"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

NI WAJIBU WA WAUMINI KUWA NA DHANA NJEMA KUWAELEKEA WAUMINI WENZAO NA WASIWE NYUMA YA UZUSHI NA UVUMI.

Hapo ndio aya zikawapa waumini somo yenye kwenda mbali mno mafundisho yake katika namna waliyotakiwa kuwa  katika mfano wa matuko haya yenye khatari.

Ilikuwa ni wajibu wa waumini kuwadhania vema waumini wenzao; wanaume na wanawake. Na wala wasingeliwasadiki waongo hawa walioueneza uvumi huu mpaka walete usahidi wa kutinda katika kuthibitisha madai yao hayo.

Na wala wasingeliwasaidia wapumbavu hawa katika kueneza uwongo wao huo mkubwa na wakazihifadhi ndimi zao kujiingiza katika hilo.

Halafu aya zikawatahadharisha kutorudia kosa kama hilo kamwe na wasiende nyendo za kueneza uovu/machafu katika jamii yao.

Kwani yote hayo ni katika jumla ya matendo ya shetani na aya zikawakumbusha neema ya imani waliyopewa na Allah kwa fadhila zake, neema ambayo inawapa kinga dhidi ya kunguwao.

Na namna ambavyo Allah amewasamehe makosa yao hayo na akawataka wale wenye mwendo mzuri na hali jema kimaisha wawasamehe wale walioleta uovu kwa njia hii.

Na kwamba wasiwanyime misaada waliyokuwa wakiwapa eti kwa sababu tu ya makosa yao hayo.

“HAKIKA WALE WALIOLETA UWONGO HUO (wa kumsingizia Bibi Aysha-mkewe Mtume-kuwa amezini) NI KUNDI MIONGONI MWENU (ni jamaa zenu). MSIFIKIRI NI SHARI KWENU, BALI HIYO NI KHERI KWENU. KILA MTU KATIKA WAO ATAPATA ALIYOYACHUMA KATIKA MADHAMBI HAYO. NA YULE ALIYEJITWIKA SEHEMU KUBWA MIONGONI MWAO, ATAPATA ADHABU KUBWA (zaidi). MBONA MLIPOSIKIA (khabari) HII, WAUMINI WANAUME NA WAUMINI WANAWAKE HAWAKUWA DHANIA WENZAO MEMA, NA KUSEMA: HUU NI UZUSHI DHAHIRI? MBONA HAWAKULETA MASHAHIDI WANE? NA WALIPOKOSA KULETA MASHAHIDI, BASI HAO MBELE YA ALLAH NI WAONGO. NA KAMA ISINGELIKUWA JUU YENU FADHILA YA ALLAH NA REHEMA YAKE KATIKA DUNIA NA AKHERA, BILA SHAKA INGELIKUPATENI ADHABU KUBWA KWA SABABU YA YALE MLIYOYASHUGHULIKIA. MLIPOUPOKEA (uwongo huo mkawa mnautangaza) KWA NDIMI ZENU NA MKASEMA KWA VINYWA VYENU MSIYOYAJUA NA MLIFIKIRI NI JAMBO DOGO, KUMBE MBELE YA ALLAH NI KUBWA. NA MBONA, MLIPOSIKIA HAMKUSEMA: HAITUJUZII KUSEMA HAYA, UTAKASIFU NI WAKO (Mola wetu!) HUU NI UWONGO MKUBWA. ALLAH ANAKUNASIHINI MSIRUDI KABISA KUFANYA MFANO WA HAYA, IKIWA NYINYI NI WAUMINI KWELI. NA ALLAH ANAKUBAINISHIENI AYA (zake) NA ALLAH NDIYE AJUAYE, MWENYE HIKIMA. KWA YAKINI WALE WANAOPENDA UENEE UOVU KWA WALE WALIOAMINI, WATAPATA ADHABU IUMIZAYO KATIKA DUNIA NA AKHERA NA ALLAH NDIYE ANAYEJUA (ya maslaha yenu) NA NYINYI HAMJUI. NA (yangetokea machafuko makubwa) ISINGELIKUWA FADHILA YA ALLAH JUU YENU NA REHEMA YAKE NA KUWA ALLAH NI MPOLE, MWENYE HURUMA. ENYI MLIOAMINI! MSIFUATE NYAYO ZA SHETANI, NA ATAKAYEFUATA NYAYO ZA SHETANI (atapotea) KWANI YEYE HUAMRISHA MAMBO YA AIBU NA MAOVU. NA LAU KUWA SI FADHILA ZA ALLAH NA REHEMA YAKE JUU YENU ASINGALI TAKASIKA MIONGONI MWENU HATA MMOJA, LAKINI ALLAH HUMTAKASA AMTAKAYE, NA ALLAH NI MWENYE KUSIKIA (na) MWENYE KUJUA. NA WASIAPE WALE WENYE MWENDO MZURI (wa dini) NA WENYE WASAA (katika maisha yao) MIONGONI MWENU (wasiape kujizuia) KUWAPA WALIO JAMAA NA MASIKINI NA WALIOHAMA KWA NJIA YA ALLAH. NA WASAMEHE NA WAACHILIE MBALI (wapuze yaliyopita). JE, NYINYI HAMPENDI ALLAH AKUSAMEHENI? NA ALLAH NI MWINGI WA MSAMAHA (na) MWINGI WA REHEMA (basi na nyinyi sifikeni kwa sifa hizi)”. [24:11-22]

 

II.          UTAKASIFU WA HESHIMA/HADHI YA MTU:

Heshima/hadhi ya mtu ni miongoni mwa vitu vitukufu kabisa anavyostahiki mwanadamu kutoka kwa jamii inayomzunguka.

Kwa hivyo basi ni kitu kinachohitajia mno kulindwa na kuhifadhiwa ili kisichafuliwe na kuvunjwa hovyo.

Kwa kulitambua hili, ndipo aya tukufu zikatahadharisha kwa ukali kabisa kuvunja heshima ya mtu kwa kuzua uzushi au kuleta utesi.

Na zikawalaani wale wanao wasingizia machafu wanawake waumini, laana ya Allah iwashukie duniani na akhera na kuwakamia kupata adhabu kubwa mno siku ya kiyama:

“BILA SHAKA WALE WANAOWASINGIZIA WANAWAKE WALIOTAKASIKA WASIOJUA (maovu), WAUMINI (wenye kuwasingizia watu hawa) WAMELAANIWA KATIKA DUNIA NA AKHERA; NAO WATAPATA ADHABU KUBWA. SIKU AMBAYO ZITAWASHUHUDIA NDIMI ZAO NA MIKONO YAO NA MIGUU YAO, KWA YALE WALIYOKUWA WAKIYAFANYA. SIKU HIYO ALLAH ATAWAPA SAWA SAWA MALIPO YAO YA HAKI, NA WATAJUA KWAMBA ALLAH NDIYE (Mwenye kulipa kwa) HAKI ILIYO DHAHIRI”. [24:23-25]

Halafu tena ndipo maudhui haya yakakhitimishwa kwa kuwekwa  kanuni jamii enevu yenye dhima ya kuvunja tuhuma kwenye msingi na mzizi wake. Kanuni ambayo inasilihi (inafaa) kuwa ni mizani ya kutolea hukumu kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla wake katika kila zama na kila mahala:

“WANAWAKE WABAYA NI WA WANAUME WABAYA, NA WANAUME WABAYA NI WA WANAWAKE WABAYA. NA WANAWAKE WEMA NI WA WANAUME WEMA, NA WANAUME WEMA NI WA WANAWAKE WEMA; HAO WAO WAMEEPUSHWA NA HAYO WANAYOYASEMA, WAO WATAPATA MSAMAHA NA RIZIKI ILIYO NA HISHIMA (peponi)”. [24:26]

Ni kama hivi kila mmoja atafuata njia yake aliyoichagua na kila chombo hukiivisha kilichomo ndani yake.

Hivi ndio kusema wanawake wachafu (wazinifu) ni stahiki ya wanaume wachafu wenziwao, kama ambavyo wanawake wazuri (wasiofanya machafu) walivyo stahiki ya wanaume wazuri mithili yao.

Kisha tena hakumuelei muumini kuyasadikisha au kuyakadhibisha anayoyasikia kutoka kwa nduguye muumini ila baada ya kuyasoma mazingira ya hayo aliyoambiwa.

Na achunguze sababu na natija na azitafiti tabia za mtoa khabari wake, chimbuko lake na mazingira aliyokulia. Si hayo tu, bali anapaswa kuchunguza ni mambo gani yaliyomsukuma huyo fulani kutenda alilolitenda au kuacha kulitenda.

Haya huo ni kwa upande wa muumini mwenziwe, seuze kwa kafiri! Ama kuufuata uvumi tu, kufanya hivyo si busara wala hekima na hili ndilo Allah Taala alilowatahadharisha waumini wasilirudie tena, katika kauli yake tukufu:

“ALLAH ANAKUNASIHINI MSIRUDIE KABISA KUFANYA MFANO WA HAYA, IKIWA NYINYI NI WAUMINI KWELI. NA ALLAH ANAKUBAINISHIENI AYA (zake) NA ALLAH NDIYE AJUAYE, MWENYE HIKIMA”. [24:17-18]

 

III.    QUR-ANI ILIKUWA KALI KATIKA KULIELEKEA SUALA LA UZUSHI HUU:

Tukio hili la uzushi kama lilivyosawirishwa na Qur-ani Tukufu, Allah Taala akaweka sheria chini ya mazingira yake ili kuilinda jamii ya Kiislamu dhidi ya jarima ya zinaa.

Na kuilinda dhidi ya jarima ya kuchafua na kuvunja hadhi/heshima ya wanawake waumini.

Na ikatia mkazo mkata katika kuithibitisha jarima hii ili watu wasio na hatia wasihukumiwe na kuadhibiwa kutokana na uzushi wa mtu tu. Mtu anaweza kusema/kuuliza:

Þ    Hivi kweli ni jambo linalowezekana mtu kuleta mashahidi wane ili kuthibitisha hali ya jarima ya zinaa kwa mwanamume na mwanamke?

Þ    Je, hili linamkinika katika hali zote?

Þ    Je, ni jambo linaloingia akilini kwamba jarima ya zinaa haiwezi kuthibiti ila kwa ushahidi wa kuona wa mashahidi wanne?

Þ    Na je, huku si kumfanya mtu ashindwe kabisa kuithibitisha jarima hii chafu yenye kufedhehesha?

    Naam, ni kweli kabisa kwamba hilo linaweza kuwa gumu kupatikana kwake na pengine kushindikana kabisa. Lakini Muweka sheria hiyo (Allah) ameyazingatia kwa upande huo mambo kadhaa yenye umuhimu mkubwa sana.

Alichoangalia na kuzingatia ni kule kufungamana kwa jambo hili na heshima/hadhi za watu. Na kwamba hili ni suala hisia lenye athari kubwa mno kwa kila mwenye kuguswa na maneno hayo ya watu, yawe ni ya kweli au uongo.

Na akazingatia kwamba tabia/maumbile ya watu ni wepesi mno wa kupokea uvumi na kuusadiki na kisha kuueneza haraka.

Kwa kuwa hayo ndiyo maneno yapendezayo nafsini mwao na ndio mazungumzo ya baraza zao kwa ghalibu.

Na akazingatia kwamba hili ni suala linalofungamana na heshima/sifa ya jamii ya Kiislamu, jamii inayopaswa kuwa mfano/kigezo cha kuigwa na jamii nyingine katika utoharifu (utakasifu), unadhifu (usafi) na sifa yake njema.

Ni kwa ajili ya kuyazingatia yote haya ndio Muweka sheria akaweka vizuizi hivi vigumu na akaweka ngome hizi imara ambazo ni kugumu mno kuzivuka.

Ili alinde na kuhifadhi heshima na hadhi ya waumini wake kwa waume na kukata ndimi za watu wazushi waenezao uvumi kwa lengo la kuuchafua utu wa watu wasio na hatia.

Na ili awawekee waislamu desturi shadidi itakayowasukuma kutafakari na kuwa makini wakati wa kusikiliza khabari za uzushi kama hizi.

Desturi itakayowalazimisha kutaka kubaini na kuthibitisha yote yasemwayo na kuweka kizuizi baina yao na wasio waumini katika suala zima la kukubali na kusadiki uvumi uwongo bila ya kuwa na ujuzi wa lisemwalo.

“ENYI MLIOAMINI! KAMA FASIKI (asiye wa kutegemewa) AKIKUJIENI NA KHABARI (yo yote ile msimkubalie tu) BALI PELELEZENI (kwanza), MSIJE MKAWADHURU WATU KWA UJAHILI NA MKAWA WENYE KUJUTA JUU YA YALE MLIYOYATENDA”. [49:06]