Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Fiqh na Sheria  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

HEKIMA/FALSAFA YA KUOA ZAIDI YA MKE MMOJA

Faida

 

     02.     Hekima/Falsafa ya kuoa zaidi ya mke mmoja:

         Hakika Uislamu umeruhusu kuoa zaidi ya mke mmoja kiasili na wala haukulifanya jambo hilo kuwa ni FARADHI iliyo lazimu. Na kwa yakini Uislamu, umeruhusu huku kuoa zaidi ya mke mmoja, kwa kuwa unalenga malengo ya mbali katika utengenefu wa jamii. Hayadiriki kuyatambua malengo hayo ila yule mwenye uoni mpevu, hizi hapa ni baadhi tu ya hikma/falsafa:

                     1.       Kwa kuruhusu kuoa zaidi ya mke mmoja, Uislamu umelenga kumuhami/kumsitiri yule asiye toshelezwa na mke mmoja. Na hilo ni jambo la kimaumbile, linaweza kumsukuma kutenda yale yasiyo pendelewa na sharia.

Basi lililo bora kwao hawa wasio tosheka na mke mmoja na kwa jamii, ni wao hawa kuoa mke mwingine kuliko kujitumbukiza katika uchafu wa zinaa.

                     2.       Hali kadhalika Uislamu unalenga kumuhifadhi mwanamke kuzengewa na wanaume wenye kuburuzwa na matamanio yao, si kwa ndoa itakayo walinda watoto wake. Bali kwa njia ya uchafu na uhawara ambayo humfanya mwanamke huyo kuwa dango la kutupwa na kunyimwa haki zote. Na kuwafanya watoto wake alio wazaa katika njia hiyo, kuwa wanyimwa wa haki za nasabu, na huruma ya ubaba.

Basi mwanamke huyu kuwa mke wa pili (mwenza) aliye na haki na heshima ni bora kwake mara alfu kuliko kuwa mjane au hawara.

Kwa hivyo basi, lengo la Uislamu katika kuruhusu kuoa zaidi ya mke mmoja ni kumuhifadhi mwanamke dhidi ya zinaa. Na wakati huo huo kumlinda mwanamke dhidi ya kuwa muhanga wa matendo machafu ya wanaume waovu wasio na soni wala haya. Na hali kadhalika kuilinda jamii dhidi ya fisadi na mmomonyoko wa kimaadili na uenda hovyo.

 

 i.          Sababu pelekeshi katika kuoa zaidi ya mke mmoja:

         Ziko sababu ambazo zinaifanya sharia ya kuoa zaidi ya mke mmoja kuwa ni suala lenye hekima iliyo dhaahiri na faida iliyo wazi. Na ili uelewe vema hili tunakupigia baadhi ya mifano:

             1.     Mwanaume mwenye umeo na wanawake ana mke mwenye ukinaifu na wanaume, ama ni kwa sababu ya maumbile au maradhi.

Basi je, lililo bora ni huyu mwanaume kuzini, ikapotea dini, mali na siha yake? Au abakie na haja yake huku akiiadhibu nafsi yake? Au aoe mke mwingine kwa sharti ya kumudu familia na kufanya uadilifu na kutofanya dhulma katika tangamano?

Hapana shaka kwamba hili la tatu ndilo bora zaidi kwa huyu mwanaume na ndilo lenye manufaa mno kwa jamii.

             2.     Mfumuko wa vita duniani ambavyo leo vimekuwa ni sehemu isiyo epukika ya maisha ya wanaadamu. Vita hivi vimeyagharimu na vinaendelea kuyagharimu maisha ya wanaume maelfu kwa maelfu. Matokeo yake ni kuzidi idadi ya wanawake kuliko ile ya wanaume kwa kiwango kikubwa.

Basi je, lililo bora kwa wanawake ni mwanaume kuoa mke mmoja tu na wanawake wengine wasalie wakiwa wamenyimwa huruma ya mume mlezi wa familia?! Na wakiwa wamekosa fursa ya kuzaa mtoto atakaye wasaidia katika utu uzima wao?! Haya ni miongoni mwa ambayo yanaweza kumsukuma kutenda dhambi na kutumbukia kwenye machafu ili kuishibisha haja yake. Au lililo bora ni kumruhusu mwanaume kujikusanyia zaidi ya mke mmoja chini ya kivuli cha uangalizi kamili wa kisheria?!

Hakika sisi hatutakuwa tumeidhulumu mantiki na haki, kwa chochote, tutakapo sema: Hakika kuoa zaidi ya mke mmoja katika hali/mazingira haya, kunazingatiwa kuwa ni kitendo cha ubinaadamu/utu kinacho faradhishwa na murua na ghera. Na wala hatutakuwa tunapingana na hali ilivyo, tutakapo sema: Hakika uoaji wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wa zaidi ya mke mmoja, sehemu yake kubwa ilikuwa ni kwa namna hii tukufu ya utu. Baadhi ya wakeze kuna ambaye alihajiri peke yake na kuwaacha jamaa zake, na yupo aliye fiwa na mume wake hali ya kuwa ni shahidi na kumuacha mjane asiye na mwangalizi. Mtume wa Allah akampunguzia uzito wake na akamkusanya nyumbani kwake na akawa kwake yeye ni msimamizi/muangalizi bora. Naye akapata sharafu ya umama wa waumini na fadhila ya kuungana na Bwana wa mitume.

             3.     Mtu amemuoa mwanamke wanaye pendana, lakini mwanamke huyu ni tasa hazai, naye anatamani kupata mtoto. Basi je, lililo bora ni sisi kumzuia mtu huyu kuoa mke wa pili na kumuacha akiwa mpweke wa moyo asiye na mwana?! Au tumuamuru amtaliki mke wake anaye mpenda au tumruhusu kuoa mke mwingine pamoja na kumuhami yule wa kwanza kudhulumiwa?! Hakika hili la mwisho ndilo suluhisho bora kuliko yote yaliyo tangulia, kwani ndilo lililo chunga maslahi ya mwanaume na mwanamke kwa kiwango sawa.

             4.     Hakika mataifa na jamii ambazo zimeharimisha kuoa wake wengi, zimetumbukia ndani ya khatari kubwa na madhara makubwa mno kuliko hayo madhara ya kuoa wake wengi kama wanavyo dai. Ni ukweli usio kanushika kwamba fisadi imekithiri katika mataifa/jamii hizo na kumeenea humo kuendeana kinyume baina ya wanandoa na nyumba ndogo za siri. Mambo haya yamewafanya wenye akili/busara wao kupaaza sauti za kutaka kuweko na sheria inayo ruhusu ndoa ya wake wengi na kondosha fisadi hizo zinazo damirisha (angamiza) maisha yao ya kijamii.

 

Tanbihi:

         Hakika utumiaji mbaya wa ruhusa ya kuoa zaidi ya mke mmoja wa baadhi ya watu majahili, hauifuti hekima/falsafa ya Uislamu na wala Uislamu haubebi zigo la ujahili wa majahili hao. Kwani Uislamu haukuruhusu kuoa zaidi ya mke mmoja ili iwe ni silaha ya kujeruhia, kuchinjia au tangamano ovu. Hakika si vinginevyo, Uislamu umelifanya hilo kuwa sharia kwa ajili ya kukidhi haja, kuilinda jamii, kumchunga mtu mmoja mmoja na kundosha maovu/uchafu.

Kwa sababu zote hizo pelekeshi na sharti hizo za kisharia, ndio Uislamu ukaruhusu kuoa zaidi ya mke mmoja na wala haukuliwajibisha hilo kwa njia ya lazima. Na Uislamu ukaizungushia ruhusa hiyo dhamana tabia za kihaki. Kwa maelezo haya, Uislamu umefanana mno na duka la dawa lililo sheheni dawa zote zinazo kidhi haja za watu wote. Kila mmoja anajitwalia dawa inayo wafikiana na haja na maradhi yake. Na si jambo linalo ingia akilini kuruhusu dawa zote zilizomo humo kwa kila mtu hata pasina haja.

   


 


| Tuandikie |