|
i) WEPESI WA UISLAMU NA MAANA YA KUTAYAMAMU
Tumekwishajua kutokana na maelezo ya masomo yaliyopita kwamba udhu ni sharti ya
kusihi kwa swala, tawafu (ibada ya kuizunguka Al -kaabu), kuushika na kuuchuka/kuubeba
msahafu. Kadhalika tumefahamu kuwa udhu hupatikana kwa kutumia maji katika viungo
makhsusi. Sote tunakubaliana na hakika/ukweli kuwa mwanadamu kama viumbe hai wengine ni
viumbe mwenye tabia ya kubadilika kutoka hali moja kwenda katika hali nyingine iliyo
tofauti na ile ya mwanzo au kutoka katika mazingira hadi mengine. Sasa kwa kuizingatia
kanuni/sheria na tabia hii ya kimazingira, inawezekana kabisa ikamtokea mwanadamu hali au
mazingira ambayo atashindwa kuyatumia maji kwa ajili ya udhu au josho. Anaweza akayakosa
maji katika maeneo aliyomo wakati ule, au maji yakawa yanapatikana maeneo ya mbali sana na
ikamuwia taabu kuyafikia, au akawa na maradhi ambayo yanamzuilia kutumia maji katika hali
na mazingira kama haya, muislamu afanye nini na ilhali imemlazimu kuitekeleza ibada ya
swala na ni maalum kuwa ibada hii haitekelezeki bila ya kuwa na udhu. Sasa je, aache
kuswali kwa sababu ya kukosa au kushindwa kuyatumia maji ? Au ayatumie maji hata kama
yanamdhuru ili apate udhu utakaomuwezesha kuswali ? La, hasha ! Hapo sasa ndio inaonekana
kazi ya msingi miongoni mwa misingi ya fiq-hi ya kiislamu usemao: "HAPANA KUDHURU
(MTU) WALA KUJIDHURU MWENYEWE." Kutokana na msingi huu tumeelewa kuwa kumbe hakuna
katika Uislamu kujitia katika madhara kwa sababu ya kuutekeleza Uislamu. Msingi huu si
dhana tu iliyosimikwa na kuwekwa na wanazuoni bali unaitegemea kauli ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu:
"
WALA MSIJITIE KWA MIKONO YENU KATIKA MAANGAMIZO
" [2:195].
Kupitia msingi huu ndipo unapojitokeza na kuonekana wepesi wa dini na mfumo huu
sahihi wa maisha unaokwenda sambamba na hali, tabia na mazingira ya mwanadamu. Katika hali
na mazingira kama hayo ndio uislamu ukamuwekea mwanadamu huyu sheria ya kutayamamu kwa
kutumia mchanga tahara badala ya kutumia maji katika udhu au josho. Uislamu umetoa ruhusa
hiyo ili kumpa fursa mwanadamu huyu ya kuitekeleza ibada bila ya tabu au madhara na kuziba
mwanya wa kuacha kutekeleza ibada kwa kisingizio cha kukosa maji au maradhi yanayozuia
utumiaji wa maji. Amesema kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu:
"
ALLAH ANAKUTAKIENI YALIYO MEPESI NA WALA HAKUTAKIENI YALIYO MAZITO ..."
[2:185]
Tusome tena ili tuzidi kuuona wepesi wa Uislamu
"
.HAPENDI ALLAH KUKUTIENI KATIKA TAABU .." [ 5:6]|
"
WALA HAKUWEKA JUU YENU MAMBO MAZITO KATIKA DINI ." [22: 78]
Baada ya kuona ni jinsi gani uislamu ulivyomuwekea muislamu mazingira mepesi
katika kuutekeleza uislamu. Hebu sasa tujaribu kuiangalia tayamamu kwa ujumla, tukianzia
na maana ya kutayamamu.
Tayamamu ni neno la Kiarabu ambalo tumezoea kulitamka kama "kutayamamu".
Neno hili lina maana mbili zifuatazo:
Maana ya kilugha: Katika lugha ya Kiarabu neno tayamamu lina maana ya kukusudia.
Maana ya kisheria: Kutayamamu ni kupakaza vumbi la mchanga twahara katika uso na
mikono kwa utaratibu maalum uambatano na nia.
(ii) HUKUMU NA DALILI YA KUTAYAMAMU
Kutayamamu ni WAJIBU/FARDHI kwa mtu katika hali mbili:
1: Wakati atakapoyakosa maji ya kutawadhia.
2: Wakati atakaposhindwa kuyatumia maji kwa sababu zilizobainishwa na sheria.
Kutayamamu kumethibiti katika Qur-ani Tukufu, Sunnah na Ijmaa. Dalili ya
kutayamamu katika Qur-ani ni kauli tukufu ya Mwenyezi Mungu: "............ NA MKIWA
WAGONJWA AU MMO SAFARINI, AU MMOJA WENU AMETOKA CHOONI AU MMEINGILIANA NA WANAWAKE NA
HAMKUPATA MAJI, BASI KUSUDIENI (tayamamuni) UDONGO (mchanga) ULIO SAFI (twahara) NA
KUUPAKA NYUSO ZENU NA MIKONO YENU
" [5:6].
Tayamamu katika Suna imo katika kauli ya Bwana Mtume Rehema na Amani
zimshukie aliposema : "
.na tumejaaliwa (tumefanyiwa) ardhi yote kuwa ni
msikiti (mahala pa kuswalia) na mchanga (udongo) wake umefanywa kwetu ni twahara
(utwahirishayo) tutakapokuwa hatukupata maji". Muslim.
Ama Ijmaa, wanazuoni wote wamekogomana na kukubaliana kuwa tayamamu imefanywa kuwa
ni sheria, itumike badala ya ya udhu na josho katika hali na mazingira maalum
yaliyobainishwa na sheria.
Hiyo ndiyo tayamamu ndani ya Qur-ani, Sunnah na Ijmaa.
(iii) FALSAFA NA HEKIMA YA KUTAYAMAMU
Kutayamamu kumefanywa kuwa ni sheria miongoni mwa sheria za uislamu ili kumfanya
muislamu aweze kuitekeleza ibada katika hali na mazingira mbalimbali yanayomzunguka. Apate
wepesi katika kulitekeleza lengo la kuumbwa kwake ambalo ni ibada kwa maana halisi ya neno
hilo. Tayamamu ni hadiya na zawadi ya Mola kwa umati Muhammad, sheria hii haikuwepo katika
nyumati zilizoutangulia uma huu. Haya yanathibitishwa na kauli ya Bwana Mtume
Rehema na Amani zimshukie: "Nimepewa (mambo) matano, hakupata kupewa mtume yeyote
kabla yangu; Nimenusuriwa na khofu kitambo cha mwezi mzima, na nimefanyiwa ardhi kuwa ni
msikiti na twahara, basi popote pale mtu katika umati wangu itakapomdiriki swala na
aswali. Na nimehalalishwa ngawira na hazikuhalalishwa kwa heyote kabla yangu, na nimepewa
shafaa (uombezi kwa watu). Mtume alikuwa akipelekwa kwa watu wake tu na mimi nimepelekwa
kwa watu wote." Bukhaariy na Muslim. Itakuwazikia kutokana na hadithi hii ya Bwana
Mtume kuwa kutayamamu ni fursa maalumu ya upendeleo uliyopewa muislamu na Mola wako ili
kukuwepesishia utekelezaji wa ibada zako.
(iv) NAMNA YA KUTAYAMAMU
Kwa kuwa tayari tumeshathibitisha kwamba tayamamu ni sheria katika uislamu, sheria
hii haikuachwa ielee angani na kumpa fursa kila mtu aitekeleze kwa mujibu wa matakwa na
matashi yake. Sheria hii imewekewa utaratibu maalumu wa kuitekeleza na mwenyewe Mwenyezi
Mungu na kubainisha na Bwana Mutume kiutendaji. Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia ndani ya
Qur-ani: "
. BASI KUSUDIENI (tayamamuni) UDONGO (mchanga) ULIO SAFI
(twahara) NA KUUPAKA NYUSO ZENU NA MIKONO YENU
.
.." (5:6).
Haya ni maelekezo na maelezo ya jumla kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia
tutayamamu kwa kutumia mchanga, tuzipakaze nyuso na mikono yetu. Swali linajitokeza
tupakaze vipi, namna ya upakaji inakuwa je ? Hapa sasa ndipo inapoonekana nafasi na
umuhimu wa Bwana Mtume na kwamba bila yeye dini hii haieleweki na wala haitekelezeki. Yeye
ndiye aliyetoa maelezo na kuonyesha namna ya kutayamamu mbele ya maswahaba ili kuitekeleza
kiutendaji aya hiyo na kuufundisha uma jinsi ya kuitekeleza sheria hii ya tayamamu. Sasa
basi ili tayamamu ya mtu ikubalike kisheria ikiwa ni pamoja na ibada atakayoifanaya kwa
tayamamu hiyo ni lazima ahakikishe kuwa anatayamamu kwa mujibu wa utendaji na maelekezo ya
Bwana Mtume. Ifuatayo ndiyo namna ya kutayamamu kama alivyofundisha Bwana Mtume:-
Kwanza kabisa andaa mafungu/marundo mawili ya mchanga ulio twahara. Halafu elekea
Qibla, sema; BISMILLAAH, piga mikono yako juu ya fungu moja la mchanga huku ukisema moyoni
mwako NAWAYTUS TIBAAHATI FARDHWIS SWALAA
Kunguta mchanga kidogo na upakaze uso wako kwa mikono yote miwili vumbi
lililobakia katika vitanga hivyo kama unavyouosha uso katika udhu. Halafu piga tena kwa
vitanga vyako katika lile fungu la pili la mchanga, kunguta mikono yako kidogo.
Kisha upakaze mkono wa kulia kwa mkono wa kushoto na upakaze ule wa kushoto kwa mkono wa
kulia. Zingatia kupakaza vumbi ni mara moja moja tu na sio mara tatu kama ilivyo katika
kutawadha.
|