyododa wala kumtia khasarani na Mola Muumba
wake. Nafsi na mali yake ambavyo vyote hivyo ni hiba na milki ya Allah
ndio bidhaa na mnunuzi wa bidhaa hiyo ni Mola wake. Na thamani ya bidhaa
zake hizo ni pepo ya Allah na njia ya kufika huko ni jihadi kwa maana zake
zote. Mwisho wa njia hii ni nusra (ushindi) au kufa shahidi na jazaa ya
kufa huko inatoka kwa yule ambaye yeye ndiye mbora wa kutoa jazaa:
“ALLAH AMENUNUA KWA WAUMINI NAFSI ZAO NA MALI ZAO (watoe nafsi zao na
mali zao katika kupigania dini) ILI NA YEYE AWAPE PEPO. WANAPIGANA KATIKA
NJIA YA ALLAH,WANAUWA NA WANAUWAWA. HII NDIO AHADI ALIYOJILAZIMISHA
(Allah) KATIKA TAURATI NA INJILI NA QUR-ANI. NA NI NANI ATEKELEZAYE ZAIDI
AHADI YAKE KULIKO ALLAH? BASI FURAHINI KWA BIASHARA YENU MLIYOFANYA NAYE
(Allah) NA HUKO NDIKO KUFUZU KULIKO KUKUBWA”. [9:111]
Aya hii tukufu
ilikuwa na taathira kubwa katika imani ya waislamu wale wa mwanzo.
Waliuitikia vema wito huu wa kufanya biashara na Mola wao. Muhammad Ibn
Ka`ab Al-quradhwiy anasema: Alisema Abdullah Ibn Rawaahah-Allah amuwiye
radhi-kumwambia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika ule usiku
wa Aqabah: Shurutiza kwa ajili ya Mola wako na kwa ajili yako mwenyewe
masharti uyatakayo. Mtume akasema: “Ninashurutiza kwa ajili ya Mola
wangu
Mumuabudu yeye pekee
na wala msimshirikishe na kitu cho chote.
Na ninashurutiza kwa
ajili ya nafsi yangu
Mnihami kama
mnavyozihami nafsi zenu na mali zenu”.
Abdullah akauliza:
Sisi tukiyafanya yote hayo tutapata nini? Mtume akamjibu: “Pepo”.
Wakasema (wote kwa pamoja): Ina faida biashara hii wala hatutaivunja.
Hisia hizi za
kiimani zikamea na kustawi katika nyoyo za waumini hawa wa mwanzo. Hisia
zao katika kutoa, kuweka mbele maslahi ya uma na kujitoa muhanga kwa ajili
ya dini ya Allah zikawa ni hisia za kweli. Hisia zenye kusadikishwa na
kauli na amali zao, kila mmoja wao akikimbilia kutoa na kukufanya kwa
mashindano. Ukarimu na utoaji huu ukazifutilia mbali fikra potofu za
shetani mpotoshaji ya kwamba kutoa ni kujitia ufakirini: “SHETANI
ANAKUOGOPESHENI UFUKARA NA ANAKUAMRISHENI UBAKHILI NA ALLAH ANAKUAHIDINI
MSAMAHA UTOKAO KWAKE NA IHSANI ( kubwa pindi mkitoa)…” [2:268]
Imepokelewa kutoka
kwa Jariyr Ibn Abdillah-Allah awawiye radhi-amesema: Tulikuwa mbele ya
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-mapema mchana. Basi wakamjia watu
wakiwa pekupeku, watupu (hawana nguo), wametoboa katikati maguo ya sufi na
kuyavaa,wamebeba mapanga. Karibu wote walikuwa wanatoka katika kabila la
Mudhwar. Uso wa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ukabadilika kutokana na
hali ya shida/haja ya watu wale aliyoiona. Mtume akaingia ndani,
akamuamrisha Bilali kuadhini,nae akaadhini na kukimu swala. Mtume
akaswalisha, kisha akakhutubu baada ya swala, akasema: “ENYI WATU!
MCHENI MOLA WENU AMBAYE AMEKUUMBENI KATIKA NAFSI (asili) MOJA. NA
AKAMUUMBA MKEWE KATIKA NAFSI ILE ILE. NA AKAENEZA WANAUME WENGI NA
WANAWAKE KUTOKA KATIKA WAWILI HAO. NA MCHENI ALLAH AMBAYE KWAYE MNAOMBANA.
NA (muwatazame) JAMAA, HAKIKA ALLAH NI MLINZI JUU YENU”. [4:1]
“ENYI MLIOAMINI!
MCHENI ALLAH, NA KILA MTU AANGALIE ANAYOYATANGULIZA KWA AJILI YA KESHO
(Akhera) NA MCHENI ALLAH; HAKIKA ALLAH ANAZO KHABARI ZA MNAYOYATENDA
(yote)”. [59:18]
Baada ya Mtume
kumaliza tu kuzisoma aya hizo, akaondoka mtu akataswadaki dinari au dirham
yake. Mwingine akatoa nguo yake, pishi yake ya ngano,pishi yake ya tende,
mpaka Mtume akasema: “…Walau nusu ya kokwa ya tende”. Anasema
Abdillah:(Mtume kwisha kusema hivyo) akaja mtu katika Maanswar na rundo la
chakula, kisha wakafuatana watu katika kutoa mpaka nikaona marundo mawili
makubwa ya chakula na nguo. Mpaka nikauona uso wa Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-uking`ara kama kwamba ni fedha iliyochovywa dhahabu, Mtume
akasema: “Atakayeanzisha katika Uislamu suna (mwenendo) njema, atapata
ujira wake (suna hiyo) na ujira wa watakaoifuata suna hiyo baada yake bila
ya kupungua cho chote katika ujira wao. Na atakayeanzisha katika Uislamu
suna mbaya, atapata dhambi zake (suna hiyo) na dhambi za watakaoifuata
suna hiyo baada yake bila ya kupungua cho chote katika dhambi zao”.
Muslim
Maisha ya maswahaba
wa Mtume-Allah awawiye radhi-mara nyingi yalitoa sura ya familia moja
katika wakati wa dhiki na faraja. Kila mmoja akikitoa anachokimiliki kwa
ndugu zake wa imani. Wakigawana na kula chakula kama watu wa familia/kaya
moja, Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anaisawirisha familia hii kwa
kauli yake: Hakika Waashiari wanapokwenda jaramba vitani au kinapopungua
chakula cha familia zao Madinah. Hukikusanya pamoja chakula walichonacho
katika nguo moja, kisha wakagawana baina yao kwa usawa. Mimi (Mtume) ni
katika wao na wao ni katika mimi”. Bukhaariy
& Muslim
Ukarimu wa mtu
kuitoa nafsi yake huambatana na ukarimu wa kutoa mali, vitu viwili hivi
ndivyo nguzo kuu ya kujitoa muhanga kwa mtu. Vita vya kiislamu ni ushahidi
wa wazi unaoonyesha msimamo thabiti na imani isiyotetereka ya maswahaba wa
Mtume. Ambao walipenda kufa katika kuitetea na kuipigania dini ya Allah
kama watu wengine wanavyopenda kuishi. Ni chini ya kivuli hiki cha kutoa,
kuweka mbele maslahi ya uma na kujitoa muhanga katika kuipigania dini ya
Allah hujengeka tabia tukufu. Tabia ambazo huifanya jamii kusimama katika
misingi ya utu, huruma, upendo na mshikamano. Misingi hii huiepusha jamii
na migongano ya kijamii na mmomonyoko wa kimaadili na kuifanya amani na
utulivu uitawale jamii hiyo.
|