"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

BWANA MTUME AGAWA NGAWIRA ZA BANIN-NADHWIYR KWA MUHAJIRINA PEKE YAO

Mwanachuoni mwenye kitabu AL-IMTAA-Allah amrehemu-amesema: [Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipoichukua ngawira mali ya Banin-Nadhwiyr.

Alimtuma Thabit Ibn Qaysi kuwaita Answari wote (wenyeji wa Madinah). Walipoitika wito wake, akasimama na akamuhimidi Allah na kumsifia, kisha akawataja Answari na mema yote waliyowatendea ndugu zao Muhajirina (wakimbizi kutoka Makkah).

Yakiwa ni pamoja na kuwahifadhi majumbani mwao na kuwapendelea zaidi katika kila kitu kuliko nafsi zao, kisha akasema:

“Ikiwa mtapenda nitagawa baina yenu na Muhajirina mali aliyonipa Allah kutoka kwa Banin-Nadhwiyr na wao wataendelea kuishi majumbani mwenu na kupata hisa katika mali zenu. Na iwapo mtapenda, niwape wao na watoke majumbani mwenu”.

 Sa’ad Ibn Ubaadah na Sa’ad Ibn Muaadh wakasema: Bali tuigawe kwa Muhajirina na wabakie majumbani mwetu kama walivyokuwa. Answari wote wakasema kwa sauti moja: Tumeridhia na tumesalimu amri ewe Mtume wa Allah! Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema:

“Ewe Mola wa haki wee! Warehemu Answari na watoto wa Answari”.

Halafu akaigawa mali aliyopewa na Allah baina ya Muhajirina bila ya kuwapa kitu Answari. Isipokuwa watu wawili tu miongoni mwao waliokuwa wahitaji; Sahli Ibn Hunayf na Abu Dujaanah, hawa aliwapa kwa sababu ya uhitaji mkubwa waliokuwa nao.

Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawagawia Muhajirina mafungu yenye kukidhi haja katika mali ya Banin-Nadhwiyr]. Na wakasilimu watu wawili katika Banin-Nadhwiyr kwa sharti ya kurejeshewa mali yao, wakasilimu na wakarudishiwa mali yao.

Vita hivi vya Banin-Nadhwiyr vilikuwa katika mwezi wa Mfunguo mosi (Shawwal), mwaka wa nne wa Hijrah (June 625 A.D).

Allah Taala akashusha Suratil-Hashri (59) kufuatia vita hivi, akavitolea hoja ndani yake vitendo vilivyotendwa na waislamu na kuonwa kuwa ni uhalifu wa kivita.

Kuanzia kukata kwao mitende ya mahasimu wao na kuwazingira mpaka wakaweza kuwatoa katika miji yao. Na Allah akawakamia wanafiki waliowaunga mkono makafiri na kuwachochea watu dhidi ya Allah, Mtume wake na waumini.

Na Allah akamtakasia Mtume wake mali aliyoichukua kutoka kwa maadui hawa. Kwa hivyo ikawa ni yake khasa, akawapa aliowapa sehemu katika mali hiyo na akabakisha sehemu nyingine.

 Na akawa anaendesha kilimo katika ardhi yao ya mitende ambayo sasa iko chini ya milki yake. Akawa anajiwekea yeye na familia yake akiba ya chakula cha mwaka mzima kutokana na shayiri na tende zinazovunwa katika ardhi hiyo.

Na sehemu ya mavuno iliyobaki baada ya kutoa chakula chake aliitenga kwa ajili ya farasi, kununulia silaha na zana nyingine za vita. Pia sadaka alizokuwa akitoa kuwapa mafakiri miongoni mwa maswahaba wake na wageni mbalimbali waliomfikia zilitokana na mavuno ya ardhi hii.

 

IV/. KUWAADABISHA WAASI.

Vita vya Banin-Nadhwiyr vilikuwa ni hatua endelevu muafaka na pigo adabishi lililowapata kwa pamoja mayahudi na wanafiki.

Likaivunja nguvu yao na kuzijaza nyoyo zao khofu na kuwafanya wanafiki kuacha kuwabeza waislamu na kueneza uvumi na fitna baina yao.

Na Baniy Quraydhwah wakabakia katika ardhi yao wakiwa katika hali ya khofu na hadhari kubwa.  Mji wa Madinah ukawa shwari kwa kipindi ambacho Mtume-Rehema na Amani zimshukie- na maswahaba wake wakaweza kuzielekeza juhudi zao zote katika kuyaadabisha makabila mengine ya mabedui waliokuwa na choko choko dhidi yao.

 

SOMO LA PILI-VITA VYA DHAATIR-RIQAA.

 

Katika mwezi wa Jumaadal-Uula (Mfunguo nane) wa mwaka huu huu, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alitambua kuwa Baniy Muhaarib na Baniy Tha’alabah wanajiandaa kuja kumpiga.

Akawatokea na kikosi cha watu mia saba, akamtawalisha Sayyidina Uthman Ibn Affaan kuendesha shughuli za utawala Madinah. Mtume wa Allah huyoo akaenda mpaka akapiga kambi “Nakhla”-hili ni eneo lililopo Najid katika ardhi ya Ghatwfaan.

Hapo akakutana na kundi kubwa miongoni mwa mahasimu wake, makundi mawili haya; waislamu na makafiri yakakurubiana, lakini hayakuzuka mapambano baina yao.

Yakaogopana kiasi cha kumlazimisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuwaswalisha waislamu swala ya khofu. Ikawa unapoingia wakati wa swala, huliswalisha kundi moja la maswahaba wake na kundi jingine likabakia limesimama likiwalinda dhidi ya shambulio la kushtukiza la adui.

Hata likesha kuswali lile kundi la kwanza, huja likasimama uelekeo wa adui na kumpa Mtume fursa ya kuliswalisha lile kundi lililokuwa likilinda.

Na vita hivi vimeitwa kwa jina hili la “Dhaatur-riqaa”, kwa sababu mawe yaliyokuwepo eneo hili yaliidhoofisha miguu yao. Hali hii ikawapelekea kufunga vitambara (Riqaa) miguuni mwao ili kuepuka kuumizwa na mawe hayo.

 

I/. PICHA/SURA YA IKHLASWI YA KWELI.

Katika vita hivi Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipiga kambi kwenye mojawapo ya njia za majabalini jangwani. Akasema:

“Nani atakayeshika zamu ya kutulinda katika usiku wetu huu?” Wakajitokeza watu wawili kuifanya kazi hiyo, mmoja akiwa ni Muanswari na mwingine Muhajiri, wakasema:

“Sisi ewe Mtume wa Allah tutaifanya kazi hiyo”. Mtume akawaambia:

“Basi kuweni mlangoni mwa njia/bonde”. Watu wawili hawa walipotoka kuelekea mahala walipoelekezwa na Mtume, yule Muanswari akamwambia mwenziwe Muhajiri:

“Ni sehemu ipi ya usiku unayopenda nikutoshelezee (nianze kushika zamu mimi); ya mwanzo au ile ya mwisho?”. Mwenzake akamjibu:

“Nitoshelezee sehemu ya mwanzo ya usiku”.

Yule Muhajiri mwenye zamu ya mwisho wa usiku akalala na yule Muanswari mwenye zamu yake akainuka na kuanza kuswali suna za usiku.

Akiwa ndani ya swala akaja mushriki mmoja akifuatilia nyendo za waislamu, alipomuona yule Muanswari akatambua kwamba yeye ni mmojawapo wa walinda doria wa waislamu.

 Akamrushia mshale ukampata, yule Muanswari akauchomoa mshale ule mwilini mwake na kuutupa chini na akaendelea na swala yake.

Adui akatupa mshale wa pili nao ukampata sawia kama ule wa kwanza, nae akauchomoa na kuutupa na kuendelea kuswali.

Adui akatupa mshale wa tatu nao vile vile ukampata, akauchomoa na kuutupa chini, kisha akarukuu na kusujudu. Halafu akamuamsha mwenzake na kumwambia:

“Amka ushike zamu nimekwishapigwa sijiwezi”.

Yule Muhajiri akavumburuka na kusimama wima, adui alipowaona akatambua kuwa sasa wamedhamiria kupambana nae, huyoo akatimua mbio.

Muhajiri alipoona damu inayomtoka nduguye Muanswari akasema:

“Sub-haanallah! Kwa nini hukuniamsha mwanzo tu alipoanza kukushambulia?” Akajibu:

“Nilikuwa nikiisoma  sura fulani,  kwa hivyo sikuweza kuikata mpaka nimalize kuisoma, aliponifululizia ndipo nikarukuu na kukuamsha. Na ninamuapia Allah lau si kupoteza doria aliyoniamrisha Mtume wa Allah kulinda, adui angelizikata pumzi zangu (angeniua) kabla mimi sijaikata sura niliyokuwa nikiisoma”.

Pima mwenyewe mpendwa msomaji wetu ni ikhlaswi ya namna gani waliyokuwa nayo maswahaba wa Mtume wa Allah-Allah awawiye radhi.

Ni jinsi gani walivyokuwa wakitaladhadhi wawapo ndani ya ibada kiasi cha kutohisi machungu yawapatayo. Eeh tu wapi sisi leo na hali hiyo?!

 

II/. SURA YA UAMINIFU NA UKWELI JUU YA ALLAH:

Na katika vita hivi Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikwenda kando peke yake kujipumzisha chini ya mti kutokana na uchovu wa joto shadidi (kali) la jangwani.

Akautundika upanga wake kwenye mojawapo ya matawi ya mti ule, mmojawapo wa maadui akajipenyeza bila ya kuonekana mpaka akamfikia Mtume akiwa amelala.

Akautwaa upanga wa Mtume wa Allah akauchomoa kutoka kwenye ala yake, Mtume akazinduka kutoka usingizini, tahamaki huyo ni mtu amemsimamia kichwani, upanga mkononi mwake akimwambia:

“Ni nani atakayenizuia nisikuue?” Mtume akasema: “Allah”, kwa kauli hiyo ya Mtume, upanga ukamuanguka adui yule na kutwaliwa na Mtume.

Upanga ulipotua mkononi mwake, Bwana Mtume akamuuliza swali lile lile alilomuuliza yeye wakati akiumiliki upanga: “Ni nani atakayenizuia nisikuue?” Akajibu:

 “Kuwa mchukuzi mwema (wa upanga huo)”.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamsamehe, kwa wema huu aliotendewa na mtu ambaye yeye alitaka kumuua na kisha nae akapata nafasi ya kumuua na akaamua kumsamehe.

Mtu huyu akasilimu, kisha akawaendea jamaa zake na kuwataka na wao wawe waislamu, akawaambia: “Nimekujieni kutoka kwa mbora wa watu”.