|
Zingatia
suna hizi zilizo ndani ya swala katika vigawanyo (sehemu) viwili vifuatavyo:-
i/.
AB-AADH na
ii/.
HAY-AAT
Hebu
sasa, baada ya kujua mgawanyiko wa suna zilizomo ndani ya swala, tuangalie
maana ya kila kigwanyo na ufafanuzi wa suna zilizo chini yake.
i/.
AB-AADH
Maana: Hii
ni kila ile suna iliyomo ndani ya swala ambayo kuacha kwako kuitenda kwa
kusahau kutakupeleka kusujudu sijidat sahwu mwishoni mwa swala yako, kabla ya
kutoa salamu. Suna hizi za Ab-aadh ni pamoja na:-
1.
Tashahudi ya kwanza {Mwanzo}
Muradi na makusudi ya Tashahudi ya mwanzo ni ile
Tashahudi inayosomwa katika kile kitako/kikazi kisichoandamiwa na salamu
{kutoa salamu} Tashahudi hii hupatikana katika rakaa mbili za mwanzo za swala
za Adhuhuri, Alasiri, Maghribi, na Al-Ishaa. Ni suna iliyothibiti kutoka kwa
Bwana mtume Rehema na amani zimshukie kukaa kitako baada ya sijida ya pili ya
rakaa ya pili ya swala hizi tulizozitaja kwa ajili ya kuisoma tashahudi hii
ya mwanzo.
Dalili/Ushahidi:
Imepokelewa kauli ya
Bwana Mtume Rehemu na Amani
zimshukie katika hadithi ya yule mtu aliyekuwa akiswali sivyo ndivyo: “ ---
Utakapokaa katikati ya swala, basi jitulize ukae mkao wa Iftiraashi, halafu
usome Tashahudi ---“ Abuu Daawoud katikati ya swala. Baada ya sijida ya pili
ya rakaa ya pili ya swala husika. Halafu usome Tashahudi: Tashahudi ya
mwanzo.
Dalili na ushahidi unaothibitisha usuna wa
Tashahudi ya mwanzo na kwamba sio fardhi ni kwamba Mtume wa Allah Rehema na
amani zimshukie aliinuka katika swala ya Adhuhuri hali ya kuwa inamlazimu
kukaa kitako (cha Tashahudi ya mwanzo) (Akaendelea na swala) alipoikamilisha
swala yake akasujudu sijida mbili.” Bukhaariy na Muslim
Hadithi inatueleza kwamba Bwana Mtume alisujudu
sijida mbili za kusahau ikiwa ni badali ya ile Tashahudi ya mwanzo iliyoiacha
kwa kusahau kukaa kitako kwa ufahamu huo basi, lau kama Tashahudi ya mwanzo
ingelikuwa ni NGUZO/FARDHI bila ya shaka Bwana Mtume (ambaye ndie
aliyetufundisha swala na mengineyo ya kheri) angelilazimika kuileta nguzo
hiyo kwa kurudi chini, akakaa kitako akaisoma Tashahudi. Kisha akainuka na
kuendela na sehemu iliyobakia ya swala yake na wala asingeliiunga nguzo hiyo
kwa kuleta zile sijida mbili za kusahau kama tunavyofahamishwa na hadithi.
Elewa hivi ewe ndugu yangu wee, na hali ya kuwa Mola wako pekee ndiye MJUZI
mno wa yote na vyote.
2.
Kumswalia Mtume baada ya Tashahudi ya mwanzo.
Ni suna baada ya kumaliza kuyasoma matamko ya
Tashahudi ya mwanzo kama yalivyopokewa kutoka kwa mtume, kumswalia Bwana
mtume kabla ya kuinuka kuiswali rakaa ya tatu. Mwenye kuswali aiunge
Tashahudi yake na swala ya Mtume kwa kusema:
ALLAHUMMA SWALLI ALAA MUHAMMAD
3.
Kitako cha Tashahudi ya mwanzo.
Hizi ni suna tatu zinazofuatana pamoja lakini kila
moja inajitegemea kwa mpango huu:
Suna ya kitako.
Kwanza akae kitako baada ya kutoka katika sijida
ya pili ya rakaa ya pili ya swala yenye rakaa nne au tatu. Ndipo inafuatia.
Suna ya Tashahudi.
Baada ya kukaa kitako ndipo inapokuja fursa ya kuitekeleza
suna ya kuisoma Tahahudi ya mwanzo. Akimaliza kuisoma Tashahudi hii ya
mwanzo, ndipo inamalizia.
Suna ya kumswalia Mtume.
Mara tu baada ya kuyakamilsiha matamko ya
Tashahudui, ni suna kuyaandamizia matamko hayo na swala ya Mtume.
4.
Kuwaswalia Aali wa Mtume baada ya Tashahudi ya mwisho.
Ni suna thabiti kutoka kwa Bwana Mtume, kuwaswalia
Aali za Mtume sambamba na kumsalia Mtume baada ya Tahahudi ya mwisho Aseme:
ALLAHUMMA SWALLI ALAA MUHAMMAD WA ALAA AALI
MUHAMMAD
Hivi ndivyo ilivyokuja katika tamko la kumswalia
Mtume kama lilivyo katika hadithi zinazoibainisha nguzo ya Tashahudi.
5.
Qunuut.
Suna
hii huletwa katika itikadi ya rakaa ya pili ya swala ya Sub-hi/Alfajiri.
Imepokelewa kutoka wa swahaba wa Mtume Anas Ibn Maalik Allah amuwiye radhi
amesema:
“Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie hakuacha
kuleta Qunuut katika swala ya Sub-hi mpaka alipoaga dunia.” Ahmad
Suna
hii hutekelezwa kwa kumsifia Allah na kuomba dua ye yote aitakayo LAKINI
ukamilifu ni kujilazimisha kuilta ile ile Qunuut iliyopokewa kutoka kwa Mtume
wa Allah. Imepokelewa kutoka kwa Al-Hasan Ibn Aliy Allah awawiye radhi
amesema: Alinifundisha Mtume wa Allah maneno Rehema na Amani zimshukie
niyasema katika swala ya Witri.
“ALLAHUMMA-HDINII
FIIMAN HADAYTA, WA AAFINII FIMAN AAFAYTA, WATAWALLANII FIMAN TAWALLAYTA, WA
BAARIK LII FIMAA A-‘TAYTA, WA QINII SHARRA MAA QADHAYTA, INNAKA TAQDHII WALAA
YUQDHAA ALAYKA, WAINNAHU LAA YADHILLU MAN WAALAYTA, WALAA YAIZZU MAN ADAYTA,
TABAARAKTA RABBANAA WATAALAYTA” Abuu
Daawoud.
Ni
vema Imamu akaileta Qunuut kwa tamko la “jamii” wingi, yaani badala ya
kusema.
“ALAAHUMMA-HDINII
……………. WA AFINII
Kwa
tamko la “fardhi” upweke/umoja, aseme
ALLAHUMMA-HDINAA
………… WA AFINAA
Kwa
tamko la “jamii” linalomchanganya na kumjumuisha yeye pamoja na maamuma wake.
Ushahidi unaoonyesha kwamba suna ya Qunuut mahala pake ni katika
Itidali
ni hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah Allah amuwiye radhi kwamba
Mtume Rehema na Amani zimshukie alikuwa anapokiinua kichwa chake kutoka
katika rukuu ya swala ya subhi kwenye rakaa ya pili, huinyanyua juu mikono
yake na kuomba kwa dua hii:
ALLAHUMMA-HDINII
FIIMAN HADAYTA ………… al-Haakim.
Dalili inayothibitisha kwamba mtu anaweza kuomba dua nyingine yo yote
katika Qunuut kulingana na mazingira na wakti aliomo ni ile riwaya iliyopokelewa
kutoka kwa Abuu Raafi Nafii amesema: “Niliswali nyumba ya Umar Ibn Khatwaab
swala ya sub-hi, akakunuti (akaleta Qunuut) baada ya rukuu, (akaendelea
kusema) nikamsikia akisema:
“ALLAHUMMA INNAA NASTAINUKA, WA NASTAGHFIRUKA WA
NUTHNII ALAYKA, WALAA NAKFURUKA, WA NU-MINU BIKA, WA NAKHLA’U WA NATRUKU MAN
YAFJURUKA, ALLAHUMMA IYYAAKA NA’BUDU, WALAKA NUSWALLI WA NASJUDU, WA ILAYKA
NAS-A’AA WA NAHFIDU, WA NARJUU RAHMATAKA, WA NAKHAAFU ADHAABAKA, INNA
ADHAABAKA BILKUFFARI MULHAKU, ALLAHUMMA ADHHIBI-LKAFARATA, WA ALKI FI
QULUUBIHIMU-RRU’BA, WA KHAALIF BAYNA KALIMATIHIM, WA ANZIL ALAYHIM RIJZAKA WA
ADHAABAKA, ALLAHUMMA ADHHIBIL-KAFARATA AHLAL-KITAABI-LLADHIINA YASUDDUUNA AN
SABILIKA, WA YUKADHIBUUNA RUSULAKA, WA YUKAATILUUNA AWLIYAA-AKA,
ALLAHUMMA-GHFIR LILMUUMININA WALMUUMINAAT, WALMUSLIMIINA WALMUSLIMAATI, WA
ASLIH DHAATA BAYNAHUM, WA ALLIF BAYNA QULUUBIHIM, WAJ-A’L FII
QULUUBIHIMUL-IIMANA WAL-HIKMATA, WA THABBITHUM ALAA MILLATA NABIYYIKA, WA
AWZI-‘IHUM AN YUUFUU BIL-A’HDI ALLADHII A’AHADTAHUM ALAYHI WANSURHUM ALAA
ADUWWIKA WA ADUWWIHIM, ILAAHAL-HAKKI WAJA’LNAA MINHUM”
Imam
Abdurazaak katika Muswanaf.
FAIDA.
QUNUUT
KATIKA SWALA TANO.
Ni sheria kuleta Qunuut
kwa sauti katika swala tano wakati waislamu wanapofikwa na maafa/majanga
mbalimbali. Hili linatokana na riwaya ya Ibn Abbaas Allah awaridhie amesema:
Alikunuti Mtume wa Allah Rehema na amani zimshukie mwezi mzima mfululizo.
(Alileta Qunuut) katika swala za Adhuhuri, Alasiri, maghribi, Ishaa na subhi,
mwishoni mwa kila swala anaposema SAMI’ALLAHU LIMAN HAMIDAH ya rakaa ya
mwisho: akiwaombea maangamivu, watu wa kitongoji cha Baniy Sulaym wa kabila
za Ri’il, Dhak-waan na Uswiyyah, na watu walioko nyuma yake wakitikia
Aamiyn.” Abuu Daawoud na Ahmad.
Kwa nini Bwana Mtume aliwaombea maangamivu watu hawa?
Kisa chenyewe kama alivyosema Imam Ahmad kinaanzia pale walipomjia Mtume wa
Allah watu wa makabila haya matatu tuliyoyataja {Ri’il, Dhakwaan na Uswiyyah}
na kudai kwamba wao wameukubali uislamu na wamesilimu. Wakamuomba Bwana Mtume
awape waalimu watakao wafundisha dini. Bwana Mtume akakubali na akawapa
waalimu sabini (70). Lakini kumbe hawakusilimu kweli, wakawaua maswahaba wale
wote sabini. Kadhia hii ilimuudhi sana na kumkasirisha mno bwana Mtume na
kumpelekea kuuchukua uamuzi huu wa kuwaombea maangamivu watu wabaya hawa.
TANBIHI: Sijidat Sahwu itaelezwa kwa
ukamilifu na ubainifu wa kutosha katika somo la NNE Inshaallah.
|