"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

JESHI LA ALLAH

Ni katika wakati huu ambamo mafungamano yalichangukana, ukweli/uaminifu baina ya majeshi shirika na nafsi zikakimwa kwa kukaa muda mrefu.

Ndimo Allah Taala aliyapelekea majeshi shirika upepo mkali katika usiku unyeshao mvua, wenye baridi kali na giza totoro.

Majungu ya vyakula yakaanza kupinduliwa na upepo, vyombo vikarushwa mbali, mioto ikazimika na mahema yakabomoka.

Nyoyo zao zikatambaliwa na khofu na fazaa iliyowapelekea kuchelea kushambuliwa ghafla na waislamu katika kipindi hicho kigumu.

Khofu na fazaa hii ikawafikisha kuchukua aumuzi wa kuacha vita na kurudi mwakwao. Ibn Is-haaq-Allah amrehemu-anasema:

“Khabari za kukhitilafiana kwao zilipomfikia Mtume wa Allah-Rahama na Amani zimshukie-na jinsi Allah alivyouvunja umoja wao. Alimuita swahaba wake; Hudhayfah Ibn Al-Yamaan-Allah amuwiye radhi-akamtuma kwenda kuchunguza mahasimu wao wamefanya nini usiku. (Hudhayfah anahadithia): Nilijikuta handakini pamoja na Mtume wa Allah, akaswali kidogo usiku ule, kisha akatugeukia na kusema:

“Nani atakayeenda kutuchunguzia mahasimu wetu wamefanya nini, kisha arudi na kutujuza khabari? Nitamuomba Allah mtu huyo awe rafiki yangu peponi”.

Basi hapana hata mtu mmojaa aliyethubutu kujitokeza kutokana na khofu kuu, njaa na baridi kali. Mtume kuona kuwa hakuna aliyejitokeza, ndipo aliponiita nami sikuwa na budi ila kumuitika, akaniambia:

“Ewe Hudhayfah! Nenda kajichanganye na watu wale uchunguze wanafanya nini na usifanye wala kusema cho chote mpaka utakaporudi hapa”.

 (Hudhayfah anaendelea kusimulia): Basi nikaenda na kujichanganya na watu wale na ilhali upepo ule mkali na majeshi ya Allah yakiendelea kuwashughulikia.

Hali ikawa mbaya kiasi cha kufikia hakuna chungu kilichothibiti bila ya kupinduka, moto uliowaka bila ya kuzimika, wala hema lililosimama bila ya kung’oka.

Abu Sufyaan akainuka na kusema:

Enyi kusanyiko la Makurayshai! Kila mtu aangalie amekaa na nani. (Hudhayfah akasema): Nikamshika mkono mtu aliyekuwa ubavuni mwangu nikamuuliza: Wewe nani?”

 Akajibu:

Fulani Ibn fulani. Abu Sufyaan akaendela kusema: Enyi kusanyiko la Makurayshi, wallah hakika nyinyi hamjapata makazi mazuri hapa, farasi na ngamia wetu wanakurubia kuhiliki kwa njaa, Baniy Quraydhwah nao wametutupa mkono.

Na imetupata shida ya upepo mkali kama mnavyoona hakuna jungu linalothibiti ila hupinduliwa, wala moto uwakao ila huzimwa, tena hakuna hema linalosimama ila huezuliwa.

Kwa hali hii fungeni safari turudi Makkah, hakika mimi ninaondoka. Alipokwisha kusema maneno yake hayo, akamuendea ngamia wake na kumpanda. Lau kuwa si ule usia wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alioniambia:

“Usifanye wala kusema lo lote mpaka utakaporudi hapa”, ningelimuua kwa mshale. (Hudhayfah anaendelea kusema):

Nikarudi kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-nae akiwa amesimama anaswali, akiwa kajitanda guo la mmojawapo wa wakeze.

Aliponiona akaniingiza miguuni mwake na kunitupia ncha ya guo lile, halafu akarukuu na kusujudu nami nikiwa humo humo ndani ya guo lile.

Alipotoa salamu nikampasha khabari za niliyoyaona na kuyasikia huko. Ghatwfaan wakapata khabari ya uamuzi uliofikiwa na Makuryashi wa kuondoka na kurudi makwao, nao haoo wakaondoka kurudi makwao.

Kulipopambazuka asubuhi, waislamu hawakumuona hata mtu mmoja katika kambi ya majeshi shirika. Hapo wakayakinisha ya kuwa msaada wa Allah u pamoja nao na kwamba jicho la Allah linawahifadhi na kuwalinda.

Imani yao ikazidi kwamba wao wako katika haki na kwamba Allah atawapa nusra dhidi ya maadui zao siku zote. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawaangalia maswahaba wake kwa jicho lililojaa matumaini na ukweli kwa Allah, akasema:

“Sasa tutawapiga na wala hawatatupiga”, halafu akatamka kwa sauti kubwa na kufuatiwa na maswahaba wake: Hapana Mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah pekee, amemnusuru mja wake, amelipa nguvu jeshi lake na ameyashinda makundi (ya majeshi shirika) peke yake, basi hapana kitu baada yake!”

 

       IV.       Mazingira ya vita hivi:

 Vita hivi vya Ahzaab havikuwa ni vita vya medani ambamo huonekana ushujaa kwa kushambulia na kurudi nyuma.

Bali hivi vilikuwa ni vita vya kutahini azma na nyoyo, ni kwa ajili hii ndio wanafiki wakashindwa mtihani na waumini kufaulu.

Wakati ambapo wanafiki na wale wote wenye maradhi ya nyoyo walidhihirisha kupapatika, shaka na udhaifu wa nafsi.

Waumini wao walionyesha ustahamilivu na subira iliyoonyesha uimara wa imani yao na yakini yao kwa Allah.

Na yakini yao kwamba nyuma ya shida hii kuna faraja iliyo karibu na kwamba hakika si vinginevyo Allah Taala ametaka kuwapa majaribu na kuwatahini imani zao kupitia shida na dhiki hii iliyowasibu.

Walipofaulu mtihani huu kwa kiwango hiki cha juu kabisa ndipo Allah alipowakunjulia mkono wake wa rehema na kuwaokoa kwa neema zake kutoka kwenye makucha makali ya adui yao:

“NA WAUMINI WALIPOYAONA MAJESHI (ya makafiri yamewashambuli hivyo) WALISEMA HAYA NDIO ALIYOTUAHIDI ALLAH NA MTUME WAKE (kuwa tutapata misukosuko, kisha tutashinda). ALLAH NA MTUME WAKE WAMESEMA KWELI, NA (jambo hili) HALIKUWAZIDISHIA ILA IMANI NA UTII. WAPO WATU MIONGONI MWA WALIOAMINI WALIOTIMIZA AHADI WALIYO AHIDIANA NA ALLAH. BAADHI YAO WAMEKWISHAMALIZA UMRI WAO (wamekwisha kufa) NA BAADHI YAO WANANGOJA (siku yao kufika), WALA HAWAKUBADILISHA (ahadi yao) HATA KIDOGO. ILI ALLAH AWALIPE WAKWELI KWA SABABU YA UKWELI WAO NA KUWAADHIBU WANAFIKI AKIPENDA (kwa kuwa hawakurejea) AU KUWAGEUKIA (kwa rehema kama wakitubia). BILA SHAKA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA KUREHEMU. NA WALE WALIOKUFURU ALLAH ALIWARUDISHA NA GHADHABU YAO, HAWAKUPATA CHO CHOTE KATIKA KHERI NA ALLAH AKAWAKIFIA WAISLAMU MAPIGANO NA ALLAH NI MWENYE NGUVU MBORA”. [33:22-25].