Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

SHARTI ZA SWALA ...

 

4. KUELEKEA QIBLAH.

Hii ndio sharti ya nne na ya mwisho miongoni mwa sharti za kusihi swala. Makusudi ya Qiblah ni Alka’aba tukufu; yaani Qiblah kiwe mbele yake makati wa kusali akielekee.

Mafaqihi; wataalamu wa fani ya fiqhi, wamekongamana na kuwafikiana kuwa inamuwajibikia mwenye kutaka kuswali kuuelekea msikiti mtukufu wa makkah ambamo humo ndimo ilimo Al-ka’aba. Kongamano hili linatokana na kauli ya Mwenyezi Mungu mtukufu ndani ya Qur-ani: “KWA YAKINI TUKIONA UNAVYOGEUZAGEUZA USO WAKO MBINGUNI. BASI TUTAKUGEUZA KWENYE KIBLA UKIPENDACHO BASI GEUZA USO WAKO UPANDE WA MSIKITI MTAKATIKFU (Al-Ka’aba) NA POPOTE MNAPOKUWA ZIELEKEZENI NYUSO ZENU (wakati wa swala) ULIKO (Msikiti huo) ---“ [2:144]

Dalili na ushahidi wa kuelekea Qiblah ndani ya Sunnah kwamba Mtume Rehema na Amani zimshukie alimwambia swahaba aliyekuwa akimfundisha namna ya kuswali: “Unapotaka kuswali, eneza udhu (tawadha udhu kamili), kisha elekea Qiblah na ulete takbirah”. Bukhaariy na Muslim.

Muradi wa “mtakatifu” uliotajwa katika aya na “Qiblah” katika hadithi ni Al-Ka’abah. Mtu mwenye kuiona Al-Ka’abah hii hapa mbele yake inamuwajibikia aielekee dhati yake na asiyeiona yuko mbali kinachomuajibikia ni kuelekea tu upande iliko Al-Ka’abah kama ilivyoelezwa na aya. Mtu asiyejua upande kilipo Qiblah na asimpate mtu wa kumuuliza kutamuwajibikia kujitahidi ndipo aswali kuelekea upande anaodhania kuwa ndio upande wa Qiblah na swala yake itakuwa ni sahihi. Lakini itakapombainikia ndani ya swala kwamba amekosea, kwa yakini upande ule sio upande wa Qiblah pale pale swala yake itabatilika na itampasa aianze swala yake upya kwa kuelekea upande ambao ana yakini kuwa ndio Qiblah. Hukumu itakuwa ni hii hii. Pia kama atakuwa na yakini ya kukosea hata baada ya kumaliza kuswali. Ama kosa lenyewe likiwa linatokana na dhana tu na sio yakini, basi hapana kurejea swala.

IX/.          NGUZO ZA SWALA.

Maana ya nguzo. 
Kabla hatujaanza kuzielezea na kuzichambua nguzo za swala moja baada ya nyingine ni vema kwanza tukajua nguzo ni nini nguzo ya kitu ni ile sehemu ya msingi ya kitu hicho kama vile kuta na msingi katika nyumba. Kwa hivyo basi nguzo ni kile kitu cha msingi ambacho upatikanaji wa jambo/kitu Fulani unakitegema. Rukuu na sijida, hizi ni baadhi ya sehemu za msingi zinazoijenga swala, nazo ndizo zinazoitwa nguzo za swala, swala haikamiliki wala kusihi ila kwa kutimia nguzo zake zote kwa namna na utaratibu uliopokewa kutoka kwa mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie kama nae alivyopokea kutoka kwa Jibril Amani ya Allah imshukie. Kwa kufupi, nguzo za swala ni kumi na saba, kama ifuatavyo.

1.  NIA.

Hii ndiyo nguzo ya kwanza ya swala.

Maana ya nia kwa ujumla
Hili ni kusudio la kutenda jambo/kitu Fulani hali ya kulikutanisha kusudio hilo na kitendo makusudi (kilichokusudiwa)

Maana ya nia katika swala.
Ni katika swala ni kuhudhurisha mwenye kuswali moyoni mwake kuingia ndani ya swala anayotaka kuiswali.

Mahala pa nia ni moyoni na wala haikushurutizwa kuitamka kwa ulimi katika kuithibitisha nia ijapokuwa ni bora zaidi  kukitamka kile anachokinuia, kwa mfano atasema anapotaka kuswali swala ya Ishaa.

USWALLIY RBAA RAKAAT FARDWHWAL ISHAAI LILLAAHI TAALA.
Akiwa anamfuata Imam atasema 
MAAMUMA

Na iwapo yeye ndiye Imam aseme 
IMAAMA

Miongoni mwa dalili zinazothibitisha kwamba nia ni nguzo ya swala ni kauli yake Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie: bila ya shaka kusihi kwa matendo yote kumefungamana na nia ---” Bukhaariy na Muslim.

Ili nia isihi ni lazima ikutanishwe na “Takbiyratul-Ihraam” – Takbira ya kuhirimia swala.

TANBIHI: Haitoshi tu ile nia anayotoka nayo mtu nyumbani kwenda msikitini kuswali. Hii kwa yakini si  nia bali ni AZIMIO kwa kuwa bado haijakutanishwa na kitendo chake ambacho ni swala yenyewe ambayo haianzii nyumbani kwake mtu. Mwenye kuswali inampasa asite kidogo kabla ya kuleta Takbiratul - Ihraam aihudhurishe nia ya swala anayotaka kuiswali kwa kuyatamka moyoni au moyoni na ulimini mfano wa maneno tuliyoyataja hivi punde tu. Hii ni kwa sababu nia aliyotoka nayo mtu nyumbani kuja msikitini ina kazi nyingine maalum ambayo sio ile ya wajibu wakati wa kuleta Takbiyratul-Ihraam. Hivyo ndiyo inavyofahamisha hadithi sahihi ya Bwana Mtume - Rehema na Amani zimshukie “Atakayejitwaharisha nyumbani kwake, kisha akaenda katika nyumba mojawapo miongoni mwa majumba ya Mwenyezi Mungu. Zitakuwa Khatua zake mbili, moja inaporomosha dhambi moja na ile nyingine inainua daraja moja”. Bukhaariy na Muslim.

Hii ndiyo kazi ya nia anayotoka nayo mtu nyumbani kwake kwenda msikitini kuswali . Nia ya swala inayozingatiwa kisheria ni ile inayokutanishwa na Takbria ya kuhirimia swala.

2. KUSIMAMA KWA MWENYE KUWEZA KATIKA SWALA YA FARDHI.

     Kuswali kwa kusimama katika swala ya fardhi ndiyo nguzo ya pili ya swala. Nguzo hii inamuhusu mtu aliye mzima, anayeweza kusimama bila ya taabu. Haya ni kwa  mujibu wa kauli tukufu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani ya Qur-ani Tukufu.
“ANGALIENI SANA SWALA (Zote kuziswali, khasa jamaa) NA (khasa) ILE SWALA YA KATI NA KATI NA SIMAMENI KWA UNYENYEKEVU KATIKA KUMUABUDU ALLAH” (2:238).
 Mradi na mapendeleo ya kauli (NA SIMAMENI KWA UNYENYEKEVU) ni kisimamo cha ndani ya swala.

     Dalili ya nguzo hii katika sunna. Imepokelewa na Imraan Ibn Huswayn-Allah amuwiye radhi - amesema: Nilikuwa na maradhi ya Bawasiri, nikamuuliza Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie - juu ya swala (niswali vipi)? Akanijibu” Swali kwa kusimama, ikiwa hauwezi (kusimama) swali kwa kukaa na kama hauwezi (kukaa) basi swali kwa kulalia ubavu”.  Bukhaariy

     Mtu atazingatiwa kuwa amesimama pale atakapokuwa  amenyooka wima, hakuinamia mbele au nyuma, kuliani na kushotoni. Akisimama kwa kupinda/kuinama japo kidogo bila ya udhuru kama uzee au maradhi swala yake itabatiklika, kwa sababu ya kukosekana nguzo ya kusimama ambayo ni sehemu inayounda swala.

     Mtu akiweza kuswali kwa kusimama katika baadhi ya swala na kushindwa katika baadhi nyingine, huyu atasimama pale awezapo kusimama na atakaa pale asipoweza.

     Ama kwa upande wa swala za sunnah, inajuzu mtu kuziswali akiwa amekaa hata  kama anaweza kusimama. Lakini atambue kuwa thawabu  anazozipata kwa kuswali akiwa amesimama ni nyingi zaidi kuliko zile atakazozipata kwa kuswali akiwa amekaa. Haya yanatokana na kauli ya  Bwana Mtume - Rehema na Amani zimshukie: “Atakayeswali kwa kusimama ndio bora, na atakayeswali kwa kukaa ana nusu ya ujira wa aliyesimama , na mwenye kuswali kwa kulala ana nusu ya ujira wa aliyekaa” Bukhaariy.

TANBIHI: Atakayeshindwa kusimama katika swala ya fardhi na akaswali kama awezavyo kwa kuwa “ALLAH HAIKALIFISHI NAFSI YOYOTE ILA YALIYO SAWA NA UWEZA WAKE.........” (2:286) atapata ujira  wake kamili sawa na yule aliyesimama. Hivyo ndivyo inavyosema hadithi iliyopokelewa na Abu Muusa Al-ash-ariy-Allah amuwiye radhi - kwamba Mtume–Rehma na amani zimshukie - amesema .”Mja atakapoumwa au kusafiri, Mwenyezi Mungu atamuandikia (thawabu) za aliyokuwa akiyatenda naye mzima mkazi (haumwi na hayuko safarini] “ Bukhaariy.  



Forum | Guestbook | Tuandikie |