|
WASIA
WA SITA: JIEPUSHE NA UBAKHILI NA UNYIMI.
Ewe
ndugu yangu-Allah akurehemu-kwa mapenzi ya Allah ninakuusia pamoja na
kuiusia nafsi yangu. Tujiepushe na tuipige teke tabia mbaya ya ubakhili na
unyimi. Viwili hivi; bakhili na unyimi si pambo na sifa ya muumini, kwani
ni miongoni mwa mambo mabaya yenye kuhilikisha. Allah Mola Mtukufu
anatuambia: “...NA WENYE KUEPUSHWA NA UBAKHILI WA NAFSI ZAO, HAO NDIO
WENYE KUFAULU. MKIMKATIA ALLAH SEHEMU NZURI (katika mali zenu,
mkazitoa katika njia za kheri) ATAKUZIDISHIENI NA ATAKUGHUFIRIENI. NA
ALLAH NDIYE ATOAYE THAWABU NYINGI, MPOLE”. [64:16-17]
Aya
inafahamisha kwamba kutokuwa bakhili ni kufaulu na kutoa katika njia za
kheri ni sababu ya kuzidishiwa mali na kupata msamaha wa Allah. Kinyume
chake kuwa bakhili ni kujinyima fursa ya kufaulu kupitia mlango wa neema
ya mali uliyopewa na Allah bila ya kupeleka maombi au kustahiki. Elewa na
ufahamu kwamba mali haizidi kwa kuifanyia ubakhili na ubakhili ni sababu
kuu ya kukukosesha maghfira ya Allah. Zidi kutambua ewe ndugu yangu
muislamu kwamba ybakhili ni shari na ni adhabu, Qur-ani Tukufu inatuambia:
“WALA WASIONE WALE AMBAO WANAFANYA UBAKHILI KATIKA
YALE ALIYOWAPA ALLAH KATIKA FADHILA ZAKE KUWA NI BORA KWAO (kufanya
ubakhili huko) LA, NI SHARI (vibaya) KWAO. WATAFUNGWA KONGWA (madude ya
kunasa shingoni) ZA YALE WALIYOYAFANYIA UBAKHILI SIKU YA KIYAMA. NA
URITHI WA MBINGU NA ARDHI NI WA ALLAH NA ALLAH ANA KHABARI ZA (yote)
MNAYOYAFANYA”. [3:180]
Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anatutahadharisha na ubakhili, anatuambia:
“Tahadharini/jiepusheni na ubakhili, kwani huo ubakhili ndio
uliowaangamiza waliokuwa kabla yenu. (Ubakhili uliwapelekea kumwaga damu
zao na kuyahalalisha waliyoharamishiwa”. Ahmad & Bukhaariy-Allah
awarehemu.
Bwana
Mtume anazidi kutuonya juu ya ubakhili kupitia kauli yake: “Bakhili yu
mbali na Allah, yu mbali na watu, yu mbali na pepo, yu karibu mno na
moto”.
Allah
Mola Mwenyezi anatubainishia ndani ya kitabu chake kitukufu fadhila za
kutoa na madhara (ubaya) ya ubakhili na unyimi, anasema: “YULE ANYETOA
(zaka, sadaka na vinginevyo) NA KUMCHA ALLAH. NA KUSADIKI JAMBO JEMA
(akalifuata). TUTAMSAHILISHIA NJIA YA KWENDEA PEPONI. NA AFANYAYE
UBAKHILI, ASIWE NA HAJA YA VIUMBE WENZAKE. NA AKAKADHIBISHA MAMBO MEMA
(asiyafanye). TUTAMSAHILISHIA NJIA YA KWENDEA MOTONI. NA MALI YAKE
HAYATAMFAA ATAKAPOKUWA ANADIDIMIA (motoni humo)”. [92:5-11]
|