KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

VITA VYA NAHAAWANDI

Ama mfalme wa Fursi, alipo kusanyikiwa na makundi hapo Nahaawandi; eneo katika mikoa ya ukanda wa majabali, Kusini mwa Hamadhaan. Akayaendea makundi hayo akitokea Marwa na wakasimama kumsaidia wafalme walio baina ya Al-Baab, Sindi, Khurasaan na Helwaan. Na maeneo yote haya ndio mipaka ya ufalme wa Fursi kwa upande wa Kaskazini/Kusini na Mashariki/Magharibi.

 

Kamanda Sa’ad akamuandikia waraka Sayyidna Umar-Allah amuwiye radhi-kumjulisha khabari hiyo. Na ni kipindi hicho hicho, ndimo kamanda Sa’ad alishitakiwa na kundi la watu wa Koufah, wakimtuhumu ya kwamba hafanyi uadilifu katika utawala wake. Akasema Sayyidna Umar baada ya kufikiwa na mashtaka hayo: Wallah, hali waliyo nayo Waislamu huko (hivi sasa) haitanizuia kuchunguza mashitaka yao haya. Akamuita kamanda Sa’ad afike mbele yake na akamkaimisha Sayyidna Abdullah Bin Abdillah Bin Itbaan kushika mahala pake. Sa’ad akaondoka kuelekea Madina kuitika wito wa Amirul-Muuminina; Sayyidna Umar. Na wakati huo huo Sayyidna Umar akamtumia Muhammad Bin Maslamah kupata ithibati ya mashitaka dhidi ya Sa’ad. Huyu akafuatilia nyenendo za wafanyakazi walio tuhumiwa, akamkuta kamanda Sa’ad hana hatia ya tuhuma alizo tuhumiwa nazo. Pamoja na uthibitisho huu unao mvua kamanda wake na tuhuma nzito za kutokuwa muadilifu, Sayyidna Umar hakupenda kuweko na chuki baina ya kiongozi na raia wake, kwa sababu hilo hupelekea kushindwa na kuregea. Kwa kulizingatia hili, akamvua Sa’ad uongozi wa Koufah na akamtawaza mahala pake Noumaan Bin Muqarrin Al-Muzaniy. Wakati wa uteuzi wake, Noumaan alikuwa amejitoma katika kundi la wazalendo wa Koufah huko Jundisaabour na Suus. Sayyidna Umar akamuandikia tamko la uongozi, na hii ndio sura yake:

KWA JINA LA ALLAH, MWINGI WA REHEMA, MWENYE KUREHEMU.

         Kutoka kwa mja wa Allah; Umar-kiongozi wa waumini.

         Kwenda kwa Noumaan Bin Muqarrin.

Amani ya Allah ikushukie!

Hakika mimi ninakuhimidia Allah ambaye hapana Mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila Yeye.

Ama baad...Hakika imenifikia khabari ya kwamba makundi makubwa ya Waajemi yamejikusanya katika mji wa Nahaawandi kwa ajili ya kukushambulieni. Utakapo fikiwa na waraka wangu huu, basi enenda kwa amri ya Allah na kwa msaada wa Allah na kwa nusura ya Allah. Enenda na Waislamu walio pamoja nawe, wala usiwapandishe jabali ikawa umewaudhi na wala usiwanyime haki yao, wasije wakakufuru na usiwatilie chuki. Kwani hakika muislamu mmoja ni bora mno kwangu mimi kuliko dinari laki moja.

Amani ya Allah ikushukie!

[TAARIKHUT-TWABARIY 02/503]

 

Na akamuamuru kwenda katika eneo la Maai ili yamkusanyikie majeshi huko, kisha ndipo ayaongoze kuelekea Nahaawandi yalipo jikusanya makundi ya makafiri. Na akamwandikia waraka Abdullah Bin Abdillah; kaimu wa Sa’ad katika mji wa Koufah, akimuamrisha kuwahamasisha watu kutoka kwenda kwa Noumaan. Na akalitumia ujumbe jeshi la Al-Ahwaaz akiliamuru kubakia hapo hapo ili wawe ni kizuizi (ngome) baina ya watu wa jimbo la Faaris na wale walio kusanyika Nahaawandi.

Majeshi ya Kiislamu yalipo kusanyika kwa kamanda mpya; Noumaan kama yalivyo agizwa. Kamanda Amrou akawatuma Amrou Bin Thaniy, Amrou Bin Ma’ad Yakrib na Twulaihah Bin Khuwailid, kwenda kuichunguza njia iliyo baina ya Maai na Nahaawandi. Ama Amrou Bin Thaniy, alirejea usiku ule ule, akaulizwa: Kipi kilicho kurejesha? Akajibu: Sikuwa mjuzi wa ardhi (nchi) ya Waajemi na (kidesturi) ardhi humuangamiza asiye ijua nayo huangamizwa na mwenye kuijua. Amrou Bin Ma’ad Yakrib, yeye alirudi asubuhi ya siku ya pili, nae akaulizwa juu ya alicho kiona, akasema: Tumetembea mchana kutwa na usiku kucha, hatukuona chochote. Ama Twulaihah yeye aliendelea kwenda mpaka akaliona jeshi la Wafursi, akalitambua na akarejea. Na akawaeleza ya kwamba baina yao na Nahaawandi hakuna lolote baya la kuwadhuru.

Kamanda Noumaan akaliongoza jeshi, akaenda ilhali kikosi tangulizi kikiongozwa na ndugu yake Nuaim Bin Muqarrin. Na vikosi viwili vya pembeni viliongozwa na ndugu yake mwingine Suweid Bin Muqarrin na Hudheifa Bin Al-Yamaan. Na kikosi tapanyi kiliongozwa na Qa’aqaa na hatamu za uongozi wa kikosi cha nyuma zilishikwa na Mujaashi’i Bin Masoud. Na wakajiwa na nguvu ya ziada kutoka Madina, ikiongozwa na Mugheera Bin Shu’ubah. Nguvu hii ilipo fika Nahaawandi, kamanda Noumaan akapiga takbira, jeshi nalo likaipokea takbira yake, kisha wakashusha mizigo. Hema la kiongozi wa mapambano; kamanda Noumaan lilijengwa na wakubwa wa Koufah; Hudheifa Bin Al-Yamaan, Uqbah Bin Aamir, Mugheera  Bin Shu’ubah, Basheer Bin Al-Khaswaaswiyah, Handwalah yule muandishi, Jarir Bin Abdillah, Ash-ath Bin Qays na wengineo. Hawakupata kuonekana wajenzi mahiri wa mahema katika Waarabu kama hawa.

Kisha Waislamu wakawasha mapambano, wakapigana siku ya Jumatano, Al-Khamisi na siku ya Ijumaa Wafursi wakajitia mahandakini mwao. Waislamu wakachelea usije kurepa muda wa kungojea mpaka watoke, wakashauriana cha kufanya na hatimaye wakapitisha azimio la kumpa Qa’aqaa uamiri wa kuwasha vita. Wafursi watakapo pambana nae, aonyeshwe kushindwa mbele yao na watakapo mfuata na wakawa baina ya Waislamu, hapo watapambana nao na Allah atalipitisha alitakalo. Kamanda Noumaan akamuamuru Qa’aqaa kuwasha mapambano, nae akatekeleza. Wafursi wakatoka mahandakini mwao kuja kujibu mashambulizi, wakamfuata wakiwa na furaha kwa sababu hawakupata kuiona hali kama hiyo kwa Waislamu hapo kabla. Wakaendelea kusonga mbele mpaka wakawa karibu na jeshi la Noumaan, nae akaliamuru jeshi lake kutopigana mpaka atakapo toa idhini ya kufanya hivyo. Na akangojea ule muda ambao Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akipenda kupigana ndani yake, pale linapo pinduka jua. Ulipo fika wakati huo akapiga takbira na kuanzisha mashambulizi na Waislamu wakamfuata na akasema: Nikiuawa, basi amiri jeshi baada yangu atakuwa ni Hudheifa.

Waislamu na Wafursi wakapambana mpambano ambao hawajapatapo kuuona wala haufanani na ule mpambano wa Qaadisiyah. Katikati ya mapambano, kamanda Naoumaan akauawa shahidi, ndugu yake Nuaim akamfunika nguo na kuficha habari ya kuuawa kwake ili jeshi lisiregee na jihadi. Bendera ya vita ikashikwa na Hudheifa na mapambano yakaendelea mpaka jioni. Usiku ulipo ingia, Wafursi wakaingiwa na ushindwa kiasi cha kushindwa kuiona njia ya kurudia mahandakini mwao, wakapotea. Na badala yake wakaelekea upande uliko kuwako moto wanao uabudu, wakaangukia humo wengi miongoni mwao. Fairazaana akaokoka, akaelekea Kaskazini upande wa Hamadhaan, kipote cha jeshi kikamfuatilia na wakafanikiwa kumdiriki na kumuua katika jangwa la Hamadhaan na wakaufungua mji wa Hamadhaan kwa suluhu. Habari hii ilipo mfikia Maheen akaharakia kutaka suluhu, akakubaliwa. Na ifuatayo ndio nukuu ya waraka wa mkataba wao kama ilivyo pokewa na Imamu Twabariy:

KWA JINA LA ALLAH, MWINGI WA REHEMA, MWENYE KUREHEMU.

         Haya ndio aliyo wapa Hudheifa Bin Al-Yamaan watu wa eneo la maji la Bahraadhaan, amewapa amani ya nafsi zao, mali zao na ardhi zao. Wasibadilishiwe mila (dini) yao na wasizuiliwe kutekeleza sheria zao. Nao wana haki ya kupata ulinzi muda wa kutoa kwao kodi kila mwaka kwa Waislamu walio watawalia. Kodi hii ni wajibu kwa kila aliye baleghe, itoke katika mali yake na nafsi yake kwa kadiri ya uweza wake. Na muda wa kufuata kwao maongozi wanayo pewa mchana na usiku na wakatekeleza ahadi. Ikiwa watafanya udanganyifu na wakabadilisha (tuliyo kubaliana), basi dhima yetu hii iko mbali nao.

Tamko hili limeshuhudiwa na Qa’aqaa Bin Amrou, Nuaim Bin Muqarrin na Suweid Bin Muqarrin na limeandikwa katika mwezi wa Muharram, mwaka wa 19.

Kisha baada ya hapo, kikosi hiki kikarejea na ilhali Waislamu wakiwa wamekusanya ngawira maridhawa. Muhasibu wa ngawira alikuwa ni Saaib Bin Al-Aqra’a, Hudheifa akamtuma kupeleka bishara ya ushindi na khumsi ya ngawira. Alipo karibia Madina, alimkuta Amirul-Muuminina; Sayyidna Umar akinusa khabari kwa kuwa alikuwa amesha itathmini vita kabla ya kupiganwa kwake, basi akawa akigaragara. Alipo muona Saaib, akamuuliza: Kuna nini huko utokako? Akajibu: Ni kheri tu, ewe Amirul-Muuminina! Allah amekupa ushindi mkubwa na Noumaan Bin Muqarrin amekufa shahidi. Sayyidna Umar akasema: INNAA LILLAAHI WA INNAA ILAIHI RAAJIUUN (Hakika sisi sote ni milki ya Allah na kwake Yeye tu tutarejea). Kisha akalia kwa kikweukweu.

Fungu la ngawira la mpanda farasi lilikuwa ni elfu sita na Waislamu wakauita ushindi/ufunguzi wa Nahaawandi “ufunguzi wa funguzi zote”, kwa sababu baada yake Wafursi hawakuweza kusimama tena.

Miongoni mwa yanayo stahiki kutajwa, ni kwamba katika ngawira zilizo patikana Nahaawandi, Waislamu walivikwaa vikapu viwili vilivyo jaa johari ghali mno katika hazina ya Kisraa (mfalme). Amiri jeshi; Hudheifa akampa Saaib ampelekee Sayyidna Umar. Hudheifa alipo vifikisha kwa Sayyidna Umar, akasema: Viweke katika Bait Maali (ya Waislamu) na rudi kwa jeshi lako. Akapanda kipando chake na akarudi. Sayyidna Umar akamtuma mtu kumfuatilia mpaka akamkuta kesha fika Koufah, akamrejesha Madina. Sayyidna Umar alipo muona akasema: Eeh nina nini mimi na huyu Saaib! Haikuwa ila nililala katika usiku ulio ondoka, malaika wakaniburuza kunipeleka kwenye vile vikapu viwili navyo vikiwaka moto. Wakinikamia kuniunguza moto kama sijaigawa, basi itwae mbali nami ukaiuze na pesa yake itiwe katika hazina ya Waislamu. Basi vikauzwa katika soko la Koufah.

Allah akuwiye radhi ewe Umar! Kwa yakini umefuata nyayo za Mtume wako, kwa ajili hiyo basi ukatukuka wewe na ukatukuka Uislamu na Waislamu.

Kisha Hudheifa karejea na jeshi lake baada ya vita vya Nahaawandi, akiwa mshindi, mnusuriwa.

 

Additional information