|
WASIA
WA NNE.
d)
IPE NYONGO DUNIA
Ewe ndugu yangu mpenzi–Allah akurehemu–ninakuusia pamoja na
kuiusia nafsi yangu tuitafakari kwa pamoja kauli hii ya Mola Muumba wetu:
“ENYI WATU! BILA SHAKA AHADI YA ALLAH NI HAKI. BASI YASIKUDANGANYENI
MAISHA YA DUNIA, WALA YULE MDANGANYAJI MKUBWA (Iblisi) ASIKUDANGANYENI JUU
YA ALLAH. KWA YAKINI
SHETANI NI ADUI YENU, BASI MFANYENI ADUI (yenu, kwa hivyo msimtii) KWANI
ANALIITA KUNDI LAKE LIWE KATIKA WATU WA MOTONI. WALIOKUFURU ITAKUWA KWAO
ADHABU KALI, NA WALE WALIOAMINI NA WAKATENDA MEMA WAO WATAPATA MSAMAHA
NA UJIRA MKUBWA”. (35:5-7)
Elewa
na ufahamu ewe ndugu yangu kwamba miongoni mwa mambo yenye kumuhilikisha
na kumuangamiza mwanadamu ni kuipenda mno dunia. Mtu akaikusudia khasa
aipate, akaipupia, akaipondokea kiasi akawa haoni wala hasikii ila dunia
tu. Akapenda na kukitafuta cheo ili aogopwe, atukuzwe na aheshimiwe,
akaenda mbio huku na huko kutafuta mali. Akajilimbikizia mali na kuihesabu
bila ya kuitolea haki yake, akawa bakhili. Yote haya ni sifa mbaya ambazo
hutakiwi kupambika nazo, ewe ndugu yangu muislamu. Mambo haya hatima yake
ni kukuangamiza na kukutupa katika adhabu kali ya milele ya moto wa
Jahanamu: “…MOTO AMBAO KUNI ZAKE NI WATU NA MAWE. WANAUSIMAMIA
MALAIKA WAKALI, WENYE NGUVU HAWAMUASI ALLAH KWA AMRI ZAKE, NA WANATENDA
WANAYOAMRISHWA (yote)”. (66:6)
Fahamu
ewe ndugu yangu katika Imani kwamba mtu mwenye kuipenda sana dunia,
akaifanya kuwa ndio lengo lake kuu na ndio kila kitu. Kwa mapenzi haya
yaliyopindukia, huyu anajiingiza na kujitia mwenyewe katika khatari kubwa
na makamio makali ya Allah. Huyu anaambiwa na Mola wake: “WANAOTAKA
MAISHA YA DUNIA NA MAPAMBO (starehe) YAKE, TUTAWAPA HUMU DUNIANI (ujira
wa) VITENDO VYAO KAMILI; HUMU WAO HAWATAPUNJWA (lakini akhera hawatapata
kitu). HAO NDIO AMBAO HAWATAKUWA NA KITU KATIKA AKHERA ILA MOTO, NA
YATARUKA TUPU WALIYOYAFANYA KATIKA (dunia) HII, NA YATAKUWA BURE
WALIYOKUWA WAKIYATENDA”. (11:15-16)
Na
akasema tena Allah: “ANAYETAKA (starehe za dunia hii)
IPITAYO UPESI (wala hana haja ya akhera), BASI TUTAMPA UPESI UPESI
HUMO (lakini) TUNAYOYATAKA (tena) KWA YULE TUMTAKAYE, KISHA TUMEMFANYIA
JAHANAMU ATAINGIA HUMO, HALI YA KUWA NI MWENYE KUDHARAULIWA NA KUFUKUZWA
(huku na huku)”. (17:18)
Na
akasema tena Allah akiwataka waja wake waipe nyongo dunia na akiwakumbusha kuondoka na kumalizika kwake: “NA WAPIGIE
MFANO WA MAISHA YA DUNIA (maisha ya dunia) NI KAMA MAJI TUNAYOYATEREMSHA
KUTOKA MAWINGUNI, KISHA HUCHANGANYIKA NAYO ( maji hayo) MIMEA YA ARDHI
(ikaistawi), KISHA (baadaye) IKAWA (mimea hiyo) MAJANI MAKAVU YALIYO
KATIKAKATIKA AMBAYO UPEPO HUYARUSHA HUKU NA HUKO. NA ALLAH ANA UWEZA JUU
YA KILA KITU”.
(18:45)
Nabii
Isa Ibn Maryam–Amani ya Allah imshukie–anatuasa kwa kutuambia: “Msiifanye
dunia kuwa ndio mungu (wenu), nayo ikakufanyeni watumwa (wake)”.
Ewe
ndugu yangu, Allah anazidi kutufahamisha juu ya dunia hii inayotughuri
hata tukamsahau, tutafakari pamoja: “JUENI YA KWAMBA MAISHA YA DUNIA NI
MCHEZO NA UPUUZI NA PAMBO NA KUFAHARISHANA BAINA YENU (kwa nasaba), NA
KUFAHARISHANA KWA MALI NA WATOTO. (Na hali ya kuwa vyote hivi hamdumu
navyo. Mfano wake) NI KAMA MVUA AMBAYO HUWAFURAHISHA (wakulima) MAZAO
YAKE, KISHA YANAKAUKA UKAYAONA YAMEPIGA UMANJANO (badala ya kupiga
uchanikiwiti), KISHA YANAKUWA MABUA (hayana cho chote). NA AKHERA KUNA
ADHABU KALI (kwa wabaya) NA (pia) MSAMAHA WA ALLAH NA RADHI (yake kwa
wema). NA HAYAKUWA MAISHA YA DUNIA ILA NI STAREHE IDANGANYAYO (mara
huondoka)”. (57:20)
Allah
Mola Muumba wetu anazidi kutuasa na kutuonya juu ya dunia, ewe ndugu yangu
tunasihike: “AMA YULE ALIYEASI NA AKAPENDA ZAIDI (akayafadhilisha
maisha) YA DUNIA. BASI KWA HAKIKA JAHANAMU NDIYO ITAKAYOKUWA MAKAZI
YAKE”. (79:37-39)
Nae
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kutokana na mapenzi na huruma yake
juu yetu, anatuambia: “Kuipenda dunia ni kichwa (chanzo/asili) CHA KILA
KHATIA (kosa/dhambi)”. Akazidi kutuambia: “Dunia ni nyumba ya asiye na
nyumba (akhera) na ni mali ya asiye na mali na kwa ajili ya dunia
hukusanya asiye na akili”.
Sasa
ewe ndugu yangu mpenzi, baada ya kuzitafakari kwa
pamoja kauli hizo za Allah Bwana Mlezi wetu na hizi kauli za Mtume
wetu ambaye Allah anatuambia: “…YANAMUHUZUNISHA YANAYOKUTAABISHENI,
ANAKUHANGAIKIENI (na) KWA WAUMINI NI MPOLE NA MWENYE HURUMA”. (9: 128)
Hebu
sasa tuinamishe na kukuna vichwa vyetu tujiulize swali moja, je, unalijua
swali lenyewe? Bila shaka hulijui, haya nitegee sikio swali linakuja hivi:
JE, HII DUNIA YENYE KUAPIZWA NA KUSEMWA VIBAYA HIVI NI NINI/NI KITU GANI
KHASA? Hilo ndilo swali tunalopaswa kujiuliza mimi na wewe ndugu yangu na
hili lifuatalo ndilo ndilo jawabu sahihi ambalo linaweza kukupa alama mia
kwa mia. Na tulipe masikio ya
usikivu: Neno dunia ni fasiri ya kila kilichopo juu ya uso wa ardhi, yaani
vyenye kutamaniwa na kuonwa tamu na namna kwa namna ya starehe zenye
kupendwa na kupondokewa na kupupiwa na wanadamu. Hiyo ndiyo dunia ielewe,
msingi wa yote haya umekusanywa na kauli yake Allah: “WATU WAMETIWA HUBA
YA KUPENDA WANAWAKE NA WATOTO NA MIRUNDI YA DHAHABU NA FEDHA, NA FARASI
WANAOTUNZWA VIZURI (leo ni magari, ndege n.k) NA WANYAMA NA MASHAMBA NA
HAYO NI MATUMIZI YA MAISHA KATIKA DUNIA, NA KWA ALLAH NDIKO KWENYE MAREJEO
MAZURI”. (3:14)
Naam,
khasa hii ndio dunia na hakuna awezaye kupinga kwani: “...NANI MKWELI
ZAIDI KATIKA MANENO KULIKO ALLAH?” (4:87) “…NA NANI MKWELI ZAIDI KWA
USEMI KULIKO ALLAH?” (4:122)
Mtu
atapoyapenda hayo mapenzi ya kupindukia na lengo lake katika kuyapata hayo
likawa ni utupu wa starehe na ladha. Huyu kwa malengo yake haya atakuwa ni
katika jumla ya wenye kuipenda dunia na wenye kuipondokea. Mapenzi yake
haya ya kuipenda dunia yakimshinda na kumkalia juu, hata yakamfanya
akachupa mipaka. Kiasi cha kumfanya kutokujali anaipataje dunia; je,
anaipata kwa njia za halali zinazomridhi Mola wake au kwa njia za haramu
zinazomuudhi Mola wake? Akafikia hatua ya kujali kupata tu na sio
anapataje, kuitafuta kwake dunia kukamfikisha kumsahau Mola wake na
kujitumbukiza katika lindi la maasi. Huyu ndiye mpenzi wa dunia ambaye
yamethibiti kwake makamio yaliyopokewa katika kuwataja wenye kuipenda na
kuifanya dunia kuwa ndio lengo lao.
Ewe
mpenzi ndugu yangu ninazidi kukuusia kuwa usia wa Mtume: “Ipe nyongo
dunia utapendwa na Allah na vipe nyongo vilivyomo mikononi mwa watu,
utapendwa na watu”. Ibn Maajah
Kisha
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie–akatubainishia kuipa nyongo
dunia ni vipi, akasema: “Kuipa nyongo dunia si kuharamisha halali na
wala si kufuja mali. Lakini kuipa nyongo dunia ni kutokuwa kilichomo
mkononi mwako unakitegemea zaidi kuliko kilichomo mkononi mwa Allah. Na
kuwa katika (kupata) thawabu za misiba (majanga) pindi utaposibiwa
kwapendeza zaidi kwako kiasi cha (kutamani) lau ungebakishiwa misiba hiyo
(ili uzidi kupata thawabu)”. Tirmidhy
Mtume
wa Allah akazidi kusema: “Kuipa
nyongo dunia huupumzisha moyo na kiwiliwili na kuipondokea dunia
hukithirisha mashaka/wasiwasi (mhangaiko wa moyo) na huzuni. Na kukaa bila
ya kazi (jambo la kufanya) huufanya moyo kuwa mgumu (mkukutavu)”.
|