"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

MGAO WA MALI NA MATEKA

Baada ya kumazika kazi ya kuwaua wasaliti, ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipowagawia waislamu mali za Baniy Quraydhwah pamoja na wake na watoto wao.

Akawapeleka Shaam na Najid baadhi ya mateka akawauza huko na pesa iliyopatikana akanunua silaha na farasi kwa ajili ya jeshi la Kiislamu. Bwana Mtume alitoa agizo la kutotenganishwa mama na wanawe katika zoezi zima la mgao na uuzaji, akasema:

“Watoto wasitenganishwe na mama zao mpaka wafikilie baleghe (wawe wakubwa)”. Bi. Rayhaanah Bint Amrou akaangukia kuwa ni katika fungu la Mtume, akaishi na Mtume mpaka alipofariki akiwa chini ya milki yake.

Ni kawaida ya kimaumbile kwamba mtu hulipwa kulingana na amali/matendo yake; mtenda wema atalipwa kwa wema wake na kinyume chake mtenda maovu atayalipia maovu yake.

Huu ni ukweli unaoishi sambamba na mwanadamu katika sayari hii, ni ukweli unaothibitishwa na tarekh (historia).

Hiki ndicho kisa kizima cha Baniy Quraydhwah kama kilivyosajiliwa na Historia, basi je ndani yake mna fursa ya kumuaibisha na kumtia dosari Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie?!

Ni kweli kama isemwavyo kwamba haya yalikuwa ni mauaji makubwa, ni mauaji yaliyolifagilia mbali kabila zima la Mayahudi.

Lakini mauaji kama haya au zaidi yake yalikurubia kuwa fungu la waislamu lau azma ya majeshi shirika ya kumuangamiza Mtume na maswahaba wake ingefanikiwa.

Kwa mantiki hii basi, mauaji haya hayakustahili kuawiliwa (kutafsiriwa) vingine zaidi ya kuwa kwake ni jazaa/malipo muafaka na stahiki ya dhamira na matendo ya Baniy Quraydhwah.

Hii ni jazaa adilifu inayohukumiwa na dini sahihi, ni malipo yanayokubaliwa na akili nyoofu na ni ujira unaokiriwa na sheria/kanuni binadamu tangu zile za kale na hata hizi za sasa.

Mwanahistoria Badwell anaukiri ukweli huu, anasema:

“Ukweli khasa lau Mayahudi wa mji wa Madinah wangelifikiria kwa makini suala hili, wangeligundua kwamba Muhammad hakutenda cho chote kikubwa au kidogo zaidi ya kutekeleza mafundisho yaliyomo katika vitabu vyao: [Utakaposongea karibu ya mji kwenda kupigana juu yake, ndipo utakapowapigia ukelele wa amani. Itakuwa utakapokujibu kwa amani, na kukufungulia, ndipo watu wote watakaoonekana humo watakufanyia kazi ya shokoa, na kukutumikia. Na kwamba hautaki kufanya amani nawe, lakini utafanya vita juu yako, ndipo uuhusuru (uuzingire kwa vita); na BWANA, Mungu wako, autiapo mkononi mwako, mpige kila mume aliyemo kwa makali ya upanga; lakini wanawake na watoto, na wanyama wa mji, na vilivyo mjini vyote, navyo ni nyara zako zote, uvitwae viwe mateka kwako; nawe utakula nyara za adui zako alizokupa BWANA, Mungu wako”.] {KUMBUKUMBU LA TORATI: 20/10-15]

Kosa la jinai la Huyay Ibn Akhtwab:

Daktari Heikal anasema:

“Katika fikra zetu ni kwamba damu ya Baniy Quraydhwah imefungamana na shingo ya Huyay Ibn Akhtwab hata kama aliuliwa pamoja nao.

Yeye bila ya shaka alikwenda kinyume na ahadi aliyoitoa kwa jamaa zake Banin-Nadhwiyr wakati Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alipowatoa Madinah.

Na wala hakumuua hata mtu mmoja miongoni mwao baada ya kukubali kwao kuingia chini ya hukumu yake.

Yeye huyu kwa kitendo chake hiki cha kuwakuwasanya Makurayshi, Ghatwfaani na Waarabu wote dhidi ya Mtume, tayari alikwishajenga uadui baina ya waislamu na mayahudi. Akawafanya waislamu kuitakidi kwamba katu Baniy Israil hawataona raha wala furaha ila kwa kumfagilia mbali Mtume na maswahaba wake.

Na ni yeye huyu ndiye aliyewasukuma Baniy Quraydhwah kuvunja mkataba wa amani na ujirani mwema na Mtume na isitoshe kujitoa katika msimamo wao wa kutounga mkono upande wo wote.

Lau wao wangeliuheshimu na kuulinda mkataba huu wasingelifikwa na yote yaliyowafika. Tena ni yeye ambaye aliyeingia katika ngome za Baniy Quraydhwah baada ya kuondoka kwa majeshi shirika akiwachochea kupigana na waislamu na kujilinda dhidi yao.

Lau wao wangelisalimu amri kwa hukumu ya Mtume tangu siku ile ya kwanza na wakalikiri kosa lao la kuvunja mkataba, bila shaka damu yao isingelimwagika.

Lakini uadui ulikita mno ndani ya nafsi ya Huyay na kuambukia katika nafsi za Baniy Quraydhwah.

Kiasi cha kumfanya Sa’ad Ibn Muaadh mwenyewe akiwa mshirika wao kuamini kuwa lau wangeliachwa hai, basi wasingelitulizana ila kukusanya upya washirika kuwapiga waislamu.

Na kama wangelifanikiwa, basi wangeliwaua waislamu mpaka mtu wa mwisho.

Kwa hiyo basi hukumu hii aliyoitoa Muhammad pamoja na ukatili na ukali wake, ilikuwa imeegemea zaidi katika upande wa kujilinda dhidi ya shari ya adui (self defence).

Na kuzingatia kwake kubakia/kuondoka kwa Mayahudi ni suala linalogusa uhai/mauti kwa upande wa waislamu.

Hii ndio rai na fikra ya Daktari Heikal, anamtwisha dhima ya mauaji ya Baniy Quraydhwah, Huyay Ibn Akhtwab. Na hivyo hivyo ndivyo alivyoona Salaam Ibn Miksham mmoja wa Banin-Nadhwiyr ilipomfikia khabari hii ya Baniy Quraydhwah, akasema:

“Hii yote ni kazi ya Huyay Ibn Akhtwab, kamwe Muyahudi hatokaa Madinah”.

 

Natija ya vita:

Vyo vyote iwavyo, vita hivi vilizifagia kabisa koo za Mayahudi katika mji wa Madinah na kuwakosesha wanafiki wasaidizi humo.

Sauti zao zikashuka chini, nguvu yao ikavunjika na kushindwa kusimama tena. Kwa upande mwingine Allah akawamakinisha waislamu Madinah baada ya vita hivi na mambo yao yakaanza kwenda kwa amani.

Na da’awah ya Kiislamu ikavaa chapya mpya; chapa ya nguvu, uwezo na heshima na kuivua ile chapa ya unyonge, umasikini na kusalimu amri kwa adui.

Tena waislamu wakazichukua ngawira mali za Baniy Quraydhwah ikiwa ni pamoja na silaha na samani.

Wakarithi ardhi, majumba, mashamba, mifugo na mali zao zote, naam ngawira ya waislamu ilikuwa nono kwa pande zote; upande wa kimaada na ule wa kimaana. Allah Taala anasema katika kushindwa huku kwa majeshi shirika:

“ENYI MLIOAMINI! KUMBUKENI NEEMA ZA ALLAH ZILIZO JUU YENU; YALIPOKUFIKIENI MAJESHI TUKAYAPELEKEA UPEPO NA MAJESHI MSIYOYAONA (ya Malaika), NA ALLAH ANAYAONA (yote) MNAYO YAFANYA”. [33:09]

Kisha Allah Taala anaielezea hali ya waumini na wanafiki ilivyokuwa wakati wa hujuma ya majeshi shirika.

Na namna yalivyoondoshwa majeshi shirika baada ya waislamu kufikwa na dhiki kuu mpaka ikawajia nusra ya Allah:

“NA WALE WALIOKUFURU ALLAH ALIWARUDISHA NA GHADHABU YAO, HAWAKUPATA CHO CHOTE KATIKA KHERI; NA ALLAH AKAWAKIFIA WAISLAMU MAPIGANO. NA ALLAH NI MWENYE NGUVU NA MBORA”. [33:25] Na katika kushindwa kwa Baniy Quraydhwah anasema: “NA AKAWA TEREMSHA WALE WALIOWASAIDIA (maadui) KATIKA WATU WALIO PEWA KITABU (kabla yenu; Mayahudi, aliwatoa) KUTOKA KATIKA NGOME ZAO, NA AKATIA KHOFU KATIKA NYOYO ZAO, BAADHI YAO MKAWA MNAWAUA, NA WENGINE MNAWATEKA. NA AKAKU RITHISHENI NCHI YAO NA MAJUMBA YAO NA MALI ZAO, NA NCHI MSIYOIKANYAGA (kabla ya hapo); NA ALLAH NI MWENYE UWEZA JUU YA KILA KITU”. [33:26-27]