|
WASIA
WA TATU.
C/.
JIEPUSHE NA MANENO MACHAFU/MATENDO MABAYA:
Ewe
ndugu yangu mpenzi muislamu, ninakuusia pamoja na kuiusia nafsi yangu
tuzipe masiko ya usikivu wa kufuata, kauli hizi za Mola wetu: “…NA
SEMENI NA WATU KWA WEMA…”
(2:83)
“ENYI
MLIOAMINI! MUOGOPENI ALLAH NA SEMENI MANENO YA HAKI.
ATAKUTENGENEZEENI VIZURI VITENDO VYENU NA ATAKUSAMEHENI MADHAMBI
YENU...” (33:70-71)
Wanawazuoni
wa fani ya mantwiq (logic)-Allah awarehemu– wanatuambia: (Mambo/vitu/maneno
hubainika/hujulikana kwa vinyume vyake kwa sababu
kila jambo/kitu kina kinyume chake).
Hebu na tuiweke wazi kanuni hii, sote tunakubaliana bila ya shaka
kwamba kinyume cha kusimama ni kukaa.
Sasa mtu anapokuambia usisimame, huwa unaelewa nini? Bila ya shaka
atakuwa anakuambia utende kinyume chake, yaani ukae/uendelee kukaa.
Hali kadhalika unapoambiwa usizungumze, maana yake unatakiwa ukae
kimya. Sasa kama hivi ndivyo basi ni dhahiri kwamba Allah anapotuambia:
“….NA SEMENI NA WATU KWA WEMA.” Ni kwamba anatukataza tusiseme na
watu kwa ubaya, tusiwatamkie maneno machafu yatakayo wavunjia heshima zao,
yatakayoumiza hisia zao, yatakayowapelekea kukata uhusiano mwema ulio
baina yenu. Maneno machafu yatakayojenga hali ya chuki na uhasama baina
yenu na kuhatarisha amani. Kadhalika
Allah anapotuamrisha: “…SEMENI MANENO YA HAKI…”, ni kwamba
anatuamrisha tusiseme maneno ya batili ambayo ni pamoja na kumsengenya
mtu, kumtukana, kumzulia uongo, kumfitini na kadhalika.
Kumbuka
ewe ndugu yangu–Allah akurehemu–kwamba kuifuata kwako amri ya Mola
Muumba wako, ukasema maneno ya haki na ukaacha kusema
maneno ya batili. Kitendo chako hiki chema na cha kibinadamu,
kitakuwa ni sababu ya:-
Kuendewa
vizuri na mambo yako, iwe ni kazi, biashara, ukulima, uvuvi, ufugaji na
kadhalika. Je, yupo miongoni mwetu asiyetaka kutengenekewa katika mambo na
shughuli zake? Bila shaka hayupo hata mmoja, basi dawa na njia pekee ni
kusema maneno ya haki
Kusamehewa
dhambi. Je, yupo miongoni mwetu asiyelemewa na mzigo mzito wa madhambi,
kiasi cha kutokuwa ha haja ya kusamehewa dhambi? Ikiwa unakiri kuwa mja wa
dhambi, basi sema maneno ya haki kwani ni miongoni mwa vifutio dhambi.
Allah
akurehemu ewe ndugu yangu, ikiwa utaamini kwamba hii ni ahadi ya Allah
Mola muumba wako ambaye: “…HAKIKA ALLAH HAVUNJI MIADI (yake).”
(13:31) “...HAKIKA AHADI YA ALLAH NI HAKI…” (10:55)
Tumesema
kuwa mambo hubainishwa na kinyume chake, sasa ikiwa kusema maneno ya haki
ni sababu ya kutengenekewa na mambo, sambamba na kufutiwa (kusamehewa)
madhambi. Basi ni ukweli usiopingika
kwamba kusema maneno ya batili ni sababu ya:-
Kuharibika
mambo na mipango yetu mpaka tukajiona tuna nuksi/mikosi tukaanza kutafuta
wachawi, na kumbe wanga ni sisi wenyewe.
Hili la kutafuta
mchawi likatufikisha kuwapigia hodi waganga, tukatupa pesa na imani yetu
na kusababisha mambo kuzidi kuharibika. Allah anatukumbusha: “NA MISIBA INAYOKUPATENI NI KWA SABABU
YA VITENDO VYA MIKONO YENU…” (42:30)
Kutokusamehewa
dhambi ambako kama kuna maanisha jambo, basi jambo hilo halitakuwa jingine
zaidi ya kuangamia duniani na akhera:
“...NA ALLAH HAKUWADHULUMU, BALI WAO WENYEWE WANADHULUMU NAFSI
ZAO”. (3: 117)
Jua
na ufahamu ewe ndugu yangu kwamba maneno machafu hayamvunjii heshima na
kumdharaulisha ila anayeyatamka na si mlengwa, hata kama yanamstahiki.
Kama ambavyo maneno mazuri hayamtukuzishi na kumpa heshima ila
anayeyasema. Ni vema pia
ukatambua kwamba Allah hampendi mtu mwenye maneno machafu, kama alivyosema
Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie: “Hakika wa Allah hampendi mwenye
maneno/matendo machafu wala mwenye kupiga makelele masokoni”. Bukhaariy
Tahadhari
sana ewe ndugu yangu, usiwe mtu ambaye watu watakuogopa na kukutenga kwa
sababu ya maneno/matendo yako machafu, kwani Mtume wako–Rehema na Amani
zimshukie anakuambia: “Kwa yakini mtu mwenye daraja/mahala pabaya mbele
ya Allah siku ya kiyama kuliko watu wote. Ni yule ambaye watu
wamemuacha/wamemuepuka kwa ajili ya kujikinga na uchafu wake (wa
maneno/matendo)”. Bukhaary, Muslim, Abuu Daawoud & Tirmidhiy.
Ee
ndugu yangu, ebu ona mwenyewe ubaya ulioje na maangamivu yaliyoje ya
maneno/matendo machafu. Hebu ihurumie nafsi yako na adhabu kali ya duniani
na akhera inayotokana na kusema ama maneno machafu au kutenda matendo
machafu. Kwani kama hukusema
maneno machafu au ikiwa hukutenda matendo machafu, utapungukiwa nini
katika utu na maisha yako?!
Ninazidi
kukuusia ewe ndugu yangu kwa mapenzi ya Imani bila ya kuisahau nafsi
yangu. Tahadhari, tena tahadhari kabisa kuondosha au kujibu ubaya
uliotendewa kwa namna/njia ambayo inayokhalifiana na kauli tukufu ya Mola
wako: “MAMBO MAZURI NA MABAYA HAYAWI SAWA ONDOSHA (ubaya unaofanyiwa)
KWA MEMA, TAHAMAKI YULE AMBAYE BAINA YAKO NA BAINA YAKE KUNA UADUI
ATAKUWA KAMA NI JAMAA (yako) MWENYE KUKUFIA UCHUNGU. LAKINI (jambo hili la
kuondosha ubaya kwa wema) HAWATAPEWA ILA WALE WANAOSUBIRI (pindipo
wanapotendewa ubaya)…” (41:34–35).
Allah
anazidi kutuasa juu ya namna ya kuondosha ubaya kwa kusema: “NA KAMA
SHETANI AKIKUSHAWISHI KWA TASHWISHI (zake ili ugombane na hao
wanaokufanyia ubaya) WEWE JIKINGE KWA ALLAH (kwa kusema): “AUDHU
BILLAAHI MINAS-SHAYTWAANIR– RAJIYM,” BILA SHAKA YEYE (Allah) NI MWENYE
KUSIKIA (mwenye kumuomba msaada), MWENYE KUJUA (namna ya kumsaidia)”.
(41:36)
Naam,
ni kweli kuwa hakuna anayemjua zaidi mwanadamu kuliko Allah Mola Muumba
wake. Kwa mantiki hii, hakuna ye yote anayeweza kumpa mwanadamu ushauri
nasaha mwema juu ya namna ya kukabiliana na uovu/ubaya/uadui anaotendewa
kuliko Allah. Kama ndugu yangu unaniunga mkono katika ukweli huu
usiokanushika, ninakuusia tushikamane na ushauri nasaha huu wa Muumba
wetu. Tuyakabili maovu/mabaya tunayotendewa na wenzetu kutokana na udhaifu wa kibinadamu kwa mema mazuri. Kwani hii
ndio njia pekee ya kumgeuza adui huyu kuwa rafiki, kwa sababu ubaya
hauondoshi ubaya bali ubaya huzidisha ubaya. Ni kwa mantiki hii ndio Allah
Mola Mwenyezi akamuasa Mtume wake nasi pamoja nae kwa kusema: “SHIKAMANA
NA KUSAMEHE NA AMRISHA MEMA NA WAPUZE MASAFIHI (watu wajinga, wenye
maneno/matendo machafu).” (7:
199)
Elewa
na ufahamu kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie–amesema:
“Ye yote atakayeizuia ghadhabu na il-hali ana uwezo wa kuipitisha. Allah
Mtukufu atamuita juu ya vichwa vya viumbe siku ya kiyama ili amkhiyarishe
mahurul-ayni (wanawake wa peponi) awatakao”. Abuu Daawoud &
Tirmidhiy
Jitahidi
ewe ndugu ndugu yangu, uwe pamoja na Allah Mola Muumba wako kama kwamba
hakuna viumbe wengine. Ni
wewe tu pamoja nae na amekuumba na kukupa jukumu la kumuabudu na
anaangalia namna unavyomuabudu wakati wote na mahala pote. Fikra, mawazo
na hisia zako ziwe kwamba wakati wo wote na
mahala po pote jicho la Allah linakuangalia na kuyajua yote
uyatendayo, uyasemayo na hata uyawazayo. Kadhalika uwe pamoja na viumbe
wenzako kama mwili na nafsi moja, wao ndio wewe na wewe ndio wao.
|