"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

KUSILIMU KWA ABUL-AASWI

I.          Kusilimu kwa Abul-Aaswi:

 Abul-Aaswi akaenda zake Makkah, alipofika huko akampa kila mwenye mali, mali yake, halafu akauliza:

“Je, kuna ye yote miongoni mwenu ambaye hajachukua mali yake kwangu?”, wakajibu: Hapana. Akauliza tena: “Je, nimetekeleza dhima yangu?”, wakajibu:

Naam, Allah akujaze kheri, bila shaka sisi tumekukuta wewe ni mtii mtekeleza amana tena karimu. Hapo ndipo aliposema:

“Hakika mimi ninashuhudia kwamba hapana Mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah na kwamba Muhammad ni mja na Mtume wake. Wallah, hakuna lililonizuia kusilimu mbele yake ila kwa kuwachelea nyinyi kunidhania kwamba hakika si vinginevyo, nimefanya hivyo ili nipate kula mali zenu tu. Basi Allah alipozirejesha kwenu nami nikamaliza kuzigawa kwa wenyewe, ndio nimesilimu”.

 Halafu huyoo akashika njia na kwenda Madinah akiwa tayari ni muislamu na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamrejeshea mkewe.

 

II.          Sariya ya Twarfu:

Na katika mwezi wa Rabiul-Aakhir wa mwaka huu (Oktoba 627 A.D.), kwa mara nyingine tena Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akampa Zayd Ibn Haarithah dhima ya sariya. Akiongoze kikundi cha maswahaba wenzake kwenda kwa Baniy Tha’alabah pande za “Twarfu”, hili ni eneo lenye maji kwenye njia ya kwenda Iraq, umbali wa maili thelathini na sita kutoka Madinah. Akatoka na watu kumi na tano, akapata ngawira ya ngamia ishirini na mabedui aliowaendea wakakimbia na hakuweza kumkamata hata mmoja miongoni mwao. Zayd akaamkia Madinah akiambatana na ngamia hao baada ya kughibu kwa siku nne.

 

III.          Sariya ya Waadil-Quraa:

Katika mwezi wa Rajabu, mwaka huu, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimtuma tena Zayd Ibn Haarithah kwenda “Waadil-Quraa”, kulipa kisasi kwa Baniy Fazaarah.

Hawa waliuzuia msafara wa biashara wa Zayd wakati akirejea Madinah akitokea Shamu, wakampokonya kila kitu na kukurubia kumuua. Alipofika Madinah na kumpasha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-khabari za yote yaliyomtokea katika safari yake.

Ndipo Mtume alipomtuma kuwaendea waporaji hao akiandamana na kundi la maswahaba wake. Wakawaendea na kuwashambulia ghafla katika makazi yao na wakafanikiwa kuliua kundi kubwa miongoni mwao.

 

IV.          Sariya ya Daumatul-Jandal:

Mnamo mwezi wa Shaaban (Novemba 627 A.D.), Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliwapelekea Baniy Kalbi pande za “Daumatul-Jandal”, kikosi cha maswahaba wake wapatao mia saba chini ya Uamiri wa Abdurahmaan Ibn Auf.

 Daumatul-Jandal, hivi ni vitongoji vilivyokuwa pande za Shamu, kati yake na Damascus kuna umbali wa mwendo wa siku tano na baina yake na Madinah ni mwendo wa siku kumi na tano. Mtume akawaambia:

“Nyote piganeni katika njia ya Allah, wapigeni waliomkufuru Allah, msifanye khiana (mkabaka wanawake), msifanye usaliti, msiwaue watu kwa kuwakatakata na wala msiwaue watoto”.

Abdurahmaan na wenzake wakawaendea, alipofika huko akaanza kuwahubiria Uislamu kwa siku tatu, akasilimu kutokana na mahubiri hayo Al-Aswbaghi Ibn Amrou. Huyu ndiye aliyekuwa kiongozi wao na alikuwa mnaswara, kwa kusilimu kwake wakasilimu watu wengi katika kaumu yake.

Wengine wakabakia na dini yao ya awali kwa sharti ya kutoa kodi, Adurahmaan akapatana nao na kuandikiana nao mkataba juu ya hilo. Ili kuzidi kuunga udugu na kabila hili la Baniy Kalbi akamuoa binti ya  Al-Aswbagh na kuja nae Madinah, huyu ndiye mama wa mwanawe Salamah Ibn Abdirahmaan.

 

V.          Sariya ya Hamaj:

 Katika mwezi wa Shaaban, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimtuma Aliy Ibn Abiy Twaalib na watu mia.

Alimtuma kuwaongoza wenzake kwenda kwa Baniy Sa’ad Ibn Bakri pande za “Fadaka”, hiki ni kitongoji kilicho umbali wa siku mbili au tatu kutoka Madinah.

Kutumwa kwao huko ni kwa sababu ilimfikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-khabari kwamba wao wanataka kusaidiana na Mayahudi kuuvamia na kuushambulia mji wa Madinah.

Na tayari Mayahudi wa Khaibar walikuwa wamejianda kwa lengo hilo, Aliy akawaendea pamoja na wenzake mpaka wakalifikia eneo lenye maji liitwalo “Hamaj”.

Eneo hili lilikuwa baina ya Khaibar na Fadaka, hapo wakamkuta mmoja wa watu wale, wakampa amani ya nafsi kwamba hawatamdhuru.

Mbinu hii ikamlainisha hata akaweza kuwafahamisha walipo wenzake, na walipohisi kuwa wanafuatwa wakatimua mbio, na hakukamatwa hata mtu mmoja. Waislamu wakaitwaa ngawira mifugo yao; ngamia mia tano na kondoo/mbuzi alfu moja, wakafika nao Madinah bila ya kufikwa na dhara yo yote.