|
8. Ni wajibu wa mke
kumuheshimu mumewe heshima iliyochanganya huruma na upendo. Asimbughudhi
mumewe kwa sababu tu ya uzuri au mali yake akiwa ni tajiri au ana hadhi
kuliko mumewe huyo.
9. Mke anapaswa kuwa
na huruma na nasaha njema kwa familia ili kuilinda dhidi ya mmomonyoko wa
kimaadili. Asijenge mazoea ya kuwatukana na kuwalaani watoto, kwani hilo
litawapelekea na wao kujengeka hivyo watakapokuwa baba/mama wa familia.
Jambo dogo tu atakalofanyiwa na mumewe lisiwe ndio kifutio cha mema na
mazuri yote aliyofanyiwa na mumewe huyo katika kipindi chote cha maisha
yao. Ni lazima tukubali ukweli kuwa haya ni maumbile na tabia ya wanawake
walio wengi. Kwamba kosa/jambo dogo tu la mumewe humfikisha kusema: (Mume
gani wewe, tangu unioe sijaona jema lako hata moja, wewe nawe mwanamume
katika wanamume!). Mambo haya hayafai kwani humsafishia mwanamke huyo njia
ya kwendea motoni. Imepokelewa kwamba Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-aliwaona wanawake ndio akthari (wengi) ya watu wa motoni,
akaulizwa sababu yake ni nini. Akajibu: “Wanakithirisha mno laana
(wanalaanilaani mara kwa mara watoto kwa jambo dogo tu) na wanakanusha
wema na ihsani ya mume”. Bukhaariy, Muslim & Ahmad.
Hizi kwa mukhtasari
ndizo baadhi ya haki za mume kwa mkewe au wajibu wa mke kwa upande wa
mumewe. Ni matumaini yetu kuwa kutokana na silsila (mlolongo) ya masomo
haya wanandoa watakuwa kwa kiasi kikubwa wamezijua haki na wajibu wa kila
mmoja wao kwa mwenziwe. Allah Mola Muumba jike na dume katika kila kitu
atuwafikishe kuwa waume na wake wema wenye kupigiwa mithali mahala
tuishipo-Aaamiyn.
7. HAKI ZA VIONGOZI
NA HAKI ZA RAIA (WAONGOZWA):
Ni maumbile ya
wanadamu kukhitilafiana kifikra, kimawazo, kiufahamu na kiakili. Na mara
nyingi watu huongozwa na matamanio na matashi ya nafsi zao bila ya kujali
sheria au haki za wenzao. Maumbile haya ya wanadamu ndio yanayowajibisha
kuwepo kwa sheria zitakazowatawala na kuwahukumu. Na ili sheria hizi
zifanye kazi na kuheshimiwa ni lazima yawepo mamlaka/nguvu itakayosimamia
utekelezaji wa sheria hizi. Hapa ndipo inapojitokeza haja ya jamii yo yote
ya wanadamu kuwa na kiongozi atakayekuwa na jukumu/dhima ya kuchunga
maslahi ya uma kwa mujibu wa sheria iliyokubaliwa na kuridhiwa na jamii
husika. Kama ambavyo ni wajibu wa raia (waongozwa) kuheshimu sheria,
kadhalika ni wajibu wa kiongozi kuhakikisha kuwa sheria zinaheshimiwa
kupitia mamlaka aliyopewa.
Ni wajibu wa
kisheria bali ni sehemu ya dini, waislamu kumsimika (kumtawalisha)
kiongozi wanayemkubali atakayewatawalia na kuwaratibia mambo yao kwa
mujibu wa sheria ya Allah (Qur-ani) na Suna (hadithi za Mtume).
Kunawawajibikia waislamu kumchagua miongoni mwao mtu anayefaa kubeba dhima
ya uongozi wa uma. Kiongozi atakayechaguliwa na uma ni lazima awe ni
muislamu kweli anayeujua Uislamu wake, mcha-Mungu, muadilifu, mwenye elimu
ya sheria, uongozi na mahusiano ya kijamii. Suala la kumsimika kiongozi si
suala geni katika historia ya jamii za wanadamu, na hii ni kutokana na
umuhimu wa suala lenyewe kwa kila jamii. Katika Uislamu, uongozi/kuwa na
kiongozi ni suala lililothibiti katika Qur-ani (sheria mama) na suna
(sheria shereheshi). Tukiyapekua mabuku ya tarekh (historia) na sira,
tutayakuta yametusajilia upelekaji wa vikosi vya vita alivyovituma Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-sehemu mbali mbali. Mabuku haya
yanaonyesha kwamba Bwana Mtume hakukituma kikosi cho chote, kikubwa au
kidogo ila alikisimikia kiongozi atakayekiongoza na akakiusia kumtii
kiongozi wao. Kadhalika Bwana Mtume hakuuacha mji wo wote wa Kiislamu bila
ya kuutawalishia Amiri kama tarekh inavyolithibitisha hilo. Kadhalika
Mtume alipokuwa anaondoka nje ya Madinah kwa ajili ya kuongoza vita au kwa
sababu nyingine, alimteua mmoja wa maswahaba wake kukaimu nafasi yake
mpaka atakaporudi. Matendo yote haya ya Bwana Mtume ni ushahidi wa wazi
unaoonyesha nafasi ya uongozi katika Uislamu na kwamba ni lazima jamii ya
Kiislamu bali jamii ya wanadamu bila ya kujali itikadi/imani kuwa na
kiongozi.
Uislamu kama dini na
mfumo sahihi wa maisha ili kuhakikisha kuwa haki na uhuru wa kila mtu
unalindwa kupitia sheria zinazosimamiwa utekelezaji wake na kiongozi
aliyekubaliwa na kuchaguliwa na uma. Ili hili lifikiwe, Uislamu umeweka
haki na wajibu baina ya kiongozi na raia (waongozwa). Kwa maneno mengine
tunaruhusika kusema kuwa majukumu/wajibu wa kiongozi ndio haki za raia na
wajibu wa raia ndio haki za kiongozi.
WAJIBU WA
KIONGOZI/HAKI ZA RAIA:
Kiongozi
akishachaguliwa ni wajibu apewe madaraka/mamlaka kamili kwa mujibu wa
sheria bila ya kupingwa au kuingiliwa katika maamuzi/hukumu azitoazo
maadam hazipingani na sheria. Raia nao wana wajibu wa kumuunga mkono na
kumsaidia kiongozi wao katika kuitekeleza dhima/majukumu waliyompa.
Miongoni mwa majukumu/wajibu muhimu wa kiongozi ni kama yafuatavyo:-
WAJIBU WAKE KWA
UPANDE WA DINI WENYE MASLAHI KWA RAIA WAKE:
Miongoni wa wajibu
mkubwa aliobebeshwa kiongozi mabegani mwake ni kusimamia, kuhifadhi na
kuiendeleza dini. Ahakikishe kuwa anapanda mbegu ya mapenzi ya dini
mioyoni mwa raia (uma) wake ili waweze kuzifuata kwa ukamilifu hukumu za
dini. Ni wajibu wa kiongozi kuona kuwa mwenendo, silka, tabia na utamaduni
wa dini ndio unaoitawala jamii (uma) yake. Kiongozi afunge mianya na
milango yote inayoweza kuleta/kusababisha mmomonyoko wa maadili miongoni
mwa raia wake. Akate mizizi ya tamaduni zote zinazopingana na sheria ya
Allah na badala yake awajengee raia wake mazingira ya kuupenda,
kuuthamini, kuujali na kuufuata utamaduni wa dini yao. Sambamba na
kushikamana na mwendo (suna) wa Mtume wao. Kiongozi na jamii kwa ujumla
itambue kuwa maovu na maasi yanayotapakaa katika jamii kwa kasi ya moto
nyikani chini wa mwavuli wa kile kinachoitwa ‘kwenda na wakati’ na
watu wakayazoea na kuyaona kuwa ni mema. Watambue kuwa hilo ni gonjwa
hatari litakaloisambaratisha na kuiangamiza jamii. Njia na dawa pekee ya
kulitibu na kuliangamiza gonjwa hili na kuiokoa jamii na athari yake ni
kwa kiongozi kuhakikisha kuwa hukumu ya sheria inamuangukia kila mtenda
maovu aendaye kinyume na sheria. Aadhibiwe na kutiwa adabu kwa mujibu wa
sheria kulingana na kosa/dhambi aliyoitenda. Mbali na usimamiaji huu wa
sheria, kiongozi anapaswa kuhakikisha kuwa raia wake wanaijua sheria
sambamba na haki zao za kisheria bila ya kusahau wajibu wao. Raia
waelimishwe mpaka watambue kuwa sheria na adhabu zitolewazo kufuatia
makosa mbalimbali zimewekwa kwa maslahi yao kama uma. Sheria na adhabu
hizi zina dhima kuu ya kuhifadhi na kulinda uhai, mali, dini, heshima na
akili ya mtu. Jamii ikipata hifadhi na ulinzi wa vitu hivi ndipo watu
wanaweza kuishi kwa amani. Na ni chini ya mwavuli huu wa amani na utulivu
raia wataweza kuendesha shughuli zao za kila siku kwa ufanisi mkubwa ili
kujiletea maendeleo yao binafsi na ulimwengu kwa ujumla. Ni katika
mazingira haya ndipo watapata utulivu mkubwa utakaowawezesha kumuabuadu
Allah Mola Muumba wao kwa unyenyekevu na utii. Watu waelewe kuwa kama
kungelikuwa hakuna sheria na wasimamiaji wa sheria (viongozi), basi
ulimwengu huu ungelikuwa ni ulimwengu wa samaki. Ambamo samaki mkubwa
hummeza aliye mdogo na hakuna wa kumuuliza.
KUSIMAMISHA
UADILIFU:
Kiongozi wa Kiislamu
anatakiwa na Uislamu kutambua kwamba kuwafanyia uadilifu raia wake ni
wajibu wake yeye. Na wao raia huo uadilifu wake ni haki yao ya kisheria
waliyopewa na Allah, kwa hivyo hakuna wa kuwapokonya. Ahakikishe kuwa
anatoa hukumu ya haki, isiyo na upendeleo kwa kigezo cho chote kiwacho
baina ya mahasimu wawili waliofika mbele ya sheria. Achukue haki ya
mdhulumiwa kutoka kwa dhalimu na kumpa huyo mdhulumiwa kwa namna
anayostahiki. Watu wote wawe sawa mbele ya sheria, usiwepo kabisa mwanya
wa upendeleo. Mfalme asipewe haki kwa sababu tu ya ufalme wake, sheria
isipindwe kwa tajiri kwa kigezo cha utajiri wake na mnyonge asionewe kwa
ajili tu ya unyonge wake. Ni wajibu wa kiongozi kuyasimamia yote haya kwa
kuhakikisha kuwa uadilifu unakuwa juu ya utajiri, cheo na umaarufu wa mtu.
Kiongozi akumbuke kuwa uadilifu ndio msingi mkuu wa haki na utawala bora
unaoenziwa na wapenda haki wote bali na Allah. Kiongozi wa Kiislamu
anatakiwa kujipangia utaratibu wa kusikiliza malalamiko na matatizo ya
raia wake. Awe karibu sana na watu wake, ashirikiane nao na kuwaenzi
katika dhiki na faraja kiasi cha kuwafanya wamuhisi na kumkubali kuwa ni
mwenzao. Kiongozi muumini hatakiwi kujenga uzio baina yake na raia wake,
akawa hana nafasi ya kukutana nao na kujua matatizo yao yanayowakabili,
kwani kufanya hivyo ni kuwaghushi raia. Bwana Mtume, kiongozi muadilifu
kuliko wote waliopata kuwepo na watakaokuwepo-Rehema na Amani
zimshukie-anasema: “Hapana mja ye yote atakayepewa uongozi na Allah
Mtukufu, akafa siku ya kiyama na il-hali amewaghushi raia wake ila Allah
atamuharamishia pepo (kiongozi huyo ghashashi)”. Bukhaariy & Muslim.
Na akasema tena:
“Ye yote atakayetawalishwa cho chote katika mambo ya waislamu, kisha
asiwatumikie upeo wa juhudi yake na asiwape nasaha zake ila hataingia
pamoja nao peponi”. Muslim
Na Allah Mola
Mwenyezi anatuambia: “HAKIKA ALLAH ANAKUAMRISHENI KUZIRUDISHA AMANA KWA
WENYEWE (wanaozistahiki) NA MNAPOHUKUMU BAINA YA WATU MUHUKUMU KWA
HAKI...” [4:58]
KUKUBALI NASAHA NA
USHAURI MWEMA WA RAIA WAKE:
Kiongozi wa Kiislamu
hawi dikteta kama ambavyo hawi bendera akafuata upepo unakomuelekezea. Ni
haki yao raia kama uma kumnasihi na kumpa kiongozi wao ushauri mzuri
unaolenga kujenga na sio kubomoa. Na ni wajibu wa kiongozi kuukubali na
kuupokea ushauri na nasaha hizo bila ya kinyongo. Pamoja na kukubali
nasaha na kupokea ushauri, kiongozi anapaswa kuwa na chujio/chekecheo la
kuchekechea nasaha na kuuchujia ushauri huo aliopewa na raia wake.
Autupilie mbali ulio mbaya unaolenga kubomoa na aukumbatie na kuufanyia
kazi ule ulio mzuri unaolenga kujenga na kudhamini maslahi ya uma.
Kukubali nasaha na kutaka ushauri ni miongoni mwa nguzo za sheria ya
Uislamu. Hebu tumuangalie Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-namna
alivyokuwa akiusikiliza ushauri na kuukubali. Katika vita vya Badri, Mtume
wa Allah alipiga kambi mahala fulani ili kukabiliana na mushrikina.
Swahaba wake Al-Habaab Ibn Al-Mundhir-Allah amuwiye radhi-akamuendea Bwana
Mtume na kumwambia kwa adabu: “Ewe Mtume wa Allah, unaionaje kambi hii,
je ndio kambi aliyokushusha hapo Allah (kama ni hivyo) hakutufalii sisi
kuhoji wala kupinga. Au hizi ni fikra (zako tu) na mbinu za vita? (Mtume)
akamjibu: Bali hii ni fikra yangu (sio amri ya Allah) na mbinu za vita.
Akasema (Al-Habaab): Ewe Mtume wa Allah, hakika hapa si mahala panapofaa
kupiga kambi. Ondoka na watu twende mpaka tufike eneo lenye maji lililo
karibu na watu (mahasimu wetu), tupige kambi hapo. Kisha tuzibe visima
vyoye vilivyo nyuma yetu, kisha tujenge mahodhi ya maji na kuyajaza maji.
Halafu ndio tuanze kupambana nao wakati ambapo sisi tutakuwa tuna maji ya
kunywa na wao hawana. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema:
“Hakika umetoa rai nzuri” na akaifuata na kuikubali rai hiyo ya
Al-Hubaab. Angalia Siyratu Ibn Hishaam.
|