"Hakika si vingine nimetumwa kuja kutimiza TABIA NJEMA" Hadith Tukufu

HAKI ZA MKE KWA MUMEWE

Haki za mke kwa mume kwa maneno mengine tunaweza kuziita (WAJIBU WA MUME KWA MKEWE). Haki za mke kwa mume zinaangukia katika mbeya (mafungu) mbili;

¨        Haki za kimali (mahari, chakula, malazi, mavazi na kadhalika).

¨        Haki za nafsi (mwili).

Miongoni mwa haki za mke ambazo ni wajibu mumewe amtekelezee ni kama zifuatazo:-

 

1)     Kuishi naye kwa wema.

Ni wajibu wa mume kuishi na mkewe kwa tabia njema, asiwe na tabia ya kuziumiza hisia za mkewe kwa kumbughudhi kwa kauli chafu au kwa kumtendea matendo yasiyo na chembe ya utu.

Akambughudhi kiasi cha kumfanya asihisi raha ya ndoa na kupelekea kuiona ndoa kuwa ni mithili ya kifungo.

Mume asimbughudhi mkewe kwa kuiitikia kauli ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Mbora na mwema wenu  ni yule aliye mwema (mbora) wenu kwa wake zenu”.

Tirmidhiy

Maana ya kauli hii tukufu ya Mtukufu Mtume wa Allah ni kwamba mbora na mzuri wa wanamume, hawezi katu kuwa ni yule mwanamume ambaye huko nje laini wa maneno kama yeye hakuna.

Huko nje hakuna mpole na mwenye kuwasikiliza watu kumshinda yeye.

Lakini msubiri arudi nyumbani kwake utafikiri kaingia simba mla watu, vicheko na furaha iliyokuwemo ndani hutoweka ghafla.

Na mahala pake kutawaliwa na khofu na wasiwasi wa litakalotokea. Hana salamu wala hana muda wa kujua khabari za kutwa za nyumbani kwake, hana maneno mazuri hata kidogo.

Huyu kwa mujibu wa kauli hii ya Mtume hana sifa wala kigezo cha ubora, kwani kigezo pekee cha ubora wa mwanamume muumini kinatokana na jinsi anavyoishi na familia yake nyumbani. Kumbuka ewe mwanamume muislamu kwamba kuishi vema na familia yako ni sehemu ya dini. Na familia yako ina haki ya kwanza ya kuufurahia wema na utu wako.

 

2)    Kuvumilia kero/adha.

Ni wajibu wa mume aliyetambua maumbile ya mkewe kustahamilia kero na maudhi anayoweza kuyapata kutoka kwa mkewe.

Ama kwa makusudi au kwa bahati mbaya, kwa sababu ya upungufu wa kibinadamu. Khasa khasa katika kipindi kigumu cha ujauzito.

Yeye mume kama kiongozi wa familia/nyumba siku zote asiangalie matokeo (kero/maudhi), bali daima aangalie chanzo na chimbuko la kero au maudhi hayo.

Kwa nini maudhi haya yako leo na wala hayakuwepo jana? Kwa uchunguzi huu anaweza akajikuta kuwa yeye ndiye aliyetoa mwanya wa kero na maudhi hayo yanayomfika na kumkuta hivi sasa.

Kwa hivyo linalompasa kufanya ni kujaribu kuuziba uchochoro huo wa maudhi ili asipate kuudhiwa akaghadhibika na kuhatarisha ndoa yao.

Mume awe mwepesi kumsamehe mkewe anapomkosea hata bila ya kuombwa msamaha.

Na yeye awe mwepesi pia kumuomba msamaha mkewe anapomkosea.

Sio kwa kuwa yeye ni mwanamume basi hakosei, hivyo sivyo mwanamume pia hukosea kama anavyokosea mwanamke.

Mume atambue kwamba kumstahamilia na kumchukulia mkewe ni ibada, kwa sababu ndani yake kuna kumtii na kumfuata Mtume. Imethibiti katika hadithi sahihi:

“Kwamba wakeze Mtume-Rehema na Amani zimshukie-walikuwa wakijibizana nae maneno na mmoja wao akimuhama (Mtume, hasemi nae na wala hataki hata kumuona) mchana kutwa mpaka usiku”.

Bukhaariy & Muslim

Imepokelewa na Anas Ibn Maalik-Allah amuwiye radhi-amesema:

“Sikupata kumuona ye yote aliyekuwa rahimu na mpole kwa familia yake kuliko Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie”.

Muslim

Hiyo ndio hali na tabia ya wanawake, hata Bwana Mtume yalimfika akasubiri. Wewe leo kusubiri unaona tabu gani mpaka unafikia hatua ya kutoa talaka au tuseme wewe ni bora na unaona uchungu sana kuliko Mtume wa Allah?!

 

3)    Mzaha, ucheshi na mchezo.

Ni haki ya mke na ni wajibu wa mume kumtengea mkewe muda maalumu.

Katika muda huo mke apate fursa ya kutoa maoni, nasaha na ushauri kuhusiana na maisha yao na mipango yao ya baadaye.

Mazungumzo ya wawili haya yatiwe kachumbari ya mzahahalali usiofikisha katika maudhi.

Yaambatane na mchezo na ucheshi utakaoyanogesha na kuyafanya matamu maongezi yao hayo. Machoni mambo haya huonekana kuwa ni mambo ya kipuuzi yasiyo na maana.

Lakini ukweli ni kwamba mambo haya yana mchango mkubwa katika kuimarisha mafungamano haya ya ndoa.

Mke ni binadamu kamili mwenye mawazo na maoni juu ya nafsi yake mwenyewe na kwa watu wengine khasa mumewe na familia yake kwa ujumla.

Kama hakupewa fursa na mumewe, akayasemee wapi maoni na mawazo yake haya?! Kama mume hakuwa katika hali ya utayarifu wa kumsikiliza, akawa katika hali ya furaha, ucheshi, mzaha, atathubutu kumtamkia kitu?!

Ni dhahiri kuwa hataweza, atashindwa, kwa mantiki hii ni muhimu mno kikawepo baina ya wawili hawa kipindi cha mzaha, mchezo na ucheshi.

Ikiwa hukumpa fursa hiyo, maumbile yake yatamsukuma kuitafuta fursa hiyo mahala pengine. Jambo ambalo litaihatarisha ndoa yenu.

Tukutane katika darsa lijalo-Inshaallah.

 

4). Kuonewa/kuliliwa wivu.

Ni haki ya mke na ni wajibu wa mume kisheria kumuonea wivu wa kisheria mkewe.

Mume awe na wivu kwa mkewe, wivu utakaokuwa wigo wa kulinda na kuhifadhi utu, cheo, nafasi na utukufu wa mkewe.

Mume anatakiwa asighafilike na kutoa mwanya ambao unaweza kuwa ni sababu ya fisadi itakayopelekea kulegalega au pengine kuvunjika kwa ndoa yao.

Naam, ni kweli mume anatakiwa kuwa na wivu kwa mkewe, lakini si haki wala sheria kupindukia katika wivu.

Wivu utakaomtumbukiza katika lindi la dhana mbaya dhidi ya mkewe.

Dhana hizi zikamgeuza kuwa kachero na jasusi wa kuchunguza nyendo na pengine mambo ya ndani kabisa ya mkewe.

Huku si kuutekeleza wajibu wako kwa mkeo, wala huambiwi kuwa ndio unampenda sana mkeo. Wivu huu wa kupindukia ni ugonjwa unaoweza kuondosha masikilizano na maelewano ndani ya nyumba.

Na mahala pake kutawaliwa na mizozo na gubu lisilokwisha. Pengine wivu wa namna hii unaweza kuwa kichocheo na kumuamshia mke ari ya kufanya uchafu anaoshukiwa kuufanya na kumbe masikini hana khabari nao kabisa.

Ni kwa kuyazingatia madhara haya na kama haya ndio tunamuona Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akiuukataza wivu huu wa kupindukia. Makatazo hayo yamekuja katika hadithi sahihi iliyopokelewa na swahaba Jaabir-Allah amuwiye radhi:

“Kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amekataza mwanamume kumgongea mlango mkewe wakati wa usiku. Akimdhania kufanya khiyana au (kwa lengo la) kutafuta kunguwao (makosa ya kuteleza) zao.” Muslim

 

5). Mahitaji ya lazima.

Ni katika jumla ya haki za mke zilizo katika dhima ya mumewe kupata mahitaji yake yote ya lazima.

Mume anawajibika kutoa gharama zote za mahitaji ya lazima ya mkewe, ikiwa ni pamoja na chakula bora cha kulinda, kujenga na kutia mwili nguvu.

Ni wajibu wa mume kuhakikisha kuwa mkewe anapata maji safi na salama ya kunywa.

Ampatie mavazi yatakayomfaa katika vipindi/majira yote ya mwaka; nguo za masika na kiangazi.

Ni haki ya mke kupatiwa maskani yatakayomsitiri na kumpa amani na usalama wa nafsi, mali na akili. Kadhalika ni wajibu wa mume kumpa matibabu mkewe anapougua na kushirikiana nae kwa kumliwaza katika kipindi kigumu cha maradhi au ujauzito.

Haya yote yamo katika agizo tukufu la Allah Mtukufu:

“...NA NI JUU YA BABA (yake) CHAKULA CHAO (hao watoto na mama) NA NGUO ZAO KWA SHARIA. WALA HAIKALIFISHWI NAFSI YO YOTE ILA KWA KADRI YA WASAA WAKE...” [2:223]

Nae Bwana mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema katika kuuonyesha wajibu huu wa mume ambao kwa mkewe ni haki:

“Wana (hao wanawake) juu yenu (haki ya) chakula chao na nguo zao kwa wema (sharia)”. Tirmidhiy

Siku moja Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-aliulizwa ni ipi haki ya mke wa mmoja wetu juu yake, akasema:

“Ni kumlisha utakapokula na kumvisha utakapovaa. Na wala usiupige uso (wake), wala usimtolee maneno machafu na wala usimuhame ila ndani ya nyumba (yenu)”. Ahmad, Abuu Daawoud & Ibn Maajah.

Allah akurehemu ewe mume ikiwa utajua kwamba juhudi na uchovu wako katika kuhangaika kumpatia mkeo mahiataji yake haya.

Hazipotei bure bali Allah anakulipa thawabu na ujira mkubwa. Imekuja katika hadithi ya Sa’ad Ibn Abiy Waqaasw-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimwambia:

“Na hakika wewe hutotoa matumizi/gharama zo zote ukiikusudia dhati ya Allah ila utalipwa kwayo (gharama hizo). Hata (gharama za) kile unachokitia katika kinywa cha mkeo (yaani chakula)”. Bukhaariy & Muslim

 

6). Mahari.

Ni haki ya mke na ni wajibu wa mume kwa mujibu wa sheria kumpa mke mahari yake kamili. Kwa kuwa hiyo ni haki yake aliyopewa na Allah Mola Muumba wake. Tusome na tukubali:

“NA WAPENI WANAWAKE MAHARI YAO, HALI YA KUWA NI HADIYA (aliyowapa Allah). (Lakini hao wake zenu) WAKIKUPENI KWA RADHI YA NAFSI ZAO KITU KATIKA HAYO (mahari) BASI KULENI KWA FURAHA NA KUNUFAIKA”. [4:4]

Mahari ni haki ya mke hata kama ulimpa nyumba, gari, shamba na...na....kuwa ndio mahari yake. Ukimtaliki na kuoa mke mwingine huna rukhsa kuchukua cho chote katika hiyo mali uliyompa. Hebu tuitegee pamoja sikio la usikivu na uzingativu kauli hii tukufu ya Allah:

“NA KAMA MKITAKA KUBADILISHA MKE MAHALA PA MKE (yaani kumuoa mke mwingine na kumuacha huyo wa zamani), NA HALI MMOJA WAO (naye ndio huyo unayemuacha) MMEMPA MRUNDI WA MALI, BASI ,MSICHUKUE CHO CHOTE. JE, MNACHUKUA KWA DHULMA NA KWA KHATIA ILIYO WAZI? NA MTACHUKUAJE, NA HALI NYINYI KWA NYINYI MMEINGILIANA?...” [4: 20-21]

 

7). Uadilifu baina ya wake wenza.

Ni haki ya wake wenza na ni wajibu wa mume kuwafanyia uadilifu wakeze hawa katika haki na mahitaji yao ya lazima.

Awalinganishe sawa katika matumizi, malazi, zamu za kulala na kila ambacho kinamkinika kugawika.

Ni vema mume akakumbuka kuwa kumpendelea mmoja wa wakeze na kumili (kuelemea) zaidi kwake ni miongoni mwa madhambi makubwa.

 

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anatutahadharisha na dhambi hii, aliposema: “Atakayekuwa na wake wawili akamili kwa mmoja wao, atakuja (atafufuliwa) siku ya kiyama na ilhali bega (upande) lake moja limeshuka”. Ahmad & Ahli Sunan.

Ama yale mambo yasiyokubali kugawika kama vile mapenzi na raha ya nafsi. Haya hayamo katika uweza wa mwanadamu, kwa hivyo hana dhambi kwa hilo maadam yale yanayogawika anayatekeleza kwa usawa. Ukweli wa hili umo katika kauli ya Allah, tuisome sote:

“NANYI HAMUWEZI KUFANYA UADILIFU (kweli kweli) BAINA YA WAKE, IJAPOKUWA MTATAKA KUFANYA HIVYO. KWA HIVYO MSIELEKEE (upande mmoja) KABISA KABISA; MSIJE KUMUACHA (huyo mwingine msiyempenda) KAMA ALIYEANGIKWA (hajijui kuwa ana mume au mjane)...” [4:129]

Alikuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akigawa siku sawa baina ya wakeze na akisema:

“Ewe Mola wa haki, hii ndio sehemu/fungu langu katika kile nikimilikicho. Basi usinilaumu katika kile ukimilikicho wewe na wala mimi sikimiliki”. Abuu Daawoud, Tirmidhiy, Nasaai & Ibn Maajah.

Lakini lau mume atampendelea mmoja wa wake zake katika zamu ya kulala, akampa siku nyingi zaidi kuliko mwenziwe.

Lakini akafanya hivyo kwa radhi yake mwenyewe (huyo mwenziwe) hakuna ubaya. Kwani hivyo ni kama alivyokuwa akifanya Bwana Mtume, alikuwa akimpa Bi. Aysha siku yake na siku ya Bi. Saudah-Allah awawiye radhi- ambayo mwenyewe Bi. Saudah alimpa hadiya (mke mwenziwe) Bi. Aysha. Hivi ndivyo ilivyokuja katika riwaya ya Bukhaariy na Muslim.

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwa kuchunga uadilifu baina ya wakeze katika zamu zao za kulala.

Alikuwa akiuliza wakati akiwa ni mgonjwa kitandani kwa maradhi yaliyokuwa sababu ya kifo chake, akisema: Kesho niko wapi (ni zamu ya nani), kesho niko wapi mimi.

Wakeze wakampa idhini augulie po pote apatakapo, nae akakhitari kuwa katika nyumba ya Bi. Aysha, akaugulia hapo mpaka akafa. Huu ni upokezi wa Bukhaariy na Muslim.

 

8). Haki ya kupata elimu.

Mke ana haki ya kupata elimu ambayo ni wajibu wa mumewe kuhakikisha kuwa anaipata.

Ikiwa mke hakupata elimu ya msingi ya dini yake huko kwao atokako, basi ni jukumu la mume kuhakikisha kuwa mkewe anapata elimu hiyo muhimu.

Amfundishe yeye mwenyewe au amtafutie mtu/mahala ambapo ataipata elimu hiyo. Aanze kufundishwa mambo ya msingi kama vile nguzo za imani na baki ya mambo mengine yanayohusiana na akida (itikadi).

Kisha afundishwe hukumu za mambo ya kisheria yanayomtokea katika maisha yake ya kila siku. Yaani hukumu za twahara, hedhi, swala, swaumu na kadhalika.

Pia si vibaya akipata elimu na taaluma ya ziada itakayoisadia familia kujikimu kimaisha, taaluma itakayomuwezesha kufanya kazi na kuchangia kuongeza pato la familia.

Afanye kazi kwa ridhaa ya mumewe na chini ya mazingira yanayokubaliwa na sheria. Kumbuka mama (mke) ni shule ya familia, kumuelimisha mama ni kuielimisha familia.

Kadhalika ni jukumu na wajibu wa mume kumuhimiza mkewe swala na mambo mengine ya kheri, hii ni amri ya Allah tuamrike:

“NA WAAMRISHE WATU WAKO (familia yako) KUSWALI NA UENDELEE MWENYEWE KWA HAYO...” [20:132]

Ni vema mume akakumbuka kuwa familia aliyonayo ni amana na dhima iliyo shingoni mwake. Yeye ni mchunga na anawajibika kwa familia yake na atakwenda kuulizwa mbele ya Allah aliichunga vipi familia yake.

Kwa hivyo ni wajibu wa mume (baba) kuhakikisha kuwa anakuwa kiwanda cha kuzalisha familia njema ya kiislamu ili hatimaye tuwe na jamii njema ya kiislamu. Familia itakayoishi katika maadili, mila, utamaduni na sheria ya Allah:

“ENYI MLIOAMINI! JIOKOENI NAFSI ZENU NA WATU WENU NA MOTO AMBAO KUNI ZAKE NI WATU NA MAWE...” [66:6]

Ni dhahiri kuwa hatuwezi kujiokoa sisi na kuziokoa familia zetu kutokana na adhabu kali ya moto kama hatukuandaa mazingira mema tangu mapema.

Mazingira yatakayopelekea kuishi chini ya twaa ya Allah na Mtume wake kwa kufuata muongozo wa Qur-ani Tukufu.

 

9). Heshima na kuthaminiwa.

Ni haki ya mke na ni wajibu wa mume kumthamini na kumpa mkewe heshima zote anazostahiki kama mke, mwandani na msaidizi wa karibu katika maisha kwa mujibu wa sheria.

Mume anatakiwa kumuangalia mkewe kama sehemu yake inayomkamilisha na kumfanya mwanamume kamili atakayeitwa mume, baba na hatimaye babu.

Haya yote yanaonyesha nafasi ya mwanamke kwa mwanamume. Ni nafasi yake hii ukiachilia mbali ubinadamu wake inayomstahikisha heshima na kuthaminiwa sambamba na kutambuliwa utu wake.

Mume asijione kuwa ana haki na kila sababu ya kufanya atakavyo kwa mkewe, hii ni dhana lemavu inayokwenda kinyume na mafundisho sahihi ya uislamu.

Si haki na wala si sheria mume kumdhalilisha mkewe kwa kumtukana na kumtolea maneno machafu peke yao chumbani, seuze mbele ya watoto au watu kando.

Si halali hata kumuabisha kwa jambo la kweli kama hali duni ya nyumbani kwao.

Haijuzu kumtukania wazazi wake kwa sababu ya magomvi yenu ya ndani, haya si matendo wala tabia za muislamu wa kweli.

Hizi ni baadhi tu ya haki za mke kwa mujibu wa sheria, haki ambazo ni wajibu mume amtekelezee.