Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

B. IQAAMA  

 

Iqaamah kama ilivyo adhana ni suna muakadah (kokotezwa) katika swala za fardhi zinazoswaliwa ndani ya wakati wake (Adaa) au zinazoswaliwa nje ya wakati wake (Qadhwaa). Iqaamah ni suna kwa jamaa na mwenye kuswali pekee kwa watu wanamume na wanawake. Iqaamah ni mithili ya adhana ila kwa tofauti chache zifuatazo:-

Matamko ya adhana ni mara mbili mbili wakati ambapo matamko ya Iqaamah ni mara moja moja tu. Dalili juu ya hili ni hadithi ya Anas-Allah amuwiye radhi: “Bilali aliamrishwa kuifanya shaf-i adhana na kuiwitirisha iqaamah, ila tamko la iqaamah (Qad Qaamatis-swalaah)”. Bukhaariy & Muslim

Shaf-i ni hesabu iwezayo kugawika kwa mbili, na witri ni ile isiyogawika kwa mbili.

 

TAMKO LA IQAAMAH:

Lifuatalo ndilo tamko kamili la iqaamah kama lilivyothibiti katika hadithi nyingi sahihi zilizopokelewa na maimamu Bukhaariy, Muslim na wengineo:

ALLAAHU AKBAR ALLAAHU AKBAR,

ASH-HADU AN LAA ILAAHA ILLAL-LAAH,

ASH-HADU ANNA MUHAMMADAN RASUULULLAAH,

HAYYA ALAS-SWALAAH, HAYYA ALAL-FALAAH,

QAD QAAMATIS-SWALAAH, QAD QAAMATIS-SWALAAH,

ALLAAHU AKBAR ALLAAHU AKBAR,

LAA ILAAHA ILLAL-LAAH.

Adhana hutolewa kwa sauti ya taratibu (kuvuta kidogo) wakati ambapo iqaamah hutolewa kwa sauti ya haraka kidogo. Hii ni kwa sababu falsafa ya adhana ni kuwaita walio mbali, kwa hiyo njia ya utuvu wa sauti (Tartiyl) ikawa ndio ifikishayo zaidi wito. Na iqaamah inakusudia kuwainua watu waliohudhuria mahala pa swala kuswali, kwa hiyo ikawa kutolewa kwa sauti ya haraka haraka mithili ya mtu aamrishaye ndio kunanasibikiana zaidi na hali hii. Hivi ndivyo Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alivyomwambia Bilali-Allah amuwiye radhi: “Utapoadhini fanya utuvu (taratibu) na utapokimu fanya haraka”. Tirmidhiy

Mtu aliyepitwa na swala na akataka kuzikidhi (kuziswali nje ya wakati wake), ataadhini kwa ajili ya swala ya mwanzo tu na atakimu kwa kila swala. Ushahidi wa hili ni kwamba Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Alijumuisha Muzdalifah baina ya swala ya Maghribi na ile ya Ishaa kwa adhana moja na iqaamah mbili”. Muslim

SHARTI ZA IQAAMAH:

Sharti za iqaamah ndizo zile zile sharti za adhana, zirejee katika somo la adhana utazikuta. Hakuna sababu wala dharura ya kurudia kuzitaja tena hapa.

SUNA ZA IQAAMAH:

Hizi nazo ni zile zile suna za adhana isipokuwa hapa katika iqaamah kuna ziada kama ifuatavyo:-

MUADHINI KUTAWALIA IQAAMAH:

Ni bora mtu aliyeadhini ndiye akimu swala kwa kufuata suna ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Atakayeadhini ndiye atakayekimu”. Lakini akiadhini mtu mmoja na akakimu mwingine itajuzu.

KUJIBU IQAAMAH:

Kumesuniwa kwa mwenye kuisikia iqaamah kusema: “AQAAMAHALLAAHU WA ADAAMAHAA” Abuu Daawoud

KUBADILISHA MAHALA PA ADHANA NA IQAAMAH:

Ni suna iqaamah isiwe mahala pa adhana, yaani mtu akiadhini hapa basi akakimu kule. Asiadhini na kukimu sehemu hiyo hiyo, usuna huu haulengi kuibatilisha adhana na iqaamah vilivyofanywa mahala pale pale. Bali unakusudia kueleza ilivyo bora na suna ni vipi. Na iqaamah iwe kwa sauti ya chini zaidi kuliko ile ya adhana.

IDHINI YA IMAMU KATIKA IQAAMAH:

Muadhini hapaswi kukimu swala ila kwa idhini ya imamu, kwani hivyo ndivyo alivyokuwa akifanya Bilali; muadhini wa Mtume. Katika hadithi ya Ziyaad Ibn Al-Haarith amesema: “Nikawa ninamwambia Mtume-Rehema na Amani zimshukie-nikimu nikimu?”

Kadhalika amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Muadhini ndiye mwenye haki ya kumiliki adhana na imamu ndiye mwenye kumiliki iqaamah”. Ibn Adiy

MAAMUMA WASIINUKE KABLA YA IMAMU WAO:

Itapokimiwa swala, maamuma wasiinuke mpaka ainuke imamu wao kwanza au awaruhusu kuinuka kabla yake. Haya yanatokana na kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Itakapokimiwa swala, msiinuke mpaka mnione mimi (nimeinuka)”. Bukhaariy & Muslim

Maamuma wanatakiwa kuinuka kuswali mara baada ya kumalizika kwa iqaamah, hivi ni iwapo wamo msikitini pamoja na imamu wao.

 

TANBIHI:

Kunashurutizwa kutokuwepo mwanya mrefu baina ya iqaamah na swala, na mwanya ukirepa (ukirefuka) au likapatikana tendo linalohesabiwa kuwa ni mkata iqaamah. Tendo hili ni kama vile mtu kula baada ya iqaamah, katika hali na mazingira kama haya kutapasa kuirudia tena iqaamah.

Ni suna imamu kuhirimia swala mara tu baada ya kumalizika kwa iqaamah. Asiache mwanya mrefu baina ya iqaamah na ihraamu ila kwa kiasi cha kujishughulisha na jambo la suna. Mithili ya imamu kuwaamrisha maamuma wake kunyoosha safu zao, ageuke kuliani na kushotoni kwake akisema: ISTAWUU RAHIMAKUMULLAAH. Maana: Linganeni sawa, Allah akurehemuni. Katika suala hili, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akisema kuwaambia maswahaba wake: SAWUU SWUFUUFAKUM, FAINNA TAS-WIYATIS-SWAFFI MIN TAMAAMIS-SWALAAH”. Bukhaariy & Muslim.

Haijuzu iqaamah ya mwanamke kwa mwanamume.

 

 

KIAMBATISHI

ADHANA ISIYO YA SWALA:

Kumesuniwa kutolewa adhana pindi kutakapotokea katika jamii ya waislamu mambo kadhaa mbali ya swala. Mambo hayo yaliyosuniwa adhana ni pamoja na:-

Kumuadhinia mtoto katika sikio lake la kulia mara tu baada ya kuzaliwa, kama ambavyo ni suna kuleta iqaamah katika sikio lake la kushoto. Suna hii inatokana na kitendo cha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kumuadhinia sikioni mjukuu wake; Hassan alipozaliwa na Bibi Faatimah (bintiye). Riwaya hii ameipokea imamu Tirmidhiy

Adhana wakati linapotokea janga la moto. Falsafa ya adhana hii ni kuwaita waislamu kuja kutoa msaada wa uokozi na kuzima moto.

Adhana wakati wa vita. Falsafa ya adhana hii ni kuwakusanya waislamu kwa lengo la kwenda vitani kuihami dini ya Allah.

Kumuadhinia mtu aliyeanguka mweleka, mtu aliyeghadhibika mno, mtu mwenye tabia mbaya na mtu aliyesibiwa/aliyekumbwa na shetani wa kijini. Falsafa ya adhana hii ni kuwaondoshea shari watu hawa kwa utajo huu wa Allah, hii ni kwa sababu shetani hukimbia mbali anapoisikia adhana.

 

b). WITO WA SWALA ZISIZO ZA FARDHI:

Imethibiti kutokana na maelezo yetu yaliyotangulia kwamba adhana na iqaamah ni suna zilizokokotezwa (Muakadah) kwa swala za fardhi. Ama swala nyingine zisizo za fardhi na ambazo zimesuniwa kuswaliwa jamaa mithili ya swala za Eid mbili (Eid ya mfunguo mosi baada ya Ramadhan na ile ya mfunguo tatu baada ya hijjah). Swala za jua kupatwa na mwezi na mwezi kupatwa na jua na swala ya jeneza. Hizi hazikusuniwa ndani yake adhana wala iqaamah, bali wito wake ni mtu kusema: AS-SWALAATU JAAMI’AH. Imepokewa kutoka kwa Abdullaah Ibn Amrou-Allah amuwiye radhi-amesema: Wakati jua lilipopatwa katika zama za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kulinadiwa: As-swalaatu jaami’ah”. Bukhaairy & Muslim

Ichukuliwe swala hii ya kupatwa kwa jua kama mizani ya kupimia swala nyingine za suna zilizosuniwa kuswaliwa jamaa.

 


 

 


Forum | Guestbook | Tuandikie |