|
KANUNI:
Kila linalopingana na suna ye
yote miongoni mwa suna za swala tulizokwisha
zibainisha katika darasa zilizotangulia. Hilo
linaingia ndani ya uzio wa yaliyo karaha
kutendwa ndani ya swala.
Na makruhu (lilio karaha): Ni
kila lile ambalo mswaliji akiacha kulitenda
ndani ya swala hulipwa thawabu na wala
haadhibiwi kwa kulitenda. Kwa mfano kuacha
takbira za maguroguro, yaani kuhama kutoka
katika nguzo moja hadi nyingine, ni makruhu. Kwa
sababu kuzileta hizo takbira ni suna. Na pia
kuacha kuleta dua ya ufunguzi wa swala ni
makruhu, kwa sababu ni suna kuileta.
Isipokuwa kuna baadhi ya mambo
maalumu ambayo ni suna kujiepusha nayo na ni
karaha kwa mswaliji kuyatenda. Yafuatayo ni
baadhi ya mambo hayo:
KUGEUKA KWA SHINGO NDANI YA
SWALA:
Ni jambo la makruhu mswaliji
kugeuka kwa kuizungusha shingo yake ndani ya
swala ila kama kuna dharura implekeayo kufanya
hivyo. Imepokelewa kwamba Bwana Mtume-Rehema na
Amani zimshukie-amesema: “Allah mtukufu haachi
kuwa ni mwenye kumuelekea mja wake ndani ya
swala yake maadamu hajageuka. Akigeuka naye
(Allah) hukengeuka naye (mja wake)”. Abuu
Daawoud & wengineo
Na Bwana Mtume amekwisha
bainisha kwamba kugeukageuka ndani ya swala
hakika si vinginevyo ila: “Ni uporaji
anaoufanya shetani katika swala ya mja”.
Bukhaariy
Hii ni kwa sababu kugeuka ndani
ya swala kunapingana na unyenyekevu unaotakiwa
ndani ya swala. Ama kukiwa na dharura
inayomlazimisha kugeuka kama vile kumuangalia
adui anayemnyemelea mathalan, katika hali hii si
karaha kugeuka. Hii ni iwapo ugeukaji huo
utahusisha shingo tu bila ya kifua. Ama iwapo
mswaliji atageuka kwa kutumia kifua akawa
amekengeuka na Qiblah, hapo swala yake
itabatilika kwa kuacha kwake nguzo ya swala
ambayo ni kuelekea Qiblah. Ama kutupa jicho tu
bila ya kugeuka si vibaya, ijapokuwa si vizuri
kufanya hivyo bila ya kuwa na dharura. Imekuja
katika hadithi ya Aliy Ibn Sheibaan-Allah
amuwiye radhi-amesema: Tulifika kwa Mtume wa
Allah-rehema na Amani zimshukie-tukaswali pamoja
naye. Akamuona kwa jicho pembe mtu mmoja
hanyooshi mgongo wake katika rukuu na sijida,
akasema: “Hana swala hasiyeunyoosha uti wa
mgongo wake”.-Yaani hatulizani katika rukuu
yake. Ibn Hibbaan
KUANGALIA JUU:
Si suna kwa mswaliji kuswali
huku anaangalia juu, kwani kufanya hivyo ni
karaha. Imepokelewa kutoka kwa Anas-Allah
amuwiye radhi-kwamba Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-amesema: “Wana nini watu
wanaonyanyua macho yao juu ndani ya swala
zao?” Kisha akasema: “Wakome kufanya hivyo
au macho yao yatapokonywa”. Bukhaariy
KUFUNGA NYWELE AU KUPANYA NGUO:
Ni karaha kwa mswaliji kuswali
huku amefunga nywele au kupanya nguo. Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Nimeamrishwa kusujudu kwa kutumia viungo saba
na wala nisikunje nguo wala nywele”.
Bukhaariy
KUSWALI NA ILHALI CHAKULA KIKIWA
TAYARI KIMETENGWA:
Ni karaha kwa mswaliji kuswali
na ilhali chakula kiko mbele yake tayari kwa
kuliwa na nafsi yake ikawa inakitamani. Ukaraha
huu unatokana na kule kushughulishwa nafsi,
jambo ambalo huondosha unyenyekevu ndani ya
swala. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah
amuwiye radhi-amesema: Amesema Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Itakapowekwa
Ashaa (chakula cha usiku) ya mmoja wenu na swala
ikakimiwa, basi na anzeni na Ashaa hiyo na wala
hasifanye haraka mpaka amalize”.
Bukhaariy & Muslim
KUSWALI KATIKA HALI YA KUBANWA
NA HAJA NDOGO AU KUBWA:
Mswaliji hatakiwi kuswali na
huku amebanwa na haja ndogo au kubwa, kwa sababu
katika hali kama hii haitamkinika kuipa swala
haki yake. Yaani unyenyekevu na kuhudhuria ndani
ya swala kutakosekana. Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-amesema: “Hakuna swala mbele
ya chakula wala mtu anaposukumwa na vichafu
viwili”. –Yaani haja ndogo na kubwa.
Muslim
KUSWALI HUKU UNASINZIA:
Ni karaha kuswali katika hali ya
kusinzia sana, kwa sababu ni muhali katika hali
hii mtu kudhibiti anachokisema na kukifanya
ndani ya swala yake. Imepokelewa kutoka kwa Bibi
Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa
Allah-rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Ataposinzia mmoja wenu na ilhali anaswali,
basi na alale mpaka usingizi umuishe. Kwani
mmoja wenu akiswali huku anasinzia, huenda akawa
analeta istighfaari na kumbe anajitukana
mwenyewe (anajilaani)”. Bukhaariy & Muslim
KUSWALI KATIKA SEHEMU ZIFUATAZO:
Ni karaha kwa mswaliji kuswali
hamamuni (mahala pa kukoga pa jumuia),
njiani/barabarani, sokoni, makaburini, kanisani,
majaani na mahala ipumzikiapo mifugo. Ukaraha
huu unatokana na dhana ya kuwepo najisi katika
baadhi ya sehemu hizo na kushughulika moyo
katika sehemu nyingine. Imepokelewa kutoka kwa
Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-amesema: “Ardhi yote ni msikiti (ni
mahala pa kuswalia) ila makaburini na
hamamuni”.
“Msiswali katika mapumzikio ya
ngamia”. Ibn Hibbaan |