KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

ALAMA KUBWA ZA KIYAMA: SABABU YA KUITWA DAJJAAL

 

Tamko “Dajjaali”, limekuwa ni jina alamu (tambulishi) kwa yule Masihi aliye chongo na mrongo mkubwa. Kwa utambulishi huo basi, patakapo semwa/tamkwa/tajwa tamko “Dajjaali”, haiji wala kupita haraka kwenye akili/ufahamu wa msikiaji maana nyingine zaidi ya huyo kiumbe mwenye chongo na sifa ya uwongo mwingi.

 

Na huyo Dajjaali ameitwa “Masihi” - Mpanguswa, kwa sababu ama jicho lake moja limeondolewa kabisa (chongo) au ni kwa sababu yeye ataipangusa (ataizunguka) ardhi (ulimwengu) kwa muda wa siku arobaini. Haya yameelezwa katika kitabu [AN-NIHAAYAH FIY GHARIIBI AL-HADIITH 04/327]

 

 

Na kauli hiyo ya kwanza ambayo inasema ameitwa Dajjaali kwa sababu ya uchongo wa jicho lake, ndio kauli yenye nguvu, na nguvu yake inatokana na Hadithi ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-inayosema: “Hakika Dajjaali ni mpanguswa jicho (chongo)”. Muslim [18/61]-Allah amrehemu.

 

Ama kwa upande wa Nabii Isa-Amani imshukie-yeye ameitwa kwa jina hilo la “Masihi”, kwa sababu yeye alikuwa akimpangusa mgonjwa kwa mkono wake na akapona kwa idhini yake Allah Mtukufu.

 

Ama tukirudi kwa Dajjaali, ameitwa kwa jina hilo la “Dajjaali”, kwa sababu ama yeye anaifunika haki kwa kutumia batili au ni kwa kuwa yeye anaufunika (anauficha) kwa watu ukafiri wake kwa kutumia uwongo wake na kuwakanganya kwake. Au ni kwa sababu yeye ataifunika dini kwa sababu ya wingi wa makundi yake (watu watakao mkubali, kumuamini na kumfuata). Allah ndiye Mjuzi mno. [Rejea LISAANU AL-‘ARAB 11/237]

 

 • Sifa (Wasifu) za Dajjaali:

 

Ndugu mwanajukwaa letu-Allah akurehemu-tambua na ufahamu ya kwamba huyu Dajjaali tunaye mzungumzia si Malaika wala jini bali yeye ni mtu atokanaye na jamii ya wanaadamu. Ni mtu atakaye pewa na Allah nguvu na uwezo usio wa kawaida, kwa hekima azijuazo Mwenyewe Allah. Wasifu wake kiumbe huyo umetajwa na hadithi nyingi kwa lengo la kuwatambulisha watu wapate kumjua na hali kadhalika kuwatahadharisha kutokana na shari yake. Wasifu huo uwasaidie waumini kumtambua pale atakapo tokea ili wasifitinike naye kwa kuwa tayari wameshamjua kutokana na sifa zake zilizo elezwa na Yule aliye Mkweli na Muaminifu-Rehema na Amani zimshukie. Na sifa hizo ndizo zinazo mtofautisha na watu wengine, kwa sifa hizo basi hataghurika naye ila tu yule mtu jahili ambaye umekwisha tangulia kuandikwa na kuhukumiwa uovu wake tangu azali. Tumuombe Allah atukinge na kutuhifadhi na shari ya kiumbe wake huyo aliye muumba kwa makusudi maalumu ambayo ayajuaye zaidi ni Yeye peke yake.

 

Na katika jumla ya sifa zake kama zilivyo tajwa na Hadithi ni kwamba yeye ni:

 

 • Mtu (mwanaadamu),

 • Kijana mwekundu wa rangi,

 • Mfupi wa umbo,

 • Matege wa miguu,

 • Mwenye nywele za maboga,

 • Mpana wa paji la uso,

 • Mpana wa kifua,

 • Chongo wa jicho la kulia, na jicho lake hilo halikutokeza bali limeingia ndani kiasi cha kufanya shimo,

 • Jicho lake la kulia lina kinyama kilicho mea pembeni yake,

 • Kumeandikwa kwenye eneo lililo baina ya macho yake neno “KAFIRI”, neno hilo litasomwa na kila muislamu; msomi na asiye msomi,

 • Na miongoni mwa sifa zake ni kwamba yeye ni tasa; hatapata mtoto.

 

Naam, hizo ndizo baadhi ya sifa zake. Haya sasa tunakunukulia baadhi ya Hadithi zilizo zitaja sifa zake hizo na kwa upande mwingine hadithi hizo ni dalili/ushahidi wa ujio wa Dajjaali, tusome pamoja:

 

 • Imepokewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Nyakati ambazo mimi nikiwa nimelala (naota) natufu Al-Ka’aba.. (akataja ya kwamba yeye alimuona Isa mwana wa Maryamu-Amani imshukie-kisha akamuona Dajjaali, akaelezea sifa zake, akasema): Tahamaki huyo ni mtu mpana wa umbo, mwekundu, mwenye nywele za maboga, chongo kama kwamba jicho lake ni boya lielealo. Wakasema (Maswahaba): Huyo Dajjaali (kwa sifa hizo) anafanana mno na Ibn Qutwni; mtu wa kabila la Khuza’ah”. Bukhaariy [13/90] & Muslim [02/237]-Allah awarehemu.

 • Na imepokewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimtaja Dajjaali mbele za watu, akasema: “Hakika Allah Mtukufu si chongo. Ehee tambueni! Hakika Masihi Dajjaali ni chongo jicho la kulia, kama kwamba jicho lake ni ..... lielealo”. Bukhaariy [13/90] & Muslim [18/59]-Allah awarehemu.

 • Imepokewa kutoka kwa Ubaadah bin Swaamit-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Hakika Masihi Dajjaali ni mtu, mfupi, mwenye matege na kama atakutatizeni, basi tambueni ya kwamba Mola Mlezi wenu si chongo”. Abu Daawoud-Allah amrehemu.

 • Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Na ama Masihi wa upotevu, hakika yeye ni chongo, mpana wa paji la uso, mpana wa kifua”. Ahmad [15/28]-Allah amrehemu.

 • Katika hadithi iliyo pokewa na Anas-Allah amuwiye radhi-amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: ...na hakika baina ya macho yake pameandikwa (neno) kafiri”. Bukhaariy [13/91] & Muslim [18/59]-Allah awarehemu.

 • Na katika upokezi wa Hudhaifa (amesema): “...atalisoma (neno) hilo kila muumini; anaye jua na asiye jua kusoma”. Muslim [18/61]-Allah amrehemu.

 

Amesema Imamu Nawawiy-Allah amrehemu: “Kauli sahihi inayo fuatwa na Wahakiki Hadithi ni kwamba huko kuandikwa ni kwa dhahiri na ni maandishi ya hakika ambayo Allah ameyafanya kuwa ni aya/alama/ishara katika jumla ya alama zenye kutinda juu ya ukafiri na uwongo wake. Allah atayadhihirisha (maandishi hayo) kwa kila muislamu; anaye jua na asiye jua kusoma. Na atayaficha kwa yule aliye mtakia/mhukumia uovu wake na kufitiniwa naye na wala hilo halishindikani”. [SHAR-HUL MUSLIM 18/60]-Allah amrehemu.

 

Hayo (maandishi) atayaona muumini kwa macho ya uoni wake hata kama hajui kusoma na wala hatayaona kafiri hata kama anajua kusoma. Hivyo ni kama ambavyo anavyo ona muumini dalili (za uwepo wa Allah Mola Muumba) kwa macho ya uoni wake na wala hazioni kafiri (pamoja na kuwa anayo macho. Allah atamuumbia muumini utambuzi pasina kujifunza, kwa sababu katika zama hizo zitabadilika kanuni za maumbile zilizo zoweleka”. [FAT-HUL BAARIY 13/100]

 

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

 

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١

 

Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41

 

"...رَّبَّنَا عَلَيۡكَ تَوَكَّلۡنَا وَإِلَيۡكَ أَنَبۡنَا وَإِلَيۡكَ ٱلۡمَصِيرُ ٤

 

...Mola wetu Mlezi! Juu yako tumetegemea, na kwako tumeelekea, na kwako ndio marejeo”. Al-Mumtahinah [60]:04

 

Hapa ndio mwisho wa jukwaa letu hili kwa juma la leo, tunatumai utakuwa umejifunza na kuelewa kitu/jambo kupitia maneno ya Mtume wa Allah, maneno yanayo tukumbusha ujio wa siku iliyo nzito; siku ya Kiyama. Na kwa hivyo basi, utakuwa umetafakari na kuanza kuchukua hatua za kujiandaa nacho.

 

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kumzungumzia Dajja

 

Additional information