Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Fiqh na Sheria  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

ULAZIMU WA WAQFU NA HUKUMU ZINAZO UANDAMIA

 

Ulazimu wa waq-fu na hukumu zinazo uandamia:

 

Waq-fu ni miongoni mwa vifungu lazimishi ambavyo vinavyo andamiwa na athari zake (vifungo hivyo), mara tu kinapo anzishwa (fungwa) kifungo kilicho sahihi. Na waq-fu si kama wasiya, kwani huo (wasiya) ni kifungo juzishi.

Ulazimu wa kifungo cha waq-fu unaandamiwa na hukumu zifuatazo:

  1. Kutokuthibiti kwa khiari katika kifungo cha waq-fu. Angalia, mtu atakapo funga waq-fu ulio sahihi katika sheria, hatakuwa na khiyari majlisi kama ambavyo pia asivyo kuwa na khiyari sharti.
  2. Uguro (uhamaji) wa umiliki wa chenye kuwekwa waq-fu kutoka kwa muweka waq-fu kwenda kwa Allah Ataadhamiaye. Kwa hivyo basi, mmiliki wa asili (mwanzo) hana haki ya kuusarifu waq-fu alio utoa kwa njia ya umiliki, si kwa kuuza au kwa kutoa hiba, wala kwa namna nyingineyo.
  3. Uguro wa haki ya kunufaika na waq-fu kwenda kwenye jiha (upande) ambao ulio wekewa waq-fu huo, ukiwa ni makhsusi (upande huo) au ni wa umma (wa watu wote).

 

Umiliki wa chenye kuwekwa waq-fu:

 

         Muweka waq-fu atakapo weka waq-fu kitu dhati (kilicho thibiti mahala pake) au mali hamishika. Au akaweka waq-fu silaha, gari au kitu kinginecho. Milki ya chenye kuwekwa waq-fu itaguria (itahamia) kwa Allah Ataadhamiaye, kwa hivyo basi kilicho wekwa waq-fu hakitakuwa tena ni milki ya muweka waq-fu, wala milki ya muwekewa waq-fu (mnufaika wa waq-fu).

 

Manufaa ya chenye kuwekwa waq-fu:

 

         Manufaa ya kitu dhati kilicho wekwa waq-fu, ni milki ya yule aliye wekewa/pewa waq-fu huo, akiwa ni muainiwa. Na kunamuelea kuyatwaa manufaa hayo yeye mwenyewe moja kwa moja, mfano wa nyumba akaishi humo. Au akayatwaa kwa kupitia kwa mtu mwingine, kwa njia ya kuazimisha au kukodisha.

Pia anamiliki faida za waq-fu huo zinazo patikana baadaye, kama vile matunda ya miti iliyo wekwa waq-fu. Na sufi na maziwa ya watoto wa wanyama walio wekwa waq-fu.

Ama pale muweka/mpewa waq-fu atakapo kuwa si muainiwa (hakutajwa), akawa ni pande miongoni mwa pande kama vile mafakiri. Hakika wao hawamiliki manufaa ya chenye kuwekwa waq-fu, bali wanamiliki haki ya kunufaika nacho.

 

Haki/mamlaka ya kutumia kilicho wekwa waq-fu:

 

         Hakujuzu kuwa na haki/mamlaka ya kutumia dhati ya kilicho wekwa waq-fu, si kwa kuuza au kununua, si kwa kutoa hiba au kurithi. Yote hayo hayajuzu si kwa upande wa muweka waq-fu tu bali hata kwa mpewa waq-fu muainiwa au asiye muainiwa. Bali dhati ya kitu hicho inaendelea kubakia chini ya umiliki wa Allah Ataadhamiaye, manufaa yake yakitolewa kwa wale walio wekewa waq-fu huo. Na utumike kadiri imkinikavyo kwa mujibu wa maelezo ya muweka waq-fu.

Hilo linafahamishwa kupitia waq-fu wa Sayyidna Umar bin Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi-kwani yeye alitoa maelezo katika waq-fu wake: “Ya kwamba hauuzwi, hautolewi hiba na wala haurithiwi”. Bukhaariy [2586] & Muslim [1632]-Allah awarehemu.

 

Masurufu ya kilicho wekwa waq-fu:

 

         Ikiwa chenye kuwekwa waq-fu kinahitajia masurufu (gharama za kujikimu), kama vile chakula cha wanyama (wawekwa waq-fu), au ukarabati wa majengo, au utengenezaji wa ala/zana. Hakika gharama hizo juu ya waq-fu, zitakuwa kwa namna aliyo ishurutizia muweka waq-fu kutoka katika mali yake mwenyewe au kutoka kwenye mali ya waq-fu wenyewe. Kama muweka waq-fu hakuweka sharti lolote, gharama zitatoka kwenye mazao/mapato ya waq-fu ikiwa unayo mazao/mapato. Angalia, iwapo kiwekwacho   waq-fu hakina mazao/mapato au manufaa yake yalisita (simama). Hapo katika hali/mazingira hayo, gharama zitaiwajibikia Baytul-Maali ya Waislamu, kwa sababu ndio inayo husika na maslahi yao. Na katika utoaji wa gharama za kiwekwa waq-fu, kuna maslahi kwao (hao Waislamu).

 

Kuhiliki/kuangamia kwa kiwekwa waq-fu na hukumu zinazo fungamana nako:

 

         Kiwekwa waq-fu kinaweza kuhiliki, basi kwa sababu ya kuhiliki huko zinatungamana hukumu kadhaa wakati huo. Hukumu zinazo tofautiana kufuatia utofauti wa kitu dhati kilicho wekwa waq-fu, kilicho hiliki na kwa utofauti wa aina ya hilaki. Na hukumu hizo ni kama zifuatavyo:

  1. Iwapo kiwekwa waq-fu ni mnyama asiye liwa, akafa, atahusishwa na ngozi yake yule aliye wekewa/pewa waq-fu huo, kwani yeye ndiye mstahiki zaidi wa kupewa kuliko mwenginewe. Angalia, ngozi hiyo ikisafishwa na kuwa mali ghafi (dabghu), itarejea kuwa ni waq-fu juu yake, atanufaika nao. Na wala hakumjuzii kuiuza ili kuendelea kuhifadhi makusudio ya muweka waq-fu, kwa kadiri itakavyo mkinika.
  2. Iwapo kiwekwa waq-fu ni mnyama aliwaye, na muwekewa waq-fu akakata shauri ya kwamba mnyama huyo atakufa kutokana na janga lililo mpata. Hapo kunajuzu kumchinja kwa sababu ya dharura hiyo na nyama yake itauzwa na kwa thamani yake atanunuliwa mnyama mwingine kama huyo na atawekwa waq-fu mahala pake. Na pamesemwa suala la nyama yake litaachwa mikononi mwa hakimu/mtawala, afanye kwa nyama hiyo lile analo ona lina maslahi.
  3. Kitakapo tilifiwa kitu dhati kilicho wekwa waq-fu, ikiwa hivyo basi ni juu ya mtilifu wake kulipa kima/thamani yake. Hilo litakuwa kama vile mtu atakapo kitilifu kwa makusudi. Muwekewa waq-fu hatomiliki kima cha kitu dhati kilicho wekwa waq-fu ambacho kimetilifiwa, lakini kitanunuliwa kitu dhati kinacho fanana na kile kilicho tilifiwa, kwa kima hicho. Na kitu dhati hicho kitakuwa   waq-fu mahala pa kile kilicho tilifiwa. Na hilo linafanyika ili kuchunga lengo la muweka waq-fu, yaani ule uendelevu wa thawabu. Na ili kufungamana haki ya tumbo la pili na la baada yake na kitu dhati hicho. Angalia, ikishindikana kununua kitu dhati kamili, basi na kinunuliwe baadhi ya kitu dhati hicho, kwa sababu hicho ndicho kilicho karibu mno na makusudio ya muweka waq-fu. Ama kitakapo tilifu hicho kitu dhati kilicho wekwa waq-fu bila ya kuwa na dhamana, au kilitilifika chenyewe, hapo waq-fu (thawabu) utakuwa umekoma kwa sababu ya kuondoka dhati ya kitu kilicho wekwa waq-fu.
  4. Yatakapo fungika manufaa ya kitu dhati kilicho wekwa waq-fu kwa sababu isiyo na dhamana, kama vile mtu kuweka waq-fu miti, kisha ikakauka au ikang’olewa na upepo au mumbwi. Na isiwezekane kuirejesha mahala pa upando wake kabla ya kukauka, (thawabu za) waq-fu haujakatika, bali itaendelea kuwa katika hukumu ya waq-fu. Yakipatiwa manufaa mashina yake kwa kukodishwa na kwa namna kama hiyo, ili kuudumisha waq-fu katika dhati yake. Wala miti hiyo haitauzwa wala kutolewa hiba. Angalia, iwapo kunufaika nayo (miti hiyo) hakutapatikana ila kwa njia ya kuimaliza kabisa, kwa kuichoma (mkaa) na mfano wake, kunamjuzia muwekewa waq-fu kufanya hivyo. Ila tu ni kwamba hakujuzu kuiuza wala kuitoa hiba.
  5. Kitakapo kuwa kiwekwa waq-fu ni majamvi/mikeka/mabusati ya msikiti, yakalowa maji. Au kitakapo kuwa ni mashina, yakakatika na yasifae ila kwa kuunguzwa moto. Hapo kumejuzu kuyauza ili yasipotee bure au yasijaze nafasi pasina faida yoyote. Na kupata mali kidogo kutokana na thamani yake, itakayo rudi kwenye waq-fu, ni bora kuliko kupotea bure. Na kwa msingi huu basi, hakika thamani yake itatumiwa katika maslahi ya msikiti. Na katika maslahi hayo, utatangulizwa ununuzi wa mfano badala wa kile kilicho tilifu, limkinikapo hilo.

Ama yatakapo faa kwa matumizi yasiyo kuunguza moto, hapo hakujuzu kuyauza, ili kuhifadhi kubakia dhati yake, ili kwenda sanjari na lengo la muweka waq-fu.

  1. Msikiti utakapo bomoka na kukashindikana kuujenga upya, hakujuzu kuuza (kiwanja) kwa hali yoyote ile, kwa sababu ya kuwepo imkani ya kuweza kuujenga tena wakati wowote. Angalia, iwapo msikiti huo unayo mapato yanayo tumika kwa maslahi yake, tukitarajia kuujenga upya, basi kunajuzu kuyatumia mapato hayo kwenye maslahi ya msikiti ulio jirani na hapo.
  2. Msikiti utakapo hofiwa kukumbwa na janga lolote, kunamjuzia hakimu/mtawala kuutengua na akayatumia mawe/matofali yake kujengea msikiti mwingine. Na wala mawe/matofali na kifusi chake kisijengewe kitu kingine, kwa ajili ya kulichunga lengo la muweka waq-fu. Na kuujenga huo (msikiti upya) karibu na ule msikiti ulio tenguliwa, ni bora zaidi.
  3. Lau mtu ataweka waq-fu mali kwa ajili ya ujenzi wa daraja kwenye korongo kavu la mto, korongo hilo likameguka na kupelekea daraja kubomoka. Na watu wakahitajia daraja jengine, hapo kunajuzu kulihamisha daraja hilo kulipeleka mahala linapo hitajika, ili kuyabakisha madhumuni ya muweka waq-fu kwa kadiri ya imkani.

   



| Tuandikie |