|
Sharti za kusihi udhu, haya ni mambo ambayo mwenye kutawadha
ayahakikishe kwanza kabla hajaanza kutawadha, ili udhu wake uweze kusihi na kukubalika
kisheria. Miongoni mwa sharti muhimu kabisa za udhu ni kama zifuatazo :
- Kutokuwepo kizuizi kinachoweza kuyazuiliya maji wakati wa kutawadha kuufikilia
ngozi, kwa sura ya maji kupita juu bila ya kufikilia ngozi. Kizuizi hiki chaweza kuwa ni
mafuta mazito ya mgando, ute wa mshumaa, rangi ya lami, na vitu vyenye kufanana na hivi
tulivyotaja.
- Lisimpate mwenye kutawadha wakati wa kutawadha kwake jambo lenye kuubatilisha na
kuutengua udhu wake, kama vile kutokwa na kitu katika mojawapo wa tupu mbili.
- Maji ya udhu yawe ni TWAHARA na yenye kufaa kutumika kwenye udhu.
- Kutakata mwanamke kutokana na damu ya hedhi na nifasi, kwani udhu hausihi wala
kumpasa mwanamke aliye hedhini au nifasini mpaka atakapotahirika.
- Uislamu wa mwenye kutawadha, kwani udhu si wajibu na wala hausihi kwa asiyekuwa
muislamu, ajapofuata taratibu zote za udhu.
- Kisiwepo juu ya kiungo cha udhu chochote kinachoweza kuharibu mojawapo ya sifa tatu
za maji, ambazo ni tamu (ladha), rangi na harufu. Vitu hivi ni pamoja na vumbi la mkaa,
chokaa, sementi na kadhalika.
viii) YALIYO KARAHA KATIKA UDHU :
- Ni karaha kwa mwenye kutawadha kuacha suna yeyote miongoni mwa suna tulizozitaja
chini ya anuani :{SUNA ZA UDHU}. Kwa sababu kuacha kuzitekeleza suna hizo kutampelekea mtu
huyo kukosa thawabu, na muislamu wa kweli siku zote hupupia kuitekeleza ibada yake kwa
ukamilifu na kwa namna ilivyofundishwa na mwenyewe Bwana Mtume Rehema na Amani
zimshukie-.
- Ni karaha kuyatumia maji kwa israfu {fujo} kama ambavyo ni karaha kujidhili katika
kutumia maji, yaani kutumia kidogo mno yasiyokidhi haja ya udhu kwa ukamilifu. Hayo yote
ni kinyume na suna ya Bwana Mtume na Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia :
. NA
WALA MSIPITE KIASI HAKIKA YEYE (Allah) HAWAPENDI WAPITAO KIASI [7:31]
- Ni karaha kutanguliza kuosha mkono/mguu wa kushoto kabla ya mkono/mguu wa kulia,
kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume na alivyotenda Bwana Mtume Rehema na Amani
zimshukie-.
- Ni karaha kukausha/kufuta viungo vya udhu kwa kutumia leso/taulo. Ukaraha huo
utaondoka kwa udhuru kama vile baridi kali, hapo itakuwa si karaha. Imepokelewa kwamba
Mtume Rehema na Amani zimshukie aliletewa leso/taulo (ili ajifutie) basi
hakuigusa (hakuitumia) Bukhaariy.
- Kuupiga uso kwa maji pia ni miongoni mwa mambo yaliyo karaha katika udhu. Kwa
sababu kitendo hiki kinapingana na utukufu wa uso.
- Ni karaha kuzidisha kuosha au kupakaza zaidi ya mara tatu au kupunguza. Alisema
Mtume Rehema na Amani zimshukie baada ya kwisha kutawadha mara tatu tatu :
Hivi ndivyo (unavokuwa) udhu, basi atakayezidisha zaidi ya hivi au kupunguza huyo
atakuwa amekosea na kudhulumu Abuu Daawoud.
- Ni karaha mtu kuoshwa viungo na mtu mwingine bila ya kuwa na udhuru ukubalikao kama
ugonjwa. Hili limefanywa kuwa ni karaha na sheria kwa sababu ndani yake mna chembechembeza
kibri na ubwana, vitu ambavyo vinapingana na uja/utumwa kwa Mwenyezi Mungu.
- Ni karaha kwa aliyefunga kuyapeleka ndani sana maji katika kusukutuwa na kupandisha
maji puani. Hii ni kwa sababu ya kuchelea kumponyoka maji na kufika kooni yakaingia ndani
na hivyo kusababisha kufisidika/kuharibika swaumu yake. Amesema Mtume wa Allah
Rehema na Amani zimshukie Na balighisha (yapeleke maji ndani sana)
katika kupandisha maji puani, ila ukiwa umefunga (usibalighishe) Abuu Daawoud.
TANBIIH : Ikiwa imekatazwa kubalighisha katika kupandisha maji puani
kwa mfungaji, basi kubalighisha katika kusukutua ni bora zaidi kukatazwa.
ix) VITENGUZI VYA UDHU :
Haya ni yale mambo ambayo mojawapo miongoni mwake
likimtokea/kumpata mtu mwenye udhu, litasababisha kubatilika kwa udhu wake huo na
kuhesabika mbele ya sheria kuwa ni MUHDITH (hana udhu). Kwa mantiki hii itamuwajibikia
kutawadha tena ikiwa anataka kuyatenda yale ambayo kisheria haruhusiwi kuyatenda pasina
udhu. Vitenguzi vya udhu ni vitano kama ifuatavyo :
- Kila kilichotoka katika mojawapo wa njia mbili; ya mbele au ya nyuma. Ni sawasawa
hicho kilichomtoka ni mkojo, mavi, damu au ushuzi. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu :
..AU MMOJA WENU AMETOKA CHOONI
.[5:6],[4:43]. Yaani ametoka
kukidhi haja yake. Naye Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie amesema
Allah haikubali swala ya mmoja wenu atakapohuduthi (atakapotengukwa na udhu) mpaka
atawadhe (tena) Mtu mmoja wa Hadharamout {Mji katika Yemen-aliyekuwepo wakati Abuu
Hurayrah akiipokea hadithi hii) akauliza : Hiyo hadathi {iliyotajwa katika hadithi) ni
nini ?, Akajibu ni ushuzi.
TANBIIH : Kisia/kadiria kwa haya
yaliyotangulia kila kitokacho katika tupu ya mbele au nyuma, hata ni twahara kilichotoka.
- Kulala usingizi mzito ambao kuwa anakuwa hana hisia kabisa na akawa amelala pasina
kuyaambatisha matako yake na ardhi, kiasi cha kuruhusu chochote kuweza kumtoka bila kuhisi
khasa ushuzi. Ushahidi wa hili ni kauli ya Mtume Rehema na Amani zimshukie
Atakayelala (akiamka) basi na akatawadhe Abuu Daawoud na wengineo. Ama ule
usingizi mwepesi ambao mtu anakuwa anazo hisia zake na akawa amekaa mkao wa kuwambisha
matako yake na ardhi, huu hautengui udhu kwa sababu atahisi kitakachomtoka. Ushahidi wa
hili ni riwaya ya Anas ibn Maalik Allah amuwie radhi isemayo : ilikimiwa
swala na il-hali Mtume Rehema na Amani zimshukie akinongona na mtu,
akaendelea kunongona naye mpaka wakalala maswahaba wake, kisha (Mtume) akaja na
kuwaswalisha. Muslim. Itabainika kutokana na riwaya hii kwamba Maswahaba walilala hali ya
kuwa wamekaa mkao wa uwambishaji. Hii ni kwa sababu walikuwa msikitini wakingojea swala
huku wakitumai kuwa Bwana Mtume atakata mazungumzo yake na kuja kuswalisha.
- Kuondokewa/kutokwa na akili kwa sababu ya uwendawazimu, kuzimia, kulewa (kwa namna
yoyote ile iwayo) au kwa kutumia madawa ya kulevya. Ni mamoja ikiwa alitumia vitu hivi kwa
kukusudia au bila ya kusudia, udhu utatenguka tu. Hii ni kwa sababu vitu hivi huiondosha
akili ya binadamu na hivyo kumfanya akose hisia za kuweza kutambua kinachomtokea. Hii
inakadiriwa na kulala.
- Mwanamume kumgusa mkewe au mwanamke wa kando pasina kizuizi, yaani wamegusana ngozi
kwa ngozi, hapo utatenguka udhu wa wote wawili; mgusaji na mguswaji. Mwanamke wa kando,
huyu ni kila mwanamke ambaye kisheria ni halali kumuoa, hakuna uharamu baina yao. Amesema
Mwenyezi Mungu Mtukufu
.AU MMEWAGUSA WANAWAKE
[4:43]
- Kugusa utupu (uchi) wake au wa mtu mwingine hata kama ni mtoto mdogo au maiti kwa
matumbo ya kiganja chake au matumbo ya vidole vyake pasina kizuizi. Dalili juu ya hili ni
kauli ya Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie Atakayeigusa dhakari
yake, basi asiswali mpaka akatawadhe (tena) Tirmidhiy.
|