Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Fiqh na Sheria  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

LIANI

 

  iii.            Liani.

(a)        Ujuvyo/fasiri ya liani:

         Neno “liani” kilugha lina maana ya “kufukuza” na “kutenga/kuweka mbali”, kutokana na maana hii tunapata ibara: ALLAH AMEMLAANI – yaani amemfukuza na kumtenga.

Na “liani” imeitwa hivi kwa sababu ya kila mmoja wa wanandoa kuwa mbali na mwenzi wake.

Ama “liani” katika sheria: Ni maneno maalumu yaliyo wekwa kuwa hoja kwa aliye songeka kumtuhumu machafu yule aliye kiboronga uchafu kitanda chake na akampatia aibu.

Na imeitwa “liani”, kwa kuwa maneno hayo yamekusanya tamko la laana na kwa kuwa kila mmoja wa wanao laaniana anajitenga na mwenzake kwa sababu ya hiyo liani.

 

(b)        Falsafa ya kushariiwa kwa liani:

         Tambua kwamba hukumu ya liani imekuja ikikhalifiana (ikipingana) na yale yanayo hukumiwa na uenevu wa hukumu za “qadhfu” – kutuhumu/kusingizia zinaa; yaani kustahiki adhabu kwa msingiziaji. Na utakaso wa msingiziwa kihukumu dhidi ya tuhuma alizo singiziwa na msingiziaji.

Basi je, ni nini hekima/falsafa ya kukhalifiana huku? Na kwa nini hukumu za qadhfu hazikumuambata yule aliye mtuhumu zinaa mke wake?

Jawabu: Ni kwamba asiye mume kwa mnasaba wa mke wake, si mwenye kusongeka/kulazimika kumtuhumu yeyote kwa uchafu wa zinaa, akiwa ni mkweli katika tuhuma zake hizo au akiwa ni mwongo. Si hivyo tu, bali adabu ya Uislamu inahukumia muislamu kusitiri aibu za watu wengine zinazo weza kumfichukia na atosheke na kuwanasihi katika stara.

Ama huyu mume kwa mnasaba wa mke wake, hakika yeye anashabihi kuwa mwenye kusongeka kufichua ukweli wa mke wake na uhalisia wa kadhia yake katika kutenda machafu. Kwa sababu kutenda kwake hilo, ni kukiboronga uchafu kitanda chake na kumtia aibu. Na huo ni udhuru wa kisheria unao mpa haki ya kutengana nae. Na lau mume atatengana nae kwa talaka, hilo lingeli mlazimishia kutumbukia katika dhuluma nyingine itakayo muandamia mwenyewe. Nayo ni kule kuhukumiwa mke kupata mahari kamili pasina kustahiki kupata chochote katika hayo mahari kwa sababu ya mwenendo wake mbaya.

Ni kwa ajili ya hayo basi, ili kumfanyia insafu ikawa hapana budi hali hii kuwekewa sheria makhsusi, inayo mdhaminia kila mmoja wa wanandoa hawa kubakia katika himaya ya uadilifu. Pasina mmoja wao kuwa muhanga wa dhuluma ya mwenzake. Na hukumu hiyo ikawa ndio hii “hukumu ya liani” ambayo tutakayo ielezea kwa ufafanuzi.

Kwa maelezo haya basi, utaitambua hekima ya kwamba tuhuma za mume kwa mkewe kuwa amefanya uchafu wa zinaa, zikija katika mfumo ulio rasimiwa na sheria ya Kiislamu, kamwe hazimuwajibishii mume huyo adhabu. Kwa sababu yule anaye toa tuhuma za zinaa dhidi ya mwenzake, hakika si vinginevyo hutiwa adabu kwa kutuhumiwa kwake uwongo kwa upande mmoja. Na kwa kutokushughulikia kwake kusitiri hali za Waislamu kwa upande mwingine. Ama huyu mume ni jambo lililo mbali mno na yeye kumtuhumu mke wake machafu kwa uwongo, kwa sababu ya aibu itakayo mpata kutokana na uwongo huo. Naye amepewa udhuru wa kutoisitiri hali ya mke wake, kwa sababu kumsitiri kwake huko, ni kujiletea aibu ambayo ni kuporomoka kwa murua wake na mwenendo wake mzuri machoni pa jamii.

 

(c)         Hukumu ya kumsingizia mke machafu:

         “Qadhfu” ni neno lililomo katika Istilahi za sheria ambalo linawakilisha dhana ya: Mume kumtuhumu mke wake kwa zinaa. Na mume anayo haki ya kumtuhumu hilo wakati atakapo ijua zinaa yake au akaidhania kwa dhana yenye mashiko. Kama vile kudhihiri/kutangaa kuzini kwake na mwanaume fulani pamoja na kuwaona wawili hao faraghani peke yao. Hukumu hii, nayo ni kule kumpa ruhusa mume kumtuhumu zinaa mke wake, ni iwapo hayupo (hakuna) mtoto. Ama kukiwa na mtoto na mume akawa anajua kwamba mtoto huyo si wake, hakika yeye katika hali hiyo ni wajibu kwake kumtuhumu zinaa mke wake. Na amkanushe mtoto kuwa sio wake, kwa sababu kuacha kumkana kunadhamini mtoto kuambatishwa nae. Na ilhali mtu kuambatishiwa mtoto asiye wake ni HARAMU kama ulivyo uharamu wa kumkana mtoto anaye tokana nae. Lakini swali ni kwamba, je atajuaje kuwa mtoto huyo sio wake? Njia ya kulijua hilo ni kuwa yeye hajamuingilia mke wake au mke huyo amezaa mtoto kwa kipindi chini ya miezi sita, tangu kuingiliwa na mume huyu. Miezi sita ambayo ndio uchache wa muda wa ujauzito (mimba). Au alimzaa kwa zaidi ya kipindi cha miaka minne tangu kuingiliwa mara ya mwisho na mume huyo. Katika hali hizi ndimo huthibiti kwamba mtoto huyo sio wa mume huyu na wakati huo ndio humuwajibikia kumkana ili asimuambate.

 

(d)        Namna/jinsi mume anavyo fanya liani:

         Mume atakapo mtuhumu/msingizia mke wake kufanya zinaa, kumemstahikia kupata adhabu ya usingiziaji ila atoe ushahidi. Na ushahidi huo ni kupatikana kwa mashahidi wanne akiwemo mume, walio lishuhudia tendo chafu hilo. Hiyo ndio hukumu enevu kwa muktadha wa kadhia ya usingiziaji zinaa. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimwambia Hilaal Bin Umayyah-Allah amuwiye radhi-pale alipo mtuhumu mkewe zinaa mbele yake: “Utoe ushahidi au upate adhabu mgongoni mwako”. Hilaal akasema: Naapa kwa yule aliye kutuma kwa haki, hakika mimi ni mkweli, basi wallah bila ya shaka Allah atateremsha kile kitakacho uondoshea adhabu mgongo wangu.

 

Hakika ikashuka hukumu ya liani, basi hiyo ikawa ndio njia ambayo mume anajiepushia nayo adhabu ya kosa la usingiziaji zinaa pale atakapo msingizia mke wake kwa zinaa. Huko kufanya liani kunakuwaje basi?

KULAANI: Ni mume kusema mbele ya hakimu/kadhi katika kadamnasi ya watu. Na kunaswihi watu hao kuwa katika wenye heshima miongoni mwao na wema wao na hilo lifanyike ndani ya msikiti, juu ya mahala palipo inuka kama vile mimbari. Aseme: “Ninashuhudia kwa jina la Allah, ya kwamba hakika mimi ni katika wakweli katika madai ya zinaa niliyo mtuhumu nayo mke wangu fulani (ataje jina lake na ubini wake). Na kwamba mtoto huyu (akiwa na mtoto au mimba) anatokana na zinaa hiyo na sio wangu”. Ayaseme maneno hayo mara nne, katika kila mara amuashirie kwa kidole mkewe huyo akiwa yupo hapo. Halafu tena ndipo aseme katika mara ya tano baada ya kuwaidhiwa na kutahadharishwa na hakimu dhidi ya uwongo, aseme: “Na inishukie laana ya Allah ikiwa mimi ni katika waongo”.

 

(e)        Dalili ya liani hii (ya mume):

         Uwekwaji wa sheria ya liani kwa upande wa mume, hutolewa dalili kwa kauli yake Allah Ataadhamiaye: “NA WALE WANAO WASINGIZIA WAKE ZAO NA HAWANA MASHAHIDI ILA NAFSI ZAO, BASI USHAHIDI WA MMOJA WAO UTAKUWA NI KUSHUHUDILIA MARA NNE KWA KIAPO CHA ALLAH YA KWAMBA HAKIKA YEYE NI KATIKA WASEMA KWELI. NA MARA YA TANO KWAMBA LAANA YA ALLAH IWE JUU YAKE IKIWA NI MIONGONI MWA WAONGO”. [24:06-07]

Na katika Sunna: Imepokewa kutoka kwa Sahli Bin Sa’ad-Allah amuwiye radhi-kwamba mwanaume mmoja wa Kianswaari alikuja kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: Ewe Mtume wa Allah! Unaonaje mtu akimfuma mkewe na mwanaume mwingine, je amuue au afanyeje? Ndipo Allah akashusha katika kadhia yake hayo yaliyo tajwa ndani ya Qur-ani; yaani suala la wafanyao liani. Mtume akasema: “Bila ya shaka Allah amekwisha kuhukumu katika suala lako na mke wako”. Anasema (mpokezi): Basi akafanya liani msikitini na mimi nikiwa shahidi. Bukhaariy [5003] & Muslim [1492]-Allah awarehemu.

 

(f)          Hukumu zinazo iandamia liani hii ya mume:

         Mume atakapo mfanyia liani mke wake kwa namna tuliyo itaja, liani yake hiyo huandamiwa na hukumu tano zifuatazo:

                            1.          Kuporomoka/kuondoka adhabu ya usingiziaji kwa mume.

                            2.          Wajibu wa adhabu ya zinaa kwa mke ILA na yeye afanye liani.

                            3.          Kukatika kwa ndoa baina yao.

                            4.          Kumkana mtoto na kukatika nasabu yake kwa mume ikiwa alimkana katika liani yake na ataambatishwa kwa mke.

                            5.          Kuharimika kwa kila mwanandoa kwa mwenzake milele.

        

Imepokewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-kwamba     Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alifanya liani baina ya mume na mke wake, akakanushika mtoto wake (mke). Basi Mtume akawatenganisha na akamuambata mtoto kwa mwanamke. Bukhaariy [5559] & Muslim [1494]-Allah awarehemu.

 

   



| Tuandikie |