Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Fiqh na Sheria  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

TATU : POSA

Faida

Tatu: Posa.

         Kukitimia na kuaminika na sifa njema na ikathibiti radhi na raghba, kwa kuona/kuangalia, hapo ndipo inapo kuja zamu ya posa. Na posa maana yake ni zile harakati na kitendo cha mwanaume (mposaji) kutaka ndoa kwa upande wa mwanamke (mposwaji).

Ni wakati gani kunahalalika kupeleka posa na wakati gani kunaharimika:

    1.          Kunahalalika kuposa kwa ufumbulizo (waziwazi) na kwa fumbo (ishara) pindi atakapo kuwa mwanamke anaye poswa hayuko katika ndoa, eda na vizuizi vyote vya ndoa ambavyo tayari vimetajwa katika kipengele cha “WANAWAKE WALIO HARAMU KUWAOA”.

    2.          Kunahalalika kuposa kwa fumbo tu na si kwa ufumbulizo, pindi atakapo kuwa mwanamke mlengwa yumo katika eda ya kufiwa au talaka baini (tatu). Allah Ataadhamiaye amesema: “WALA SI VIBAYA KWENU KATIKA KUPELEKA POSA KWA ISHARA TU KWA WANAWAKE WALIOMO EDANI AU MKADHAMIRIA KATIKA NYOYO ZENU. ALLAH ANAJUA KWAMBA NYINYI MTAWAKUMBUKA. LAKINI MSIWAAHIDI KWA SIRI, ILA MNENE MANENO MEMA. WALA MSIAZIMIE KUFUNGA NDOA MPAKA EDA IFIKE MWISHO WAKE. NA JUENI KWAMBA ALLAH ANAJUA YALIYOMO KATIKA NAFSI ZENU. BASI TAHADHARINI NAYE. NA JUENI KWAMBA ALLAH NI MWENYE KUSAMEHE NA MPOLE”. [02:235]

    3.          Ni haramu kupeleka posa kwa fumbo na ufumbulizo katika hali/mazingira ambayo hayakutajwa katika nambari moja na mbili.

Kwa kuyajengea hayo basi, ni haramu kumposa mwanamke ambaye bado yuko katika hifadhi ya mume wake. Kama kunavyo harimika kumposa kila mwanamke aliye chini ya kipengele cha “WANAWAKE WALIO HARAMU KUWAOA”. Ni mamoja umekuwa uharamu huo ni wa milele au ni muda tu.

Na ni haramu kumposa mwanamke aliye katika eda ya talaka rejea (moja/mbili). Ni mamoja imekuwa posa hiyo ni ufumbulizo au fumbo, kwa kuwa bado ni mke au yumo katika maana ya mke. Hii ni kwa sababu mume wake anayo haki ya kumrejea, Allah Atukukiaye amesema: “...NA WAUME WAO WANA HAKI YA KUWAREJESHA KATIKA MUDA HUO, KAMA WAKITAKA KUFANYA SULUHU...” [02:228] – Yaani na waume zao wanayo haki kuwarejea katika ule muda wa eda. Na waume wanapo tumia haki hiko wakusudie kupatana na si kudhuru.

 

Maana ya kufumbuliza posa:

         Ufumbulizo katika posa, maana yake ni: Kila tamko linalo tinda katika kuonyesha waziwazi nia ya kuoa. Kama vile mwanaume kumwambia mwanamke: “Ninataka kukuoa”, au “Eda yako itakapo malizika nitakuoa”.

 

Maana ya kufumba/kuashiria posa:

         Kufumba posa maana yake ni: Ni mwanaume kutumia tamko ambalo linalo beba kwa pamoja dhamira ya kuoa na kitu kingine. Kama vile kumwambia mueda (mwanamke aliye edani): “Wewe ni mrembo” au “Huenda yuko akutakaye” au “Nani  atampata mwanamke kama wewe” na mfano wa kauli kama hizi.

 

Posa juu ya posa:

         Ni haramu mtu kupeleka posa juu ya posa ya ndugu yake (mwenzake) ikiwa amekwisha pewa jibu la ufumbulizi, ila kwa idhini. Hivi ndio kusema kuwa, ikiwa mtu ameposa mahala na ikawa amekwisha jibiwa, basi ni haramu mtu mwingine nae kwenda kuposa mahala pale pale ila kwa idhini ya mtangulizi katika posa.

Angalia, ikiwa hakujibiwa, basi si haramu mtu mwingine kupeleka posa. Na uharamu huu ulio tajwa ni ule uharamu unao pasisha kupata dhambi na wala haupasishi kubatilika kwa kifungo cha ndoa. Hii ni katika sura ambayo atakapo posa juu ya posa ya mwenzake, akakubaliwa na akaoa.

Dalili ya uharimisho huu, ni kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Asipose mtu juu ya posa ya ndugu yake (muislamu mwenzake), mpaka aache mposaji wa kabla yake au huyo mposaji ampe idhini”. Bukhaariy [4848] & Muslim [1412]-Allah awarehemu.

 

Hukumu ya kutaka ushauri katika kumjua mposaji au mposwaji:

         Mtu atakaye takwa ushauri utakao pelekea kumjua mposaji au mposwaji, kumemuwajibikia kutaja aibu na mabaya anayo yajua kwa ukweli ili wapate kuchukua tahadhari. Kufanya hivyo ni kutoa nasaha na wala hilo halihesabiki kuwa ni katika jumla ya usengenyi ulio harimishwa. Hivi ni iwapo kutajitokeza haja ya kutaja aibu/kasoro. Ama pakiondoshwa bila ya kuyataja hayo, mathalan mtu kusema: “Mwanaume huyu hakufai” au “Mwanamke huyu hakufai”, kumewajibika kutosheka na kauli hiyo.

Dalili ya hukumu hii, ni hadithi ya Bi. Faatimah Bint Qays-Allah amuwiye radhi-kwamba yeye alimwambia Mtume-Rehema na Amani zimshukie: Hakika Muawiyah Ibn Abu Sufyaan na Abu Jahm, wote wawili wameniposa. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Ama Abu Jahm, huyu yeye habandukani na fimbo yake (mkali) na Muawiyah ni hohehahe; hana mali. Olewa na Usamah Ibn Zaid”. Sikumpenda (Usamah). Kisha (Mtume) akasema: “Olewa na Usamah”. Basi nikaolewa nae. Allah akanijaalia kheri nyinyi kwake...” Muslim [1480] & Tirmidhiy [1135]-Allah awarehemu.

 

Walii kutangaza kuwa anaye binti wa kuolewa kwa watu wema wenye uchaMngu:

         Kumesuniwa kwa walii wa mwanamke ambaye anataka kumuoza, kumtangazia kuolewa kwa watu wema, wacha-Mngu. Kufanya hivyo ni kuiga na kufuata kile alicho kifanya Mtume Shuaib kwa Mtume Musa-Rehema na Amani ziwashukie. Pale alipo mtangaza binti yake kwake kwa sababu ya uaminifu wake na kujizuia kwake na machafu. Amesema Allah Atukukiaye katika kukihadithia iisa hicho: “AKASEMA: MIMI NATAKA KUKUOZA MMOJAWAPO KATIKA BINTI ZANGU HAWA WAWILI KWA KUNITUMIKIA MIAKA MINANE. UKITIMIZA KUMI KHIARI YAKO; LAKINI MIMI SITAKI KUKUTAABISHA. INSHALLAH, UTANIKUTA MIUONGONI MWA WATU WEMA. MUSA AKASEMA: HAYO YAMEKWISHA KUWA BAINA YANGU NA WEWE. MUDA MMOJAPO NIKIUMALIZA SITIWI UBAYANI. NA ALLAH NI MLINZI JUU YA HAYA TUNAYO YASEMA”. [28:26-28]

Na pia kwa ajili ya kuiga alicho kifanya Sayyidna Umar Ibn Al-Khataab-Allah amuwiye radhi-pale alipo mtangaza binti yake Hafsah kwa Sayyidna Uthman, kisha kwa Sayyidna Abu Bakri-Allah awawiye radhi wote. Mwisho wa mzunguko huo akaja kuolewa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

   


 


| Tuandikie |