|
Huduma/utumishi ni suala lisilopuuzwa wala kudharauliwa
katika mfumo sahihi wa maisha (Uislamu). Umuhimu wa suala hili unatokana
na ukweli kwamba maisha ya watu katika jamii yo yote ile ni maisha ya
kutegemeana na kushirikiana. Ni ukweli usiohitaji ubishi kwamba hakuna
mwanadamu anayeweza kujitegemea mwenyewe kwa kila hali. Kwa mantiki hii
maisha ya mwanadamu ni maisha ya nihudumie nikuhudumie ili tusonge mbele
kimaisha. Huduma na utumishi unaotolewa katika jamii unatofautiana baina
ya mtu na mtu. Tofauti hii inatokana na uwezo, ujuzi na vipawa vya watu
kwani kama alivyosema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Kila
mmoja amewepesishiwa aliloumbiwa kwa ajili yake”. Ahmad, Bukhaariy,
Muslim & Abuu Daawoud.
Katika anga la udugu wa kiislamu, ndugu hawa wa imani wote
husaidiana katika misingi ya wema na taqwa (ucha-Mungu). Hii ni katika
jumla ya kuitekeleza amri ya Mola wao: “...NA SAIDIANENI KATIKA WEMA NA
TAQWA...” [5:2] Na kigezo na kipimo cha ubora wa mtu katika Uislamu
hakitokani na elimu, cheo, mali au kazi aifanyao. Bali msingi wa ubora umo
katika tamko tukufu la Allah: “ENYI WATU! KWA HAKIKA TUMEKUUMBENI
(nyote) KWA (yule) MWANAMUME (mmoja; Adamu) NA (yule yule) MWANAMKE
(mmoja; Hawwa). NA TUMEKUFANYENI MATAIFA NA MAKABILA (mbalimbali) ILI
MJUANE (tu basi, siyo mkejeliane). HAKIKA AHISHIMIWAYE SANA MIONGONI MWENU
(mbora) MBELE YA ALLAH NI YULE AMCHAYE ALLAH ZAIDI KATIKA NYINYI. KWA
YAKINI ALLAH NI MJUZI, MWENYE KHABARI (za mambo yote)”. [49:113]
Taqwa (ucha-Mungu) kama ijielezavyo aya ndio kigezo pekee
cha ubora wa mtu katika Uislamu. Kwa yakini Uislamu umelihimiza sana suala
la mtu kufanya kazi na kula kutokana na jasho lake. Uislamu unawataka
waumini wake kujifunza kazi/ufundi mbalimbali utakaowawezesha kujitafutia
riziki zao kwa njia za halali. Kwani kufanya kazi ndio njia pekee ya
kuistawisha na kuijenga dunia yetu hii. Uislamu umetangaza kwamba chakula
chema na kizuri anachokila mtu kwa raha na furaha ni kile anachokipata
baada ya taabu na uchovu mkubwa unaotokana na harakati za kukitafuta.
Mwanadamu huonja katika chakula hicho shida/taabu ya kazi yake na starehe
ya matunda yake. Kuhusiana na hili Mtukufu Mtume wetu-Rehema na Amani
zimshukie-anatuambia: “Kamwe hajapatapo ye yote kula chakula kilicho
bora kuliko kula kutokana na kazi ya mikono yake. Na kwa yakini nabii wa
Allah; Daawoud alikuwa akila kutokana na kazi ya mikono yake”. Bukhaariy
Mja anapojitahidi kufanya kazi kwa ajili ya kutafuta
maisha na riziki/chakula chake binafsi na cha familia yake. Na kwa ajili
ya kujizuia na vilivyomo mikononi mwa watu, mtu huyu afahamu kwamba ana
ujira adhimu mbele ya Allah kutokana na amali yake hiyo. Imepokelewa
kwamba: “Mtu mmoja alimpitia Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-maswahaba wa Mtume wakaiona juhudi na bidii yake ya utendaji
kazi. Wakasema: Ewe Mtume wa Allah, (waonaje) lau (juhudi na bidii) hii
ingelikuwa (ingelitumika) katika njia (ya kuipigania dini) ya Allah? Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema:-
Ikiwa ametoka akifanya juhudi kwa ajili (ya riziki ya)
wanawe wadogo (ambao hawajaweza kujitegemea), basi yeye yuko katika njia
ya Allah.
Na ikiwa ametoka akifanya juhudi kwa ajili (ya chakula
cha) wazazi wake wawili walio watu wazima wakongwe, basi huyo yuko katika
njia ya Allah.
Na akiwa ametoka akifanya juhudi kwa ajili (ya riziki ya)
nafsi yake ili aizuie na kuomba, basi huyo yuko katika njia ya Allah.
Na ikiwa ametoka akifanya juhudi kwa ajili ya kujionyesha
na kujifakharisha (mbele za watu kuwa yeye ni mfanyakazi bora), basi huyo
yuko katika njia ya shetani”. Twabaraaniy
Kadhalika imepokewa kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-kwamba yeye amesema: “Hakika Allah anampenda muumini
mwenye ustadi/ujuzi wa kazi”. Al-Baihaqiy
Pamoja na Uislamu kuwahimiza waumini wake kufanya kazi,
kadhalika haukulisahau suala la haki za msingi za watumishi, vibarua
sambamba na waajiriwa. Uislamu umeweka katika misingi ya sheria yake haki
zinazolinda maslahi, hadhi na heshima ya watumishi, vibarua na waajiriwa.
Katika jumla ya haki ambazo Uislamu umeziweka ni kama zifuatavyo:-
HAKI YA UDUGU WA KIISLAMU NA KUSHIRIKIANA KATIKA CHAKULA
NA MAVAZI:
Uislamu unasema muislamu ni ndugu ya muislamu na
mafungamano ya udugu huu wa kiislamu ni mafungamano ya imani/itikadi.
Imani ambayo inawajumuisha na kuwakusanya pamoja watumishi na watumikiwa,
waajiri na waajiriwa na wafanyakazi na wafanyiwa kazi (mabwana). Uhusiano
na mafungamano ya wawili hawa ni huu udugu wa kiimani. Kwa mantiki hii, ni
wajibu chakula na mavazi ya ndugu hawa yawe mamoja kwa njia ya kusaidiana
na si kwa njia ya usawa wa moja kwa moja (wa kila kitu). Wale chakula cha
aina moja hata kama hawakukaa pamoja wakati wa kula, haya ndiyo mafundisho
sahihi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Watumishi wenu ni
ndugu zenu (katika imani), Allah amewaweka chini ya mamlaka yenu. Basi ye
yote ambaye nduguye (huyo) atakuwa chini ya mamlaka yake na amlishe
anachokula yeye na amvishe anachokivaa yeye”. Bukhaariy & Muslim.
HAKI YA UJIRA (MSHAHARA):
Ujira/malipo ya kazi au utumishi, hii ni haki
iliyowajibishwa na Uislamu. Hili linatokana na ukweli kwamba kila amali
(kazi) ina ujira wake bila ya kuzingatia uzuri au ubaya wa amali hiyo.
Kigezo na kipimo cha ujira wa amali katika Uislamu ni msingi usemao:
(Jazaa/malipo ni kwa kadri ya amali iliyotendwa). Yaani ujira uzingatie
ukubwa, uzito, hatari, mazingira na muda uliotumika katika kuitenda kazi
husika. Mtumishi/muajiriwa/kibarua atapoitekeleza kazi yake kama
walivyokubaliana na kuelekezwa na muajiri wake. Tayari amestahiki kulipwa
ujira wa kazi hiyo kwa ukamilifu, uadilifu na kwa mujibu wa makubaliano na
maagano yao kabla ya kuanza kwa kazi. Kuhusiana na haki hii ya ujira Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anatuambia: “Mpeni muajiriwa ujira
wake kabla jasho halijakauka”. Ibn Maajah
Yaani apewe ujira wake bila ya kucheleweshewa au
kusumbuliwa kwa kuambiwa njoo kesho, kesho akija anaambiwa tena njoo
kesho, basi ilimradi kesho hiyo haitofika kamwe. Huu si Uislamu na
muislamu wa kweli anayemtii Allah, Mtume wake na siku ya mwisho hathubutu
katu kuyafanya hayo. Vipi atathubutu kuyafanya na ilhali anaikiri,
anaiamini na kuikubali kauli ya Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie:
“Mbea tatu za watu, mimi ni khasimu wao siku ya kiyama”....akataja
miongoni mwao....
“Mtu aliyemuajiri muajiriwa akamtekelezea kazi yake (kwa
ukamilifu), naye asimpe ujira wake”. Ahmad & Ibn Maajah
Na hoja si tu kulipa ujira, bali je huo ndio ujira
mliokubaliana au baada ya kufanyiwa kazi unaamua kumlipa kinyume na
makubaliano yenu. Na je, ujira huo unalingana na kazi aliyoifanya? Kama
wewe ndio ungekuwa katika nafasi yake-yaani muajiriwa na yeye ndio muajiri
wako, ungeridhika na ujira huo unaompa yeye?! Ni vema ndugu muislamu
ukajiuliza kwanza maswali haya kabla hujaamua kutoa ujira unaotaka kuutoa.
|