|
Ndugu
zanguni Waislamu, jamii yoyote ya wanadamu inahitaji sera na utaratibu
maalumu wa malezi ili kupata kizazi na jamii njema itakayoufanya ulimwengu
huu kuwa ni kisiwa cha amani. Sera utaratibu huu na malezi ni lazima ujengwe
juu ya nguzo tatu zifuatazo:-
1.
Nguvu
2.
Upendo, na
3.
Unyenyekevu.
Tunakusudia
nini tunaposema nguvu? Nguvu
zikusudiwazo hapa ni nguvu za mwili, roho na akili, ama mradi wa upendo ni
kuiangalia jamii ya kiislamu, kwa
jicho la rehema na upole na kuitazama jamii ya wanadamu kwa ujumla mtazamo
wa kusaidiana na kufahamiana. Kwa neno unyenyekevu hatukusudii kingine
zaidi ya kuondosha tofauti na matabaka katika jamii ya kiislamu (Umma).
Tajiri asijikweze juu ya fakiri kwa sababu tu ya utajiri wake, wala watu
waliobeba dhamana mbalimbali serikalini wasijione kuwa ni bora kuliko
wananchi wa kawaida eti kwa sababu
tu ya nyadhifa zao. Kadhalika watu wasijifakharishe na kujivuna kwa
nasabu, mavazi, na mali zao, bali kigezo chao cha ubora, heshima
na utukufu kiwe ni ucha-Mungu (Taq-wa) tu basi. Tusome na
tuwaidhike’…..HAKIKA AHISHIMIWAYE SANA MIONGONI MWENU MBELE YA ALLAH
NI YULE AMCHAYE ALLAH ZAIDI KATIKA NYINYI…….” (49:13) Bahati kubwa
na sudi njema waliyonayo Waislamu ni kuwa na sheria bora na kamilifu
kuliko sheria zote zilizobaki kuwepo, zilizopo na zijazo. Sheria ambayo
imehodhi sera/utaratibu huu wa malezi, sera ambayo imewafanya watu wote
kuwa ni sawa. Kigezo na dalili kubwa juu
ya hili ni ibada kama vile swala, swaumu n.k.
kitu ambacho Uislamu umekifanya kuwa ndio msingi na nguzo yake madhubuti.
Hebu sasa
na tupekue na kubahithi kwa pamoja ili tuone ni vipi tunavyoweza kuipata
misingi ile mitatu ya malezi
katika ibada ya swala. Tuanze
na ule msingi wa kwanza.
1.
NGUVU
Hivi
huoni kuwa udhu ambao ndio msingi wa ibada nzima ya swala kuwa ni NGUVU ya
mwili, NISHATI ya roho na ni NADHAFA ya kiwili wili kwa ujumla ? Je, huoni
kuwa kuifungua swala kwa tamko lenye kudumu milele “ALLAHU AKBAR” ni
nguvu ya roho inayomfanya mtu ahisi kuwa Allah ni Mkubwa kuliko wakubwa
wote? Allah ni Mtukufu
kuliko watukufu wote? Hakuna Mkubwa wala Mtukufu mbele yake ila ni
yeye tu. Ni hisia hizi ndizo zilizowafanya wachawi kutotetereka na kurudi
nyuma mbele ya mabavu, nguvu na vitisho vya Mungu mtu- Firauni Tujikumbushe
hali ilivyokuwa: (Firauni) AKASEMA: OH! MNAMUAMINI KABLA SIJAKUPENI
RUHUSA! BILA SHAKA YEYE NDIYE MKUBWA WENU ALIYEKUFUNZENI UCHAWI. KWA HIVYO
NITAKUKATENI MIKONO YENU NA MIGUU YENU KWA KUTAFAUTISHA (mkono wa kulia na
mguuu wa kushoto na mkono wa kushoto na mguu wa kulia ) NA NITAKUSULUBINI
KATIKA MASHINA YA MITENDE, NA BILA SHAKA MTAJUA (wakati huo) NI NANI
KATIKA SISI (mimi au Mungu wake Musa) ALIYE MKALI WA KUADHIBU NA
KUJIENDESHA (kuindeleza adhabu yake) “ WAKASEMA : “HATUTAKUKHITARI
WEWE KULIKO ZILE ISHARA WAZIWAZI (za haki) ZILIZOTUJIA. TUNAAPA KWA YULE
ALIYETUUMBA. BASI FANYA UNAVYOTAKA KUFANYA, WEWE UNAWEZA KUTOA HUKUMU
INAYOHUSIANA NA MAISHA HAYA YA DUNIA TU” (20: 71-72).
Ni
hisia hizi hizi zitokazo na nguvu ya kiroho izalishwayo na kukuzwa siku
hata siku ndani ya swala iliyomfanya Mtume Mussa – Amani ya Allah
imshukie – kutobabaika wala kuyumba wakati wafuasi wake (bani Israil )
walipokata tamaa kabisa na kuona kuwa mwisho wao umefika. Hawana
kitakachowaokoa na jeshi kubwa la Firauni linalowafukuza na mbele yao kuna
habari nyekundu (Red sea). Tuitegee sikio Qur-ani ikituelezea hali
ilivyokuwa . “NA YALIPOONANA MAJESHI MAWILI (haya , watu na Nabii Musa
wanakimbia, na Firauni na watu wake wanawafuatia) WATU WA MUSA WALISEMA
“ HAKIKA TUTAKAMATWA” (Musa) AKASEMA: “ LA, KWA YAKINI MOLA WANGU YU
PAMOJA NAMI, BILA SHAKA ATANIONGOZA (tuokoke sote)”…………….NA
TUKAMUOKOA MUSA NA WALE WALIOKUWA PAMOJA NAYE WOTE” ( 26:61-62, 65). Ni
hisia hizi pia ndizo zilizomtia nguvu na kumuondolea wasiwasi Bwana Mtume
– Rehema na Amani zimshukie – alipokuwa pangoni na swahibu yake Abu
Bakri – Allah amuwiye radhi. Makurayshi wamesimama mdomoni mwa
pango, miguu yao inaonekena na waliomo ndani kama yanavyosikiwa
maneno yao. Hapo Abuu Bakri akitetemeka kwa khofu kuu anamnong’oneza
Mtume –“ Ewe Mtume wa Allah, lau mmoja wao atatazama chini ya miguu
yake bila shaka atatuona (Mtume) akamwambia, “ Nini dhana yako we Abu
Bakri kwa wawili ambao Allah ni watatu wao?! “ Bukhariy na Muslim.
Hebu
tuipe nafasi Qur-ani Tukufu: “KAMA HAMTAMNUSURU (Mtume ) BASI ALLAH
ALIMNUSURU WALIPOMTOA WALE WALIOKUFURU, ALIPOKUWA (mmoja tu na mwenziwe) WA PILI WAKE (peke yao) WALIPOKUWA WOTE WAWILI
KATIKA PANGO, (Mtume) ALIPOMWAMBIA SAHIBU YAKE, “ USIHUZUNIKE KWA YAKINI
ALLAH YU PAMOJA NASI” ………….”
(9:40).
Ni
hisia hizi ndizo zilizompa Bwana Mtume ushujaa na kutokubabaika mbele ya
upanga wa Daathuuri katika vita vya Ghatwafaani. Waislamu walipiga kambi,
Mtume akawa amejitenga jpembeni amepumzika chini ya mti akiwa ameanika
nguo zake zilizoloa kutokana na mvua iliyowapata. Hapo ndipo Daathuuri
mmoja wa maadui akaona amepata fursa nzuri ya kummaliza Mtume. Akamuendea
Mtume mpaka akamsimamia kichwani, upanga mkononi, Akamuamsha, Mtume na
kumwambia: ni nani atakayekuzuia nisikuue, ewe Muhammad? Mtume akamjibu:
Allah! Pale pale mtu yule akapatwa na kitisho na woga uliomtambaa mwili
mzima na kutetemesha kiasi cha kuacha upanga umuangukie Mtume akauokota na
kumuuliza hasimu yake swali
lile lile: Ni nani atakayenizuia nsikuue, ewe Daathuiru? Akajibu: Hapana
ye yote. Mtume akamsamehe. Rejea vitabu vya sira kwa ukamilifu wa kisa
hiki, ukitaka safu zilizonyooka na kukamatana nyuma ya Imam mmoja,
zikisikiliza kisomo chake (Qur-ani aisomayo), zikiunyenyekea waadhi
upatikanao ndani ya kisomo hicho, zikimfuata Imam wao katika harakati na
vitulizano vyake. Huoni kuwa nidhamu hii inaonyesha nguvu ya jamii
iliyoungana pamoja na yenye lengo moja? Kuna nguvu ipi ulimwenguni iliyo
bora ziadi inayoweza kuilea jamii kuliko nguvu hii inayopandikizwa na
swala katika nafsi ya muislamu?
2.
UPENDO:
Hebu
sasa tuingalie swala ni kwa kiasi gani inaweza kuwa ni kiwanda
kinachozalisha bidhaa adimu na muhimu “Upendo”. Hebu itazameni swala
wakati waislamu wanapokusanyika mahala pamoja mbele ya Bwana Mlezi wa
viumbe wote, sio Bwana wa uma mmoja, Taifa moja wala dini/mfumo mmoja wa
maisha bali ni Bwana Mlezi wa viumbe wote Mwingi wa Rehema Mwenye
kurehemu. Ambaye huwabubujishia na kuwamiminia rehema yake woote, waislamu
na wasio waislamu (makafiri) watiifu na waasi, wema na waovu, wadogo na
wakubwa kisha angalia namna muislamu anavyoikhitimisha swala yake kwa
kusema, Amani iwe juu yetu na juu ya waja wema wa Allah! Hapa anawakumbuka
ndugu zake waliotapakaa mashariki na magharibi ya ardhi. Kisha anatoka
ndani ya swala kwa REHEMA na AMANI, husema Amani na Rehema ya Allah iwe
juu yenu.
Aliianza
swala yake kwa tuamko la “ALLAAHU AKBAR!”
Allah ni Mkubwa kuliko wakubwa wote, na sasa anaikhitimisha kwa tamko la
Amani na Rehema. Haya yote ni vigezo na vielelezo tosha kwamba nguvu ya
Uislamu ni nguvu inayokomelea na Rehama na Amani vitu ambavyo ndio
chemchem ya upendo. Hivi ndivyo swala inavyoweza kupandikiza nguvu ya
upendo na moyo wa kuzoeana na kupendana baina ya waislamu khasa khasa
katika swala za jamaa,
3.
UNYENYEKEVU
Unyenyekevu
unapatikanaje ndani ya swala? Huoni kuwa ni upeo wa unyenyekevu usio ni
mithali pale muislamu anapokiweka mavumbini kiungo chake kitukufu
“Uso” kumsujudia Mola wake. Tena wakalingana sawa katika unyenyekevu
huu watu wote, wakubwa kwa wadogo, wanaume na wanawake, mabwana na
watwana. Hapana kichwa cho chote kinachoweza kuwa juu ya kichwa kingine
katika rukuu na sujudi. Ndani ya swala katika majumba ya Allah (Misikiti)
mwanadamu hupata heshima na utukufu kuangalia matabaka na nyadhifa zao.
Swala kuwakumbusha viongozi/watawala usawa wao na wananchi wa kawaida pale
wanaposimama safu moja, bega kwa bega, mguu kwa mguu, wakiwa nyuma ya
Imamu mmoja.
Mbali
na nguzo tatu hizo, nguvu, upendo na unyenyekevu, swala ina hekima na
manufaa mengi yasiyomalizwa kuzungumzwa na maneno ya kinywa cha binadamu
mpungufu. Katika jumla ya falsafa ya swala ni kumshukuru Mwenyezi Mungu
Mtukufu juu ya neema zake zisizodhibitika alizotuneemesha :
“…………NA KAMA MKIHISABU NEEMA ZA ALLAH, HAMTAWEZA KUZIHISABU BILA
SHAKA MWANADHAMU NI DHALIMU MKUBWA ASIYE SHUKRANI (mwizi wa fadhila) “
(14:34). Pia swala hujenga mahusiano na mawasiliano mazuri baina ya kiumbe
(mja) na Muumba wake kwani mja huwa karibu zaidi na Mola wake anapokuwa
ndani ya swala, ambamo humo hupata raha na utulivu wa moyo.
Kadhalika
swala humfinyanga muislamu kuwa ni mtu mwenye nidhamu. Hii ni kwa sababu
ndani ya swala muislamu hulazimika kumfuata Imamu wake kwa utaratibu
maalumu ili swala yake ikubaliwe kitendo cha kurudiarudia utaratibu huu
ndio humjengea muislamu tabia ya kuwa na nidhamu.
Katika
jumla ya mambo yanayoonyesha kwamba swala ina athari kubwa na nzuri katika
kuwalea wanadamu na kudumisha tabia na maadili mema ni kitendo cha Nabii
Ibrahim-Allah amshushie Amani- kumuomba Mola wake amjaalie yeye na kizazi
chake kuwa ni wasimamishaji wa swala, aliposema: MOLA WANGU! NIJAALIE NIWE
MSIMAMISHAJI SWALA, NA KIZAZI CHANGU (pia
kiwe hivi) MOLA WETU ! NA UPOKEE MAOMBI YANGU” (14:40).
Swala
ndio zana ya kumkumbusha mwanadamu hakika na ukweli kuwa yeye ni mja na
mtumwa anayemilikiwa na Allah. Aendelee kuukiri ukweli huu usio na
mjadala, kila harakati na mishughulisho ya maisha inapomsahaulisha ukweli
huu, swala hujitokeza na kumkumbusha tena, naye husema awapo ndani ya
swala! ‘ WEWE TU NDIYE TUNAYEKUABUDU NA WEWE TU NDIYE TUNAYEKUOMBA
MSAADA’ (1:5). Kwa hiyo, swala humfanya mwanadamu kuyakinisha kuwa
hakuna msaidizi wala mneemeshaji wa kweli ila ni Allah pekee. Hata kama
ataona katika maisha yake ya kila siku vitu/mambo/sababu ambazo kwa sura
ya nje huonekana kuwa ndizo zinazomsaidia na kumneemesha. Lakini ukweli
unabakia pale pale kwamba ni
Allah pekee ndiye aliyemuumbia vitu, mambo au sababu hizo zote.
Kazi
inaposahaulisha mwanadamu na kumfanya aamini kuwa kazi ndio inayompatia
riziki na kuisahau nguvu iliyo nyuma ya kazi, hapo ndipo huja swala na
kufanya kazi yake. Ikamkumbusha kuwa msababishaji na muunganishaji wa
riziki na kazi ni Allah pekee ambaye ni yeye tu ndiye mpaji riziki,
Mneemeshaji, Msaidizi, Mwenye kudhuru na kunufaisha, Mtoa uhai na
Mfishaji, KWA YAKINI ALLAH NDIYE MTOAJI WA RIZIKI MWENYE NGUVU, MADHUBUTI
“ (51:58).
|