|
Bila ya shaka kila mmoja wetu amepata kuliona jengo refu,
imara na madhubuti, likampendeza na kumvutia kiasi cha kujikuta anasimama
kulishangaa. Ni dhahiri kuwa jengo hili zuri ni natija ya msingi imara,
nguzo madhubuti, kuta zilizoundwa na mkusanyiko wa matofali, vyuma vya pua
na baki ya vifaa vingine vya ujenzi. Mkamatano na mshikamano wa matofali
umezaa kuta imara, mkusanyiko wa kuta hizi ukazaa jengo zuri lililosimama
juu ya msingi madhubuti usiotetereka ukiungwa mkono na nguzo thabiti. Ni
kutokana na mchanganyiko na muungano wa vitu vyote hivi ndio likapatikana
jengo imara na madhubuti likushangazalo. Huu ndio mfano wa uma wa Kiislamu
kama jengo moja, madhubuti na imara. Kama unavyoelezwa na kauli ya Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Muumini kwa muumini mwenzie ni kama
(mfano wa) jengo likamanatalo baadhi moja na nyingine.” Bukhaary, Muslim
& Tirmidhiy. Matofali hapa ya kulijenga na kulisimamisha jengo hili
juu ya msngi imara ni umoja, mshikamano na mapenzi chini ya udugu wa
Kislamu. Sasa ni lazima vipatikane mchanga, saruji na maji ya kutengenezea
matofali ya umoja mapenzi na mshikamano utakaowafikisha katika kuitekeleza
amri ya Mola wao: “NA SHIKAMANENI KWA KAMBA (dini) YA ALLAH NYOTE NA
WALA MSIACHANE (msitengane/msifarikiane)…..” (3:103)
Sasa basi ili kuwafikisha waislamu kuwa uma mmoja kama
anavyowataka Mola wao: “KWA YAKINI HUU UMMA WENU NI UMMA MMOJA, NA MIMI
NI MOLA WENU (mmoja) KWA HIVYO NIABUDUNI.” (21:92)
Na kuwafikisha kujihisi mwili mmoja kama alivyosema Mtume
wao-Rehema na Amani zimshukie: “Mfano wa waumini katika kupendana kwao,
kuhurumiana kwao na kuoneana kwao sikitiko ni mithili ya mwili mmoja.
Kinapoumwa kiungo kimoja katika (mwili) huo, baki ya mwili hushirikiana
nacho katika homa na kukesha .” Bukhaariy & Muslim
Ndio uislamu ukaweka haki za kila muislamu juu ya nduguye
muislamu. Haki ambazo kama zitafuatwa na kila muislamu kama itakiwavyo,
bila ya shaka zitakuwa na msaada mkubwa katika kuleta umoja, mapenzi na
mshikamano baina ya waislamu. Haki hizi pia zina dhima ya kulinda na
kuhifadhi umoja na mshikamano wa uma wa Kiislamu. Haki za muislamu kwa
muislamu mweziwe ni nyingi mno, miongoni mwa hizo ni kama zinavyoelezwa na
kauli ya Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie: “Haki za muislamu
kwa muislamu ni sita:
-
Ukikutana nae mtolee salamu, na
-
Akikuita (akikualika) muitike,
-
Akikutaka nasaha/ushauri mnasihi
-
Akipiga chafya na akamuhimidi Allah, mshemue (mwambie
“Yarhamukal-laah”),
-
Akiumwa mkague (mjulie hali) na
-
Akifa lifuate jeneza lake (kamzike)”.
Katika hadhithi hii Bwana Mtume anatubainishia haki kadhaa
baina ya waislamu kama ifuatavyo:
SALAMU:
Muislamu anapompitia nduguye muislamu, anapomzuru au
anapotaka idhini ya kuingia nyumbani au kazini kwake ni haki ya ndugu yake
huyo kumtolea tamko la amani. Tamko litakalomuhisisha amani na kuituliza
nafsi yake, kwa kumtolea salamu kwa tamko la: ASSALAMU ALAYKUM
WARAHMATULLAAH. Hayo ndio maamkizi ya waislam leo duniani na kesho kule
akhera: “…MAAMKIANO YAO HUMO YATAKUWA SALLAMUN ALAYKUM (za kila
upande, yaani Amani tu juu yenu na furaha na salama).” (14:23)
Maamkizi haya ya kiislamu ni suna kokotezwa (muakadah)
kama ilivyothibiti kutoka kwa Bwana Mtume. Na maamkizi haya ni katika
jumla ya sababu za kuleta mshikamano, mtungamano na mapenzi baina ya
waislamu kama umma. Hili linashuhudiwa na kauli yake Mtume wa Allah-
Rehema na Amani zimshukie: “Wallah, hamtangia peponi mpaka muwe waumini
na hamtakuwa waumini mpaka mpendane. Basi hivi nikuambieni jambo
mtakapolitenda mtapendana, enezeni salamu baina yenu.” Muslim
Bwana Mtume ambaye anasifiwa na Mola wake: “NA BILA
SHAKA UNA TABIA NJEMA KABISA.” (68:4)
Alikuwa akimuandiliza kwa salamu kila anayekutana nae,
yaani anapokutana na mtu yeye ndiye huanza kumtolea salamu mtu huyo.
Kadhalika hakuwapuuza watoto wadogo, bali ili kuwajengea mapenzi alikuwa
akiwatolea salamu anapowapitia. Huyu ndiye Mtume ambaye Allah anatuambia:
“BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA (ruwaza nzuri) KWA MTUME WA ALLAH (lakini
mfano huo ni) KWA MWENYE KUMUOGOPA ALLAH NA SIKU YA MWISHO NA KUMTAJA
ALLAH SANA.” (33:21)
Ilivyo suna katika salamu ni mdogo kuanza kumtolea salamu
mkubwa wake na wachache wawatolee salamu walio wengi. Aliyepanda kipando
(mnyama/gari n.k) amsalimu mwenda kwa miguu. Lakini iwapo mtu mwenye
kuwajibika kutoa salamu hakuifuata suna hii ya Mtume, isiwe ni sababu ya
kutokuamkiana. Huyu aliyekuwa na haki ya kuanza kusaliminwa, atoe salamu
isipotee. Kwa hivyo itakaposadifu kuwa mdogo hakumtolea salamu mkubwa,
basi yeye amtolee salamu huyo mdogo ili ahodhi ujira na fadhila ambazo
agezipata lau angeanza yeye kutoa salamu. Amesema swahaba wa Mtume Ammaar
Ibn Yaasir–Allah awawiye radhi: “Mambo matatu mtu akiyakusanya
hukamilika imani yake:-
Uadilifu kwa nafsi yako, na
Na kuutolea salamu ulimwengu, na
Kutoa wakati wa dhiki”. Bukhaariy
Muradi wa kuutolea salamu ulimwengu ni kumsalimia na
kumuamkia kila unayekutana nae. Ikiwa kuanza kutoa salamu ni suna, basi
bila ya shaka kuijibu salamu ni fardhi toshelezi (kifayah). Yaani mmoja wa
wanakundi waliosalimiwa akiitikia atakuwa amewatoshea wenzake kutokana na
kuitikia kwake huko. Uwajibu huu wa kuitikia salamu ni amri ya Allah
katika kitabu chake kitukufu: “NA MANPOAMKIWA KWA MAAMKIO YO YOTE YALE,
BASI ITIKIENI KWA YALIYO BORA KULIKO HAYO, AU REJESHENI YAYO HAYO HAKIKA
ALLAH ANAFANYA HISABU YA KILA KITU.” (4:86)
KUITIKA WITO:
Humtokea mwanadamu neema za Allah zikamfurahisha mithili
ya kuoa au kuozesha, kuruzukiwa mtoto, kuponywa maradhi, kufaulu mtihani,
kupata cheo na kadhalika. Ili kumshukuru Allah Mola mneemeshaji huamua
kufanya karamu halali na kuwaalika ndugu na majirani zake kuja
kushirikiana nae katika furaha yake hiyo. Ndio Bwana Mtume–Rehema na
Amani zimshukie–akatuambia: “Akikuita (akikualika) muitike,” kwani
kuitika wito wa ndugu yako muislamu ni “Suna kokotezwa”. Usuna huu
unatokana na yale yanayopatikana katika kuitika wito, ikiwa ni pamoja na
kuimarisha udugu wa Kiislamu na kujenga mapenzi na mshikamano. Ni kweli
kuwa mtu anapokualika katika jambo lake, huwa amekuthamini upeo, sasa kama
hukumuitika huwa umemvunja moyo na kumfanya ajiulize kwa nini. Na pengine
akahisi kudharauliwa na hivyo kumfanya ajenge chuki badala ya mapenzi. Kwa
hivyo basi ni suna kuitika wito wa nduguyo muislamu kama hauna udhuru
mkuu. Na hata kama umeudhurika basi ni vema ukamfahamisha kabla pamoja na
kumuomba akuwiye radhi. Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie
anatuambia: “Akialikwa mmoja wenu chakula, basi na aitike (mualiko huo),
akiwa hakufunga na ale na akiwa amefunga basi na awaombee Mungu
(waliomualika)”. Ahmad, Muslim, Abuu Daawoud, Tirmidhiy & Ibn
Maajah.
TANBIHI: Si suna kuhudhuria karamu ambayo:-
Wamealikwa matajiri au watu mashuhuri pekee na kubaguliwa
masikini na wanyonge Mtume wa Allah– Rehema na Amani zimshukie anatuasa:
“Shari ya chakula (ni) chakula cha karamu, wanaalikwa matajiri na
kuachwa mafakiri…” Bukhaariy, Muslim, Abuu Daawoud, & Nasaai.
Inawachanganya pamoja wanamume na wanawake na wanamume
ambao si maharimu.
Ndani yake kuna jambo la haramu kama ulevi na kucheza
muziki au karamu kufanywa mahala pa shari kama baa.
NASAHA:
Mwanadamu kimaumbile ni kiumbe anayekumbana na magumu
yake. Kadhalika kimaumbile mwanadamu ni kiumbe tegemezi anayeishi katika
kundi na asiyeweza kujitegemea mwenyewe katika uamuzi khususan wa magumu
ya maisha. Sasa mwanadamu anaposibiwa na jambo gumu likamuhemeza asijue la
kufanya na kuhitajia ushauri nasaha kutoka kwako. Hapo ndipo Mtume wako–
Rehema na Amani zimshukie–anakwambia: “Akikutaka nasaha/ushauri,
mnasihi.” Yaani atapokujia nduguyo muislamu kukutaka ushauri katika
lililomsibu au analotaka kulifanya, basi ni wajibu wako kumpa
ushauri/nasaha njema. Na utambue kwamba hilo alilojia ni haki yake
aliopewa na Uislamu, na wewe kumpa nasaha na ushauri unaolenga kujenga au
kutatua ni sehmu ya dini kwani Mtume wa Allah–Rehema na Amani
zimshukie– ametuambia: “Dini ni nasaha kwa ajili ya Allah, kitabu
chake, Mtume wake, viongozi wa waislamu na watu wote.”
Muslim, Ahmad, Nasaai & Abuu Daawoud.
Hata kama hakukujia kukutaka ushauri na ukaona kuwa
atafikwa na madhara au janga fulani kutokana na mwenendo fulani alionao.
Basi ni wajibu wako umkusudie na umnasihi kwa mapenzi ya udugu wa
Kiislamu, lakini ni vema ukatambua kuwa wajibu wako ni kutoa nasaha tu na
sio kumlazimisha kufuata nasaha. Kadhalika ni kheri ikiwa utatambua kwamba
nasaha/ushauri ni amana, kwani anayekuja kukutaka ushauri huwa ameakuamini
na kukuthamini. Kwa hivyo basi ni wajibu wako nawe kujithaminisha kwake na
kuonyesha kuwa unastahiki heshima aliyokupa kwa kumpa ushauri mzuri. Kama
hukufanya hivyo, yaani kwa makusudi mazima ukaamua kumpa ushauri nasaha
utakaomtosa, utakuwa umemkhini (umemfanyia khiyana). Bwana Mtume–Rehema
na Amani zimshukie anatuambia: “…Atayempa nduguye ushauri kwa jambo
ambalo anajua uongofu uko katika jingine, kwa yakini amemkhini” Abuu
Daawoud & Al-Haakim
Na Allah Mola Mwenyezi anatuambia: “…HAKIKA ALLAH
HAWAPENDI WAFANYAO KHIYANA.”
|