Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Akhlaaq-Tabia  

"Hakika si vingine nimetumwa kuja kutimiza TABIA NJEMA" Hadith Tukufu

MISINGI YA MAISHA YA NDOA KATIKA UISLAMU

 Faida

 

       I.          Lengo la ndoa:

         Ni ukweli ulio dhahiri shahiri na usiopingika kwamba ndoa ni kifungo (mkataba) kitukufu kilichobarikiwa. Allah Taala amekiratibu na kukifanya sheria kifungo hiki kwa ajili ya maslahi na manufaa ya waja wake ambao ndio walengwa wa kifungo hiki. Wanadamu wameratibiwa kifungo hiki na Mola wao ili waweze kuyafikia malengo mema na shabaha tukufu. Malengo/makusudio mama ya kifungo ndoa ni mawili ambayo ni kupata watoto na kujihifadhi na haramu.

 

LENGO LA KWANZA: WATOTO (KIZAZI):

     Kunalazimu kwa mwenye kutaka kuvaana na kifungo cha ndoa (kuoa/kuolewa), lengo lake la kwanza liwe ni kupata watoto. Ili awe na kizazi chema kitakachomuabudu Allah na kumuombea Mungu baada ya kufa kwake, kitakachoendeleza utajo wake akiwa akhera. Imepokewa kutoka kwa Anas Ibn Maalik-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akituamrisha kuoa na akitukataza vikali kabisa uruhubani na akisema: “Oeni mzazi mwenye kupendeka, kwani hakika mimi nitajifakharisha nanyi siku ya Kiyama”. Siku ya Kiyama Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-atajifakharisha kwa mitume wengine kwa sababu ya wingi wa umati wake. Hii ni kwa sababu Mtume atakayekuwa na umati mkubwa, wingi huo wa umati haumaanishi ila wingi wa thawabu zake. Kwa sababu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anapata mithili ya ujira wa kila amfuataye mpaka siku ya Kiyama. Lengo hili tukufu la ndoa ndilo linaloashiriwa na kauli tukufu ya Allah: “NA ALLAH AMEKUUMBIENI WAKE KATIKA JINSI YENU NA AKAKUJAALIENI KUTOKA KWA WAKE ZENU WATOTO NA WAJUKUU....” [16:72]

      Mwanadamu kwa uhalisia wa maumbile yake kama alivyofinyangwa na Allah Mola Muumba wake ni kiumbe apendaye watoto. Hiyo ni kwa sababu Allah Taala amewapambia watu kupenda watoto, kama alivyosema kupitia kauli yake hii: “WATU WAMETIWA HUBA (mapenzi) YA KUPENDA WANAWAKE NA WATOTO NA MIRUNDI YA DHAHABU NA FEDHA...” [3:14] Mwanadamu anapenda watoto kwa sababu Allah Taala amejaalia watoto kuwa ni pambo la maisha ya dunia, kama alivyosema: “MALI NA WATOTO NI PAMBO LA MAISHA YA DUNIA...” [18:46] Kwa sababu ya kumili mno katika suala la kupenda watoto, mwanadamu anaweza kutumbukia katika fitna/mtihani kwa sababu/ajili yao, hivi ndivyo anavyobainisha Allah Taala: “BILA SHAKA MALI ZENU NA WATOTO WENU NI JARIBIO (kwenu, mtihani kutizamwa mtakhalifu amri za Allah kwa ajili yao au mtafuata amri zake). NA KWA ALLAH KUNA UJIRA MKUBWA” [64:15] Mtihani/fitna hii ya watoto ikimtawala mwanadamu na kumsukuma kutenda haramu mithili ya chumo la haramu ili kuwakimu wanawe hao kimaisha. Au ikamsukuma kuacha kutenda la wajibu mithili ya kuacha kwenda katika jihadi kwa sababu ya kuwachelea wao ikiwa atafia huko watakosa mtu wa kuwaangalia. Watoto katika mazingira kama haya huwa ni mithili ya adui, kwa hivyo ni wajibu wa mja kutahadhari kuwapenda kwa kiwango hiki kiasi cha kuwafanya kuwa ndio kila kitu kwake. Huu ndio ukweli unaolezwa kupitia kauli tukufu ya Allah: “ENYI MLIOAMINI! KWA YAKINI BAADHI YA WAKE ZENU NA WATOTO WENU NI MAADUI ZENU; BASI JIHADHARINI NAO. NA MKIWASAMEHE NA KUPUUZA (yaliyopita) NA KUYAFUTA (kabisa katika nyoyo zenu, basi Allah atafurahi) KWANI ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA KUREHEMU”. [64:14] Imepokewa katika kutaja sababu ya kushuka kwa aya hii, kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-amesema: Aya hii: “KWA YAKINI BAADHI YA WAKE ZENU NA WATOTO WENU NI MAADUI ZENU; BASI JIHADHARINI NAO...”. Imeshuka kwa sababu ya baadhi ya watu wa Makkah waliosilimu, wake na watoto wao wakawazuia kuhamia Madinah. Walipokwenda Madinah kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wakawaona wenzao walio tangulia kuhama wamekwishajua mambo mengi ya dini. Wakataka kuwatia adabu wake na watoto wao hao, kwa ajili hiyo ndio Allah Taala akateremsha kauli yake: “...NA MKIWASAMEHE NA KUPUUZA (yaliyopita) NA 

KUYAFUTA...” Tirmidhiy, Al-Haakim & wengineo-Allah awarehemu.

 

  LENGO LA PILI – KUJIZUIA NA HARAMU (ZINAA):

         Miongoni mwa mambo yasiyokubali kutiliwa shaka ni kuwa miongoni mwa malengo mama ya ndoa ni mwanandoa kujizuia na zinaa na baki ya machafu mengine. Na wala halikuwa lengo la ndoa kwa muumini ni utupu wa kukidhi matamanio ya kimwili tu basi. Tunakubali na wala hatupingi kuwa kukidhi matamanio ndio sababu ya huko kujiepusha na haramu, ni kweli. Lakini tunachosema ni kuwa huko kujihifadhi na haramu (zinaa) hakutafikiwa ila kwa kupatikana nia ya kutinda na kusudio la kweli. Kwa hivyo basi, hakusihi kuyatenganisha mambo mawili haya; kukidhi matamanio na nia/kusudi, kwani mawili hayo kwa upamoja wake ndio humfikisha mwanandoa kujiepusha na haramu. Mwanadamu atakapoyaelekeza makusudio yake yote katika ndoa katika kushibisha tamaa za kimwili na akili yake yote ikaelekezwa katika jimai (tendo la ngono) mara kwa mara. Na wala lengo lake halikuwa ni kuihifadhi nafsi yake na uchafu wa zinaa, basi i wapi tofauti baina yake na baki ya hayawani wengine?! Na ni mara ngapi tumewaona au kuwasikia watu wameoa/kuolewa na bado wakawa wanazini, ni kwa nini?! Kwa mantiki hii, hapana budi wanandoa wawe na lengo tukufu katika kuendesha na kuliendea zoezi lao zima la jimai wanalolifanya ikiwa ni starehe na haki ya kila mmoja wao. Lengo hili tukufu lisiwe lingine zaidi ya kukidhi matamanio ndani ya wigo halali (ndoa) ili wajitosheleze kimaumbile sambamba na kupata kinga dhidi ya uchafu na uoza wa zinaa. Lengo hili ndilo alilotuongozea Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika agizo lake: “Enyi kusanyiko la vijana! Ye yote miongoni mwenu atakayeweza kushi na mke, basi na aoe. Kwani (huko kuoa) kwake kunalifumba zaidi jicho na kunahifadhi mno tupu (na uchafu). Na asiyeweza, basi na ajilazimishe kufunga, kwani huko (kufunga) ni kinga kwake yeye (dhidi ya maasi)”.

Lililo wazi kutokana na hadithi hii ni kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ameiratibia ndoa mambo mawili ya msingi yanayo patikana humo, ambayo ni:

v     Kulifumba jicho dhidi ya kuwaangalia kwa matamanio maovu wanawake wasio halali kwa mtu.

v     Kuihifadhi tupu dhidi ya zinaa na baki ya machafu mengine yafungamanayo na tupu.

Hii ndio maana inayoelezwa na hadithi tukufu iliyopokelewa na Jaabir-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilimsikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema: “Mmoja wenu atakapopendezwa na mwanamke na kumgusa moyo wake, basi na amuendee mkewe amuingilie, kwani (tendo) hilo huzuia (azma ya machafu) iliyoingia nafsini mwake”. Muslim-Allah amrehemu.

Ama wale wanaooa na hima yao yote katika ndoa ikawa ni jimai (kufanya ngono) tu na si vinginevyo. Hawa jimai haitawazidishia cho chote zaidi ya matamanio, kwa sababu hii hawatatosheka na wake zao wa halali na hivyo kuangukia katika haramu.

  | Tuandikie |