"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

MASHAHIDI WA RAJII

Tukio la kuuawa kwa hila kwa kiongozi wao lilikuwa kubwa sana katika nyoyo za watu wa kabila la Hudhayl, wakaanza kutafuta mbinu za kulipa kisasi.

Baadhi ya watu wa makabila mawili ya Adhwal na Al-qaraah walimuendea Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wakadai kwamba watu wao wana raghba na Uislamu.

Kwa hivyo wanaomba awape baadhi ya maswahaba wake wakawafundishe dini na kuwasomesha Qur-ani. Bwana Mtume akawapa kundi la maswahaba wake bora likiongozwa na Aaswim Ibn Thabit. Wakaondoka pamoja nao hata walipofika kwenye eneo la maji la kabila la Hudhayl liitwalo “Rajii”.

 Wakawasaliti na kuomba msaada wa kunusuriwa nao kutoka kwa kabila la Hudhayl, tahamaki waislamu wamezungukwa na watupa mishale wa Hudhayl wapatao mia mbili hivi.

Waislamu kuona hivyo, wakawa hawana hila ila kupambana tu pamoja na uchache wao ukilinganisha na maadui zao wenye uchu wa kulipa kisasi cha kiongozi wao.

 Wakatumia mbinu ya kujihifadhi na jabali ili wasije kushambuliwa kutokea nyuma, ndipo wakaanza kupambana na adui kufa kupona.

Wakapigana kishujaa kweli kweli bila ya kusalimu amri mpaka wakauawa wote ila watatu tu miongoni mwao. Hawa walihadaika na hila ya kujisalimisha iliyotolewa na mahasimu wao, wakatekwa nao ni Khubaybu Ibn Adiy, Zayd Ibn Duthunnah na Abdullah Ibn Twaariq.

Ama Abdullah Ibn Twaariq yeye aliona dalili za usaliti machoni mwa adui tangu walipojisalimisha kama walivyowataka. Akachomoa mkono wake katika kamba waliyofungiwa, kisha akatwaa upanga wake na kurudi kinyumenyume, wakampopoa kwa mawe mpaka wakamuua. Ama wale wenzake wawili waliwachukua na kwenda kuwauza kwa Makurayshi Makkah.

Khubaybu alinunuliwa na Uqbah Ibn Al-Haarith ili amuue kulipiza kisasi cha baba yake; Al-Haarith Ibn Aamir.

Na Zayd akanunuliwa na Swafwaan Ibn Umayyah ili amuue kwa ajili ya kulipa kisasi cha baba yake; Umayyah Ibn Khalaf aliyeuawa na waislamu.

 

MAUAJI YA MASHAHIDI; KHUBAYBU IBN ADIY NA ZAID IBN DUTHUNNAH YALIUTIKISA MJI WA MADINAH.

Mauaji ya maswahaba wawili hawa yalikuwa ni tukio kubwa lililoushtua mno mji wa Makkah na kuzitetemesha nyoyo za wengi miongoni mwa makurayshi.

Imepokelewa kwamba maswahaba wawili hawa waliwekwa  mahabusu katika mojawapo ya majumba ya Makkah na kushikiliwa humo mpaka miezi mitukufu imalizike ndipo wauawe.

Miezi mitukufu ilipomalizika walitoka nao mpaka Tan-iym; hili ni eneo la wazi lililokuwa umbali wa maili nne kutoka mjini Makkah.

Walifuatiwa na kundi la wanaume, wanawake na watoto ili kushuhudia mauaji ya watu hawa.

Zayd akauawa na mtumwa wa Swafwan Ibn Umayyah aitwaye Nistwaasi. Alipoletwa tayari kwa kuuawa, Abuu Sufyaan alimwambia:

“Ninakuuliza kwa jina la Allah ewe Zayd, je ungependa Muhammad awe mahala pako hivi sasa uipige upanga shingo yake na wewe uwe nyumbani kwako?”. Zayd akajibu:

“Wallah, nisingependelea Muhammad hapo alipo hivi sasa kuchomwa na mwiba na mimi nikiwa nimekaa nyumbani kwangu (seuze huko kuwa hapa)!”. Abuu Sufyaan akasema:

“Sijapatapo kumuona ye yote katika watu akimpenda mtu kama maswahaba wa Muhammad wampendavyo Muhammad!”.

Khubaybu nae aliwaambia wakati walipotaka kumuua:

“Ikiwa mnaona vema kuniacha nikaswali rakaa mbili kwanza, basi fanyeni hivyo”.

Wakamwambia: “Swali tafadhali”.

Akaswali rakaa mbili kwa uzuri na kwa kuzitimiza, kisha akawaelekea wauaji wake na kuwaambia:

“Ama wallah, lau isingekuwa kudhania kwenu kwamba nimerefusha swala kwa sababu ya kuogopa kufa, basi ningekithirisha kuswali”.

 Kisha akawaendea mwenyewe, wakamnyanyua juu kwa juu na kumuweka katika ubao ili wamsulubu. Walipokwishamfunga barabara juu ya ubao ule, akaunyanyua uso wake  kuuelekeza mbinguni na kusema:

 “Ewe Mola wa haki wee! Hakika sisi tumekwishafikisha ujumbe wa Mtume wako, basi na wewe nakuomba umfikishie khabari za haya tufanyiwayo asubuhi ya leo”.

Kisha akawatupia jicho watu wale na kusema:

“Ewe Mola wa haki wee! Ninakuomba uwadhibiti kwa idadi, uwauwe kwa mtapanyo na usimbakishe ye yote miongoni mwao”.

Watu wale wakaenda pembeni kidogo kwa kuchelea kupatilizwa na dua yake hiyo.

Al-Waaqidiy anasema:

“Kwamba walimkusanyia watoto wa wale aliowaua katika vita vya Badri na kumshakizia, nao wakawa wanamchoma kidogo kidogo kwa mikuki mpaka wakamuua-Allah amuwiye radhi”.

Ibn Is-haaq-Allah amrehemu-amepokea kwamba Sayyidina Umar Ibn Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi-alimpa Said Ibn Aamir Al-Jamhiy uliwali wa baadhi ya miji ya Shamu.

Akawa anapatwa na maradhi ya kuanguka mbele za watu, khabari zikaenda kwa Amirul-Muuminina. Nae akachukua khatua za kumuita, alipokuja akamuuliza:

Ewe Said, hebu nambie ni kitu gani hiki kinachokusibu?” Akajibu:

“Wallah, ewe Amirul-Muuminina mimi sina tatizo lo lote. Isipokuwa tatizo langu ni kwamba mimi nilikuwa ni miongoni mwa walioshuhudia mauaji ya Khubaybu Ibn Adiy na nikaisikia dua yake. Basi wallah, haijapatapo kunipitikia moyoni nami nikiwa katika baraza ila huanguka mweleka!”

Mauaji ya mashahidi hawa yalikuwa katika mwezi wa Swafar (mfunguo tano) mwaka wa nne Hijiria.

 Machungu ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwa mauaji yao yalikuwa makubwa sana, kwa sababu walikuwa ni katika jumla ya wasomaji bora wa Qur-ani katika maswahaba wake. Na kwa sababu ya khiana, usaliti na kukatwakatwa walikofanyiwa-Allah awawiye radhi wote.

 

MASHAHIDI WA BI’IRI MAUUNAH.

Kabla nafsi ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-na nafsi za maswahaba wake-Allah awawiye radhi-hazijapata kutulizana kutokana na uchungu wa tukio hili.

Likawapata tukio jingine lenye kutia uchungu zaidi katika sura nyingine ya usaliti mbaya kabisa. Tukio zima linaanzia pale alipokuja mbele ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-mmojawapo wa viongozi wa kabila la Baniy Aamir, aitwaye “Abuu Baraai”.

Bwana Mtume akamkunjulia maelezo juu ya Uislamu lakini hakusilimu na wala hakuwa mbali na kusilimu na akasema:

“Ewe Muhammad, unaonaje lau ungeliwapeleka baadhi ya maswahaba wako kwa watu wa Najid wakawalingania jambo lako hili, mimi ninataraji watakuitika”.

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akamjibu:

 “Mimi ninawachelea juu yao watu wa Najid kuwadhuru”, Abuu Baraai akamwambia:

“Mimi ninawachukulia dhamana, basi wewe watume tu wakawalinganie watu katika jambo lako hili”.

Baada ya ahadi hiyo ya dhamana, Bwana Mtume hakuwa tena na sababu ya kuukataa wito wa bwana huyu. Akampeleka Al-Mundhir Ibn Amrou kuliongoza kundi la maswahaba arobaini katika waislamu bora bora kama ilivyotajwa katika riwaya ya Ibn Is-haaq-Allah amrehemu.

Wakaenda zao mpaka “Bi’iri Mauunah”, wakapiga kambi hapo. Hiki ni kipande cha ardhi kilicho baina ya eneo la kabila Baniy Aamir na ardhi yenye mawe iliyokuwa ikimilikiwa na ukoo wa Baniy Sulaym.

Walipokwishakupiga kambi hapo wakamtuma Hiraam Ibn Mal-haan kumpelekea Aamir Ibn Twufail; kiongozi wa kabila la Baniy Aamir, barua ya Mtume wa Allah.

Alipofika na kumpa barua, hakuwa na muda wa kuisoma zaidi ya kumrukia na kumuua mjumbe huyu. Kwa kitendo chake hiki kiovu akawa ameivunja kanuni na utaratibu waliojiwekea wao wenyewe na kujilazimisha kuufuata, hii ni ile kanuni isemayo: (Mjumbe hauawi).

Baada ya kumuua mjumbe yule, akawapigia mbiu Baniy Aamir waende wakawaue wale maswahaba wengine waliopiga kambi Bi’iri Mauunah.

Baniy Aamir wakakataa kumtii kwa sababu ya kuheshimu dhima na dhamana aliyoichukua Abuu Baraai kwa Mtume wa Allah.

Alipoona hakuitikiwa na watu wake, akayapigia mbiu ya mgambo makabila ya Baniy Sulaym, hawa wakamuitika. Wakatoka na silaha zao na kuja kuwazingira walinganiaji dini wale katika kambi yao.

 Maswahaba walipowaona wakaanza kuchomoa panga zao na kuanza kupambana nao, wakiua na kuuliwa. Mpaka wakauliwa wote-Allah awarehemu-ila Ka’ab Ibn Zayd, huyu walimuacha akiwa anapumua pumzi za mwisho mwisho.

Katika msafara wa wanyama wa watu wale walikuwepo Amrou Ibn Umayyah na Muanswari mmoja, hawa walipowaona ndege wakiambaambaa angani juu ya kambi ile.

Wakajongea kuja kuangalia kulikoni hata ndege wakawepo pale. Walipofika wakawakuta wajumbe wa mjumbe wa Allah wamelala maiti katika dimbwi la damu zao na wabaya wao wangali pale pale wakijipongeza kwa uovu wao huo.

Yule Muanswari hakuweza kujimudu kuona mandhari ile ya ukatili uliokithiri, akauchomoa upanga wake na kuanza kuzivuna shingo za makhabithi wale kwa ushujaa mkubwa mpaka alipozidiwa na kuuawa.

 Akabakia Amrou Ibn Umayyah, yeye akachukuliwa mateka, walipomsaili kuwa yeye ni mtu wa kabila gani, akawaambia kuwa yeye ni mtu wa kabila la Mudhwar, wakamuachia huru.

Akaondoka kurudi Madinah hata alipofika “Baqarqaratul-Kudri”-hili ni eneo lenye maji linalomilikiwa na Baniy Sulaym, kiasi cha maili 96 kutoka Madinah.

 Akaamua kupiga kambi hapo kupumzika na wakaja kujumuika nae watu wawili wa kabila la Baniy Aamir. Watu wawili hawa walikuwa na makubaliano ya amani na dhamana ya siri na Bwana Mtume ambayo Amrou hakuijua.

Alipowatambua kuwa ni watu wa kabila la Baniy Aamir, akawavizia hata walipolala akawaua na kuona kuwa amelipa kisasi kwa Baniy Aamir kutokana na mauaji ya maswahaba wa Mtume waliyoyafanya.

Akaondoka na kwenda zake kwa Bwana Mtume na kumpasha khabari za yote yaliyojiri huko atokako. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamwambia:

“Hakika umewaua watu wawili wenye mapatano nasi, nitalipa nitalipa fidia yao!”

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawahuzunikia sana maswahaba wake hata akafikia kusema: “Hii ni kazi ya Abuu Baraai”.

Akawa mwezi mzima katika kila swala anaomba dua (Qunuut) dhidi ya wauaji wa maswahaba wake katika Bi’iri Mauunah na Rajiy’i mpaka Allah Taala akamshushia kauli yake:

“WEWE HUNA LAKO KATIKA SHAURI HILI-AU (Allah) AWAONEE HURUMA AU AWAADHIBU, MAANA WAO NI MADHALIMU (atafanya anavyoona yeye mwenyewe)”. [3:128] Hapo ndipo nafsi yake ikatulizana, huzuni ikamuondoka na akaacha kuwaapiza waovu hawa waliowaua maswahaba wake.

Hii ndio athari iliyoachwa na vita vya Uhud kwa waislamu.