Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

VI) SHARTI ZA SWALA

Faida

Sharti tunazozikusudia hapa ni zile sharti za kusihi swala.

 Maana ya sharti :-

 Sharti ya kitu ni lile jambo au tendo ambalo upatikanaji wa kitu husika unalitegemea jambo/tendo hilo lakini lenyewe si sehemu ya kitu hicho.

 Mfano :  wa ufafanuzi

Mmea ili upatikane/uwepo juu ya uso wa ardhi unahitaji mvua pamoja na ukweli kwamba mvua sio sehemu ya mmea huo.  Kwa hivyo basi mvua ni sharti katika upatikanaji na kuwepo kwa mmea kwani bila ya mvua hakuna mmea lakini bado mvua haiwi ni sehemu ya mmea huo.

Baada ya kujua ainisho la sharti, hebu sasa tuziangalie sharti za kusihi kwa swala moja baada ya jingine kwa ufafanuzi wa kina sharti za kusihi swala ni nne zifuatazo:-

1.                TWAHARA:-

Hii ndio sharti ya kwanza ya kusihi swala:  Twahara nni nini, tayari umekwishajifunza katika sura ya kwanza, somo la kwanza, rejea huko na utaona. Twahara ambayo ni sharti ya kusihi swala imegawanyika katika matapo yafuatayo:-

(i)                 Twahara ya mwili kutokana na hadathi .  mtu mwenye hadathi haisihi swala yake.   Ni mamoja ikiwa ni hadathi ndogo ambayo ni ukosefu wa udhu au ni hadathi kubwa kama vile janaba.  Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume – Rehema na Amani zimshukie katika hadithi sahihi “Haikubaliiwi swala bila ya twahara – Muslim.

(ii)              Twahara ya mwili kutokana na najisi.   Rejea sura ya kwanza, somo la pili ili ujikumbushe maana ya najisi na aina zake.  Kabla ya kuvaana na ibada ya swala ni lazima mtu ahakikishe kuwa mwili wake ni twahara, hauna najisi ya aina yoyote ile.  Haya ndio tunayoyafahamu kutokana na kauli ya Bwana Mtume – rehema na Amani zimshukie:  “Jiepusheni na mkojo kwani hakika sehemu kubwa ya adhabu (zimpatazo mja) kaburini ni kwa sababu ya kutojikinga nao”

Mkojo hapa unakuwa ndio kigezo na mfano wa najisi nyingine zote ambazo Mtume hakuzitaja hapa katika hadithi hii.   Bwana mtume Rehema na Amani zimshukie – alimwambia Bi. Fatmah Bint Abiy Hubaysh – Allah amuwiye radhi;  :Itakapokuja hedhi basi acha kuswali.  Ikikoma, basi jikoshe damu (jitwaharishe na uanze) kuswali”  Bukhaariy na Muslim.

iii.              Twahara  ya nguo kutokana na najisi.  Haitoshi tu mwili kuwa na twahara usio na  najisi bali hapana budi nguo anazozivaa mwenye kutoka kuswali, pia ziwe ni twahara, zisiwe na najisi ya aina yoyote ile.  Hivyo ndivyo tunavyoambiwa na Mwenyezi mungu Mtukufu kupitia kauli yake :  NA NGUO ZAKO UZITWAHARISHE (74:4)   Haisihi swala ya mtu aliyeswali huku akiwa kavaa nguo yenye najisi isiyosameheka kisheria hata kama mwili wake utakuwa ni twahara.   Imepokelewa kutoka kwa Abu- Hurayrah – Allah amuwiye radhi – Kwamba Bi., Khaulah Bint Yassar – Allah amuwiye radhi alimuendea Mtume na kumwambia :  Ewe Mtume wa Allah mimi sina ila nguo  moja tu, nami ninapata hedhi katika nguo hiyo, basi nifanyeje?   (Mtume) akamwambia “Utakapotwaharika ifue (itwaharishe) (pia) na iswalie |” Akauliza (tena)  Kama (athari ya) damu haikutoka?  (Mtume) akamjibu “ Kunakutosha kukosa damu, na wala athari ya damu haikudhuru :  Abuu Dawood.

d.          Twahara ya mahala pa kuswalia.    Ni lazima kwa mwenye kutaka kuswali ahakikishe  mahala anapotaka kupatumia kwa ajili ya utekelezaji wa ibada yake hiyo ya  swala ni twahara, hapana najisi yoyote ile.   Sharti hili tunaliegemeza katika riwaya iliyopokelewa na Abu Hurayrah – Allah amuwiye radhi amesema   Alisimama mkazi mmoja wa majangwani akakojoa msikitini (msikiti wa Mtume) watu (mwaswahaba) wakamuinukia ili wamtie adabu.  Mtume – rehema na Amani zimshukie akawaambia

 “ Muacheni (amaliza haja zake) na (kisha) mumwagie mkojo wake ndoo ya maji, kwani hakika si vinginevyo mmetumizwa kuwa wawepesishaji (wa mambo) na wala hamkutumwa kuwa wafanya uzito/ugumu – Bukhaariy.

 

2.                ELIMU/MAARIFA YA KUINGIA WAKATI WA SWALA

Hii ndio sharti ya pili ya kusihi kwa swala umekwishajua kutokana na maelezo ya darasa zilizotangulia kwamba kila swala ya fardhi ina wakati wake maalum.  Ili swala  yako isihi ni lazima uiswali ndani ya wakati huo.  Haitoshi tu kuwa swala inaswaliwa ndani ya wakati kwa sadfa au kubahatisha.  Bali ni lazima mwenye kutaka kuvaana na swala aijue wakati kupitia elimu/maarifa.  Hii ni kwa sababu ya kutokusihi kwa swala  ya mwenye kuswali bila ya kujua kuingia itambarikiwa baada ya kumaliza kuswali kuwa amesadifu wakati Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia ………………… kwa HAKIKA SWALA KWA WAUMINI NI FARDHI ILIYOWEKEWA NYAKATI MAKHSUSI  4:103.

NAMNA YA KUJUA KUINGIA WAKATI WA SWALA 

NI vipi basi tunaweza kutambua kuwa wakati wa swala fulani umeingia ?  Hili litawezakana kwa kutumia mojawapo ya njia tatu  zifuatazo:-

 1.     maarifa yakinifu:

Mtu atumie dalili hisia (zinazofahamika kupitia milango ya fahamu) kama vile kuliona jua likizama baharini (upande wa bahari)

2.     Jitihada binafsi

Mtu anaweza kutegemea dalili dhahania hizi ni dalili zisizo za moja kwa moja.  Dalili hizi ni pamoja na kivuli, kipimo cha kazi fulani yaani muda inaochukua kazi hyo.  Mtu anaweza kusema mathalan kwa kawaida nikianza kushona suruali baada ya adhuhuri mpaka nimaliza huwa ni alasiri tayari.

3.     Kufuata Mjuzi

Itakaposadifu kwamba mtu hana maarifa yakinifu wala hawezi kufanya jitihada binafsi.   Huyu  ni yule mtu ambaye hazijui nyakati za swala zinaingia saa ngapi na hana maarifa ya kutumia dalili hisia wala dhania kumsaidia kujua wakati wa swala.  Yeye huyu ina ataamua kumfuata mtu mjuzi mwenye maarifa ua kuingia na kutoka kwa, nyakati za swala kwa kutegemea dalili hisia.  Akimwambia wakati bado haujaingia basi na asubiri au, atamfuata mtu mwenye kutumia jitihada binafsi kwa kutegemea dalili dhania.

FAIDA:   HUKUMU YA SWALA ILIYOSWALIWA NJE YA WAKATI.

Tunaposema swala iliyoswaliwa nje ya wakati hatumaanishi zaidi ya ile swala iliyosaliwa kabla ya kuingia wakati wake.  Ni vipi basi  hukumu ya swala hii?   Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu tunasema na il-hali   Yeye ndiye Mjuzi mno.  Itakapombainikia mtu kwamba swala aliyoiswali;  ameiswali nje ya wakati, yaani kabla ya kuingia wakati wake.  Kisheria swala hiyo itazingatiwa  kuwa ni  BATILI na ITAMUWAJIBIKIA kuiswali tena ndani ya wakati, bila ya kujali kuwa akiswali kwa kutegemea.

·        Maarifa yakinifu

·        Jitihada binafsi au kwa

·        Kumfuata mjuzi

Swala itakuwa ni batili kwa sababu ya kukosekana sharti mojawapo ya kusihi swala.

3.          KUSITIRI UTUPU-UCHI

Hii ndio sharti ya tatu miongozi mwa zile sharti nne za kusihi kwa suala.  Ili  tuweze kuijua vema sharti hii hatuna budi kwanza  tuyajue mambo yafuatayo:

i)                   maana ya utupu

Kisheria utupu ni kila ile sehemu ya mwili ambayo ni wajibu lkuisitiri au ni haramu kuiangalia/kwaangaliwa

ii)                Mipaka ya utupu ndani ya swala, ndani ya swala ni lile aneo lote lililo baina ya kitovu na magoti yake.   Ni wajibu eneo lote hili lisitiriwe .  Mwenyezi MUNGU  anasema  “ENYI WANAADAMU CHUKUENI MAPAMBO YENU WAKATI WA KILA SWALA” (7.32)

Muradi wa neno Mapambo ni nguo inayositiri utupu.  Hivi ndivyo ilivyotasfririwa na wataalamu wa fani ya tafsiri.  Fahamisho la aya ni kuwa Enyi wanadamu sitirini tupu zenu mnapotaka kuswali.  Imepokelewa hadithi na Said – Al-Khudriy – Allah amuwiye radhi kwamba mtume Rehema na Amani zimshukie amesema  “ Utupu na mwaname ni baina ya kitovu chake mpaka gotini kwake.

(iii)  Kwa  upande wa mwanamke :  Ni mwili wake wote    ukiondoa uso na vitanga vya mikono; Sehemu yote hiyo ya mwili ni wajibu isitiriwe.  Hivyo ndivyo tunavyoelewa kupitia kauli ya Mwenyezi Mungu … wala wasidhihirishe viungo vyao isipokuwa VINAVYODHIHIRIKA

Jamhuri ya Mafaqihi wamesema kuwa muradi wa kauli “vinavyodhihirika” ni uso na vitanga

-  Imeshurutizwa nguo ya kujisitiri-

-         Isiwe nyeupe sana kiasi cha kuonyesha  rangi ya mwili mpaka 

Mtazamaji akatambua weupe  ua weusi wa mwili.

-         Isiwe inabana kiasi cha kiliacha finyango la mwili lidhihirike.

Inapendeza  kwa muumini kuitekeleza ibada  ya swala akiwa katika mavazi twahara , nadhifu,  mazuri ayapendayo , akiyavaa roho yake hutua  na kuburudika. Tunasema hivi kwa sababu  nguo inaweza kuwa twahara lakini sio nadhifu  wala nzuri

C/. Mipaka ya utupu nje  ya swala

i/. Mwanamume mbele ya mwanamume wenziwe na wanawake walio maharimu zake ni  sehemu ya mwili iliyo baina kitovu na magoti.

Ama mbele ya wanawake “ajnabiyyat” wa kando na kando wasio  maharimu ni mwili wake  wote isipokuwa na  vitanga kauli yenye kutegemewa katika riwaya ya Ummu Salamah –Allah aminiye radhi –asema Nilikuwa mbale ya Mtume  wa Allah Rehema na Amani  zimshukie akiwepo na Bi Maimuna (wote hawa ni wakeze) Akaja ibn Ummi Maktuum  na (tukio) hilo lilikuwa  ni baada ya kuamrishwa Hijaab Mtume akasema : “Jihifadhini nae”  tukamwambia : Ewe Mtume wa Allah,YEYE SI KIPOFU, HATUONI NA WALA HATUJUI Mtume akasema :

“Je, na nyinyi ni vipofu, hamuoni” Abuu Daawaoud na Tirmidhiy.

Kwa hiyo haijuzu kwa wanawake “Ajnabiyaat”  kuangalia zaidi ya uso na vitanga kwa mwanaume “Ajnabiy” NA WAAMBIE WAUMINI WA KIKE WAINAMISHE MACHO YAO NA WAZILINDE  TUPU ZAO………”(24: 31)

ii/.Ama mwanamke mbele ya wanawake  wenziwe waislamu utupu wake ni sehemu yote ya mwili iliyo baina ya uso na kitovu na mbele ya wanawake makafiri ni mwili wake wote ila sehemu inayodhihirika kwa dharura wakati wa kufanya kazi za nyumbani  na nyingine kama hizo.

Mbele ya wanaume maharimu zake  ni eneo lote lililo baina ya kitovu na magoti. Yaani  inajua kuwa wazi sehemu nyingine ya mwili isiyo hiyo tuliyoitaja mbele  ya naharimu zake lakini kwa sharti ya kutokuzuka fitna. Ikiwa fitna haiaminiki basi si ruhusa  Tusome pamoja    WALA WASIONYESHE MAPAMBO YAO ILA KWA WAUME ZAO,AU BABA ZAO, AU BABA ZA WAUME ZAO, AU WATOTO WAO, AU WATOTO WA WAUME ZAO, AU KAKA ZAO, AU WANA WA KAKA ZAO, AU WANA WA DADA ZAO, AU WANAAKE WENZIO ( Waislamu) AU “(24:31)

Ama mbele za wanaume “Ajaanibu” wa kando na kando : wasio waharimu zake ni mwili wake  wote Haijuzu kuonyesha sehemu yoyote ya  mwili wake mbele yao ila kwa udhuru unaokubalika kisheria haijuzu  kwa wanaume hao kumuangalia tusome:

“WAAMBIE WAUMINI WA KIUME WAINAMISHE MACHO YAO (wasitazame yaliyokatazwa ) NA WAZILINDE TUPU ZAO, HILI TAKASO KWAO…………24: 30

Imepokelewa kutoka kwa Bi. Aysha- Allah amuwiye  radhi – amesema : Alikuwa Mtume wa Allah –Rehema  na Amani zimshukie- akiswali alfajiri basi  wakihudhuria pamoja nae (SWALA) wanawake waumini wakiwa wamejiviringizia nguo zao Kisha  ( Ibada ya swala ) hurejea majumbani mwao, hapana  yeyote aliyeweza kuwatambua (kutokana na namna walivyovaa)  Bukhaariy.

FAIDA HALI/MAENEO AMBAYO KISHERIA INAJUZU KUFUNUA UTUPU NA KUUNGALIA

Inaruhusiwa na sheria kufunua na  kuuangalia utupu kwa nyudhuru zifuatazo:

1               Wakati wa kuposa kwa lengo la kuoa.  Hapa mposaji anapewa  ruhusa na sheria  kumtazama mwanamke anayetaka kumposa .

Anachoruhusiwa kuangalia ni uso na vitanga  tu na zoezi hili hufanyika mbele ya  mawalii wa binti sio faraghani baina ya  wawili hao peke yao.Tena ni kuangaliana  tu na sio kugusana.

2               Kutazama kwa ajili ya ushahidi au muamala.  Ili shahidi akubaliwe 

Na mahakama ya  Kiislamu  kutoa ushahidi dhidi  au kwa mwanamke ni lazima anamtambua. Hapo ndipo sheria inampa ruhusa ya  kumuangalia uso tu. Eneo lingine ni pale  anapochanganyika na mwanamke huyo katika  shughuli fulani kama vile biashara au ajira pia ni lazima ajue anafanya biashara  na nani au anamuajiri/anaajiriwa na  nani. Hapa pia anaruhusiwa kutazama uso tu.

3.                 Kutazama kwa sababu ya kutibu na kufanya dawa. Mwanamke anaumwa, Daktari ni mwanamume na hakuna daktari mwanamke.Sheria inamruhusu daktari  kumuangalia popote

Mwanamke huyo kwa lengo la tiba tu. Zoezi hili lifanyike mbele ya  maharimu wa mwanamke mgonjwa na sio  baina ya wagonjwa na daktari peke yao.

Imepokelewa na Jaabir ibn Abdillah –Allah amuwiye radhi:- kwamba Umu Salamah Allah amuwiye radhi – alimuomba Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie ya kupiga chuku.

Mtume akamuamrisha Abu Twaybah ampige chuku “ Muslim”

CHUKU (cupping) hii ni aina ya tiba inayohusisha ukataji wa mshipa maalum kwa lengo la kutoa  damu chafu mwilini 

Sharti la nne itatajwa katika somo lijalo.   inshaallah


TUJIFUNZE NA TUKUBALI: kuwa elimu ya swala ni  muhimu katika kuiswali swala itakiwavyo.


Forum | Guestbook | Tuandikie |