Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Fiqh na Sheria  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

SUNNA ZA POSA

Faida

Suna za Posa:

         Kunasuniwa kwa mposaji au wakili wake, kutanguliza khutuba kabla ya kuleta tamko la posa na kabla ya kifungo cha ndoa. Aianze hiyo khutba kwa kumuhimidi Allah na kisha kumswalia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Hayo ni kwa mujibu wa hadithi isemayo: “Kila jambo jema lisilo anzwa kwa kumuhimidi Allah, basi jambo hilo ni lenye kukatika (baraka)”. Ibn Maajah [1894]-Allah amrehemu. Baada ya kumuhimidi Allah, ausie kumcha Allah, halafu ndipo ayadhihirishe matashi yake kwa kusema: Nimekujilieni kumposa binti yenu.

Pia kunasuniwa kwa walii wa mposwaji (binti/mwanamke), nae kukhutubu na kusema baada ya kumuhimidi Allah, kumswalia Mtume na kuusia kumchaMngu: Wewe si mwenye kukataliwa.

Na khutba itolewayo kabla ya kufungwa kwa ndoa, imekokotezwa mno kuliko ile khutba itolewayo kabla ya posa. Kwa sababu ya kupokelewa hilo kwa Salafu wema-Allah awawiye radhi.

Maimamu-Allah awawiye radhi-wametabaruku kwa yaliyo pokewa kutoka kwa Ibn Masoud-Allah amuwiye radhi-amesema: “Atakapo taka mmoja wenu kukhutubu kwa haja ya ndoa au jambo jinginelo, basi na aseme: INNAL-HAMDA LILLAAH, NAHMADUHU WANASTA’INUUHU WANASTAGHFIR-HU. WANAUDHU BILLAAHI MIN SHURUURI ANFUSINAA WASAYYIAATI A’AMAALINAA. MAN YAHDIHIL-LAAHU FALAA MUDHWILLA LAHU, WAMAN YUDHWLIL FALAA HAADIYA LAHUU. WA ASH-HADU AN LAA ILAAHA ILLAL-LAAHU WAHDAHU LAA SHARIYKA LAHUU. WA ASH-HADU ANNA MUHAMMADAN ABDUHU WA RASUULUH. {YAA AYYUHAL-LADHIYNA AAMANUT-TAQUL-LAAH HAQQA TUQAATIHI WALAA TAMUUTUNNA ILLA WA ANTUMUM-MUSLIMUUN}. {YAA AYYUHAN-NAASUT-TAQUU RABBAKUMUL-LADHIY KHALAQAKUM-MIN NAFSIN WAAHIDAH, WA KHALAQA MIN-HAA ZAUJAHAA WA BATTHA MIN-HUMAA RIJAALAN KATHIYRAA WA NISAA. WAT-TAQUL-LAAHAL-LADHIY TASAALUUNA BIHII WAL-ARHAAM, INNALLAAH KAANA ALAYKUM RAQIYBA}. {YAA AYYUHAL-LADHIYNA AAMANUT-TAQUL-LAAH WAQUULUU QAULAN SADIYDAN. YUSWLIH LAKUM A’AMAALAKUM WAYAGHFIR LAKUM DHUNUUBAKUM. WAMAN YUTWI’IL-LAAH WA RASUULIHI FAQAD FAAZA FAUZAN ADHWIYMA}.

Tafsiri ya khutuba:

“Hakika himidi zote njema ni zake Allah, tunamuhimidi Yeye, tunamuomba msaada na tunamtaka maghufira Yeye. Na tunajilinda kwa Allah kutokana na shari ya nafsi zetu na matendo yetu maovu (mabaya). Aongolewaye na Allah, basi hapana wa kumpoteza. Na ampotezaye, basi hapana wa kumuongoa.

Na ninashuhudia kwamba hapana Mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah peke yaka, hana mshirika. Na ninashuhudia kwamba Muhammad ni mja na mjumbe wake.

“ENYI MLIOA AMINI! MCHENI ALLAH KAMA IPASAVYO KUMCHA; WALA MSIFE ILA NANYI NI WAISLAMU”. [03:102]

“ENYI WATU! MCHENI MOLA WENU MLEZI ALIYE KUUMBENI KUTOKANA NA NAFSI MOJA, NA AKAMUUMBA MKEWE KUTOKA NAFSI ILE ILE. NA AKAENEZA KUTOKANA NA WAWILI HAO WANAUME NA WANAWAKE WENGI. NA TAHADHARINI NA ALLAH AMBAYE KWAYE MNAOMBANA, NA JAMAA ZENU. HAKIKA ALLAH NI MWENYE KUWAANGALIENI”. [04:01]

“ENYI MLIO AMINI! MCHENI ALLAH NA SEMENI MANENO YA SAWA SAWA. APATE KUKUTENGENEZEENI VITENDO VYENU NA AKUSAMEHENI MADHAMBI YENU. NA ANAYE MT’II ALLAH NA MTUME WAKE, BILA YA SHAKA AMEFANIKIWA MAFANIKIO MAKUBWA”. [33:70-71]

 

Hukumu ya wachumba kukaa faragha na kuchanganyika pamoja kabla ya ndoa:

         Ni jambo lililo tangaa na kuenea katika baadhi ya familia za Kiislamu, familia zilizo mbali na uelewa wa Uislamu katika wigo wa ndoa. Kwamba mposaji akisha leta posa tu, tayari anakuwa huru kukaa faragha, kuchanganyika na hata kuwa na matembezi ya pamoja na mchumba wake. Haya yanafanyika chini ya mwavuli wa kile kinacho itwa “kuzoena na kufahamiana kitabia”. Zoezi hili linafanyika kwa kila mmoja wao kujitahidi kujivika na kujipamba sifa/tabia ambazo si za uhalisia wake, ili tu kumuonyesha mwenzake kuwa yeye ndiye chaguo lake halisi, sahihi na stahiki.

Kwa janibu ya sharia inayo randana sawa na maumbile ya mwanaadamu, hakika kadhia ya wachumba kuchanganyika na kukaa faragha pamoja. Ni jambo lililo harimishwa na wala si tu haliridhiwi na Allah na Mtume wake, bali hata na akili ya kawaida tu. Katika hili Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anatuongoza kwa kusema: “Mwanaume asikae faraghani na mwanamke ila awe pamoja nao maharimu”. Bukhaariy [4935] & Muslim [1341]-Allah awarehemu.

Chini ya mwangaza wa sharia ya Kiislamu, binti/mwanamke mchumbiwa/mposwaji kabla ya kufungwa kwa ndoa, huzingatiwa kama mwanamke ajinabiya na hivyo kuchukua hukumu zake zote.

Ama baada ya kufungwa na kusihi kwa kifungo cha ndoa, hapo tena faragha na mchanganyiko umesha halalika. Kwa sababu binti/mwanamke huyo amekiwsha kuwa mke wake aliye na uhuru nae kama ule ambao yeye mke anao kwake yeye mume.

   


 


| Tuandikie |