"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

USHUJAA WA SALAMAH IBN AL-AKWAA

Kwa hakika Salamah Ibn Al-Akwaa-Allah amuwiye radhi-alidhihirisha ushujaa mkubwa katika vita hivi, ushujaa uliompelekea Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kummwagia sifa, akisema:

“Bora ya askari wapanda farasi wetu leo ni Abu Qataadah na bora ya askari wetu wa miguu leo ni Salamah”.

Na akampa mafungu yote mawili; fungu la mpanda farasi na lile la mpiganaji wa miguu. Salamah mwenyewe anasimulia hali ilivyokuwa:

“Nilitoka kabla ya kuadhiniwa kwa adhana ya kwanza (ya swala ya Alfajiri) na ngamia wa Mtume wa Allah walikuwa wakichunga Dhiy Qirdi. (Anaendelea kusema): Njiani nikakutana na kijana (mtumishi) wa Abdirahmaan Ibn Auf, akaniambia:

 Ngamia wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wameporwa. Nikamuuliza: Ni nani aliyewachukua? Akajibu: Ghatwafaan.

(Anaendelea kusema): Nikapiga mayowe matatu yaliyowafikia watu wa Madinah. Kisha nika chapua mwendo mpaka nikawakuta (waporaji) Dhiy Qirdi wakiwa wamepumzika wakinywa maji. Nikaanza kuwarushia mishale huku nikiimba ubeti huu:

Mimi, mimi ndiye Ibn Al-Akwaa *** Na leo hii ni siku ya mapambano tu.

Nikaendelea kuimba na huku nikiwatupia mishale mpaka nikafanikiwa kuwaokoa ngamia na kuchukua maguo yao thelathini waliyoyaacha kwa haraka ya kukimbizana.

(Anaendelea): Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akafika na kundi la watu, nikamwambia: Ewe Mtume wa Allah, hakika mimi nimewazuilia watu wale (waporaji) kunywa maji nao wakiwa na kiu, basi waendee upesi sasa hivi. (Mtume) akasema:

Ewe Ibn Al-Akwaa, tulia na fanya mambo taratibu”. (Akasema):

Kisha tukaanza kurejea na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akinipandisha nyuma yake juu ya ngamia wake mpaka tukaingia Madinah)”. Bukhaariy & Muslim kutoka kwa Yazid Ibn Abiy Ubeid-Allah awarehemu.

Ama yule mwanamke, yeye alifanikiwa kuwapumbaza watekaji nyara wake na hatimaye kuwatoroka akimtumia ngamia wa Mtume wa Allah, aliyekuwa miongoni mwa ngamia waliokuwa wameporwa.

Kabla waislamu hawajaanza kulijadili suala lake, tahamaki huyoo anaingia Madinah na kuwaacha wakipigwa na butwaa. Alipofika kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamsimulia khabari yake ilivyokuwa hata akaweza kutoroka na kufika Madinah salama.

Halafu akasema: Ewe Mtume wa Allah, hakika mimi niliweka nadhiri ya kumchinja ngamia huyu ikiwa Allah ataniokoa juu yake. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akatabasamu na kusema:

“Malipo mabaya yaliyoje unayotaka kumlipa ni kumchinja baada ya Allah kukubeba juu yake na kukuokoa! Hakika hapana nadhiri kwa ye yote katika kumuasi Allah na wala mtu hawezi kuweka nadhiri kwa asichokimiliki. Hakika si vinginevyo, huyo ni mmoja wa ngamia wangu (walioporwa), haya rejea kwenu kwa baraka za Allah!”

Katika mwezi huu huu wa Rabiul-Awwal, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimtuma Ukaashah Ibn Mihswan kuliongoza kundi la askari wapandaji kwenda “Ghamri”.

Hili ni eneo lenye maji lililo kuwa likimilikwa na Baniy Asad kwenye njia iendayo Najid. Akatoka shoti ili awashambulie watu hao kwa kuwashtukiza, lakini wapi tayari walikwishapata khabari zake na wakakimbia kabla hajawafikia.

Alipofika mahala pao, akaanza kuulizia khabari zao mpaka akaitokea mifugo yao akaiswaga na walikuwa jumla ya ngamia mia moja. Halafu huyoo akarejea Madinah bila ya kukumbana na upinzani wo wote wala kupata madhara.

    II.          Kikosi (Sariya) cha vita cha Dhil-Qiswah:

Mnamo mwezi wa Rabiul-Aakhir wa mwaka huu huu wa sita (Agosti 627 A.D.), Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimtuma Muhammad Ibn Maslamah pamoja na watu kumi kuwaendea Baniy Tha’alabah upande wa “Dhil-Qiswah”.

Hili ni eneo lililokuwa umbali wa maili ishirini na nne kutoka Madinah kwa upande wa Hijaaz. Mushrikina wakapata khabari ya kutoka kwao, wakajificha watu mia moja miongoni mwao, wakawangojea waislamu mpaka walipolala.

Ndipo walipowatokea na kuwashambulia kwa ghafla na kwa nguvu na kufanikiwa kuwaua wote isipokuwa Muhammad Ibn Maslamah waliyemdhania amekufa baada ya kuanguka akiwa kajeruhiwa vibaya sana.

Wakamuacha hapo, mmoja wa waislamu aliyekuwa akipita hapo akamuona na kumchukua mpaka Madinah. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akajua yaliyotokea, akamtuma Abu Ubeidah Ibn Al-Jaraah na watu arobaini.

Hao wakatoka hata walipofika kwenye makazi ya watu wale, hawakuwakuta ila baadhi ya wanawake, mifugo na samani chakavu. Wakavichukua ngawira hivyo walivyovikuta bila ya kuwapata mushrikina wale.

 III.          Sariya (kikosi) ya Al-Jumuum:

Katika mwezi huu wa Rabiul-Aakhir, pia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimpeleka Zaid Ibn Haarithah kwenda kwa Baniy Suleim pande za “Al-Jumuum”, akiwa na kundi la waislamu.

Mahala palipokuwa umbali wa maili nne kutokea Madinah kwenye njia ielekeayo Basrah. Walipofika kwenye maboma yao, walikuwa tayari wamekwisha tawanyika, wakamkuta mwanamke mmoja wa kabila la Muzeinah wakamchukua.

Huyu ndiye aliye wafahamisha na kuwaonesha baadhi ya maboma ya Baniy Suleim, humo wakawapata ngamia, kondoo na mbuzi.

Wakawakuta na baadhi ya wanamume wakawachukua mateka, miongoni mwa mateka hawa alikuwemo mume wa mwanamke huyu. Zayd aliporejea Madinah na ngawira aliyoipata kutoka kwa maadui wale, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamuacha huru mwanamke yule na mumewe.

  IV.          Sariya ya Al-Iyswi:

Mnamo mwezi wa Jumadaal-Uula wa mwaka huu (Septemba 627 A.D.), Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimtuma tena Zayd Ibn Haarithah kuliongoza kundi la askari wapanda wanyama mia moja na sabini.

Alimtuma kwenda “Al-Iyswi”, mahala palipokuwa umbali wa mwendo wa siku nne kutoka Madinah, ili kuuzuia msafara wa biashara wa Makureishi uliokuwa ukitokea Shamu kuelekea Makkah.

Zayd akafanikiwa kuukata njiani na kuuteka, ndani ya msafara huo kulikuwa na madini mengi ya fedha ya Swafwaan Ibn Umayyah. Na katika waliowachukua mateka alikuwemo Abul-Aaswi Ibn Ar-rabee; mumewe Bi. Zaynab Bint ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Walipofika Madinah, Abul-Aaswi (mkwewe Mtume) akaomba dhamana kwa kumtumia Bi. Zaynab, nae akamchukulia dhamana mumewe huyo.

Akawatangazia watu wakati Mtume alipokwisha kuswali swala ya Alfajiri, akisema:

“Hakika mimi nimemdhamini Abul-Aaswi”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akauliza: “Enyi watu, je mumeyaelewa mliyoyasikia?”, wakajibu: Naam. Mtume akasema:

 “Namuapia yule ambaye nafsi ya Muhammad i mikononi mwake, sikujua cho chote katika khabari hii mpaka niliposikia niliyoyasikia. Waumini wote ni mkono (kitu) mmoja, mmoja wao huzungumza kwa niaba yao na wote wakayaheshimu maneno yake na kuipitisha dhamana yake. Nasi tumemkubalia dhamana ya aliyechukua dhamana na kutoa hifadhi”.

Kisha Mtume akaingia nyumbani mwake, Bi. Zaynab akamfuata na kumuomba amrudishie Abul-Aaswi mali yake iliyochukuliwa.

Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawaambia maswahaba wake:

“Bila ya shaka mnamjua vema mtu huyu (Abul-Aaswi) alivyo kwetu na mmemchukulia mali. Iwapo mtafanya ihsani na mkamrejeshea mali yake, hakika sisi tunalipenda hilo na ikiwa mtakataa, basi mali hiyo ni mali mliyopewa na Allah nanyi mnaistahiki kuliko yeye”.

Wakasema: Ewe Mtume wa Allah, tumekhitari kumrudishia mali yake.

Wakaanza kurudisha walivyovichukua mpaka ikafikia mtu analeta hata ndoo na mwingine analeta chombo cha kujitwahirishia. Mpaka wakamrejeshea mali yake yote bila ya kubakisha hata chembe ya kitu”.