|
Ni vema ikaeleweka
kwamba tunapozungumza kuhusu watoto, tunazikusudia jinsia zote mbili.
Yaani watoto wa kiume sambamba na wale wa kike. Katika Uislamu hakuna
chembe ya ubaguzi, watoto wote wana haki sawa kwa wazazi wao kwa mujibu wa
sheria. Watoto wamepewa haki nyingi na Uislamu, kubwa kuliko zote ni haki
ya malezi. Wazazi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata
malezi bora. Malezi ambayo yatawaandaa kimwili na kiroho. Wapate elimu
itakayowapa ufahamu wa kutosha juu ya ulimwengu wao, wakaweza kuyafurahia
maisha ulimwenguni humu. Sambamba na malezi haya yatakayo wahakikishia
maisha bora, watoto wana haki ya kupata malezi ya kiroho. Ili kuwafanya
waendelee kuwa binadamu wenye ubinadamu na utu. Ipandwe mbegu njema ya
imani na tabia njema ndani ya nafsi zao. Kuhusiana na hili tunasoma:
“ENYI MLIOAMINI! JIOKOENI NAFSI ZENU NA WATU WENU, NA MOTO AMBAO KUNI
ZAKE NI WATU NA MAWE…” [66:6]
Ni dhahiri kuwa
wazazi hawatoweza kuwaokoa watu wao wa nyumbani (familia) na adhabu ya
moto kama wanavyotakiwa na Mola wao, ikiwa hawatowalea watoto wao kwa
mujibu wa imani yao. Nae Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-analielezea
jukumu hili la wazazi kupitia kauli yake hii: “Nyote nyie ni wachunga na
nyote mnawajibika (wenye kuulizwa) kwa wachungwa (mliopewa kuwachunga)
wenu. Mwanamume ni mchunga kwa watu wake wa nyumbani na ataulizwa juu ya
wachungwa wake (aliwachungaje)”. Bukhaariy & Muslim
Kutokana na kauli
ile ya Allah na kauli hii ya Bwana Mtume, utaona kuwa watoto ni amana
iliyomo shingoni mwa wazazi. Na kwamba siku ya Kiyama wataulizwa kuhusiana
na amana hii waliyopewa. Ni kwa kuwapa watoto malezi ya kiroho (kidini)
ndio wazazi wanaweza kujitoa katika dhima ya uchunga huu na hivyo kuwa na
la kujibu mbele ya Mola wao. Ni kwa malezi haya ndio watoto watatengenea
na kuongoka na hapo ndipo watakapokuwa ni burudani/pozo la macho (nyoyo)
ya wazazi, leo duniani na kesho akhera. Allah Mola Mwenyezi anatuambia
ndani ya Qur-ani: “NA WALE WALIOAMINI NA WAKAFUATWA NA VIZAZI VYAO NA
WATOTO WAO KATIKA IMANI. TUTAWAKUTANISHA NA HAO JAMAA ZAO, WALA
HATUTAWAPUNJA KITU KATIKA (thawabu za) VITENDO VYAO; KILA MTU ATALIPWA KWA
KILA ALICHOKICHUMA”. [52:21]
Bwana Mtume-Rehema
na Amani zimshukie-anasema: “Anapokufa mja hukatika amali zake ila mambo
matatu:
Sadaka yenye
kuendelea, au
Elimu yenye
kunufaisha baada yake, au
Mtoto mwema
atakayemuombea Mungu”.
Muslim.
Haya ndio matunda ya
kumlea mtoto malezi mema ya kiroho (kidini), malezi ambayo yatamfanya awe
mtoto mwenye manufaa kwa wazazi wake hata baada ya mauti. Leo ulimwengu
unataabika na kupiga kelele kuwa watoto wa siku hizi hawana adabu na
maadili yameporomoka. Janga hili halitusibu kwa bahati mbaya, bali ni
kutokana na wazazi wengi kughafilika na jukumu lao la malezi na khasa
malezi haya ya kiroho. Wazazi hawajali na wala hawaulizi watoto wao
wamekwenda wapi, wamerudi nyumbani saa ngapi. Wala hawajishughulishi kujua
wanasuhubiana na nani kama marafiki na wenza. Wazazi hawachukui taabu ya
kuwaelekeza watoto wao lipi lifaalo kutendwa na kwa nini. Na lipi
lisilofaa kutendwa na kwa nini, bali huuachia ulimwengu kuwafanyia kazi
hiyo. Kwa kuupa ulimwengu jukumu si lake, ndio leo tumefika hapa tulipo.
Hali imekuwa mbaya kiasi ambacho mtoto anafikia hatua ya kumpiga mzazi
wake. Hebu tujifunze kwa kumuiga mzazi/mlezi mwema kama tunavyoelezwa na
Qur-ani: “…KILA MARA ZAKARIA ALIPOINGIA CHUMBANI (kwake) ALIKUTA
VYAKULA PAMOJA NAYE (huyo Maryamu). AKASEMA: EWE MARYAMU! UNAPATA WAPI
HIVI? AKASEMA: HIVI VINATOKA KWA ALLAH NA ALLAH HUMRUZUKU AMTAKAYE BILA
KUWAZA (mwenyewe)”. [3:37]
Huyu ndiye mlezi
alijuaye vema jukumu na dhima yake ya ulezi. Leo wewe mzazi unafahamu fika
kwamba binti yako hana kipato wala chumo lo lote, bado anakutegema wewe
katika mahitaji yake yote. Binti huyu anakuja nyumbani na nguo nzuri,
viatu vya gharama, vitu vya dhahabu na simu ya mkononi. Wewe kimya
unakodolea macho, humketishi chini ukamuuliza anakovipata. Unangojea mpaka
siku moja atakapokuja na mtumbo ndio umfukuze nyumbani na kumkana kuwa sio
mwanao! Kumbuka hajipigaye mwenyewe huwa halii. Jambo la kustaajabisha ni
kuwa utawaona wazazi hawa wanaowanyima watoto wao haki yao ya msingi ya
malezi, wanapupia kwa pupa zote suala la mali. Wanatumia sehemu kubwa ya
muda wao katika kuwekeza mali na kukesha katika kupanga mikakati ya
kuiendeleza. Ni ukweli usiopingika kwamba, ghalibu mali hii inayowapeleka
mbio pengine huja kuifaidi watu wengine kabisa. Wasio na uchungu nayo,
washindwe hata kumtaja kwa wema na kumuombea Mungu. Ama watoto ambao ndio
tumaini na tegemeo lake duniani na akhera, hawajali na wala hana muda wa
kuhakikisha kuwa wanapata malezi ya kidini. Mzazi ni vema ukakumbuka
kwamba, kama ambavyo ni jukumu lako kuulea mwili wa mwanao kwa kumpa
chakula, maji na nguo. Ni vivyo hivyo imekuwajibikia kuulea moyo na roho
ya mwanao kwa kumpa elimu kama chakula. Kumpandikizia imani ya kweli kama
maji na kuivisha roho yake kwa vazi la taq-wa (ucha-Mungu): “ENYI
MLIOAMINI! HAKIKA TUMEKUTEREMSHIENI NGUO ZIFICHAZO TUPU ZENU NA NGUO ZA
PAMBO, NA NGUO ZA UTAWA (yaani kucha Mungu) NDIZO BORA…” [7:26]
Na miongoni mwa haki
za watoto zilizo katika dhima ya wazazi wao ni kuwapa huduma zote muhimu
wanazozihitajia kwa ajili ya ustawi wao wa baadae. Ni wajibu wako kama
mzazi uliyejibebesha dhima ya ulezi, kuhakikisha kuwa mwanao anapata elimu
itakayomsaidia kimwili na kiroho leo duniani na kesho akhera. Anapata
chakula bora cha kujenga, kutia nguvu na kuulinda mwili dhidi ya maradhi.
Chakula kitakacho dhamini afya njema ya kiwiliwili, akili na haiba.
Anapata maji safi na salama ya kunywa, anapata nguo za heshima na sitara
zinazoendana na majira aliyomo. Anapata mahala pazuri na salama pa kulala,
mahala ambapo patamuhakikishia mapumziko mazuri. Yatakayoupumzisha mwili
na akili yake na hivyo kumfanya aamke kesho akiwa na nguvu na akili mpya.
Hii ni sehemu ya wajibu wako kwa mwanao, na kuutekeleza wajibu wako huu ni
namna moja ya kuishukuru neema uliyoneemeshwa na Mola wako. Neema ya
watoto na neema ya mali. Ni sehemu ya wendawazimu kwa mtu aliyekunjuliwa
riziki na Mola wake, kisha akafanya ubakhili katika kuwahudumia wanawe.
Elewa watoto wamepewa haki na sheria kuchukua sehemu ya mali yako kwa
ajili ya kukidhi haja na mahitaji yao ya msingi. Lakini bila ya kufanya
israfu wala ubadhirifu. Hivi ndivyo alivyofutu Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-katika kadhia (suala) ya Hind Bint Utbah, kama ilivyokuja
katika riwaya ya Bukhaariy na Muslim.
Katika jumla ya haki
za watoto ni kupata mapenzi sawa ya wazazi. Mzazi asionyeshe kumpenda sana
mtoto mmoja kuliko wengine, khasa anapokuwa ni baba mwenye zaidi ya mke
mmoja. Au ikawa anawapenda zaidi watoto wa kiume kuliko wale wa kike.
Mapenzi haya yakamuongozea kumpa mtoto kipenzi zawadi na kuwanyima wale
wengine. Elewa ewe mzazi, hayo si mapenzi bali ni kuwagawa wanao na
kuwajengea chuki baina yao. Kufanya hivi ni dhuluma na Allah hawapendi
watu madhalimu. Hutokea wazazi wengine wakampenda zaidi mtoto wao fulani
na kumpa kila akitakacho. Pengine hata kumuandikia wasia kuwa wakifa apewe
kitu fulani na kuwanyima wale wengine. Hufanya hivi eti kwa sababu mtoto
fulani huyu ndiye anayewatii, kuwasikiliza, kuwahudumia na baki ya wema
mwingine. Wema wake mtoto fulani huyu hauwi mbele ya macho ya sheria ndio
sababu inayompa haki zaidi kwenu wazazi kuliko nduguze. Haya ni masuala
mawili tofauti; suala la wajibu na suala la haki. Mtoto kuwatendea wema
wazazi wake ni wajibu wake na ujira wake uko mbele ya Allah. Na sio kupewa
vitu vya wazazi na kuwanyima wale wengine. Imepokelewa kutoka kwa
Nu’umaan Ibn Bashiyr-Allah awawiye radhi-kwamba baba yake (mzee) Bashiyr
Ibn Sa’ad alimpa yeye (Nu’umaan) hiba ya kijana mtumishi. (Baba)
akamueleza Mtume-Rehema na Amani zimshukie-khabari ile, Mtume akamuuliza:
“Je, umewapa watoto wako wote kama hivyo?” Akajibu: Hapana, (Mtume)
akasema : “(Kama hukuwapa wote), basi irejeshe hiba yako”.
Na katika riwaya
nyingine Mtume alisema (kumwambia Bashiyr): “Mcheni Allah na fanyeni
uadilifu baina ya watoto wenu”.
Na katika tamko
lingine alisema: “ Mshuhudize juu ya jambo hili mwingine, kwani mimi
sishuhudii dhulma”. Bukhaariy & Muslim
Bwana Mtume anauita
upendeleo kwa baadhi ya watoto kuwa ni DHULMA na dhulma ni HARAMU. Lakini
lau mzazi atampa mmoja wa wanawe kitu anachokihitaji na mwingine
hakihitajii. Mathalan mtoto mmoja anahitaji vifaa nya shule, au tiba au
kuoa, si UPENDELEO kumkidhia haja yake hiyo kwa sababu yule mwingine
hahitajii kitu hicho wakati huo.
Mzazi
atakapoutekeleza vema wajibu wake kwa wanawe kwa kuwapa malezi yale ya
kimwili na kiroho. Utekelezaji huu wa wajibu utawajengea watoto hisia na
mazingira ya kuwatendea wema wazazi wao na kuchunga haki zao. Kinyume
chake, yaani mzazi atakapoacha kuutekeleza vema wajibu wake huo, itakuwa
ni sababu itakayowapa watoto uhalali wa kuwatupa wazazi na
kutowashughulikia watakapokuwa wakubwa.
|