Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

C) SUNA ZILIZO (ZINAZOFUATIA) BAADA YA KUMALIZIKA SWALA

 

Hizi ni aina ya suna za swala ambazo huletea baada ya swala kumalizika. Hizi zinakusanya:-

1.    Kuleta Istighfaari, dhikri na dua.

Imepokelewa kwamba Mtume Rehama na Amani zimshukie alikuwa anapomaliza swala yake huleta Istingfaari mara tatu na kisha akasema.

ALLAHUMMA ANTASSALAAM, WA MINKASSALAAM, TABAARAKTA YAA DHALJALAAL WAL-IKRAAM

Muslim

 Si vibaya kunyanyua sauti kwa Imamu wakati wa kuleta Istighfaari, dhikri na dua, kwa lengo la kuwafundisha maamuma wake. Wakishajua na kuzoea hasi walete dhikri hizo kwa sauti ya chini, isiyo ya kusikika kiasi cha kuwa ni kishawishi kwa watu wengine wanaoswali.

 Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbaas Allah awawiye radhi kwamba kunyanyua sauti kwa dhikri wakati watu wanapomaliza swala ya fardhi, kulikuwepo zama za Mtume – Rehema na Amani zimshukie.

Bukhaariy na Muslim.

 Imepokelewa kutoka kwa Ka’ab Ibn Ujirah – Allah amuwiye radhi kwamba Mtume Rehema na Amani zimshukie amesema “Viandamizi, harejei patupu msemaji wake baada ya kila swala ya faradhi (Viandamizi hivyo ni) Tasbih (Sub-haanallaah) thelathini na tatu, Tahmiydah (Al-hamdulillaah) thelathini na tatu, na Takbiyrah (Allaahu Akbar) thelathini na tatu” Muslim

 Imepokelewa kutoka kwa Muaadh Ibn Jabal – Allah amuwiye radhi – kwamba Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie alimshika mkono wake na kusema: “Ewe Muaadh, Wallah hakika mimi ninakupenda, akasema: “Ninakuusia ewe Muaadh, usiache usiache baada ya kila swala kusema:

ALLAHUMMA A’INNI ALAA DHIKRIKA WA SHUKRIKA WAHUSNI IBAADATIKA

Abuu Daawoud

Zipo dua na adhkaari nyingi sana za baada ya swala zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume, unaweza kurejea vitabu vya hadithi na Adhkaari ikiwa unapenda kuzijua.

 

2.    Kugura kwa ajili ya swala ya suna kutoka mahala paliposwaliwa swala ya fardhi.

Ni suna iliyothibiti kutoka kwa Bwana Mtume, mtu kugura (kuhama) mahala aliposwalia swala ya fardhi kwa ajili ya kuswali  swala ya suna baada ya swala mahala pengine Falsafa ya suna hii ni kwamba mahala anaposujudu mja patamshuhudia mbele ya Allah, kuitekeleza suna hii hakutamaanisha kingine zaidi ya kukithiri kwa sehemu zitakazomshuhudia (zitakazomtolea ushahidi).

Lakini ni bora zaidi kama hakuna kipingamizi (dharura) kwenda kuswali swala ya suna  nyumbani kwake mtu baada ya kuiswali swala ya faradhi msikitini pamoja na jamaa. Hayo ndiyo maelekezo na mafundisho kutoka kwa Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie:

“Enyi watu, swalini majumbani mwenu, kwani bora ya swala ni mtu  kuswali nyumbani kweke ila swala ya fardhi” Bukhaariy na Muslim.

Xi NAMNA YA KUSWALI

Baada ya kujifunza mambo mengi yahusianayo na swala, sasa ni vema tukajifunza namna ya kuswali ili kulitekeleza agizo la Mtume wa Alalh – Rehema na Amani zimshukie – lisemalo:

“Swalini kama mlivyoniona mimi nikiswali Bukhaariy.

Ni dhahiri kwamba amri na maelekezo haya ya  Bwana Mtume yalikuwa yanawagusa moja kwa moja maswahaba wake, kwa kuwa wao ndio walikuwa pamoja nae wakamuona anavyoswali. Ama sisi amri hiyo nasi inatugusa lakini si kwa njia ya moja kwa moja kama maswahaba. Sisi hatuwezi kuswali kama alivyoswali Bwana Mtume kwa kuwa hatukuishi nae kwa hiyo hatukupata bahati ya kumuona akiswali kama alivyofundishwa na mwalimu wake Malaika Jibril-Amani ya Allah imshukie kwa amri na maelekezo ya Allah: “Alinijia Jibril – Amani imshukie mwanzo kabisa mwa wahyi (ufunuo) akanifundisha udhu  na swala………………..”  Al-haakim, Baihaqiy na Ahmad.

Sisi tunaswali kama maswahaba wa Mtume wa Allah – Allah awawiye radhi, kwani wao ndio waliotufundisha dini ndani yake ikiwemo swala. Ni kwa kuwafuata wao tu ndio tunaweza kuswali kuwa alivyoswali  Mtume wa Allah. Sasa hebu tufuatane nao kwa makini watufundishe swala ili nasi tuweze kuswali kama alivyokuwa akiswali mwenyewe Bwana Mtume, nae kama alivyofundishwa na Jibril kwa amri ya Allah. Ewe Mola wa haki wee! Tuongoze na utuwafikishe kuswali, kufunga, kuhiji, kutoa zakkah na baki ya amali nyingine kama alivyofundisha kipenzi chako, Nabu Muhamaad Aamiyn!

Haya na tuswali sasa:

1.    Baada ya kujitwaharisha na kuingia wakati wa swala unayotaka kuiswali na kujistiri tupu (uchi) kama tulivyobainisha katika darasa zilizotangulia, simama wima uelekee Qiblah kwa kuitekeleza amri ya Mola wako. “NA POPOTE UENDAKO GEUZA USO WAKO KWENYE MSIKITI MTAKATIFU.NA POPOTE MLIPO GEUZENI NYUSO ZENU UPANDE ULIKO (msikiti huo)……………………. (2: 150)

Muradi na makusudio ya “msikiti Mtakatifu” hapa ni dhati ya Al-ka’abah”, hivi ndivyo inavyobainishwa na hadhiti kadhaa. Miongoni mwazo ni hii:

Imepokelewa na Ibn Abbaas – Allah awawiye radhi amesema: Mtume Rehama na Amani zimshukie alipoingia ndani ya Al-ka’abah aliomba dua katika pande zake zote na hakuswali (mle ndani) mpaka alipotoka nje. Alipotokea nje akaswali rakaa mbili mbele ya Al-kaabah na akasema “Hiki ndio Qiblah. Bukhaariy na Muslim.

2.    Baada ya kusimama na kuelekea Qiblah, ni wajibu utie nia ya swala unayotaka kuswali moyoni. Huko ni kumfuata Mtume kwa kutekeleza kauli yake, “Hakika si vinginevyo amali zote zimefungamaan na nia na kila mtu atalipwa kwa kadri ya nia yake………”  Bukhaariy

Nyanyua vitanga vya mikono mpaka mkabala wa mabega yako hali ya kuleta nia na kisha useme (Allah Akbar) Hivyo ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Ibn Umar – Allah awawiye radhi – amesema: “Alikuwa Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie anaposimama kuswali, hunyanyua mikono yake (vitanga) mpaka ikawa mkabala na mabega yake kisha akakabiri (akasema Allahu Akbar)………..”Muslim.

3.    Halafu funga swala kwa kuiteremsha mikono na kuiweka chini ya kifua, huku ukiushika mgongo wa kitanga cha mkono wa kushoto kwa kile cha kulia. Hivi ndivyo atufundishavyo swahaba Waail Ibn Hijri – Allah amuwiye radhi amesema: “Nilimuona Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie anapoingia ndani ya swala  huushika mkono wake wa kushoto kwa ule wa kulia’ Ibn Mundhir, Ibn Khuzaymah na Abuu Dawoud.

4.    Kisha fungua swala yako kwa kuleta dua ya ufunguzi wa swala (Iftilaahi). Hili linatokana na kauli ya Imam Aliy-Allah amuwiye radhi amesema: “Alikuwa Mtume wa Allah- anaposimama kuswali husema.

WAJJAHTU WAJHIYA LILLADHI FATARASWAMAAWATI WAL-ARDHI HANIIFAN WAMAA ANA MINALMUSHRIKIIN, INNA SWALAATIY WA NUSUKII WA MAHYAAYA WA MAMAATIY LILLAHI RABBIL-AALAMIIN LAA SHARIIKA LAHU WABIDHALIKA UMIRTU WA ANAA MINAL-MUSLIMIIN. Muslim na Ibn Hibban.

5.    Baada ya kumaliza kusoma dua hiyo ya ufunguzi wa swala, lete “Audhubillah kabla ya kuanza kusoma Al-hamdu. Hayo ndiyo maelekezo ya Mola wako, sikia: “NA UKITAKA KUSOMA QUR-ANI PIGA AUDHU (Kwanza, jikinge) KWA ALLAH (akulinde) NA SHETANI ALIYEFUKUZWA (Katika rehema ya Allah)” (16: 98)

Kadhalika imepokelewa kutoka kwa Mtume – Rehema na Amani zimshukie kamba: “Alikuwa akisema baada ya Iftitaahi (dua ya ufunguzi) na kabla ya kisomo (cha Al-hamdu).

 AUDHU BILLAHI-SSAMI’UL-ALIIM MINAS-SHAITAANI-RRAJIIM. Abuu Daawoud.

6.    Halafu soma Suuratil – Faatihah (Al-hamdu) kwa kuanza na Bismillahi kwani hiyo Bismillahi ni aya miongoni mwa aya zake (Al-hamdu). Hivyo ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Abuu Huray-rah-Allah amuwiye radhi – amesema: Amesema Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie: “ Mnaposoma Al-hamdulillah” someni BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM kwani hiyo ndiyo Umul-Qur-ani, Umul-Kitaab na Sab-ul-mathaaniy, na BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM  ni mojawapo ya aya zake. Daaru qutwniy na Baihaqiy.

7.    Unapofikia mwisho wa Al-hamdu WALADHWAAALIIN itikia “Amiyn” Hivi ndivyo ilivyopokelewa na Abuu Hurayrah – Allah amuwiye radhi – kwamba Mtume wa Allah – rehema na Amani zimshukie amesema: “Atakaposema  Imamu WALADHWAAALIIN Semeni Aamiyn, kwani itakayewafikiana Aamiyna yake na Aamiyna ya malaika, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia (yaliyopita)” Bukhaairy.Forum | Guestbook | Tuandikie |