"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

VITA VYA BANIL-MUSTWALAQ

Mnamo mwezi wa Shaaban wa mwaka huo huo wa tano Hijiria (Desemba 626 A.D.), Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alitoka kuwaendea Banil-Muswtwalaq.

Hawa ni katika ukoo wa Khuzaa, kiongozi wao akiwa ni Al-Haarith Ibn Abiy Dhwiraar. Khabari ilimfikia Bwana Mtume ya kwamba wao wanawakusanya watu kwenda kumpiga, kabla hawajatoka yeye akawatokea na kundi kubwa la maswahaba wake.

mshangao wa wengi, wengi miongoni mwa wanafiki ambao hawakuwa na mazoea ya kutoka kwenda vitani nao pia walitoka pamoja na jeshi hili wakisukumwa na tamaa ya kupata ngawira.

Safari hii Mtume alitoka na wakeze wawili; Bi. Aysha na Bi. Saudah-Allah awawiye radhi wao na wote wakeze Mtume wa Allah.

Bwana Mtume akaenda zake mpaka akalifikia eneo lenye maji liitwalo “Al-Marsii”, hapo ndipo alipokutana na Al-Haarith akiwa pamoja na watu wake.

Makundi mawili haya; kundi la Mtume na lile la Al-Haarith yakajipanga tayari kuanza mapambano.

Makundi mawili haya yalipoonana ana kwa ana, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamuamrisha Sayyidina Umar kuwatolea wito watu wale ya kwamba:

“Semeni: Laa Ilaaha Illal-laahu {hapana afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah}, mtazizuia nafsi na mali zenu kwa tamko hilo”.

Wakakataa kulitamka tamko hili litakalowafanya kuwa waislamu, makundi mawili haya yakaanza kurushiana mishale kwa kitambo kidogo.

Halafu tena ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawaamrisha maswahaba wake kuwashambulia, wakawa shambulia ushambulizi wa mtu mmoja.

Wakawaua watu kumi miongoni mwao na kuwateka wengine, hapana hata mmoja wao aliyeweza kuponyoka na kukimbia.

Waislamu wakapata ngawira ya ngamia alfu moja, mbuzi alfu tano na kuwachukua mateka watu wa kaya mia mbili; wanamume, wanawake na watoto.

Miongoni mwa mateka hawa alikuwemo Juwayriyah Bint Al-Haarith; binti wa kiongozi wa Banil-Muswtwalaq.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akataka kulivutia kwenye Uislamu kabila la Juwayriyah, akamuacha huru na kisha akamuoa.

Kuolewa kwake bibi huyu na Mtume wa Allah kukawa ni baraka, neema na faraja kwa ukoo wake mzima.

Kwani waislamu waliwaachilia huru mateka wao waliokuwa wakiwashikilia kwa ajili ya kuwatukuza na kuwaheshimu wakweze Mtume. Na uachaji huru huu wa mateka ukawa ni sababu ya wengi wao kusilimu.

 

II.            WANAFIKI WAJARIBU KUCHOCHEA FITNA BAINA YA WAISLAMU.

Vita vya Banil-Muswtwalaq vilikuwa ni vita vilivyopangwa barabara katika kila hatua yake na waislamu walikuwa na ari na pupa ya kufurahikia kile walichoandikiwa na Allah katika vita hivi.

Yaani kuwezeshwa kupigana na kisha kuibuka na ushindi lau si wanafiki kutaka kuitibua furaha hii.

Wanafiki hawa waliitumia fursa ya matukio mawili yaliyotokea baada ya vita hivi. Matukio ambayo yalistahiki kupishwa yapite kama yanavyopita matukio mengine ya kawaida bila ya kuvuta hisia za mtu ye yote au kumuacha akishangaa.

Lakini kwa tabia ya wanafiki hawakuridhika kuyaacha matukio haya  kupita hivi hivi tu, wakaamua kulitumia tukio la mwanzo kuchochea na kupalilia fitna.

Fitna ambayo ilikurubia kuufagilia mbali umoja baina ya Muhajirina na Answari. Na kulitumia tukio la pili kuinajisi na kuichafua twahara ya nyumba ambayo ni toharifu na takatifu kuliko nyumba zote.

Nyumba yenye heshima, daraja na cheo kitukufu katika nyoyo za waislamu.

Ama tukio la mwanzo lilisababishwa na kugombea maji baina ya kibarua wa Sayyidina Umar Ibn Al-Khatwaab na mshirika wa Khazraj.

Wakazozana kwa ajili ya maji na hatimaye kupigana, yula mshirika wa Khazraji akapiga ukelele kuomba msaada kutoka kwa washirika wake:

“Enyi kusanyiko la Answari!” Kibarua kusikia hivyo nae akapiga ukelele kuomba msaada, akaita: “Enyi kusanyiko la Muhajirina!” Washirika wa kila mmoja wa wagomvi hawa wakauitika ule wito wa msaada uliotolewa, wakatoka walio wepesi miongoni mwao kuja kuangalia kulikoni na kutoa msaada ulioombwa.

Makundi yote mawili yakakutana na kukurubia kuzuka mapigano baina yao na kuamka fitna baina ya Muhajirina; washirika wa kibarua, na Answari; washirika wa mshirika wa kabila la Khazraji. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliposikia zogo hilo akatoka nje haraka akisema: “Ni ya nini hii miito ya Kijahilia?”

Wakampasha khabari nzima inayojiri hata kusababisha zogo hilo alilolisikia, Mtume akapiga ukelele wa ghadhabu:

 Hebu liacheni neno hili (la ukabila), kwani linanuka na kutoa harufu ya uvundo.

Kwa kauli yake hii, Bwana Mtume akaweza kuyatuliza makundi mawili yale ya waislamu na hali ikarejea kuwa shwari.

Mtume wa Allah akamgeukia yule mtu aliyepigwa katika ule mzozo wa maji, akazungumza nae mpaka akakubali kusamehe, kwa njia hii moto wa fitna ulioanza kuwaka ukazimika na kuashiria kuhizika, kufedheheka na kushindwa kwa maadui; wapikaji wa fitna hii.

Kuzimika na kuruka patupu kwa fitna hii hakukumfurahisha mpishi mkuu wa fitna hii; Abdullah Ibn Ubayyi.

Kuzimika kwa cheche za moto huu kabla ya kulipua moto mkubwa kama alivyotarajia na kufa kwa fitna hii kabla ya kuusambaratishia mbali umoja na mshikamano wa waislamu kama alivyotamani.

Jambo hili lilimkera na kumuudhi upeo Ibn Ubayyi, khasa pale ilipomfikia khabari ya namna suala la kibarua na mshirika lilivyomalizwa na Mtume wa Allah kwa amani na salama. Akaanza kuwaambia wafuasi wake:

“Wallah, sijapatapo kuuona udhalili kama huu wa leo! Wametukimbiza na kutuzonga katika mji wetu na wamekosa hata shukrani kwa wema wetu tuliowatendea! Wallah, mimi sijioni na hii mikanzu ya Makurayshi ila kama vile alivyosema msemaji: Mnenepeshe mbwa wako akule! Tukirudi Madinah, mwenye utukufu (Ibn Ubayyi) atamfukuza mnyonge (Mtume)”.

Kisha akawaelekea jamaa zake waliohudhuria pale akiwalaumu na kuwatupia maneno makali:

“Haya ndio mliojitakia wenyewe, mmewahalalishia mji wenu, mkawakaribisha majumbani mwenu na mkawasaidia katika mali zenu mpaka wakajikwasia (wakawa matajiri). Wallah, lau mngeliwazuilia vilivyomo mikononi mwenu, bila ya shaka wangelihama. Basi msitoe mali kuwapa wafuasi wake ili waondokelee mbali”.