|
WASIA
WA KUMI NA MBILI-ZISHUKURU NEEMA ZA ALLAH:
Ndugu yetu katika imani-Allah azithibitishe imani zetu-kwa mara nyingine
tena tunamshukuru Allah kwa kutukutanisha tena katika ukumbi wetu huu wa
wasia maridhawa. Leo kwa mapenzi ya imani ninakuusia kuzishukuru neema za
Allah alizotuneemesha bure. Yatupasa kufahamu kuwa kushukuru neema ni
katika jumla ya makamu matukufu na daraja za juu. Hivi ndivyo Allah Mola
Mtukufu anavyotuambia kuhusiana na suala zima la shukrani ya neema, haya
na tuzingatie pamoja: “KULENI KATIKA VILE ALIVYOKUPENI ALLAH, VILIVYO
HALALI NA VIZURI. NA SHUKURUNI NEEMA ZA ALLAH, IKIWA KWELI
MNAMUABUDU YEYE”. [16:114]
Mpenzi ndugu yangu-Allah atuhidi-ikiwa tutaitafakari aya hii, basi tutambua
kwamba:-
ü
Vyote tulivyo
navyo ambavyo pengine hutusahaulisha tukaacha kumuabudu Mola wetu tumepewa
na Allah. Kwa hivyo vyote ni mali na milki yake ambayo: “...HIYO NI
FADHILA YA ALLAH, HUMPA AMTAKAYE. NA ALLAH NI MWENYE FADHILA KUU (kabisa
juu ya viumbe vyake)”. [57:21]
ü
Katika jumla ya
alivyotupa Allah, viko ambavyo hivyo ni halali na vizuri na viko vile
ambavyo ni haramu na vibaya. Tunatakiwa tule vile vilivyo halali na vizuri
na tumshukuru Allah kwa neema zake hizo. Na tuache kuvikurubia vile vya
haramu ambavyo tukiwafikiwa kuchunguza tutatoka na natija kuwa ni vibaya
vyenye madhara na si vingine.
ü
Kumshukuru
Allah Mruzukuji kwa neema zake ni kielelezo tosha kuwa tunamuabudu na ni
sehemu ya ibada isiyo na shaka.
Haya baada ya tafakuri hii ya pamoja na tuendelee kuiangalia shukrani ya
neema za Allah ndani ya Qur-ani Tukufu, tusome kwa mazingatio: “...KULENI
KATIKA RIZIKI YA MOLA WENU NA MUMUSHUKURU...” [34:15]
Qur-ani inazidi kutupa khabari za shukrani, haya tusome na
tuwaidhike: “....(Tukawaambia) FANYENI (amali nzuri), ENYI WATU WA DAUDI
KWA KUSHUKURU (neema mlizopewa). NA NI WACHACHE WANAOSHUKURU KATIKA
WAJA WANGU”. [34:13]
Ndugu yangu mpenzi-Allah atuwafikishe kupendana kwa ajili yake-aya
inatufahamisha pamoja na mambo mengine kwamba:-
ü
Kuishukuru
neema ya Allah ni kutenda amali njema ambazo faida na manufaa yake
huturejea sisi wenyewe bila ya kumzidishia Mruzukuji cho chote.
ü
Kumbe
wanaomshukuru Mola wao kwa neema alizowapa ni wachache, basi tujitahidi
kuwa miongoni mwa wachache hao kwa fadhila zake Allah.
Tuelewe na tuyakinishe kuwa tunapomshukuru Mola wetu kwa neema zake
alizotupa kwa kutenda amali njema zimridhishazo. Shukrani zetu hizi
haziruki patupu bali tuna jazaa maridhawa kwa Mola wetu. Hivyo ndivyo
Qur-ani Tukufu; kitabu kisicho na shaka inavyotuambia, haya tusome na
kusadiki: “...NA ALLAH ATAWALIPA WANAOMSHUKURU”. [3:144]
Ni kheri kwetu ikiwa tutambua kwamba asili ya shukrani ni mja kujua kuwa
neema zote alizonazo za dhahiri na zile za batini zinatoka kwa Allah. Na
kwamba hakupewa kwa kuwa anastahiki bali ni kutokana na fadhila na ihsani
ya Allah tu. Mja akiukiri ukweli huu usiokufurika (usiopingika)
utamuongozea katika kuzishukuru neema hizo za Mola wake. Pia tutambue kuwa
ni sehemu ya shukrani kufurahikia kuwepo kwa neema za Allah juu ya waja
wake. Furaha hii iwe ni kwa kuzingatia kuwa neema hizo ni wasila (njia na
msaada) katika kutenda amali za twaa na kupatia ukuruba wa Allah. Shukrani
haikomelei hapo katika kuzifurahikia neema, bali pia kukithirisha
kumuhimidi Allah na kumsifia kwa neema hizo ni katika namna ya shukrani.
Hali kadhalika haipungui kuwa ni shukrani kumtii Allah kupitia msaada wa
neema zake na kuzitumia neema hizo kwa namna airidhiayo na kuipenda.
Kufanya hivi ndio upeo na ukomo wa shukrani. Ni katika kuonyesha shukrani
zetu juu ya neema za Allah kutokuwa na kibri kwa sababu tu ya neema
tulizoneemeshwa nazo. Na ambazo kwa hakika hatuzimiliki na ndio maana
tukifa tunaziacha hapa hapa kama tulivyozikuta wakati wa kuzawa kwetu.
Kutokujifakharisha na kujivuna kwa waja wa Allah kwa sababu ya neema za
Allah na kutokuzifanyia fisadi neema hizo, hivi ndivyo Qur-ani Tukufu
inavyotunasihi: “NA UTAFUTE KWA YALE ALIYOKUPA ALLAH MAKAZI MAZURI YA
AKHERA, WALA USISAHAU SEHEMU YAKO YA DUNIA NA UFANYE WEMA KAMA
ALIVYOKUFANYIA. WALA USITAFUTE KUFANYA UFISADI KATIKA NCHI, BILA SHAKA
ALLAH HAWAPENDI MAFISADI”. [28:77]
Haiachi kuwa ni sehemu ya shukrani kutokuruka mipaka ya Allah na kuzidi
katika jeuri na kuwafanyia uadui waja wake Allah Mtoaji bure neema hizo
zikupazo jeuri. Ndugu yangu katika Allah-Allah ayazidishe mapenzi
yetu-elewa kuwa ye yote mwenye kuacha kumtii Allah, mwenye kuwa na kibri,
mwenye kujifakharisha na kujivuna. Mwenye kufanya fisadi na jeuri, mwenye
kuchupa mipaka na kuwafanyia uadui waja wa Allah. Akayafanya yote haya kwa
sababu tu ya neema alizoruzukiwa na Allah, huyu bila ya shaka yo yote
atakuwa amezikufuru (amezikanusha) neema za Allah na wala hazishukuru kwa
anavyopaswa. Tuelewe bayana kuwa kitendo cha kuzikufuru neema za Allah ni
sababu tosha ya kupokonywa neema hizo, na ziada ya hayo ni kuzibadili
kuwa nakama (adhabu na mateso). Hebu na tuitafakari pamoja kauli
hii ya Allah Mola Mtukufu: “HAYO (ya kuwafika balaa hizi) NI KWA SABABU
ALLAH HABADILISHI KABISA NEEMA ALIZOWANEEMESHA WATU, HATA WABADILISHE WAO
YALIYOMO NYOYONI MWAO (wende nyendo mbaya ndipo Allah awaondoshee neema
yao)...” [8:53]
Na kitendo cha kuzishukuru neema za Allah hakimaanishi ila kumzidishia
mwenye kushukuru ziada ya neema. Hii ndio ahadi ya Allah anayowatangazia
waja wake, haya na tuipokee kwa mikono miwili: “NA (kumbukeni)
ALIPOTANGAZA MOLA WENU (kuwa) KAMA MKISHUKURU NITAKUZIDISHIENI NA
KAMA MKIKUFURU (jueni) ADHABU YANGU NI KALI SANA”. [14:7]
Mpenzi ndugu katika imani, yatakikana tufahamu kwamba ni sehemu ya shukrani
kuiona kubwa neema hata kama ni ndogo na duni machoni mwako au kwa mtazamo
wako. Wewe usiangalie udogo au uduni wa neema bali uangalie ukubwa na
utukufu wa Mneemeshaji wa neema hiyo unayoidogesha na kuidunisha. Kisha
utambue kuwa Allah ana neema adida kwa waja wake zisizodhibitika. Mja kama
kiumbe dhaifu hawezi kuzidhibiti zote akazesha seuze kuzishukuru
imuwajibikiavyo. Allah anatuambia ndani ya Qur-ani yake aliyotushushia ili
iwe muongozo kwetu, haya na tumsikilize: “NA MKIHISABU NEEMA ZA ALLAH
HAMTAWEZA KUZIHISABU...” [16:18]
Yampasa mwanadamu asimuangalie mtu aliyemzidi kineema kwa jicho la kupata
kama yeye au kumzidi. Hii ni kwa sababu hili linaweza kumpelekea kuitweza
na kuidharau neema hiyo ya Allah aliyomneemesha kwa kuilinganisha na ile
aliyopewa mwenziwe aliyemzidi. Dharau na twezo hili litamfanya asiishukuru
neema hiyo aliyopewa yeye na ikawa ni sababu ya kupokonywa neema hiyo
anayoidharau. Natija ikawa hakupata kingi mithili ya alichopewa mwenziwe
kwa hekima azijuazo Mpaji Mneemeshaji. Na kuondokewa na kile kidogo
alichopewa kwa sababu ya kutokumshukuru Mola wake kwa kidogo hicho
alichompa bila ya kujaza fomu ya maombi. Tuelewe na tukiri kuwa Allah
amewafadhilisha katika neema zake baadhi ya waja wake kuliko wengine kwa
sababu, hekima na siri anazozijua yeye mwenyewe: “TAZAMA JINSI
TULIVYOWAFADHILISHA (hapa duniani) BAADHI YAO (viumbe) KULIKO WENGINE; NA
BILA SHAKA AKHERA NI YENYE VYEO VIKUBWA ZAIDI NA VYENYE KUFADHILIANA ZAIDI
(pia)” [17:21] Na hakuna yo yote katika viumbe wake mwenye haki ya
kuhoji ugawaji wake wa neema na fadhila zake kwa waja wake. Kwa hali hii
basi, linalomuelea mja ni kuridhia mgao wa Mola wake na kisha kumshukuru
kwa fungu alilomgawia miongoni mwa neema zake. Na amuombe ziada ya fadhila
na neema zake huku akiamini kuwa: “...HAZINA ZA MBINGU NA ARDHI NI MALI
ZA ALLAH...” [63:7]
Na aamini kuwa Allah hutenda alitakalo na ni Muweza juu ya kila kitu. Haya
na tuukhitimishe wasia wetu huu kwa kumuomba Allah kama alivyoombwa na
Mtume Sulayman-Amani imshukie: “EE MOLA WANGU! NIPE NGUVU
NISHUKURU NEEMA YAKO ULIYONINEEMESHA MIMI NA WAZAZI WANGU, NA NIPATE
KUFANYA VITENDO VIZURI UVIPENDAVYO, NA UNIINGIZE KWA REHEMA YAKO KATIKA
WAJA WAKO WEMA”. [27:19]
|